Picha: Mwandishi wa makala haya, Ezekiel Kamwaga, akihojiwa na Shirika la Utangazaji wa Rwanda kama sehemu ya jopo la waandishi wa habari wa nchi mbalimbali za Afrika walioripoti kuhusu Uchaguz Mkuu wa Rwanda wa mwaka 2017. Picha ya Maktaba
Na Ezekiel Kamwaga
UMEWAHI kujiuliza ni kwa namna gani makundi mbalimbali ya waasi huwa wanaishi wanapokuwa msituni wakiishi kusubiri kupindua serikali zilizo madarakani? Nimekuwa najiuliza swali hili kwa muda mrefu na majibu niliyapata nchini Rwanda hivi karibuni.
Nkomeje Jean Claude (36) mmoja wa waliokuwa waasi katika kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), alinipa sentensi moja tu (kwa Kiswahili chake chenye lafudhi ya Kicongo) iliyonipa majibu yote; “Mwenyewe yuko na bunduki halimagi (Mtu mwenye bunduki halimi).”
Kwa maelezo yake mwenyewe, bunduki ndiyo inakupa kila unachotaka. Ukisikia njaa unavamia kwa wananchi na kupora chakula chao. Ukihitaji nguo au viatu unavamia sokoni na bunduki yako na unateka vitu. Kila unachotaka unaweza kukipata kwa kutumia bunduki yako !
“Bunduki pia inakupa fursa ya kumnunulia zawadi mpenzi wako. “ Kama akipita mwanamke amevaa vizuri na amependeza na nguo yake mpenzi wako alikuwa anaitaka kwa muda mrefu, unakwenda na kumvua yule mwanamke na kisha unampelekea zawadi mwanamke wako. Unatumia bunduki yako kupata kila unachotaka,” anasema Nkomeje huku akitabasamu.
Nkomeje ni sehemu ya waliokuwa askari katika kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR ) ambao sasa wameamua kurejea nyumbani (Rwanda) kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako kundi hilo limeweka makazi yake ya kudumu.
FDLR ni kundi lililoundwa kutokana na mabaki ya waliokuwa askari katika Jeshi la Rwanda chini ya serikali ya hayati Rais Juvenal Habyarimana –wanaotumiwa kushiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 kabla ya mauaji hayo.
Mara baada ya majeshi ya Rwanda Patriotic Front (RPF) yaliyokuwa yakiongozwa na Jenerali Paul Kagame kutwaa madaraka, waasi hao walikimbilia nchini DRC ambako walitumia majina mbalimbali kabla ya jina la sasa la FDLR.
Kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Rwanda, katika kipindi cha kati ya mwaka 1996 hadi mwaka huu, jumla ya askari 51,000 waliokuwa wakitumikia FDLR nchini DRC wamerejea kwao baada ya kukiri makosa waliyoyafanya na kukubali kujenga taifa jipya lisilo na ubaguzi.
“Baadhi ya waliokuwa waasi walijiunga na kundi hilo pasipo kujua nini haswa wanakipigania. Waliambiwa maneno ya uongo na kuyaamini. Ukiwauliza wanakwambia hawakujua chochote. Kazi yetu sasa ni kuwajenga kisaikolojia ili warejee uraiani na kuwa raia wema,” anasema Frank Musonera, Mkuu wa kambi ya kuwapokea na kuwafundisha waasi hao wa zamani iliyopo wilayani Rubavu.
Nilifanikiwa kuhudhuria katika darasa la mafunzo ya waasi hao wa zamani na nilikuta wanafundishwa uzalendo, ujasiriamali na masuala mengine ya kujenga amani na mshikamano. Waasi hao walikuwa wanaimba nyimbo za Kinyarwanda na mwenyeji wangu alinitafsiria kwamba nyingine zilikuwa zinahusu msamaha wanaoomba kwa Mungu na waliowakosea wakati walipokuwa wakiasi au wale walioua wakati wa mauaji ya kimbari.
“Nimeua watu wengi ingawa sikumbuki idadi. Unajua unapokuwa kwenye vita wewe unapiga tu risasi na hujui ya kwako imempiga nani na haikumpiga nani. Hata wakati ule tunakimbia kimbia kutoka Rwanda (mwaka 1995), nilikuwa naua tu mtu ninayekutana naye njiani na kumtilia mashaka. Lakini hayo yamepita na sasa niko tayari kujenga nchi yangu,” anasema Nkomeje.
Kijana mwingine wa umri wa makamo, Ibrahim Bizihalimana, alinisisimsha kwa vile alinieleza namna alivyokimbia kutoka Rwanda na kujikuta yuko Kigoma, Tanzania. Kwa maelezo yake, kuna wakati alikuja nchini ili asaidie kusafirisha madawa yaliyokuwa yakitumika kutibia waasi hao.
“Nilifurahia maisha ya Kigoma. Pale tulikuwa na antena yetu (antenna kwa tafsiri yake inamaanisha mtawanyiko wa kundi kwa maana kwamba kama kuna masalia ya FDLR popote pale, wao wanaita kwa jina hilo). Niliishi vizuri na hakukuwa na shughuli za kijeshi. Ila tukitaka kusafirisha madawa tunayapokea na kuyasafirisha kupitia Ziwa Tanganyika,” anasema kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
Uso kwa uso na muuaji
Wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, mji mmoja kusini mwa Rwanda uitwao Murambi, ulijipatia sifa ya kipekee. Katika eneo ambalo ilijengwa Shule ya Ufundi, zaidi ya Watutsi na Wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani 45,000 waliuawa na kundi la Interahamwe lililokuwa likiungwa mkono na serikali ya Rwanda.
Mara baada ya ajali ya ndege iliyopoteza maisha ya Habyarimana mnamo Aprili 6 mwaka huo, Watutsi walianza kuhisi kwamba hatari inawasogelea maana propaganda za chuki kwamba wao ndiyo waliomuua rais huyo kutoka kabila la Wahutu, zilikuwa zimewajaza watu chuki.
Naambiwa wakaanza kukimbia majumbani mwao na kuelekea kwenye nyumba za ibada ili kuokoa maisha yao. Hata hivyo, viongozi wa serikali wa Wilaya ya Murambi waliwashauri kwamba ni vema wakakimbilia kwenye shule ya ufundi ya Murambi ambako ingekuwa rahisi kwao kupata huduma.
Inaelezwa takribani watu 60,000 walikuwa wamekwenda kujihifadhi kwenye shule hiyo. Ghafla, serikali ikakata huduma za maji na umeme. Wananchi wakaanza kushindwa kupika na kula. Wakadhoofika. Ilipofika Aprili 16, wananchi hao wakiwa wamedhoofu, Interahamwe wakavamia na kufanya mauaji hayo ya kutisha wakitumia bunduki, visu, mishale, mapanga, nyundo na marungu.
Nilipotembelea katika Makumbusho ya Murambi ambayo yamejengwa katika eneo hilo ambako zamani ilikuwapo shule, nilijionea jiografia ya mahali hapo. Japo na yenyewe ilikuwa iko juu kutoka usawa wa bahari, imezungukwa na vilima vingine pande zote. Ni wazi kwamba waliowashauri wananchi wakimbilie kule walikuwa wamewatafutia sehemu ambayo wangeweza kuwaona kwa urahisi na kuwazunguka pia.
Miili ya waliouawa, wengine walizikwa wakiwa hai, imehifadhiwa katika makumbusho hayo. Niliingia na kwenda kuiona na ingawa sasa yamebaki mafuvu na mifupa mitupu, harufu ya maiti bado inavuma na ilinichukua siku mbili kuacha kuihisi kwenye mikono na nguo niliyovaa. Ni kitu cha kusikitisha kuona maiti ya mtu anayezikwa akiwa hai, anakufa huku akiona kifo chake na mwili unapambana. Mifupa yake inaonyesha namna alivyokufa akiogopa kifo chake.
Nilipotoka nje ya makumbusho hayo, nakutana na Nyirimbuga Emmanuel (52), mmoja wa watu waliofanya mauaji hayo lakini sasa wamekiri makosa yao, wametumikia adhabu zao na sasa wanaishi katika jamii hizohizo walizoziletea maafa makubwa.
“Wakati wa mauaji yale nilikuwa nikiishi kwenye nyumba ile (ananionyesha nyumba moja iliyojengwa juu ya miongoni mwa vilima vinavyoizunguka shule ya Murambi). Wale waliokimbilia hapa nilikuwa nikiwaona kila siku wakiongezeka. Viongozi wetu wa serikali, redio na magazeti walikuwa wakitufundisha kwamba wakati wa kuwamaliza Watutsi umefika,” anasema Nyirimbuga kwa Kinyarwanda ambacho nilitafsiriwa na mwenyeji wangu.
“Kwa kweli nakumbuka kuua watu kama saba hivi. Ila ninakumbuka zaidi watu watano kwa vile walikuwa ni watu niliowafahamu vizuri. Walikuwa ni jirani zangu na kuna mmoja wakati namuua aliniuliza kwanini unaniua? Wakati huo sikujali nafanya nini maana propaganda ya chuki ilikuwa imenijaa.
“Kuna mtoto nilimuua kwa kumpiga rungu. Kuna watu wazima niliwaua kwa kutumia panga. Nilitumia silaha za jadi maana zilikuwa zikigawiwa na viongozi wetu kwa kila aliyetaka. Sikuchagua nani wa kumuua, mradi nilijua huyo mtu ana sifa za Watutsi mimi nilikuwa naua tu.
“Mara tukasikia kwamba RPF wameshinda vita na sisi tulioua tunatafutwa sana ili nasi watuue. Nikaanza kukimbia. Huko njiani ukiona mtu anakuhisi au vipi unaua. Sasa sijui nao walikuwa wanakufa au wanapona lakini la msingi nilikuwa nadhuru.
“Kwanza nilikimbilia DRC kujiunga na waliokuwa waasi. Hata hivyo, baadaye nikabaini kwamba Wakongomani walikuwa hawatupendi sana na maisha yalikuwa magumu. Baadaye nikaenda kutafuta maisha Angola lakini askari wa kule hawakunipenda. Nikaondoka tena.
“Lakini, wakati ule wa mauaji nilikuwa na mke na watoto wanne na nilipoondoka sikujua wanaendeleaje. Hata hivyo, nilipokwenda ugenini na kuanza kutafakari kuhusu maisha yangu, nikaanza kuona dhambi niliyoitenda. Nikasema nitarudi nyumbani (Rwanda) nikatubu.
“Wakati ule kulikuwa na maneno mengi kuhusu sisi tulioua. Wenzangu ambao tulishiriki pamoja kuua walikuwa wakiniambia nisirudi nyumbani. Hata hivyo, kila nilipokimbia niliona kama nakimbia dhambi niliyoifanya. Nikasema afadhali nirudi nyumbani ili hata nikiuawa, nife nikiwa na amani moyoni.
“Ndipo nikarudi na kutubu makosa yangu. Sikuuawa. Nimeamua kusema yote haya ili niwe na amani moyoni mwangu. Kuna watoto zangu hawazungumzi nami. Mke wangu pia kanitoroka. Naishi mwenyewe tu lakini nina amani.
“Nikipita njiani watu wananionyeshea vidole kwamba Yule ndiyo muuaji aliyeua watoto wetu, ndugu na jamaa zetu. Lakini nimeamua kuishi hivyo. Hata hivyo, nahisi nina amani moyoni kuliko wale walioamua kukimbia maisha yao yote. Angalau mimi nitazikwa nyumbani kwangu nitakapokufa. Kuna wakati unatamani kufa ili yote haya yaishe lakini nina misheni kwenye maisha yangu na nitaitekeleza,” anasema Nyirimbuga.
Shati alilovaa limechakaa. Suruali yake pia na viatu vyake vinaonyesha kwamba ni mtu anayeishi kwenye mazingira magumu. Hata uso wake umepoteza mng’aro na anaonekana mkubwa kuliko umri wake wa miaka 52. Lakini angalau Nyirimbuga atakufa akiwa na amani moyoni mwake. Nilimuaga nikimwita shujaa kwa maana anachokifanya ni kitu kigumu sana.
Ana kwa Ana na Bwana wa Vita
Kwa wafuatiliaji wa siasa za Afrika Magharibi, watakuwa wanafahamu kitu kuhusu vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyochakaza nchi za Sierra Leone na Liberia kwenye miaka ya 1999. Katika vita hiyo, maelfu ya watu waliuawa, kuporwa mali zao na kufanywa walemavu wa kudumu.
Kwa kiasi kikubwa, vita hiyo ilichochewa sana na biashara mbili kubwa; ya almasi na ya silaha. Kwamba wafanyabiashara wa silaha walikuwa wakiuza bidhaa hiyo kwa kubadilishana na almasi. Ni vita hiyo ndiyo ambayo ilikuja baadaye kutoa filamu ya Blood Diamonds na ile documentary maarufu ya War Don Don iliyotayarishwa na mwanamama Rebecca Richmann Cohen.
Nilipokwenda nchini Rwanda, nilifanikiwa kutembelea Gereza Kuu la Nyanza lililopo katika wilaya ya Nyanza. Lengo lilikuwa kuangalia namna tu wafungwa wa nchi hiyo wanavyoishi na kuendesha maisha yao.
Kwa bahati tu nikaambiwa kuna wafungwa kutoka Sierra Leone ambao wamo ndani ya gereza hilo. Nikaomba kwenda kuwasalimia na nilipofika, hamad !- Nikakutana na mtu ambaye nimemsoma kwenye vitabu na kumwona kwenye documentary. Anaitwa Issa Hassan Sesay.
Mwaka 2009, Sessay alihukumiwa na Mahakama ya Kimataifa Kuhusu Sierra Leone kwenda jela kwa muda wa miaka 52 kutokana na maovu aliyoyafanya wakati wa vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe. Sesay alikutwa na hatia ya makosa 16 kati ya 18 aliyotuhumiwa kuwa nayo. Baadhi ya makosa yake yalikuwa ni mauaji, ubakaji, kukata watu viungo vya mwili, utesaji, uporaji wa mali, uingizaji watoto jeshini na mambo mengine chungu nzima. Hakuna uovu wa kivita ambao hakushitakiwa kwayo.
Sesay ambaye ndiyo kwanza ana umri wa miaka 43 sasa, alipewa cheo cha Jenerali na kundi la waasi la United Revolutionary Front (RUF) wakati akiwa na umri wa miaka 30 tu. Nilimkuta kwenye chumba chake akiwa anasoma biblia. Amevaa tisheti yenye jezi ya timu ya Arsenal ya England na mezani akiwa na picha za mchezaji Cristiano Ronaldo.
Nilimuuliza, “wewe ndiye Issa Hassan Sesay?”, akanijibu mimi ndiye. Kwa sadfa tu (nikiazima neno la mwandishi nguli, Ahmed Rajab”, kumaanisha neno coincidence), wakati nakwenda Rwanda nilikuwa nasoma kitabu cha mwandishi wa Afrika Kusini, Andrew Feinstein kiitwacho The Shadow World: Inside the Global Arms Trade, ambacho kimeeleza mengi kuhusu Sierra Leone na hivyo picha nzima ya matukio ilikuwa kichwani kwangu.
Nilipojitambulisha kwake kama Mtanzania, Sesay alitabasamu na akaniambia anafahamu Tanzania ina chuo kizuri cha kijeshi ambapo baadhi ya maofisa wa kijeshi wa taifa lake walikuwa wakija kupata mafunzo.
“Mna chuo kizuri (Tanzania Military Academy-TMA). Askari waliokuwa wametoka kufundishwa Arusha walikuja kuwa askari wazuri sana. Mimi sikupitia lakini kwetu kule tunafahamu kwamba askari aliyepitia Tanzania ni mzuri,” ananiambia.
Nilimuuliza kama anajutia alichokifanya wakati wa vita ile ya wenyewe kwa wenyewe na jibu lake lilikuwa fupi; “Its war, my friend…. You either Kill or be Killed.” (Ni vita, rafiki yangu, ama unaua wewe au unauawa.”
Miongoni mwa ukatili mkubwa kuwahi kufanywa katika vita ya Sierra Leone ilikuwa ni ile iliyoitwa Operation No Living Thing ambapo maelfu ya watu walikatwa mikono na miguu, kuuawa na kuchomewa mali zao.
Nilimuuliza Sesay nini ilikuwa dhamira ya ukatili wa namna ile; “Kile kinachoitwa Operation No Living Thing kilitengenezwa na vyombo vya habari vya Magharibi. Hakukuwa na operesheni kama hiyo na unajua wazungu wanapenda tu kutengeneza maneno ambayo wakati mwingine hayapo.
“Nakubali kwamba nimeua watu. Tena nimeua watu wengi sana. Sikuzaliwa ili niwe muuaji. Mfumo ulionikuza ndiyo ulionifanya baadaye niwe nilivyo. Kama mfumo ungekuwa mzuri au usingetengeneza mazingira haya, leo tungekuwa tunazungumza mengine,” anasema.
Ushauri wowote kwa Watanzania? Sesay anaasa umakini wa hali ya juu kwenye kuangalia rasilimali za taifa. Kilichowaponza Sierra Leone, ananiambia bwana huyu wa vita ni utajiri wake wa almasi na kama Tanzania ina utajiri wowote ule, basi ijitazame.
Watoto hawa masikini
Ukienda nchini Rwanda na hatimaye ukafika jijini Kigali, nakushauri ukatetembelee Makumbusho ya Gisozi. Hapo ndiyo utaona ni kwa vipi mwanadamu anaweza kugeuka kuwa mnyama mkatili kuliko wanyama wenyewe.
Utaona sura ya mtoto mzuri wa kike, Fidele Ingabire aliyekuwa na umri wa miaka tisa lakini akauawa kwa kupigwa risasi ya kichwa na wauaji wakati wa mauaji ya kimbari. Kuna mwingine aliyekuwa na umri wa miaka minane tu, Chanelle Ruterana, ambaye alikatwakatwa mapanga hadi kufa.
Wapo watoto wengine wadogo zaidi kama Honore Gatera waliouawa kwa kupigwa marungu. Katika sehemu zote ambazo nilitembelea na kuona unyama wa wanadamu, hakuna nilipoumia kama Gisozi. Wakati mtu anapochochea vita au ubaguzi wa namna yoyote ile, ni vema kwanza akakumbuka watoto wake na madhila watakayoyapata.
Wakati nilipozungumza na Sesay alikuwa ametoka kula wali na nyama. Wakati nazungumza na Nyirimbuga alikuwa akinywa maji. Wanavyokula hao watu na wanavyokunywa ndivyo hivyohivyo ambavyo Watanzania wanavitumia.
Rwanda, Sierra Leone na kwingineko hawakupigana kwa sababu wako tofauti na sisi. Walipigana kwa sababu mfumo ulilea mazingira hatarishi. Kama alivyopata kuniambia Sesay, hakuzaliwa muuaji lakini mazingira yalimtengeza akawa alivyo sasa.
Tutazame kauli zetu. Tutazame matendo yetu. Tuangalie kalamu zetu. Isifike wakati tukaanza kuabudu bunduki na mapanga ili tusiende shambani kulima au maofisini kufanya kazi.
Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.