Picha: Leila Sheikh Khatib
Na Mohamed Said
WASOMAJI wangu, niruhusuni niweke meseji niliyomtumia Leila Sheikh tarehe 12 December 2022.
(Mtaniwia radhi nimeifanyia uhariri kidogo ili ipate kueleweka kwa wasomaji).
Wakati huo CCM na serikali yake walikuwa katika pilikapilika ya kuandaa tamasha la kumuadhimisha Bi. Titi Mohamed. Maofisa wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo wakanitembelea nyumbani kwangu kwa kunialika Ikwiriri, Rufiji ambako ndipo kutakapokuwa na shughuli yenyewe na pia kurekodi kipindi cha radio na televisheni.
Meseji yenyewe ilisomeka hivi;
“Bi. Leila,
Asalaam Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh. Leo nilitembelewa na wataalamu kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.Tuliweka barza tukamzungumza Bi. Titi lakini mimi nilizungumza kwa majonzi nikawaambia mtu aliyekaa kwa muda mrefu na Bi. Titi hadi anafariki ni wewe Leila Sheikh.
“Nikawaomba pamoja na mazungumzo yetu haya wafanye hima sana wakufate Tanga wasome historia ya Bi. Titi ambayo wewe umeipokea kutoka kinywa chake mwenyewe kipenzi chetu Bi. Titi Mohamed.”
Leila Sheikh kwangu mimi alikuwa dada na pia shemeji yangu kwani aliolewa na rafiki yangu Shariff Ahmed Sagaf kwa hiyo nikimmudu na yeye akinimudu na hapakuwa na pazia kati yetu. Katika huu uhusiano wetu ndiyo siku moja katika yeye kujua shauku yangu katika kuhifadhi historia ya uhuru wa Tanganyika akanieleza kuwa amekusanya ”material” ya kutosha kwa maandishi na sauti ya kuandika kitabu cha Bi. Titi Mohamed, kitabu ambacho kitashangaza wanahistoria.
Leila akanidokeza akaniambia watu watajua ile ”intellect” aliyokuwanayo Bi. Titi msichana wa darasa la nne tu vipi aliweza kusimama bega kwa bega katika jukwaa moja na Julius Nyerere msomi wa Makerere na Chuo Kikuu Cha Edinburgh na wakawa ndiyo sauti ya Watanganyika hadi uhuru ukapatikana.
Katika kipindi hiki ambacho mimi nikawa sasa namwandama Leila kuanza kazi ya kuandika kitabu hicho ikawa kila nikifanya mahojiano kuhusu historia ya Mwalimu Nyerere nitamtaja Bi. Titi na Leila nikisisitiza kuwa Bi. Titi kitabu chake ndiye kitamweleza Nyerere kwa ukamilifu unaostahili. Hili likaja kufahamika katika duru za uandishi mitandaoni na ”wajanja” wakajua kuwa Leila ana mgodi wa dhahabu unaongoja kuchimbwa. Ikawa sasa ni kama vile nimemponza Leila. Kila mtafiti na mwandishi anataka kujua Leila amefutika nini? Wasomaji wangu nakuwekeeni hapo chini msg moja aliyoniletea. Leila alikuwa amekasirika:
“Huyo kijana hana busara. Nimefanya tafiti miaka saba. Nilimhoji Bi. Titi Mohamed kwa miaka mitatu.Huyo kijana uliyemtuma kwangu anataka yeye, eti awe Director kwenye production yangu. Aingie tu, awe Mkurugenzi. Not only is he a leech, he doesn’t know the first thing about production. Nimefatwa na watu na mashirika yasiyopungua 34, kutaka kushirikiana na mimi. Siyo Ukurugenzi ushirikiano tu. Yeye anataka kuwa Mkurugenzi. Kazi yote nifanye mimi, yeye aingie tu, anyakue top position in a film production. Hana adabu. Aishie huko. Nahisi ni dalali. Katumwa na watu kupata original notes na script yangu on Bi. Titi Mohamed.”
Nilichoshukuru ni kuwa Leila hakunikasirikia mimi labda alitambua nia yangu ilikuwa njema. Nilikuwa nikimsikiliza Leila akimweleza Bi. Titi ni kama vile naangalia senema ya kuvutia. Mimi nilikuwa tayari nina mswada wa kitabu cha Bi. Titi lakini kwa yale niliyosikia kwa Leila nikaona mimi siwezi kufua dafu nikachukua mswada wangu nikampa Leila nikamwambia kuwa mimi mswada wangu sitauchapa kwani nitakuwa sijamtendea haki Bi. Titi.
”Sikiliza Mwanleila (Hivi ndivyo Bi. Titi alivyokuwa akipenda kumwita Leila).
Bi. Titi alipata kumwambia Leila kuwa katika miaka ya 1950 wakati anazunguka Tanganyika nzima kupigania uhuru, alipata kufikia nyumbani kwa wazee wake Leila (Korogwe). Bi. Titi anamuuliza Leila; “Unaniambia unataka kutengeneza senema ya maisha yangu. Sasa sikiliza bibi wewe nikueleze…siku nilipoimba na Anisaa Siti Biti Saad.
Siti Biti Saada tulialikwa nyumbani kwa Said Sudi Zanzibar hapo bado TANU haijaanza sijaingia katika siasa. Siti Biti Saad alialikwa kuja kutumbuiza wageni wa Said Sudi huyu alikuwa Prince, mmoja katika watoto wa Sultani. Basi Siti akaimba nyimbo moja kufika kati akaniachia nimalize wakati huo mimi nikiimba Egyptian…”
Haikuwa shida kwangu kutambua kuwa Leila amakikomba kichwa chote cha Bi. Titi Mohamed. Mimi namaliza mazungumzo kwa kumsihi Leila afanye hima aandike hicho kitabu na yeye siku zote hunijibu, ”In Shaa Allah.”
”Mwanleila unataka kujua uhusiano wangu na Nyerere…” Leila kanieleza swali hili ilielekea lilikuwa zito kwake Bi. Titi lakini kwa ujuzi na stahamala aliyokuwanayo Bi. Titi aliligeuza swali lile kuwa maskhara baina yao. Hapa hakika :”vichwa” viwili vilikuwa vimekutana.
Mwanleila umekuja kwa kadha au kadha wa kadha?”
Hapa ikawa wote wanacheka.
Leila alipokea mengi kutoka kwa Bi. Titi na tushukuru kuwa yamehifadhiwa.
Leila Sheikh kaondoka bila ya kuandika historia ya Bi. Titi. Mohamed.
Allah amrehemu na amtie mahali pema peponi.
Amin.
Mwandishi wa makala haya ni mwandishi na mwanahistoria. Anapatikana kwa simu namba 0687500699.