Picha: Picha ya pamoja ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, na Balozi na Waziri Mstaafu, Ali Karume. Kwa Hisani ya Jambo TV.
Mzingile ni tafsiri ya Kiswahili ya neno labyrinth
Na Ezekiel Kamwaga
SAKATA la mwanasiasa na mwanadiplomasia mwandamizi wa Zanzibar, Ali Karume, kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) limeibua swali moja kubwa kwa wafuatiliaji wa siasa za visiwani humo; Nini kinaendelea?
Balozi Karume si mwanasiasa wa kawaida wa Zanzibar. Yeye ni mtoto wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) lakini pia ni mdogo wa aliyepata kuwa Rais wa SMZ, Amani Karume. Kama Zanzibar ingekuwa nchi ya kifalme, tungesema Ali anatokea kwenye ukoo wa kifalme.
Pasi na shaka yoyote – na kama ilivyoeleza taarifa ya kumvua uanachama, maneno na matendo ya karibuni ya Karume ndiyo yamelazimisha viongozi wake kuchukua hatua waliyochukua.
Kabla ya kujibu kuhusu nini kinaendelea visiwani Zanzibar, ningependa kwanza kutoa muktadha wa hatua hiyo iliyochukuliwa kwa mwanasiasa huyo mkongwe.
Zanzibar na wanasiasa wa aina ya Karume
Kihistoria, tangu enzi za chama cha Afro Shirazi (ASP) kilichoungana na TANU kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977, wanasiasa wenye tabia ya kubishana na kupingana waziwazi – na wakati mwingine sirini, na viongozi wa serikali wamekuwa si watu wanaovumiliwa kwenye siasa za Zanzibar.
Wakati wa utawala wa Mzee Karume – baba wa Ali, kwenye miaka ya 1964 hadi mwaka 1972, Zanzibar ilipitia kile ambacho wasomi kama Marie Aude Fouere, wamewahi kukiita Dark Age (1964 – 1975). Hiki ni kipindi ambacho kuna viongozi na wanasiasa ambao waliuawa au ‘kushughulikiwa’ kisiasa kwa sababu ya tofauti zao na serikali iliyokuwa madarakani.
Kwa ujumla, kumekuwa na namna takribani tatu ambazo zimetumiwa na watawala wa Zanzibar kupambana na wale inayoona wanawapinga walio madarakani. Namna ya kwanza ni ile iliyowakuta akina Abdullah Kassim Hanga kwenye miaka ya 1960 – ya kupotea katika mazingira yenye utata.
Namna ya pili ilitokea zaidi kwenye miaka ya 1980 – wakati utawala wa Rais Idris Abdul Wakil, ulipoamua kuwafungulia kesi za uhaini akina Maalim Seif Sharif na kuwafunga gerezani.
Namna ya tatu – na pengine ya kiungwana zaidi, imekuwa ya kuwapa majukumu wanasiasa wa aina hiyo Tanzania Bara. Ipo mifano mingi, kwa mfano ya watu kama Abdulrahman Babu, walioletwa kufanya kazi katika serikali ya Muungano.
Wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar walikuwa na dhana pia kwamba uteuzi wa mtu kama Dk. Mohamed Ghalib Bilal, kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ulikuwa na lengo pia la kumwondoa kwenye siasa za Zanzibar.
Baada ya matukio ya kuchafuka kwa hali ya kisiasa visiwani Zanzibar mwaka 1984, CCM iliamua kuwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, ataishi Kigamboni, Tanzania Bara, kwa maisha yake yote yaliyobaki pasi na kurejea visiwani humo alikozaliwa.
‘Majukumu’ ya nje ya Zanzibar yalikuwa na maana ya kumpa Rais wa visiwa hivyo, muda wa ‘kupumua’ na kutekeleza majukumu yake pasipo kuangalia mgongoni mwake kila wakati.
Lakini kuna upande mwingine wa shilingi. Huu unahusu ni kipi wanasiasa binafsi wamekuwa wakifanya dhidi ya CCM. Mifano si mingi sana. Lakini kuna ule wa Maalim Seif na wenzake kuhamia upinzani. Lakini, kuna wengine ambao huamua kujiweka pembeni na kufanya mambo kwa namna wanayotaka – mfano mzuri ukiwa wa hayati Mzee Hassan Nassor Moyo.
Hata hivyo, CCM kama chama kimewahi kufukuza wanachama wake miaka ya nyuma. Kimsingi, Katiba ya chama hicho inaeleza utaratibu wa kufukuza wanachama na aina ya makosa yanayoweza kusababisha mwanachama kufukuzwa.
Kwenye miaka ya 1960, wakati CCM ingali ikijulikana kama TANU, ilifukuza kundi la wanachama wake akina Elly Anangisye, waliokuwa wapinzani wa siasa za Ujamaa zilizokuwa zinafuatwa mara baada ya Azimio la Arusha la mwaka 1967.
Katika miaka ya karibuni, CCM pia imewahi kumfukuza uanachama – na baadaye kumsamehe, aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT), Sophia Simba, pamoja na waliokuwa Wenyeviti wa Mikoa wa chama hicho kufuatia matukio yaliyotokea kwenye mchakato wa kusaka mgombea urais wa chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
Ukifuatilia kwa karibu, kuna mwenendo unaofanana unaohusu namna CCM inavyoshughulika na wanachama wake wanaoonekana kwenda nje ya mstari. Kwa mfano, jambo la kwanza linahusu nguvu ya kisiasa ya mwanachama husika.
Chukulia mifano miwili kwenye kipindi cha miaka 30 iliyopita. CCM haikuwahi kumfukuza uanachama Augustine Mrema, hata kama alikuwa akionyesha dalili za kutaka afukuzwe na Rais Ali Hassan Mwinyi, baba wa Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi.
CCM ilimwacha Mrema alalamike, agombe na kubwatuka, hadi alipoamua mwenyewe kuhama chama hicho na kujiunga na kile cha upinzani cha NCCR Mageuzi.
Pamoja na kumfukuza Sofia Simba mwaka 2017, CCM haimkufuta uanachama Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye kimsingi ndiye aliyezungumza na waandishi wa habari kueleza kutokubaliana na uamuzi wa kumpitisha John Magufuli kuwa mgombea urais wa CCM.
Miaka michache iliyopita, CCM iliwahoji na kutowachukulia hatua makatibu wakuu wake wastaafu, Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba, walioandika waraka uliolalamikia vitendo vya udhalilishaji na kashfa vilivyokuwa vikifanya na watu dhidi yao – bila wahusika kuchukuliwa hatua zozote kichama au kiserikali.
Kwa maana hiyo, wakati Sofia Simba na wenzake walifukuzwa; Mrema, Nchimbi, Kinana na Makamba, hawakuwahi kufukuzwa. Hawa ni wanasiasa waliojulikana kuwa na uungwaji mkono mkubwa kwenye chama, jamii au wenyewe kuwa wanasiasa wenye ushawishi.
Ni kama vile kuna kanuni isiyoandikwa popote inayosema kwamba CCM kwa kawaida huwa haimfukuzi mwanachama wake mwenye walau mojawapo ya sifa mbili; mwenye ushawishi binafsi kwenye chama au jamii au anawakilisha kundi maslahi muhimu miongoni mwa yale yaliyo ndani ya chama hicho.
CCM ilipata shida na Edward Lowassa wakati anazunguka katika nyumba za ibada akichangisha misaada na kuzungumza na waumini katika namna ambayo chama hakikuwa kimekubali au kuzoea. Lakini kilimvumilia mpaka alipoamua mwenyewe kuhamia Chadema.
Turudi kwa Karume sasa.
Swali ambapo msomaji utakuwa unajiuliza kufikia hapa ni moja; Je, Balozi Ali Karume anaangukia katika kundi lipi miongoni mwa niliyoyataja hapo juu? Jibu langu ni kuwa Ali anaangukia katika kundi ambalo kwa kawaida si aina ya wanachama wanaofukuzwa.
Hana ushawishi mkubwa ndani ya jamii ya Wazanzibari kwa sasa – kwamba yeye kama yeye anaweza kuwania urais na kuisumbua CCM; kama ambavyo Lowassa au akina Maalim Seif, Hanga au Jumbe wangeweza, lakini anatoka katika kundi muhimu ndani ya CCM Zanzibar.
Hili ni kundi la wanasiasa wa CCM wanaojinasibu kama walinzi na wahafidhina wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Kuna taarifa kwamba hili ni kundi ambalo halikumuunga mkono Mwinyi kwenye kinyang’anyiro cha mwaka 2020.
Mwinyi hawezi kumfanyia Balozi Karume mambo ambayo utawala wa Mzee Karume uliwafanyia waliokuwa wapinzani wake. Nyakati, tabia na nguzo ya kisiasa ya Mwinyi wa sasa na Karume wa nyakati zile ni tofauti. Balozi huyu hadi sasa hajafanya kosa linaloweza kufanya apate kesi ya aina waliyopata akina Maalim Seif wakati wa utawala wa Abdul Wakil.
Kwa sababu ya umri wake mkubwa, ni vigumu kuona akipangiwa majukumu Tanzania Bara, ili ampe Mwinyi nafasi ya kupumua. Kimsingi, sidhani kama mamlaka za Tanzania Bara zina hamu ya kuwa na mtu wa aina ya Balozi Karume kwenye upande wa pili wa Muungano.
Kete ambayo CCM Zanzibar inaweza kufanya ni kumweka Karume kwenye mazingira ambayo yeye mwenyewe ataamua kuhama chama na kwenda upinzani. Hivi ndivyo CCM ilivyofanya pia kwa Mrema na Lowassa huku Tanzania Bara. Kwa sababu ya asili ya siasa za Tanzania/Zanzibar, endapo Karume ataamua kuhamia upinzani, hakutakuwa na wa kumfuata huko.
Maneno atakayokuwa akizungumza yatakuwa sawa na yale ambayo akina Jussa Ismail Ladhu na Mansour Himidi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo wanayazungumza. Ni rahisi kwa maneno kutoka nje ya CCM kuonekana kama ‘’siasa tu” kuliko maneno hayohayo yakizungumzwa na mtu kutoka miongoni mwa makundi yaliyo ndani ya chama.
Nini kinaweza kutokea baada ya kufukuzwa?
Nimeandika huko juu kwamba kwa kawaida, Karume si aina ya wanachama ambao CCM huwa inawafukuza. Lakini yeye tayari amefukuzwa. Kama ambavyo CCM iliwahi pia kumfukuza Mansour Himidi akiwa Katibu Mwenezi na akitoka katika kundi la walinzi wa mapinduzi kama Karume.
Tofauti ya Mansour na Balozi Karume ni kwamba inaonekana ACT Wazalendo haina mshawasha wa kumpokea. Huyu ni mtu ambaye amewahi kutoa kauli za kuudhi dhidi ya wapinzani na mwenye sifa tofauti na yale ambayo chama hicho kikuu cha upinzani kinayasimamia.
Pia ACT Wazalendo ni chama kilichojengwa kwenye misingi ya kinidhamu isiyoruhusu wanasiasa wanaopenda kukosoana na kusemana hadharani kama Karume. Vigogo wa ACT wanajiuliza kama kuwa na Karume ndani yao haitakuwa sawa na kuhamisha matatizo ya CCM ndani yao.
Naamini kwamba uamuzi wa ghafla wa kumvua Ali uanachama una lengo ka kumwonyesha kile ambacho CCM inaweza kumfanyia. Tofauti na namna – kwa mfano, alivyofukuzwa Mansour ambapo vikao vilifanyika mchana kweupe, hili la Ali limefanyika usiku na katika mazingira yanayoonyesha kuwepo kwa shinikizo la aina fulani.
Pengine hatua hii ina kazi moja kubwa – ya kumfanya Balozi huyu machachari afanye jambo moja; kufunga mdomo wake. Kauli za Ali Karume zina mwangwi mkubwa wakati zikizungumzwa na mwana CCM.
Kama CCM itabaki na msimamo wake wa kumvua uanachama na hakutakuwa na mazungumzo ya nyuma ya pazia kumtaka anyamaze ili arudishiwe uanachama, Karume atakuwa na machaguo mawili; kuhamia ACT, ambako hakuna mshawasha wa kumtaka, au kuzungumza kama kiongozi mstaafu – akifuata njia iliyofuatwa na Mzee Moyo.
Tatizo la kuzungumza kama kiongozi mstaafu ni kwamba itabidi naye aanze kujiangalia mambo yake ya zamani. Kuwa kwake CCM kulilinda nyumba yake ya vioo, nyumba hiyo haitakuwa na ulinzi wakati anaporusha au kurushiwa mawe nje ya CCM.
Kwa sasa, mpira uko kwa Balozi Ali Karume.