Afrika Kusini ilicheza na shingo ilitoa

Picha: Mmoja wa waandamanaji akifurahia hukumu ya Mahakama ya Haki ya Kimataifa (ICJ) dhidi ya Israel jijini The Hague hivi karibuni. Picha kwa hisani ya Foreign Policy

 

Na Ahmed Rajab

 

ISRAEL haina uso.  Inajaribu kujikaza kisabuni na kujitoa kimasomaso lakini Mahakama ya Kimataifa (ICJ), mjini Hague, Uholanzi, yameiumbua kwa unyama inaoufanya dhidi ya wakaazi wa Gaza.

 

Ijumaa iliyopita, Januari 26, 2024, Mahakama hayo — ambayo ni ya juu kabisa kimataifa — ilitoa uamuzi wake kuhusu mashtaka yaliyowasilishwa na Afrika Kusini. Nchi hiyo iliishitaki Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

 

Afrika Kusini iliyataka mahakama hayo yailazimishe Israel isimamishe mashambulizi yake Gaza ili kuepusha hayo mauaji ya kimbari.

 

Hatua ya Afrika Kusini ilikuwa ya kijasiri.  Ni nchi pekee duniani iliyothubutu kuifanya Israel iwajibike katika mahakama ya kimataifa miaka yote 75 tangu taifa hilo la Kiyahudi liundwe.  Serikali ya Afrika Kusini imeonesha ushujaa na papo hapo kuwa inayajali maadili ya kimataifa.

 

Kwa hivyo, ushujaa wake ni ushujaa adilifu — ni ushujaa wenye kuongozwa na imani ya kuwa wanaadamu wote ni sawa na maisha yao wote ni adhimu na ni lazima yaheshimiwa na yalindwe.

 

Hilo ni funzo kubwa ililolitoa Afrika Kusini. Si funzo kwa Israel pekee lakini lilikuwa somo pia kwa madola makubwa ya Magharibi yenye kuibeba Israel. yakiongozwa na Marekani.

 

Madola hayo yalikuwa yakiikebehi Afrika Kusini kwa kuishitaki Israel mbele ya Mahakama ya Kimataifa.

 

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, kwa mfano, alikuwa miongoni mwa waliokuwa mbele mbele wakisema kwamba mashitaka ya Afrika ya Kusini hayakuwa na msingi.  Kejeli zake zilikaririwa na kushadidiwa na vyombo vikuu vya habari vya mataifa ya Magharibi.

 

Vyombo hivyo hivyo vya habari pamoja na serikali za nchi zao vilikuwa vikiyarudiarudia matamshi ya kijeuri ya kuitoa maanani hatua ya Afrika Kusini. Jeuri hiyo ilikuwa ikitamkwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na wakuu wenzake wa serikali ya Israel.

 

Hata kabla ya Mahakama ya Kimataifa kutoa uamuzi wake, wakuu hao walikuwa wakisema kwamba wataendelea kufanya wayafanyao na hawatoujali uamuzi wa Mahakama, ikiwa utakwenda dhidi ya Israel.

 

Walikuwa wakisema hivyo huku wakidokeza kwamba walikuwa na hakika ya kuwa Mahakama itayatupilia mbali mashitaka ya Afrika ya Kusini.

 

Yaliyojiri Ijumaa iliyopita mbele ya Mahakama ya Kimataifa yaliifedhehesha Israel. Ilikuwa ni aibu tupu kwake.  Ingawa itabidi tusubiri kwa muda mrefu, pengine wa miaka kadhaa, kabla ya Mahakama kutoa hukumu ya mwisho iwapo Israel imekuwa ikifanya mauaji ya kimbari, hata hivyo Mahakama yalilikataa ombi la Israel la kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali.

Badala yake yalizikubali hoja zote zilizotolewa na Afrika Kusini kuunga mkono mashitaka yake dhidi ya Israel.

 

Kwa ufupi, Mahakama yalikubali kwamba mashambulizi yanayofanywa na Israel Gaza yanaashiria mauaji ya kimbari. na yakaitaka Israel ihakikishe kwamba haiwaui ovyo raia

 

Baada ya kuzikubali hoja hizo na hivyo kuthibitisha kwamba kesi ya Afrika Kusini ina msingi, Mahakama ya ICJ yalitoa maamuzi sita ya dharura.  Maamuzi yenyewe yanaishurutisha Israel ihakikishe kwamba wanajeshi wake hawatowaua watu ovyo ovyo na kusababisha mauaji ya kimbari Gaza.

 

Pia, Mahakama yameitaka Israel ichukuwe hatua zitazozifanya ziwe nzuri hali za kibinadamu za wakaazi wa Gaza.

 

Mahakama hayo yalikuwa na jopo la majaji 17, wakiongozwa na Rais wao kutoka Marekani, Jaji Joan Donoghue, na makamu wake, Kirill Gevorgian, kutoka Urusi.

 

Majaji 15 walikubaliana kuyaunga mkono maamuzi yote ya Mahakama.

 

Jaji mmoja, Aharon Barak, kutoka Israel, aliyaunga mkono maamuzi mengi ya Mahakama hayo.  Lakini kulikuwa na jaji mwengine aliyeushangaza ulimwengu.  Jaji huyo Julia Sebutinde, kutoka Uganda, aliyapinga maamuzi yote.  Na maamuzi yote yalikuwa dhidi ya Israel.

 

Kulikoni? Walimwengu wamekuwa wakijiuliza ilikuwaje hata Sebutinde akawa jaji pekee aliyeyapinga maamuzi yote dhidi ya Israel?  Wakuu wa serikali ya Uganda mbio mbio walijaribu kujitenga na Sebutinde.

 

Ilibidi wafanye hivyo kwa sababu matamshi yake yangeweza kuiadhiri serikali ya Uganda.  Sebutinde alikuwa akisema maneno kana kwamba yeye ni Israel. Alithubutu hata kuituhumu Afrika Kusini kuwa na uhusiano na Hamas.

 

Matamshi yake yangeweza pia kumweka pabaya Rais wake, Yoweri Museveni. Mwezi uliopita Museveni alishika wadhifa wa uwenyekiti wa Mvuvumko wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.  Nchi nyingi zilizo kwenye mvuvumko huo zinawaunga mkono Wapalestina.

 

Hadharani, serikali ya Uganda imekuwa ikionekana kama inawaunga mkono Wapalestina.  Sebutinde, kwa upande wake, hadharani alikuwa akionesha wazi kwamba anaiunga mkono Israel, tena kwa nguvu hata zaidi ya mwanajopo mwenzake kutoka Israel, jaji Barak.

 

Wakuu wa Uganda walifanya hivyo licha ya kuwa serikali yao ilifanya kampeni kubwa ya kumpigania Sebutinde achaguliwe kwenye jopo la majaji wa Mahakama ya Kimataifa.

 

Na kuna wanaokumbusha kwamba Uganda ina mahusiano mazuri na Israel, hasa na makampuni ya ulinzi na ya kijasusi.

 

Maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa  yalikuwa ya kihistoria ingawa Mahakama hayakuiamuru Israel isimamishe kabisa mashambulizi yake ya Gaza. Maamuzi hayo yaliipa ushindi Afrika Kusini.

 

Kwa ushindi huo, Afrika ya Kusini imejitukuza na imelitukuza bara zima la Afrika kwa kusaidia kuiumbua Israel.

 

Hivi sasa, Israel imekwama.  Imekwama katika medani ya sheria za kimataifa na imekwama katika medani ya mapigano.

 

Miezi mitatu imekwishapita tangu itangaze vita vya kulipiza kisasi Gaza dhidi ya muqawama wa Hamas na Islamic Jihad.  Israel ilianza mashambulizi yake baada ya mavamizi ya ghafla Israel yaliyoongozwa na Hamas. Mamavizi hayo yaliwaua watu 1,139 nchini humo.

 

Miongoni mwa waliouliwa walikuwa raia 695 wa Israel (wakiwa pamoja na watoto 36), watu 71 waliokuwa raia wa nchi nyingine, na wanajeshi wa Israel 373.

 

Wapiganaji wa muqawama pia waliwashika watu wasiopungua 250 na wakawachukua hadi Gaza. Wengi wa mateka hao walikuwa Waisraeli, wanajeshi na raia wa kawaida, wakiwa pamoja na watoto 30.

 

Hamas na Islamic Jihad waliwashika mateka hao ili kuilazimisha Israel iwafungue maelfu ya Wapalestina kutoka magereza ya Israel, wengi wao wakiwa wamefungwa bila ya kufikishwa mahakamani.

 

Kufikia Septemba 2023 ilikisiwa kwamba Wapalestina wanaokaribia elfu tano walikuwa wamefungwa katika magereza ya Israel. Tarakimu hiyo ilitajwa na B’tselem, kituo kinachoshughulikia haki za binadamu katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa nguvu na Israel.

 

Waziri Mkuu Netanyahu, na wakuu wengine wa serikali yake walisema kwamba mashambulizi ya Israel Gaza yana malengo mawili makuu: kuwaokoa mateka wanaoshikwa na Hamas pamoja na Islamic Jihad na kulishinda nguvu na, hatimaye, kulimaliza kabisa kundi la Hamas.

 

Hadi sasa Israel imeshindwa kuyatimiza malengo hayo. Ilichoweza kufanya ni kuwaua kinyama maelfu ya Wapalestina, wakiwemo wanawake na watoto na kuangamiza miundombiu pamoja na taasisi za Gaza.

 

Inakisiwa kwamba tangu yaanze mashambulizi yao majeshi ya Israel yamewaua zaidi ya watu 26,000 wa Gaza.  Majeshi hayo ya Israel yamewatia vilema maelfu ya wakaazi wa Gaza au wamewajeruhi vibaya sana.

 

Inakadiriwa pia kwamba makombora ya Israel na wanajeshi wamezibomoa au kuziharibu asilimia 61 ya nyumba zilizokuwa Gaza.

 

Kwa mambo yalivyo, haioneshi kama Israel ina mizungu yoyote ya kuweza kujikwamua na kuyaondosha majeshi yake Gaza. Kwa hali hii ni wazi kwamba Israel imeshindwa katika mashambulizi yake Gaza.

 

Israel imeua, inaendelea kuua, imebomoa, na inaendelea kubomoa, lakini bado wapiganaji wa Hamas wanapambana na wanajeshi wa Israel.  Bado Hamas inarusha makombora yake Israel.

 

Kundi hilo la wapiganaji linayakabili majeshi ya dola zima la Israel lenye kuungwa mkono, kwa hali na mali na kwa mikakati, na madola makubwa yenye uwezo usiosemeka wa kiuchumi, kiteknolojia na wa mbinu za kivita.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; X/@ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.