#Siasa

Bandari inavyorarua vazi la Nyerere

 

 

Na Peter Nyanje

 

KATI ya mambo yaliyoibuka kwa hisia kali kwenye mjadala wa uwekezaji katika bandari nchini ni suala la Muungano. Ingawa hivi sasa hoja hii inaonekana kama imekufa pengine kwa sababu haikuwa katika kiini cha mjadala yaani vifungu vya mkataba, lakini hisia zilizotolewa kwenye kulijadili suala hilo zimeacha makovu ambayo pengine ni makali zaidi kuliko makovu kwenye Muungano yaliyopata kuachwa huko nyuma.

 

Hisia hizo ziliibuliwa na kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ambaye, pamoja na mambo mengine, alihoji kwa nini bandari za Zanzibari hazikuhusika katika mkataba huo wakati bandari ni kati ya masuala ya Muungano.

 

Lakini lililoibua hisia zaidi ni kuhusisha kwake kwa viongozi wakubwa wawili waliohusika katika mkataba huo, Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ujenzi, Prof. Makame Mbarawa, na asili yao (Zanzibar) na kuachwa kwa bandari za Zanzibar katika mkataba huo unaotajwa kuwa na manufaa makubwa kwa nchi.

 

Mbowe alihoji iwapo mkataba una faida kubwa kwa nchi kwa nini viongozi hawa wawili hawakuhusisha bandari za eneo ambako wao wanatoka? Awali, hoja hii ya Mbowe ilionekana kama suala la kuvamia faragha za viongozi hawa wawili lakini yalipoanza kutoka majibu ya hoja hii ndipo mjadala ukaegemea na kujikita kwenye suala la Muungano.

 

Unapozungumzia Muungano unazungumzia moja ya mambo ambayo Mwalimu Julius Nyerere alilitumia kushona moja ya tunu za taifa ya umoja na mshikamano. Muungano ni moja ya mavazi maridadi ambayo Mwalimu Nyerere si tu aliyashona, bali alijivika na kutembea nalo kifua mbele huku na kule akiona fahari kwalo. Muungano na lugha ya Kiswahili ni kati ya vitu ambavyo vilimsaidia sana Mwalimu Nyerere kuiweka nchi pamoja, hali iliyodumu hadi hii leo.

 

Sasa, mjadala wa bandari umeendelea kulirarua vazi hilo kama ambavyo limekuwa likiraruriwa na mijadala mingine kadhaa iliyoibuka siku zilizopita.

 

Pamoja na hilo, mjadala huu wa bandari pia umerarua vazi jingine la Nyerere ambaye hakuamini katika uwekezaji kutika nje ya nchi. Katika moja ya hotuba zake aliwahi kuonya hatua za nchi kutegemea uwekezaji kutoka nje ya nchi. Anasimulia jinsi walivyoikataa sheria ya uwekezaji iliyopendekezwa na serikali kwa sababu tu msisitizo wa sheria ulikuwa ni kukaribisha wawekezaji kutoka nje, wakati msimamo wake yeye ulikuwa ni kuendelea wawekezaji kutoka ndani.

 

Hili la msimamo wa Mwalimu katika uwekezaji linaweza kuwa linajibiwa kwa hoja kuwa mazingira ya uchumi wa wakati Nyerere anatoa onyo hilo ni tofauti sana na hali ya sasa kiuchumi. Na pia serikali haitotoa bandari yote kwa wawekezaji kutoka nje bali sehemu yake tu (tumeambiwa kuwa ni asilimia nane tu kwa Bandari ya Dar es Salaam).

 

Kuhusu Muungano, ndani ya mjadala wa bandari, wengi tunakumbuka jinsi ambavyo mmoja wa wanasiasa nguli visiwani, Ismail Jussa, mmoja wa viongozi makini na mtu ambaye anachagua vizuri maneno anapozungumza ili kumaanisha kile anachokisema, alivyojibu suala hili akilihusisha na suala la Zanzibar kunyang’anywa haki zake kadhaa kupitia Muungano na Tanganyika. Hapo wakaibuka watu wengi kutoka serikalini na kwenye vyama vya siasa, hasa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakikemea mwelekeo wa mjadala huo na kuonya kuwa unahatarisha umoja na amani ya taifa.

 

Hadhari hizo zilitolewa kwa sauti kubwa ambayo kimsingi ikanyamazisha hoja zilizogusa uasili wa Rais Samia na Prof. Mbarawa na hatua yao ya kusaini mikataba inayohusu bandari za upande mmoja wa Muungano.  Lakini hadi kufikia hatua hiyo Muunganio ulikuwa umesharururiwa vya kutosha.

 

Lakini kama unadhani kuwa hadhari hizo zimefanikiwa kuzima hoja za watu wanaohoji kuhusu uhalali wa Muungano, basi utakuwa unakosea sana kwa sababu historia inatuonyesha kuwa suala la bandari ni moja ya mambo mengi ambayo yanahusisha suala la Muungano na kuibua mjadala ambao kama kawaida ya mijadala ya Muungano, inakuwa ya hisia kali.

 

Mathalani, mwaka 2013 iliibuka hoja ya Hati ya Muungano. Ilikuwa inajadiliwa kwa hisia kali sana kiasi kuwa baadhi ya watu waanza kuamini kuwa mwisho wa Muungano umekaribia. Katika moja ya makongamano yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka huo kule Zanzibar, wastaafu wa kada mbalimbali serikalini waliitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wakati huo ikiwa chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohammed Shein, kuonyesha Hati ya Muungano hadharani ili kuuridhisha umma kuwa kweli visiwa vya Unguja na Pemba viliingia katika Muungano na Tanganyika kwa hiyari na Muungano huo ulikuwa na nguvu kisheria.

 

Lakini kabla ya hapo, mnamo mwaka 2001, kundi la wazee kutoka Pemba, wakiongozwa na mwenyekiti wao, Hamad Ali Mussa, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Ole kisiwani Pemba, walitinga katika ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam na madai ya kutaka kisiwa cha Pemba kijitenge na Unguja ili kiwe na mamlaka yake kamili. Walifika ofisi hizo wakiwa na ombi la kutaka kupatiwa hati za utawala wa kisiwa cha Pemba, wakisema wamechoka kuwa chini ya Unguja ambako kwa muda mrefu wanasiasa wake wengi wameonekana kuukumbatia Muungano licha ya athari zake kwa Zanzibar.

 

Ukiliangalia suala hilo unaweza kudhani kuwa migogoro kuhusu Muungano inamomonyoa umoja baina ya Unguja na Pemba. Lakini hali halisi ni kinyume chake kwani mara nyingi hoja za Muungano zinapoibuka, zinawaunganisha Wazanzibari nyuma ya himaya yao bila kujali tofauti zao kiitikadi.

 

Ndio maana haikushangaza kuwa katika hoja ya Mbowe iliyogusa Muungano katika mjalada wa Bandari, aliyetoa jibu kwa mara ya kwanza kutoka Zanzibar ni Jussa, ambaye ni kiongozi wa ACT Wazalendo (ingawa chama hicho kimo katika serikali ya Umoja wa Kitaifa). Hili hutokea mara nyingi hoja za Muungano zinapoibuka kama ilivyotokea wakati ilipoibuka hoja ya Zanzibar ni nchi au la na wakati wa mijadala kwenye Bunge la Katiba, kwa kutaja mifano michache.

 

Wakati Bunge la Katiba likijadili muundo wa Muungano, katikati ya hoja ya kuundwa kwa serikali tatu, Wazanzibari waliungana nyuma ya hoja hiyo lakini wakakoleza mjadala kwa kudai mamlaka kamili ya Zanzibar ndani ya Muungano.

 

Mara nyingi hoja za kuushambulia Muungano zinapoibuka, watu wengi huwaona wale wanaoibua hoja hizo kama maadui wa Muungano. Hakuna anayeangalia kwa undani wale wanaojibu. Lakini kama hilo lingefanyika basi watu wangegundua kuwa umoja wa Wazanzibari katika kutetea visiwa vyao ndani ya Muungano wanapojibu hoja ni moja kati ya mambo hatari kwa Muungano. Ni hatari kwa sababu kwa mujibu wa msemo wa Kiswahili, umoja ni nguvu. Kwa maana hiyo Wazanzibari wanaendelea kujijenga nguvu kubwa nyuma ya harakati zao za kuitetea himaya yao ndani ya Muungano.

 

Mara nyingi, kama ambavyo mmoja wa wanasiasa nguli visiwani humo, Asha Bakari, alivyowahi kusema, kila Wazanzibari wanapoibuka kusema yale wanayoyaona kuwa ni mabaya ndani ya Muungano na kuhitimisha kwa hoja ya kutaka mabadiliko, wanapigwa na rungu la chama chao wakiambiwa kuwa wanalolidai ni kinyume cha sera ya chama chao.

 

Umoja huu wanaoendelea kuujenga Wazanzibari kama utafika mahali utaizidi nguvu sera za vyama vyao na hapo ndipo tutakaposhuhudia jambo ambalo wengi wetu hatupendi kuona likitokea. Umoja huu wa Wazanzibari ni tishio kwa Muungano kwa sababu kuna wakati unajidhihirisha pia kupitia mambo yanayofanyika kupitia SMZ. Kubwa kati ya mambo yaliyofanyika chini ya uratibu wa SMZ ni mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2010.

 

Zipo hisia ambazo hazijapatiwa majibu ya kuridhisha kuwa mabadiliko hayo yalikuwa ni majibu kwa hoja ya Zanzibar si nchi na pia yalifanyika ili kuipa Zanzibar nguvu zaidi kama nchi. Mabadiliko haya yalifanyika baada ya mjadala mkali wa ‘Zanzibar ni nchi au si nchi’ ambao uliibuka bungeni na kutolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda, akihitimisha kuwa Zanzibar si nchi bali ni semhemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Miaka miwili baada ya Pinda kusema hivyo, SMZ ikapeleka muswada wa mabadiliko ya Katiba katika Baraza la Wawakilishi. Mambo mengi yaliingizwa katika Katiba ya Zanzibar likiwamo kuitambua Zanzibar kama nchi yenye mipaka yake na kuwa ndiyo nchi ambayo iliungana na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Pamoja na mambo mengine mengi mabadiliko haya pia yakampa Rais wa Zanzibar mamlaka ya kugawa maeneo ya Zanzibar bila kuhitaji mashauriano na mtu au kiongozi mwingine yeyote.

 

Ipo hofu kuwa upande mmoja wa Muungano unapojiongezea nguvu, basi nguvu za Muungano zinamomonyoka. Watu wanaogopa kulisema hili tangu Zanziabar ifanye marekebisho hayo.

 

Jambo hili linaonyesha upeo wa umoja wa Wazanzibari linapokuja suala la kutetea himaya yao. Kama ulikuwa bado unadhani kuwa hakuna uwezekano wa umoja huu kuizidi nguvu sera ya chama, basi hiki ni kiashiria kingine kinachoonyesha uwezekano wa jambo hilo kutokea.

 

Wakati Wazanzibari wakiwa wamoja hivyo katika kutetea himaya na hadhi yao ndani ya Muungano, kwa upande mwingine Tanganyika imekuwa ikipata msemaji mmoja mmoja, kwa nyakati tofauti na hivyo kutokuwa na sauti moja yenye nguvu katika suala hilo.

 

Mmoja wa watu walioacha alama katika suala hilo ni marehemu Mchungaji Christopher Mtikila ambaye katika kikao cha Bunge la Katiba aliwahi kusema kuwa huo ulikuwa wakati wa kurekebisha makosa yaliyofanywa kwa kuiua Tanganyika. Mchungaji Mtikila aliwataka wabunge wenzake kutofungwa na “misimamo ya marehemu” (akimaanisha Mwalimu Julius Nyerere na Aman Abeid Karume – walioasisi Muungano), na kukumbatia mawazo mapya ambayo yataipa nchi nuru.

 

Katika Bunge la Muungano tunamkumbuka aliyekuwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kesi, ambaye hakuficha kuchukizwa kwake kwa Zanzibar kupewa uwakilishi mkubwa katika masuala ya Muungano. Yeye aliliona hilo kama upendeleo usiojali haki wala usawa akisema ukubwa wa nchi hiyo na mchango wake ndani ya Muungano haustahili haki zote inazopewa ndani ya Muungano.

 

Lakini kuna wakati fulani, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, naye ‘alichafua hali ya hewa’ kuhusu Muungano kupitia hotuba yake aliyoitoa kanisani huko Dodoma. CCM nayo, kwa namna fulani imeshiriki katika kulirarua vazi hili la Mwalimu Nyerere kupitia taratibu zake. Awali chama hicho kilituzoesha utaratibu wa kugawana vipindi vya urais kati ya Bara na Visiwani. Ndio maana haikushangaza alipong’atuka Mwalimu Nyerere, mtu kutoka visiwani, Ali Hassan Mwinyi, akachukua kijiti na kuendeleza uongozi.

 

Baada ya Mwinyi alifuatia Benjamin Mkapa na lipo kundi kubwa la watu, hasa Wazanzibari ambao waliamini kuwa baada ya Mkapa itafuata ‘zamu’ yao ya kutoa Rais. Lakini hilo halikuwa maana Mkapa alifuatiwa na Jakaya Kikwete kutoka Bara. Wazanzibari wakajipa moyo kwamba pamoja na kuwa utaratibu huo ndani ya CCM ulikuwa si jambo lililowekwa kama kanuni kwenye maandishi lakini litaheshimiwa katika uchaguzi unaofuata kwani linaweka usawa kati ya pande mbili za Muungano.

 

Wakapigwa mshangao pale Kikwete aliporithiwa na Dk. John Magufuli. Hadi kufikia hapo, Wazanzibari wakaanza kukata tamaa kuhusu suala la kuwekeana zamu ya kutoa mgombea urais kupitia CCM. Lakini baada ya kifo cha Magufuli, nchi ikajikuta inapata Rais Mzanzibari baada ya muda mrefu. Rais Samia akaingia madarakani kwa matakwa ya Katiba kwa sababu ndiye alikuwa Makamu wa Rais.

 

Hilo lingeweza kuleta ahueni kwa Wazanzibari kuwa angalau sasa, kwa kudra za Mungu, wamepata Rais katika serikali ya Muungano. Lakini wanaona ‘Rais wao’ bado anasakamwa kama vile ambavyo amesakamwa na Mbowe kwenye hoja yake kuhusu bandari. Hapa wakajikuta wanaendeleza ule umoja wao katika kutetea maslahi, himaya na haki zao kwenye Muungano. Kuingia madarakani kwa Rais Samia kukaifanya Tanzania kuwa na marais wawili kutoka Zanzibar kwa wakati mmoja baada ya kipindi kirefu tangu enzi za Rais Mwinyi.

 

Ukichanganya na mabadiliko aliyoyafanya na anayoendelea kuyafanya Rais Samia ambapo ameonekana kuwakumbuka Wazanzibari (na wanawake) kila anapofanya uteuzi, wahafidhina wanaanza kuhisi hatari kwenye mwelekeo wa uongozi wa nchi na Muungano. Si ajabu kuwa ziliibuka harakati nyingi za chinichini za kutaka Rais Samia asigombee muhula wa pili wa Urais pale awamu yake ya kwanza itakapokamilika mwaka 2025, lakini yeye mwenyewe akakata mzizi wa fitina kwa kueleza kinagaubaga kuwa atagombea nafasi hiyo mwaka 2025.

 

Mlolongo huu wa matukio dhidi ya Muungano unaonyesha kuwa lile vazi nadhifu la Muungano alilojishonea Mwalimu Nyerere katika uongozi wake, limekuwa likiraruruiwa taratibu kwa muda mrefu.

 

Ni kwa kiasi gani vazi hilo limeraruriwa ni suala linalohitaji utafiti ambao rejea yake itajikita katika yale aliyoyasema Mwalimu Nyerere katika hotuba yake maarufu aliyoitoa pale Hoteli ya Kilimanjaro ijulikanayo kama nyufa za Muungano, kwa kuangalia ni kwa kiasi gani kile alichoonya Mwalimu kupitia hotuba hiyo kimetimia.

 

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari mwandamizi aliyewahi kufanya kazi katika vyombo tofauti vya habari ndani na nje ya Tanzania. Kwa maoni anapatikana kupitia pnyanje@gmail.com

 

Bandari inavyorarua vazi la Nyerere

Jecha

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *