Picha kwa hisani ya Gazeti la JAMHURI.
Na Ezekiel Kamwaga
KATIKA moja ya mikutano ya karibuni kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na wabunge wa Bunge la Tanzania, mmoja wa wabunge alisimama na kuzungumza maneno ya kumhakikishia Rais kwamba kwa mujibu wa mila na desturi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) suala la urais wake mwaka 2025 halina shaka na kwamba hakutakuwa na wa kumpinga.
Baada ya kumsikiliza, Rais Samia aliamua kumjibu hapohapo kwamba “Kama mtataka kunipa urais kwa sababu ya mila na desturi na si kwa sababu ya kutimiza majukumu yangu ipasavyo, ni afadhali msinipe”. Pasi na shaka, ujumbe wa Rais kwa wabunge na wana CCM waliokuwemo kwenye mkutano ule ulikuwa mmoja tu; “sitaki kubebwa, nachapa kazi”.
Binafsi sikushangaa nilipoambiwa Rais ametamka maneno hayo. Kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais Samia alikuwa mgombea mwenza wa hayati Dk. John Magufuli na kauli mbiu yao ya kampeni wakati huo ilikuwa ni HapaKaziTu. Ilikuwa wazi kuwa yao itakuwa serikali ambayo utendaji kazi wenye matokeo yanayoonekana kwa wananchi ndiyo itakuwa njia yao ya kukonga nyoyo za wananchi.
Ndiyo sababu nilifadhaika na kushangaa wakati nilipomsikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akizungumza mbele ya Rais Samia kwenye shughuli rasmi ya kiserikali ijini Dar es Salaam kwamba amepanga kufanya mkutano na viongozi wa kidini mkoani kwake kuhakikisha kwamba “Rais hapingwi”. Kauli ile ilikuwa ya hatari kutamkwa mbele ya Rais na umma pia.
Nitamke mapema kwamba wakati uteuzi wa Chalamila ulipotangazwa, nilihisi moja kwa moja kwamba kwa maana ya kazi za siasa, atakuwa na msaada zaidi kwa Rais na CCM kwa ujumla kuliko ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Amos Makalla. Ingawa wote ni makada wa chama hicho, Chalamila ana ulimi mwepesi na anajua kuzungumza lugha ya wananchi kumzidi mtangulizi wake huyo.
Hata hivyo, kwa maana ya kazi ya siasa, sioni ni kwa namna gani kauli ile ya Chalamila inamsaidia Rais au chama chake kwa namna yoyote. Ikrari, kwa upande wangu, nadhani ni kauli inayotoa picha kwamba wapo viongozi serikalini ambao bado wanafanya kazi kwa kufikiri nchi yetu ni ya chama kimoja na tunaishi kwenye zama za “Zidumu Fikra za Mwenyekiti”.
Kwa kuangalia nchi yetu ilikotoka katika kipindi cha miaka mitano hadi sita iliyopita, kauli kama ya Chalamila inatonesha vidonda ambavyo kwa wengine bado ni vibichi. Kuna Watanzania wanaoishi leo ambao wanajua nini maana ya kuwa na “Rais asiyepingwa”. Jambo la ajabu ni kwamba Chalamila alizungumza hayo akijua kwamba Rais Samia ametumia sehemu kubwa ya muda wake madarakani, kujiondoa kwenye mzingile wa utawala wa kiimla.
Kama kuna kitu wanafunzi wa siasa za kidunia wamejifunza, ni kwamba mabadiliko ya kiongozi kutoka kuwa mtu wa watu hadi kuwa yule wa kiimla hutengenezwa mara nyingi si na mazingira ya ukuaji wake au nchi yake ilivyo, bali aina ya watu waliomzunguka na maneno wanayomtakia kila siku. Maneno yanayozungumzwa hapa kidogo, pale kidogo, kule kidogo, asubuhi, mchana na usiku, ndiyo mwishowe huanza kuwa na athari kwenye kumjenga kiongozi asiyesikia. Mifano ya hayo iko mingi.
Hayati Rais mstaafu wa Kenya, Daniel arap Moi, alipenda kutamka mbele ya Rais Jomo Kenyatta – enzi akiwa Makamu wa Rais, kwamba yeye hana mawazo yoyote na kwamba anachofanya ni kufuata nyayo za Kenyatta. Ziko hotuba alizozungumza hadharani kwamba kazi ya viongozi wengine itakuwa ni kusikiliza na kufanya kile anachosema yeye tu.
Wakati hayati Rais Robert Mugabe akianza kuharibikiwa kwenye urais wake, wabunge kama Tony Gara, ndiyo walianza kumharibu kwa kutamka hadharani kuwa “Mugabe ndiye mtoto pekee wa Mungu aliyebaki duniani baada ya kupaa kwa Yesu Kristo”. Inanikumbusha msemo maarufu pia wa dikteta Kamuzu Banda wa Malawi aliyepata kusema; “Staili ya Malawi ni kuwa Kamuzu anasema kitu na baada ya hapo hakuna mwingine wa kusema chochote kingine.
Mifano iko mingi na kwa Watanzania wenye kumbukumbu watakumbuka namna katika miaka ya karibuni ilivyoanza kujengeka tabia ya viongozi mbalimbali wakiwemo wa kidini, wasanii, taasisi zinazoheshimika na watu maarufu kuzungumza kwa kusifu – kabla ya Kiongozi Mkuu kuzungumza na wananchi baada yao. Huko ndiko tulikokuwa tunaelekea.
Ni muhimu sana kwa viongozi na watu wenye mamlaka kuepuka kuzungumza hadharani kauli zenye lengo la kuonyesha kwamba kiongozi hatakiwi kupingwa. Katika simulizi za Roma ya kale, kuna ngano inayozungumzia maneno memento mori (Kumbuka, kuna siku utakufa). Katika siku ambazo Mfalme wa Dola ya Warumi alikuwa akipongezwa kwa ushindi mkubwa vitani au jambo lolote kubwa – kuna mtu alikuwa anatumwa kwenda kumtamkia sikioni; “Mheshimiwa Mfalme, kumbuka kuna siku utakufa” halafu anaondoka zake.
Lengo la tabia hiyo halikuwa kumtisha au kumfanya Mfalme ajisikie vibaya, lengo lilikuwa kumfanya ajione mwanadamu mwenye mapungufu yote ambayo wanadamu wengine wote wanayo. Na nadhani, kama kuna kitu muhimu ambacho watu kama akina Chalamila wangeweza kufanya ni kumwonyesha na kumtambulisha Rais Samia kama mwanadamu anayejitahidi kwa kadri ya uwezo wake kubadili maisha ya Watanzania.
Suala la Rais kupingwa ni suala la kidemokrasia. Tanzania inafuata mfumo wa demokrasia ambapo vyama tofauti vina wajibu wa kuonyesha mbadala wa maono yao wenye kuifanya nchi yetu kuwa nzuri zaidi. Nchi yetu ina watu zaidi ya milioni 60 sasa, inakuwaje tuwajengee dhana kichwani kwamba kuna mtu mmoja miongoni mwa hao ambaye hatakiwi kupingwa?
Chalamila ni msomi mzuri na bila shaka atakuwa amesikia maneno mashuhuri ya Mao Zedong aliposema “acha maua 1,000 yachomoze” akimaanisha wakati mwingine wingi wa mawazo ndiyo kitu kinachotakiwa kwenye ujenzi wa nchi. Ni vema tukaacha viongozi wetu wapingwe kwa lengo la kuchochea kilicho bora zaidi.
Bahati nzuri, Watanzania ni werevu na wanajua pumba na mchele vilipo. Kama watu watakuja na hoja au ajenda zilizokengeuka, Watanzania watawajua kwa namna hiyo. Kama hao wanaopinga watakuja na ajenda nzuri zaidi na zenye faida kwa maslahi ya nchi yetu, si sisi ndiyo tutafaidika zaidi? Ni muhimu kwa viongozi kuchunga ndimi zetu.
Mwandishi ni mwandishi wa habari