Sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam. Picha ya gazeti la serikali la Daily News.
Na Ezekiel Kamwaga
KAMA kuna kitu ambacho mjadala kuhusu uwekezaji unaopangwa kufanywa kwenye bandari za Tanzania na kampuni ya DP World kutoka Dubai umefanikiwa kufanya ni kufichua kuhusu uwezo, hulka na silka za Watanzania – hasa wale wenye ushawishi au mamlaka katika jamii yetu.
Kimsingi, makundi makubwa manne yalijionyesha bayana kupitia mijadala na mazungumzo yaliyodumu kwa takribani mwezi mmoja; kundi la wale walioamua kuunga mkono tu bila kuhoji chochote, waliopinga tu – wakati mwingine wakipotosha makusudi au kuendeleza hoja ambazo zina majibu, waliochambua mjadala kwa kutoa majawabu na viongozi wa taasisi za serikali walioingia vitani kutoa maelezo ya kitaalamu – huku wengine wakionekana waliopaswa kusema wakishangazwa kwa ukimya wao.
Tangu suala hili lifikishwe rasmi bungeni kwa ajili ya Azimio la Kuridhia Mkataba wa Ushirikiano (IGA) baina ya Tanzania na Dubai mwezi uliopita, hoja kubwa nne zilionekana kuzua mjadala; suala la kutokuwepo kwa ukomo wa mkataba, suala la mkataba huo kutojali Uhuru wa Tanzania kujiamulia mambo yake, kuuzwa kwa bandari zetu kwa watu wa Dubai na endapo Dubai ilikuwa na uwezo wa kuingia kwenye mkataba ingawa yenyewe ni sehemu ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Makundi yaliyoibuka kwenye mijadala ya jambo hili yalijaribu kufanya mambo tofauti ikiwamo; kuchochea hasira za wananchi kuhusu jambo hilo, kukataa kujadili hoja na badala yake kushambulia watu, kutoa majibu ya hoja zilizokuwa zikipinga uwekezaji huo na wengine wakajikita kwenye kutoa mbadala wa nini kinaweza kufanyika katika mazingira haya.
Kundi la waliounga mkono hoja tu au kushambulia watu badala ya hoja
Katika kundi hili, hakuna mfano mzuri ninaoweza kuutumia kuzidi ule wa Sheikh Said Mwaipopo, ambaye alifanya mkutano na waandishi wa habari kuunga mkono mkataba huo lakini akatumia fursa kumshambulia hadharani Profesa Issa Shivji, ambaye alikuwa ametoka kukosoa baadhi ya vifungu alivyoona vina shida kwenye mkataba huo.
Ingawa Shivji ni mmoja wa wasomi wanaoheshimika nchini na mwanasheria nguli, Mwaipopo alimshambulia kwamba “anazeeka vibaya” na kutoa kauli nyingine ambazo zilikuwa na sura ya kibaguzi. Badala ya kujibu hoja za Shivji, Mwaipopo aliamua kumshambulia binafsi na kutoa maneno yasiyofaa.
Kundi hili la watu wanaosifu na kupongeza tu ni matokeo ya siasa za Tanzania katika kipindi cha miaka 10 hadi 15 iliyopita ambapo masuala mengi ambayo hayakutakiwi kuwa ya kichama au binafsi, hujadiliwa au kuzungumzwa kwa namna ya “ama zao ama zetu”.
Kuna utamaduni umeanza kujengeka kwenye jamii yetu kuwa jukumu la watu walio kwenye upinzani ni kukosoa pekee na walio kwenye chama tawala ni kusifia. Wakati mwingine – hasa kutokana na aina ya utawala uliokuwepo Tanzania wakati wa utawala wa hayati John Magufuli, watu wengine wameamua kuwa waunga hoja wakihofu kukutwa na madhila yaliyowakuta waliokuwa wakosoaji wa Magufuli; au kupata faida walizokuwa wakipata wale waliokuwa wakisifu serikali iliyo madarakani.
Waliojipambanua kwa uwezo
Mjadala huu wa bandari umeibua watu na majina ambayo kabla hayakuwa maarufu sana masikioni mwa Watanzania. Mmoja wa wazungumza wa serikali aliyejipatia umaarufu wa ghafla kutokana na uwezo wake wa kupangua hoja ni Mohamed Salum ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria katika Wizara ya Uchukuzi.
Mahojiano tofauti ambayo aliyafanya na vyombo vya habari yalikuwa yakizunguka katika makundi sogozi mbalimbali ya mtandao wa WhatsApp na mitandao mingine ya kijamii. Ni yeye ndiye aliyetoa maelezo ya ufasaha kuhusu kufanana kwa IGA hii na ile iliyotumika kwenye mradi wa bomba la mafuta baina ya Tanzania na Uganda, kueleza kutouzwa kwa bandari zetu wala kusainiwa kwa mikataba yenye kueleza hivyo na mambo mengine.
Mwingine aliyejipambanua kupitia sakata hili ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Plasduce Mbossa. Yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa kwanza miongoni mwa watendaji wa Wizara ya Uchukuzi aliyekwenda kufanya ziara kwenye vyombo vya habari kufafanua kuhusu suala la uwekezaji wa bandari.
Katika hatua za awali za mijadala ya suala hili, serikali nzima ni kama ilikuwa imepigwa ganzi huku sehemu tofauti za vifungu vya mkataba baina ya DP World na TPA vikiwa vinasambazwa mitandaoni. Wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eliezer Feleshi, akiwa kimya bila kutoa ufafanuzi wowote, ni Mbossa ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungukia vyombo vya habari na kueleza.
Na katika muda wote wa mjadala, TPA haikutoa taarifa yoyote au hali ya kuonyesha kughadhabika au kukerwa na mambo au mjadala ulivyokuwa ukiendelea. Badala yake, Mbossa alikuwa akiitikia wito wa kuhojiwa kila alipoitwa kwenye vyombo vya habari katika wiki ambayo kwa maoni yangu nadhani ilikuwa ngumu zaidi tangu kuanza kwa sakata hili.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Ally Possi na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari, nao wanaangukia katika kundi hili. Katika wiki ya pili baada ya Bunge kuwa limepitisha Azimio la kuridhia IGA na wakati maji yakiwa bado ya moto, wao walitumia elimu yao ya sheria kufafanua na kueleza kwa kina kuhusu mkataba huo.
Suala hili la bandari pia limeweka bayana uwezo wa kueleza mambo wa Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo. Hotuba yake bungeni siku ya mjadala wa IGA bungeni ndiyo iliyosambaa zaidi kwenye mitandao ya kijamii miongoni mwa wabunge waliozungumza lakini ufafanuzi wake wa kisiasa kuhusu mkataba huo pia ulitoa afueni kubwa kwa serikali kwenye suala hili.
Katika mazungumzo yasiyo rasmi niliyofanya na mmoja wa viongozi wastaafu wa serikali, alinieleza kwamba kama kuna jambo zuri ambalo mijadala ya DP World imefanya kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ni kumwonyesha ni aina gani ya viongozi na watendaji wa chama na serikali anao kwenye serikali yake – kuanzia uwezo wao wa kujenga hoja na kuingia vitani kutetea serikali hata katika mazingira magumu ya kupingwa.
Kigogo huyo ambaye hakutaka nimtaje jina lake kwenye makala haya, alisema suala la nani anazungumza na kutetea serikali ni jambo lililowahi kujadiliwa sana hasa enzi akiwa waziri kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete.
“Nakumbuka siku moja Rais Jakaya Kikwete aliwahi kuwauliza viongozi wa UVCCM, ‘wako wapi akina John Mnyika, Zitto Kabwe wetu?’ Kikwete alikuwa akiwaambia vijana kuwa ni muhimu kujenga kada ya viongozi wenye uwezo wa kujieleza kwa kujenga hoja na si kupiga hoja nyundo”, alisema.
Kwa kigogo huyo mstaafu, jambo ambalo suala hili limeonyesha pia ni upungufu wa vijana na viongozi ndani ya serikali na Umoja wa Vijana wa CCM wenye uwezo wa kutoa hoja na kushindana na hoja za vyama vingine kwenye mijadala mikali kama huu wa Bandari. Kama hatimaye suala hili litapita, wa kupongezwa watakuwa ni watendaji wa aina ya Mbossa walioingia vitani kutetea.
Waliotoa hoja za kujenga
Hili ni kundi linalojumuisha wanasiasa na wasomi ambao walilitazama suala la uwekezaji huo kwa jicho la kuangalia ni wapi panaweza kuboreshwa zaidi ili hatimaye Tanzania ifaidike na rasilimali ya bandari ambayo ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya mapato kwa nchi.
Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kiliunda kikosi kazi kilichoongozwa na Wakili Aisha Sinda, ambacho kazi yake ilikuwa kusoma na kufanya uchambuzi wa yaliyomo katika IGA. Uchambuzi wa TLS ndiyo ulioeleza kuwa suala la ukomo limeelezwa kwenye mkataba huo lakini pia ikapendekeza mambo ya kufanywa ili mkataba huo uwe wa manufaa.
Kwa mfano, ni uchambuzi huo wa akina Wakili Aisha ndiyo ulioweka bayana kuwa serikali inatakiwa iangalie eneo la namna ya kuvunja mkataba huo endapo pande hizo mbili zitashindwana kwenye utekelezaji wa mradi na kupendekeza suala la kama Dubai ni nchi inayoweza kuingia mkataba peke yake – nje ya UAE lifanyiwe utafiti zaidi.
Mtu mwingine aliyechangia mjadala huo kwa hoja za kujenga ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe. Yeye ndiye aliyeipa serikali pendekezo la kuanzishwa kwa kampuni ya ubia baina ya DP World na TPA na Mifuko ya Hifadhi za Jamii ambayo itajenga uwezo wa Watanzania kusimamia bandari na kuweka mgawanyo wa faida unaofanana baina ya wabia hao.
Profesa Kitila naye anaangukia katika kundi hili pia. Kwenye mjadala wa bungeni ambako wabunge wengi wa CCM waliamua kuzungumza kwa mrengo wa kichama na kuwaponda waliokuwa wakipinga suala hilo, ni Kitila aliyezungumza na kusema ni muhimu kwa serikali na wabunge kusikiliza hoja na hisia za wananchi katika suala hilo.
Wakati akitoa hotuba ya kufunga Mkutano wa Bunge la Bajeti wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema kwamba serikali imesikiliza hoja na hisia za wananchi waliotoa maoni yao kwenye suala hili na kwamba yote yaliyopendekezwa yatafanyiwa kazi.
Kwenye siku ile, ilikuwa rahisi zaidi kwa Kitila kuzungumza kwa kuponda vyama vya upinzani na wakosoaji wengine wa mkataba huo kwa namna ileile ambayo wachangiaji wengine kama Mbunge wa Tarime, Mwita Waitara, walifanya lakini yeye aliamua kutoa hoja kwa namna ya kujenga zaidi kuliko kubomoa.
Profesa Shivji naye alizungumza kwa kutoa mapendekezo kwamba kwa kuwa IGA imeshasainiwa tayari, serikali inaweza kuzungumza na wenzao wa Dubai ili wautengeneze upya kutokana na maoni ya wananchi yaliyotolewa na kisha kupelekwa upya bungeni. Zitto, ambaye ni Mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, alisema serikali pia inaweza kuweka nyongeza ‘addendum’ kwenye IGA hiyo na kushawishi Dubai kukubali.
Kundi la wapingaji
Mtu ambaye anaweza kuwa kiongozi wa kundi la wanaopinga – kwa kutazama kauli yake dhidi ya mradi huo, ni Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Balozi mstaafu, Dk. Wilbrod Slaa. Katika mahojiano aliyofanya na kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Star Tv, Slaa alisema wananchi wanaweza kuamua “kupindua serikali” kama hawaridhiki na mkataba huo.
Mbunge huyo wa zamani wa Karatu ambaye katika siku za karibuni amekuwa akitoa kauli zinazoonyesha kutokubaliana na mwenendo wa serikali ya Rais Samia, katika mahojiani hayohayo alifananisha baadhi ya masuala yaliyopo katika mkataba huo na karatasi za chooni (toilet papers) na kwamba mkataba huo ni mbaya kwa nchi.
Kundi la wapingaji pia lilikuwa na waunga mkono wake wengi kwenye mitandao ya kijamii ambako watu wanaojulikana na wengine wanaotumia majina ya bandia au walikuwa wakiposti masuala ambayo wakati mwingine tayari yalikuwa yametolewa majibu na wawakilishi wa serikali.
Ni katika mitandao hiyo ya kijamii ndipo ambapo wanaopinga uwekezaji huo bila hoja za msingi waliamua kutengeneza vipeperushi na ujumbe wa mitandaoni ulioonyesha kuwa watu waliokuwa wakiunga mkono uwekezaji huo wengi wao walikuwa wasioelimika, wanaodaiwa kuwa ni mashoga na waandishi wa habari uchwara, huku majina ya watu wanaoheshimika wakitajwa kuwa wapinzani wa mkataba huo.
Badala ya kundi hili kuzidi kujenga hoja kwa kuvutia wanaowapinga na wale waliokuwa wakiunga mkono upande wao, wao waliamua kutumia kashfa na lugha nyingine za kuudhi ili kuzuia waliounga mkono nao wasipaze sauti kwa kuhofia majina haya mabaya yaliyowekwa dhidi yao.
Aina hii ya kutengeneza mijadala ya kupeana majina mabaya ni sehemu ya utaratibu wa aina mpya ya siasa zinazotawala dunia hivi sasa. Maandishi kadhaa ya kisomi yanaonyesha kwamba mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na wanasiasa au viongozi wenye mrengo wa kiimla na wasio na hoja ni kutumia lugha chafu na za vitisho dhidi ya wapinzani wao na kujenga dhana ya “vita ya wao dhidi yetu” miongoni mwa wafuasi wao na watu wengine katika taifa lao.
Kwa viongozi na wanasiasa wa aina hiyo, ni lazima atafutwe adui – wa kweli au kufikirika, ili siasa zao ziweze kupata wafuasi. Kama ambavyo Donald Trump alitumia sehemu kubwa ya kampeni yake kuwagawa Wamarekani weupe dhidi ya wageni wahamiaji – kama ambavyo tawala nyingine za Ulaya sasa zinafuata nyayo zake dhidi ya wahamiaji wa kigeni nchini mwao.
Hitimisho
Makundi niliyoyataja hapa na majina niliyoyataja si kwamba ndiyo pekee ambao wangeweza kutajwa kwenye makala haya. Hata hivyo, niliamua kutaja majina machache kwa lengo la kutoa uwakilishi wa aina ya watu niliotaka kuwajadili.
Kuna watu wengine walitoa hoja za kujenga lakini kwa ujumla walizungumza maneno mengine ya kupotosha na hivyo nimeshindwa kuwaweka katika mojawapo ya makundi husika niliyoyataja kwa sababu wana ndimi mbili katika jambo moja.
Kuna kundi lingine la watu au viongozi ambao walitakiwa kusema chochote kwenye sakata hili kutokana nav yeo na majukumu waliyonayo ndani ya CCM na serikali lakini kwa sababu ambazo haziko wazi hadi sasa, waliamua kukaa kimya – wengine wakija kuzungumza wakati mambo yameanza kupoa.
Hili ni kundi ambalo ni vigumu kujua kama walikuwa wanaunga mkono hoja, wanalipinga suala lenyewe bila kuzungumza au hawakujua waseme nini au kuzungumzia yapi na kuacha yapi. Hili ni kundi ambalo muda unaweza kutupa majibu kuhusu ukimya wao.