“Hata kama wataniua, usiwaache wakaliua jina langu” – Dedan Kimathi

 Na Ahmed Rajab

WAINGEREZA walipomtia kitanzi na kumnyonga Dedan Kimathi, mimi nilikuwa mdogo — sikuwa nimebalehe kimaumbile wala kisiasa.  Wala siku hizo sikujua Dedan Kimathi alikuwa nani. Hata kumsikia sikumsikia.

Kimathi alinyongwa asubuhi ya Februari 18, 1957 katika gereza la Kamiti karibu na Nairobi.  Kamiti ni gereza lenye ulinzi mkali tangu zama hizo za ukoloni hadi leo.  Ni gereza lenye mazingira machafu, lenye ukosefu wa maji na hata nafasi ya kutosha kwa idadi kubwa ya wafungwa wake.

Wafungwa gerezani humo huteswa kinyama. Na wenyewe kwa wenyewe hufanyiana mabaya. Baadhi ya wafungwa wana tabia ya “kuwasaka” na kuwalawiti kwa nguvu wafungwa wenzao wa kiume. Si pahala pa mtu kuwako.

Aliponyongwa, Kimathi alikuwa na miaka 36. Nchini Kenya akivuma na akiwatia khofu watawala wa kikoloni pamoja na Waafrika wenzake waliokuwa vibaraka wa wakoloni.

Akivuma kwa sababu alikuwa mmoja wa Maamiri Jeshi Wakuu (Field Marshal) waliokuwa wakiwaongoza wapiganaji wa Mau Mau.

Maamiri Jeshi wenzake walikuwa Jenerali China, Musa Mwariama, pamoja na Amiri Jeshi Mkuu wa kike, Muthoni Kirima.  Kwa hakika, walikuwepo wanawake wengi kwenye Jeshi la Mau Mau na walisaidia sana katika mapigano dhidi ya wakoloni.  Ili kuwatia adabu, serikali ya kikoloni iliwaweka kizuizini wanawake wasiopungua elfu nane walioshukiwa kuwa ni Mau Mau.  Waliteswa na baadhi yao walibakwa na wakoloni Waingereza.

Kimathi ndiye aliyekuwa “kubwa” lao hao Maamiri Jeshi Wakuu wa Mau Mau.  Alilipanga jeshi lao liwe na muundo rasmi kama wa jeshi la serikali. Yeye ndiye aliyeliandaa na kulizindua Baraza la Vita la Mau Mau, mwaka 1953.

Nasikitika kwamba kunyongwa kwake kulinikosesha fursa ya kukutana naye na pengine kunywa naye chai na kumdadisi kuhusu maisha yake.  Kwa hivyo, siwezi kupima kama kweli kiongozi huyo wa Mau Mau alikuwa fedhuli kama wanavyodai baadhi ya waliokuwa wakimjua au kama kweli alikuwa mshabiki wa mashairi kama wasemavyo wengine.

Binafsi niliwasikia Mau Mau wakitajwa kwa mara ya kwanza nilipokuwa chuoni, katika madrasa ya Msikiti Barza, Mkunazini, Unguja, ambako ndiko nilikosomeshwa Kurani.  Sijui siku hizi lakini zama zetu Msikiti Barza kilikuwa chuo cha Kurani kilichokuwa kikiendeshwa tafauti na vyuo vinginevyo vya Unguja. Nidhamu yake na mipango yake ilikuwa kama ya skuli za serikali.

Hatukuwa tukichanjishwa kuni au kubebeshwa ndoo za maji kama wanafunzi wa Kurani wa vyuo vingine.

Tulikuwa na vipindi vya mapumziko kama ilivyo katika skuli za serikali.  Hatukuwa na tabia ya kutoroka chuoni lakini kila tulipopata wasaa wakati wa mapumziko tukimzunguka mwenzetu Ahmed Masoud Borafiya kusikiliza masoga yake. Borafiya alikuwa kama sumaku iliyoyavuta masikio yetu. Soga lake lilikuwa tamu.

Tulikuwa hatutii letu alipofungua yeye mdomo. Tukiziacha hekaya zake zimdondoke kinywani mwake kwani masikio yetu yakiona raha fulani kumsikiliza. Sijui akiziokota wapi hadithi zake lakini zikitusisimua.

Siku moja Borafiya alitutajia Mau Mau.  Aliyotueleza yalinitisha. Khofu ikanigubika. Nikaanza kuwafikiria Mau Mau kuwa mijitu ya ajabu iliyotoka dunia nyingine. Nikazidi kujitisha kwa kujiuliza itakuwaje Mau Mau watapoingia mjini Unguja? Sikumbuki Borafiya kumtaja Kimathi, kiongozi wao Mau Mau. Pengine naye pia alikuwa hamjui.  Wakoloni wa Kiingereza wakimwita “gaidi” lakini kwa Waafrika wengi, ndani na nje ya Kenya, Kimathi alikuwa mkombozi, mwanamapinduzi na shujaa.

Hii leo kuna barabara zilizopewa jina lake Nairobi, Lusaka, Kampala, Mombasa, Nyeri, Nanyuki, Mpumalanga (Afrika Kusini) na Mwanza (Tanzania).  Huko Nyeri, Kenya, jina lake limepewa Skuli Kuu ya Sekondari, uwanja wa michezo, Chuo Kikuu cha Ufundi na uwanja wa michezo.

Dedan Kimathi Waciuru, maarufu Dedan Kimathi, alizaliwa Nyeri Oktoba 31, mwaka 1920.  Baba yake alifariki mwezi mmoja kabla hajazaliwa.  Alipozaliwa, mamake aliyeitwa Waibuthi na aliyekuwa mmoja wa wake watatu wa baba yake, alimpa jina la Kimathi wa Waciuru.  Waibuthi ndiye aliyemlea.

Alipokuwa barobaro wa miaka 15, Kimathi aliingia skuli ya msingi iliyokuwa ikiendeshwa na wamisionari na akaanza kusomeshwa Kiingereza.  Aliendelea kusoma katika skuli ya sekondari huko Tumutumu. Kimathi aliinukia kuwa na shauku kubwa ya uandishi na aliandika makala mengi kabla na hata wakati wa Vita vya Mau Mau.  Huko skuli alijiunga na Klabu ya Mijadala akijadiliana na wenzake kuhusu mada mbalimbali.

Kuna wasemao kwamba alipokuwa skuli na hata baadaye yeye na nidhamu walikuwa kama mbingu na ardhi.  Inasemekana utundu wake ulifurutu ada.  Kwa mfano, siku moja yeye na wenzake waliiba kengele ya skuli wakakimbia nayo hadi kwenye kilima cha Tumutumu. Walipofika juu ya kilima wakaanza kuipiga. Siku hiyo wamisionari walimsamehe, hawakumtia adabu.

Waingereza waliweza kuwashinda nguvu Mau Mau kwa msaada wa vibaraka wao, wale Waafrika waliowatumia dhidi ya Waafrika wenzao, wakombozi.  Vibaraka hao walikuwa askari wa jeshi la mgambo lililoundwa na Waingereza na waliloliita Home Guard (Ulinzi wa Nyumbani).  Hawa ndio waliotajwa juzi na Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, kuwa waliwasaliti Mau Mau na walijinyakulia mashamba makubwa makubwa ambayo baadhi yao yamekaa tu yakijitumbulia macho bila ya kupandishwa mazao yoyote.  Gachagua aliwataka wanyakuzi hao wazipe serikali baadhi ya hizo ardhi ili zipate kugaiwa Wakenya masikini wenye njaa ya ardhi za kulimia.

Hata baada ya Kimathi kunyongwa, Waingereza hawakupumua. Waliendelea kuingiwa kiwewe na kuwaogopa wanamapinduzi wa Mau Mau.  Khofu kubwa ya Waingereza ilikuwa kwamba Mau Mau watajikusanya tena na kuendeleza mapambano yao dhidi ya ukoloni na hususan dhidi ya wezi wa ardhi zao na mashamba yao.

Waingereza walikuwa na mkakati ambao walidhani kuwa utawanusuru. Waliwapika Waafrika maalumu wawe warithi wao; Waafrika wataouendeleza mfumo wa utawala wa ukoloni mamboleo.

Kwa kufanya hivyo, Waingereza walikabiliwa na kibarua kingine kipevu: kuhakikisha kwamba Waafrika waliowachagua wawe warithi wao watakuwa salama na hawatotimuliwa madarakani na wenzao waliokuwa wakipigania ukombozi halisi wa Kenya.

Pia Waingereza wakikhofia usishindwe mpango wao wa kusuasua suluhisho la kisiasa litalowapa madaraka vibaraka wao wa Kiafrika ambao wao wakiamini watayalinda maslahi yao na ya mfumo mzima wa kibepari nchini Kenya.  Kwa hakika, mpango huo ulifanikiwa kwani viongozi wote wa Kenya tangu nchi hiyo ipate uhuru wamekuwa wakiyalinda maslahi ya wakoloni waliokuwa wakiwakandamiza wanyonge wa Kenya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Si hayo tu. Viongozi wapya wa Kenya wamekuwa wakiukumbatia na kuulinda mfumo wa  kiuchumi unaohakikisha kwamba Kenya inaendelea kubanwa kwa makucha ya kibepari na ya utandawazi.

Inasemekana kwamba kweli baada ya Kimathi kutekwa wapiganaji wa Mau Mau, wengi wao Wakikuyu, walikuwa wakikusanyika na kupenyeza silaha misituni Kenya.

Nini kilichowafanya  wazalendo wa Kenya, wengi wao Wakikuyu, watwae silaha kupigana na Waingereza?  Jawabu fupi ni ardhi. Tangu Waingereza walipoanza kuingia Kenya walifanya ujanja, ghiliba na wizi kuwapora Waafrika ardhi zao, tena zile zilizokuwa za rutuba. Kama wakoloni wengine waliokwenda kwingi kwingine, wakoloni wa Kiingereza waliokwenda Kenya hawakualikwa nchini humo. Walijiingilia tu nchini mwa watu wakawafukuza wenyeji kutoka kwenye ardhi zao na mashamba yao na wakayatwaa wao.  Wakayafanya yao mali yao. Ulikuwa wizi wa mchana kweupe

Waafrika waliopokonywa ardhi walikuwa na njaa ya ardhi.  Na ardhi nayo ilikuwa na kiu, kiu ambacho Kimathi na wazalendo wenzake waliamini ni wao tu walioweza kukikata. kwa damu yao wenyewe.

Ndipo wapoamua kuanzisha vuguvugu la siri la kuwapiga vita wakoloni. Waliliita vuguvugu lao

Jeshi la Kupigania Ardhi na Uhuru. Lakini watu wengi wakilijua vuguvugu hilo la kwa jina la Mau Mau. Kuna mabishano na hadithi nyingi kuhusu asili ya jina “Mau Mau.”  Wapo wanaoeleza kwamba jina hilo ni ufupisho wa “Mzungu arudi Ulaya, Mwafrika apate uhuru.”

Inasemekana kwamba Kimati alijiunga na Mau Mau mwaka 1951 na aliwahi kukamatwa lakini akatoroka kwa kusaidiwa na askari wa Kiafrika.  Kimathi aliwapa taabu Waingereza katika vita vya msituni vilipopamba moto mwaka 1952 hadi vilipomalizika mwaka 1960 – miaka mitatu baada ya yeye kunyongwa.  Naye, kwa upande wake, alipata taabu kutoka kwa Mau Mau wenzake.

Ingawa alikuwa na haiba na akipendwa na wengi miongoni mwa Mau Mau, Julai 1953 aliparurana na wenzake waliokasirishwa na barua aliyomuandikia Gavana, Sir Evelyn Baring. Ingawa viongozi wenzake watatu walikubaliana naye na walimtaka akutane na Gavana, Mau Mau wa kawaida walipinga.

Kimathi alidokezwa kwamba kulikuwa na njama za kutaka kumuua na kwa hivyo, akiandamana na wasiri wake watano walikwenda mafichoni msituni.  Kukazuka mzozo mwingine baina yake na wenzake Februari 1954.  “Hapo ndipo nilipoamua kuachana na wenzangu,” alisema Kimathi kwenye nyaraka zilizo mikononi mwa serikali; nakala zikiwa zimepewa familia yake.

Akiwa mgonjwa na baada ya kutafakari kwa muda mrefu tarehe 20 Oktoba, 1956 Kimathi aliamua kuwaacha Mau Mau msituni na yeye atoke ende kusalimu amri kwa serikali ya kikoloni.  Ilisadifu kwamba tarehe hiyo hiyo mwaka 1952 Waingereza walimkamata Jomo Kenyatta na kumshitaki kuwa ndiye aliyekuwa akiwaongoza Mau Mau.  Kenyatta alikanusha lakini Waingereza walimpa kifungo cha miaka tisa.

Mambo mawili yalimzuia asitoke mapema msituni. La kwanza, ni kwamba akisubiri majibu ya barua ambazo alikuwa mara kwa mara akiiandikia serikali akitaka aonane nayo.  Jambo la pili, ni kwamba akijua ya kuwa akijitokeza hivi hivi tu basi angeuliwa ama na polisi au “home guard” ili hao wauaji wapewe zawadi na serikali kwa kumuua.

Ingawa alikuwa na azma ya kusalimu amri Kimathi, alipigwa risasi mguuni na akatekwa na askari wawili waliopewa zawadi ya shilingi 3,000 kila mmojawao.

Palipopambazuka Jumatatu ya tarehe 18 Februari, 1957 Kimathi, aliyekuwa Mkatoliki, alikuwa tayari keshayakubali mauti na akiamini kwa dhati kwamba ataingia peponi. Hakuwa mwoga.  Saa saba za usiku wa kuamkia siku hiyo, Kimathi alichukua penseli na karatasi akamwandikia barua Kasisi Marino wa Kanisa la Katoliki.

Alimuomba mambo matatu makuu: kwanza, alimtaka Father Marino asisahau kumpitia mamake Kimathi ambaye alikuwa mzee; pili, alimtaka mkewe asaidiwe hasa na watawa wa Kikatoliki kwa vile atakuwa mpweke baada ya kifo chake; na mwisho alimtaka amsaidie mwanawe asome skuli.

Vile vile  Kimathi aliandika: “Kwaheri dunia na vitu vyake vyote. Nisalimie wasomaji wote wa Wathiomo Mukinyu, [gazeti la Kikatoliki la huko Nyeri].”

Kimathi aliomba na ombi lake lilikubaliwa kwamba mkewe, Mukami, aliyekuwa pia amefungwa Kamiti aruhusiwe kwenda kumuona kabla hajanyongwa.  Mukami alipoingia chumbani alimuona mumewe akiwa na uso wa bashasha. Kimathi akasimama, akaruka kwenda kumkumbatia.  Akamnong’oneza: “Hata kama wataniua, usiwaache waliue jina langu.”

Aliendelea kumueleza mkewe kwamba ana hakika Waingereza wameazimia kumuua. “Sikufanya uhalifu wowote. Uhalifu wangu ni kwamba mimi ni mwanamapinduzi wa Kenya niliyeongoza jeshi la ukombozi. Sisikitiki ikiwa nitakuacha na familia yangu. Mti wa uhuru utakunywa damu yangu.”

Baada ya Uhuru, marais wawili wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi wote walimdharau Kimathi.  Hawakuwa wakimtaja kwa wema wala hawakumpa hadhi yoyote.  Mambo yalibadilika wakati wa Rais Mwai Kibaki.  Yeye ndiye aliyemtukuza kwa kumtambua rasmi Kimathi na Mau Mau wenzake kuwa ni mashujaa wa Kenya na  mwaka 2007 sanamu la Kimathi likafunuliwa jijini Nairobi.

Julai 11, 1990, Nelson Mandela alipozuru Kenya mara yake ya mwanzo baada ya kufunguliwa gerezani hamu yake kuu ilikuwa kuzuru kaburi la Dedan Kimathi, kumuona Mukami, mjane wa Kimathi na Jenerali China, kamanda wa zamani wa Mau Mau.  Bahati mbaya, Moi hakumruhusu. Siku mbili baadaye katika Uwanja wa Moi Kasarani, Mandela alimuaibisha Moi alipowataja kina Kimathi kuwa walikuwa wakombozi aliokuwa akiwahusudu na akasema hadharani kwamba ingekuwa heshima kubwa kwake akiwa mpigania uhuru kuwazuru mashujaa kama Kimathi na China na wengine “waliokuwa mishumaa katika vita vyangu virefu na vigumu dhidi ya dhulma.”

Miaka 15 baadaye akiwa si Rais ndipo Mandela, katika ziara yake ya pili Kenya, alipopata fursa ya kukutana na mjane wa Kimathi pamoja na mwanawe mkubwa wa kiume na binti yake.  Hakuweza lakini kulizuru kaburi la Kimathi. Hakuna anayejua lilipo.

Picha kwa Hisani ya Gazeti la Standard la Kenya.

Email: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab