Aina tano za UONGO wa ubeberu, ukweli mmoja wa umma

Picha: Mmoja wa waandamanaji barani Ulaya akiwa ameshika bango linalotaka majeshi ya Israel yasitishe mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina hivi karibuni. Picha kwa hisani ya mtandao wa Forward.

 

Na Issa Shivji

 

KUNA mtu aitwaye Joseph Goebbels aliyekuwa Waziri wa Propaganda katika utawala wa fashisti Adolf Hitler. Goebbels aliwahi kusema ukirudiarudia uongo hatimaye unakuwa ukweli. Inaelekea hiyo ndio mbinu inayotumiwa na Wazayuni wa Israel. Mimi nitaigusia mifano michache ya uongo wao wanaoutumia katika hivi vita dhalimu dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

 

Uongo #1: Hamas ni chombo cha ugaidi cha Kiislamu kinachoamini kuua Wayahudi wote. Uongo. Ukweli ni kwamba Hamas ni chama cha ukombozi kinachodai uhuru kamili wa Palestina. ‘Uhuru kamili” maana yake ni uhuru wa eneo lote kutoka mto wa Jordan mpaka Bahari ya Mediterranean (from river to sea/Palestine shall be free). Nia ya Hamas ni kuyakinga maisha na mali ya wakaazi wa Gaza dhidi ya Jeshi la Israel. Kwa lengo hili Hamas wana kitengo cha wanamgambo kiitwacho Al Qassam Brigade (Brigedi ya Al Qassam).

 

Mara kwa mara, wanamgambo wa Hamas hurusha roketi nchini Israel, ili kupambana na mashambulizi ya Israel. Roketi hizi hazina uwezo mkubwa wa kuua halaiki ya watu au kubomoa majengo. Inasemekana kwamba kati ya 2001 na 2023, yaani katika kipindi cha miaka 23, watu waliouawa na roketi za Hamas walikuwa 68.

 

Hamas pia ni chama cha kisiasa ambacho kiligombea na kushinda uchaguzi wa bunge mnamo Januari 2006 na kuunda utawala wa Gaza chini ya himaya na uangalizi wa Israel. Gaza haina serikali inayojitegemea bali utawala unaoundwa na Hamas ni kama wa kinyapara. Hata hivyo, Hamas ilipata mafanikio makubwa kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wakaazi wa Gaza, zikiwa pamoja na afya, elimu na maji. Hiyo hasa ndio nguvu ya Hamas — yaani kuwahudumia wakaazi wa Gaza.

 

Lakini huduma hizi hutegemea Israel kuruhusu malori yaliyobeba mahitaji muhimu kuingia Gaza.  Mahitaji yenyewe ni chakula, maji, mafuta, madawa na vifaa vya kutibu wagonjwa. Kila siku, katika siku za kawaida, malori takriban 400 hadi 500 huingia Gaza. Tangu mashambulizi yaanze Oktoba 7, hakuna hata lori moja lililoruhusiwa kuingia Gaza. Juzijuzi baada ya shinikizo kubwa la umma, malori kati ya 20 hadi 30 yameruhusiwa. Hii ni tone tu katika bahari ya mahitaji.

 

Wazayuni pia wamekata umeme na maji kwa matumizi ya Gaza. Isitoshe, wamefunga njia zote za mawasiliano. Wakaazi wa Gaza hawawezi kutoka nje ya Gaza —  hawana uwanja wa ndege. Imezoeleka kusema kwamba Gaza ni jela lenye wafungwa takriban milioni 2 na laki tatu. Ukweli ni kwamba Gaza ni zaidi ya jela. Gaza ni kambi ya mateso (concentration camp).

 

Lengo la Wazayuni ni wazi: kuua mamia ya watoto, wanawake na wazee wa Gaza kwa kuporomosha makombora bila kikomo, kwa upande mmoja, na kuwanyima maji na vyakula ili mamia wengine, pamoja na wagonjwa mahututi na watoto wachanga, wafe. Wanachotaka Wazayuni ni Wapalestina wote wahame Gaza na wawe wakimbizi katika nchi zingine na Israel iimeze ardhi yote ya Palestina.

 

Uongo #2: Israel ina haki ya kujilinda. Huo ndio wimbo wa viongozi wote wa kibeberu waliokwenda kumuona na kumkumbatia Benyamin Netanyahu. Uongo. Kwani jeshi gani limeivamia Israel? Israel inajilinda kutoka kwa nani? Watoto wa Wapalestina? Kisingizio hicho sio tu hakina mashiko bali ni dharau kubwa kwa akili ya binadamu.

 

Hao waliokwenda eti kumfariji Netanyahu hawana aibu. Rishi Sunak, waziri mkuu wa Uingereza, alikwenda kumfariji Netanyahu akisafiri katika ndege iliyojaa silaha. Hakwenda na shehena ya madawa kwa ajili ya watoto wa Palestina bali alikwenda na silaha za kuwaua watoto wa Palestina. Yaani huyu mtu kauweka ubinadamu wake rehani!

 

“Hoja” ya nchi za kibeberu kwamba Israel ina haki ya kujilinda ni kisingizio tu cha kufunika ukweli kuhusu dhuluma na mateso dhidi ya Wapalestina. Wao ni washirika wakubwa katika maauaji ya kimbari yanayoendeshwa na Israel. Nchi za kibeberu kwa kuendelea kupeleka silaha Israel na kufunika dhambi za Israel zinazifanya ziwe washirika katika lengo la kuwaua na kuwatesa Wapalestina na kufuta kabisa maono ya Taifa la Palestina na dai la Wapalestina la kuwa na taifa lao ambamo wataishi kama watu huru. Kufuta maono na madai haya kamwe hakutowezekana. Vizazi na vizazi vya Waplaestina vitaendelea kudai haki zao, kwa njia moja au nyingine.

 

Uongo #3: Wazayuni na washirika wao na vyombo vyao vya mawasiliano karibu vyote katika nchi za magharibi wanadai kwamba chanzo cha mashambulizi ya halaiki yanayoendelea Gaza ni uvamizi wa Oktoba 7 uliofanywa na wanamgambo wa Hamas nchini Israel, kuwaua raia na kuwateka nyara watu. Huu ni uongo wa kusukwa. Ndio wanamgambo wa Hamas waliingia nchini Israel; ndio mamia ya watu waliuawa; na ndio wanamgambo wa Hamas waliwashika mateka. Lakini, mashambulizi ya Gaza, mateso na dhuluma na ukatili wa Israel dhidi ya Wapalestina, hayakuanza Oktoba 7. Dhuluma hili na ukatili huo ulianza na kuendelea kwa zaidi ya miongo saba tangu nchi ya Israel ibuniwe mwaka wa 1948.

 

Mnamo mwaka huo wa 1948 peke yake wanamgambo wa Kiyahudi walivamia miji na vijiji takriban 530, wakauua watu tarkriban 15,000 na kuwafukuza kwa mabavu wakaazi wa Kipalestina karibu 800,000 ambao waliishia katika makambi ya wakimbizi katika nchi za Kiarabu. Wapalestina hukumbuka siku hiyo kama siku ya NAKBA, yaani siku ya janga kwa watu wa Palestina, sio janga la asili bali ni janga lililopangwa makusudi na Wazayuni.

 

Nakba haikuishia 1948. Imekuwa ikiendelea mwaka hadi mwaka. Sitaki kuorodhesha kwa sababu majanga yamekuwa mengi na kila mara mamia ya wakaazi wa Gaza wameuliwa. Leo Gaza haina uchumi wa maana; wakaazi wake wanaishi kwa misaada na kudra ya Mungu; vijana wasio na kazi ni zaidi ya aslimia 50. Watu wa Gaza hawana tena matumaini na uhakika wa kuishi. Katika mazingira na hali hii, mwanadamu na utu wake afanye nini? Asalimu amri na kuwapigia magoti madhalimu wao au ajilinde na apigane akiwa amesimama kwa miguu yake? Watu wa Gaza ni binadamu kama sisi. Wana utu wao, wana heshima zao na wana fahari yao. Kamwe hawatasalimu amri. Wanataka uhuru wao maana hakuna chochote chenye thamani zaidi ya uhuru.

 

Kama alivyoimba mwimbaji wa Palestina hayati Rim Banna:

 

Sarah Sarai was taking her first steps on the soil of

Palestine

And her laugh was covering, covering the sky of

Palestine

 

       The sniper took her by surprise with a shot in

the head, in Sarah’s little head

 

Take the blindfold off of Sarah’s eyes so she can see

the face of her killer

 

Tafsiri ya Kiswahili

 

Sarah Sarai alianza kupiga hatua za kwanza juu ya ardhi ya

Palestina

Na kicheko chake kilifunika, kilifunika anga ya

Palestina

 

Mlenga shabaha stadi alimshitua kwa kumfyatulia risasi

kichwani mwake, kichwa kichanga cha Sarah

 

Ondoeni barakoa aliyofunikwa macho yake, ili aweze kuiona

sura ya muuaji wake

 

Mpaka liini mnataka watu wa Gaza wafunikwe macho yao kwa barakoa?! Wana haki ya kuwaona wauaji wao…na kuwashughulikia kwa njia zinazowezekana.

 

Uongo #5: Kwamba mapambano yanayoendelea na yaliyoendelea kwa miongo zaidi ya saba ni kati ya Waislamu na Wakristo; ni kati ya Wayahudi na Waarabu. Uongo mtupu. Tunatakiwa tuelewe vizuri mambo yafuatavyo:

 

Mosi, Wapalestina wote sio Waiislamu. Wako Wapalestina ambao ni Wakristo. Na makombora ya Israel hayachaguii kuua Waislamu tu. Juzijuzi yalibomoa Kanisa. Mapambano haya ni ya ukombozi; sio vita vya dini.

 

Pili, Wayahudi wote sio Wazayuni. Uzayuni ni itikadi ya kibaguzi na yenye imani kali kwamba Wayahudi ni wateule wa Mungu wenye haki zaidi ya wengine. Wayahudi wengi tu hawakubaliani na imani hii ya Wazayuni. Wayahudi wengi tu wameandamana kuilaani Israel na kuwaunga mkono Wapalestina pamoja na kutaka Israel isitishe mara moja kunyesha mabomu.

 

Tatu, Waarabu wote sio Wapalestina. Wapalestina ni wakaazi wa nchi iliyokuwa inaitwa Palestina kabla ya Israel, yaani kabla ya mwaka 1948, na ilikuwa chini ya usimamizi (mandate) wa Uingereza.

 

Nne, wako Wayahudi waliokuwa wakiishi na Waarabu nchini Palestina, wote wakijitambulisha kama Wapalestina. Wazayuni wengi kwa kweli ni wahamiaji kutoka nchi za Ulaya na ndio waliokuwa chanzo cha ugaidi dhidi ya Waarabu wa Palestina ili wahame na wao Wazayuni wabaki kuunda nchi yao ya kikaburu ya Israel.

 

Hatimaye walifanikiwa mwaka wa 1948 wakiungwa mkono na nchi za kibeberu, hususan Marekani.  Baada ya vita vya pili, kulikuwa na vuguvugu la nchi za Mashariki ya Kati kupata uhuru. Katika hali hiyo, Marekani ilitaka kulidhibiti vuguvugu hilo pamoja na kuhakikisha nchi hizo za Kiarabu zisiangukie katika kambi ya Ujamaa wa Kirusi. Kwa hivyo, waliona nchi kama Israel ingekuwa “wakala” wake mzuri wa kendeleza himaya yao ya kibeberu.

 

UONGO wote huo unaendelezwa na nchi za kibeberu na vyombo vyao vya mawasiliano, ambavyo vingi vinamilikiwa na Wazayuni, kwa maslahi yao ya kuendelea na himaya yao na kuutawala Umma ulimwenguni.

 

Kujumuisha, hatuna budi kila mmoja wetu aelewe kwamba yanayoendelea Gaza ni mapamabano dhidi ya ubeberu wa kibepari na Uzayuni wa kikaburu. Kwa mantiki hii, Wapalestina wako mstari wa mbele na wanajitoa mhanga kwa maslahi yao na maslahi ya nchi zote ambazo bado ziko chini ya himaya ya ubeberu.

 

Safari hii Umma duniani kote umeungana kufichua uongo na kutekeleza kwa mshikamano upingamizi wao dhidi ya ubaguzi wa Kizayuni na ukatili wa ubeberu. Wasiwasi wa Umma ni, moja, kwamba Wazayuni na Washirika wao wako mbioni kutekeleza mauaji ya kimbari mbele ya macho yetu, na, pili, vita dhidi ya Palestina vinaweza kufurika na kusababisha vita vya dunia ambavyo havitaiacha nchi yoyote wala watu wowote salama.

 

NI WAJIBU WA KILA BINADAMU POPOTE PALE ALIPO,

MWENYE MOYO UNAODUNDA,

MWENYE MAPAFU YANAYO PUMUA,

MWENYE AKILI TIMAMU,

NA UBINADAMU UNAOJALI,

KUZUIA MAUAJI YA KIMBARI,

NA VITA VYA DUNIA VISITOKEE.

 

USIKAE KIMYA,

PASHA HABARI,

PAZA SAUTI,

ONGEZA NENO.

 

SHINIKIZA MAMLAKA YA NCHI YAKO,

KUTOKUCHEZA KAMARI NA MAISHA YA WANANCHI WAKE,

KUTOKUJIPENDEKEZA KWA UBEBERU

ETI YANAYOENDELEA GAZA HAYATUHUSU.

 

Issa Shivji ni Profesa Stahiki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  Shivji ni miongoni mwa mabingwa wakuu barani Afrika wa masuala ya sheria na maendeleo ya nchi.  Amesomea shahada yake ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki (Dar es Salaam).  Ana shahada ya uzamili katika sheria (LLB) kutoka Chuo cha London School of Economics cha Uingereza na shahada ya Uzamivu PhD kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  Ameandika vitabu visivyopungua 18 vikiwa pamoja na cha mashairi.  Kwa miaka 36 alikuwa profesa wa hadhi ya juu wa masuala ya sheria ya katiba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na profesa wa kwanza wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere.  Amesomesha katika taasisi na vyuo vikuu vya nchi mbalimbali duniani zikiwa pamoja na Mexico, Zimbabwe, Uingereza, Hong Kong, Afrika Kusini na Senegal.