Fungulia John Heche Suguta

Picha: John Heche (kwa hisani ya mtandao wa Millard Ayo)

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

MWAKA 2016 utabaki kuwa na historia ya kipekee kwenye miaka ya karibuni na pengine mingi inayokuja. Huu ndiyo mwaka ambapo neno moja lilitajwa kuwa neno lililotumika zaidi katika lugha za Kijerumani na Kihispania mtawalia; Postfaktisch na Posverdad. Kwenye Kiingereza, linajulikana kama Post-Truth. Neno hili lina maana ya nyakati ambazo ukweli unawekwa kapuni na badala yake siasa zinatawaliwa na mambo yaliyo rahisi kugusa hisia za watu. Si ajabu kwamba matumizi ya neno hili yalikuja sambamba na ujio wa Donald Trump kama Rais wa Marekani.

 

Chukulia mfano wa Trump mwenyewe. Kila mmoja anamjua kama mwanasiasa laghai, mkwepa kodi, asiye mwaminifu na mwenye matatizo binafsi. Lakini ni yeye anayeongoza kwa kuwaita wenzake waongo, laghai na habari zote za ukweli akiziita za uongo. Na anapendwa na wafuasi wake kwa kusema hayo. Na kwa bahati mbaya, ujio wa Trump haukuwa wa kwake peke yake. Dunia nzima, huu umekuwa wakati ambao viongozi wanaotaka ukweli wao pekee ndiyo uwe ukweli na si vinginevyo wameibuka. Kuanzia kwa Trump mwenyewe, Narendra Modi, John Magufuli, Viktor Orban na wengine wa aina hiyo.

 

Hawa ni viongozi walioibuka wakati dunia ikipita katika kipindi kigumu kiuchumi. Mtikisiko wa uchumi wa dunia mwaka 2008 uliondoa dhana kwamba mfumo wa soko na demokrasia ya kiliberali ni dawa ya kutibu matatizo ya kiuchumi. Na katika maeneo mengi duniani, mfumo wa demokrasia umeonekana kutokidhi mahitaji ya watu kuanzia kiuchumi hadi kiusalama. Dunia ikawa tayari kusikiliza viongozi wenye mawazo mbadala ya namna ya kukabili changamoto za sasa za dunia yetu. Ndiyo wakaja akina Magufuli. Na kwa sababu changamoto zile zingalipo, na Google na Facebook zinatumika vizuri na wataalamu kujua watu wanataka kusikia nini katika wakati husika, tutaendelea kuwa na viongozi wa aina hii.

 

Leo si siku ya kueleza maoni yangu kuhusu kuteuliwa kwa Paul Makonda kuwa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hilo litakuja siku yake. Lakini ni wazi baada  ya uteuzi wa Makonda, ni kama CCM imepigwa shoti– sijui kwa muda gani, katika ulingo wa siasa. Naweza kusema kwa hakika kwamba tangu enzi za Abdulrahman Kinana na Nape Nnauye, sijaona tena mikutano ya CCM ikiwa inafuatiliwa au kutajwa mara nyingi kwenye vyombo vya habari kama ilivyo sasa tangu kurejea kwa Makonda.

 

Tofauti na sayansi halisi, siasa ni mchezo ambao hisia na mwonekano vina ushawishi mkubwa kuliko uhalisia. Kama mikutano ya CCM itaendelea kuandikwa na kuvutia kwenye vyombo vya habari, ndiyo taswira na ushawishi wa chama hicho itakavyobadilika kwenye mioyo ya Watanzania.

 

Makonda ana vitu kadhaa vinavyombeba binafsi kwenye ziara zake hizi. Mosi ni ukweli kwamba tayari ana uhusiano binafsi na vyombo vya habari ambao kazi yake kubwa ni kuuzimua tu na pili yeye ni mtu anayejulikana. Kwenye taaluma ya uandishi, suala la kujulikana kwa mhusika ni mojawapo ya vitu vinavyoamua kama habari inafaa kwa matumizi au haifai.

 

Kama chama kikuu cha upinzani nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinatakiwa sasa kujiweka katika mazingira ambayo kinaweza kutumia fursa hii ya kurejea kwa siasa za majukwaani kutanua misuli yake. Na kazi yake ya kwanza ni kuwa na mtu anayeweza kujibu changamoto hii ya CCM. Katika siasa, hakuna kitu kibaya kama chama kubaki na msimamo au namna yake ya kufanya kazi wakati mazingira yamebadilika. Bingwa wa Dunia za zamani wa mchezo wa chesi, Gary Kasparov, alikuwa na msemo wake mashuhuri; “Don’t change your strategy unless the fundamentals have changed”.

 

Kitendo cha CCM kumfanya Makonda kuwa Katibu Mwenezi wake kinamaanisha kwamba tayari mchezo umebadilika. Na kwa sababu hiyo, mkakati wa chama cha upinzani kinachotaka kushika dola hauwezi kubaki kama ulivyokuwa zamani. Kuna namna mbili ambazo Chadema inaweza kukabili mabadiliko yaliyotokea karibuni; Mosi ni kwa kuepuka mpambano wa moja kwa moja – kwa kuwekeza zaidi katika namna inavyowasiliana na Watanzania kwa ujumla, au kupambana ngumi kwa ngumi. Kwa sababu tuko katika postfaktisch, napendelea zaidi mpambano wa ngumi kwa ngumi.

 

Na hapa ndipo sasa ninapokuja kwa msingi wa mada yangu ya leo kuhusu Chadema. Ninafahamiana vema na John Mrema ambaye ndiye Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema. Ni mtu mzuri, makini na anayejua siasa na kukifahamu chama chake ndani na nje. Lakini kuna vitu viwili ambavyo  ambavyo hana. Hajawahi kuwa kiongozi wa hadhi ya mbunge au Mkuu wa Mkoa ya kumpa umaarufu wa kufanya yeye mwenyewe ajitanabaishe nje ya chama chake. Na ingawa ana marafiki wa kutosha ndani ya vyombo vya habari – mimi binafsi nilifahamiana naye zaidi ya miaka 10 iliyopita, hajapata bahati ya kuwa na mvuto wa kuvuta watu majukwaani yeye binafsi.

 

Kupambana na changamoto hii ya Makonda, Chadema inahitaji Mkurugenzi wa Mawasiliano – na nadhani kuna haja ya kubadili jina na hadhi ya cheo hiki ili ikidhi mahitaji ya sasa, ambaye anaweza kwenda na mabadiliko haya ya fundamentals kama vile samaki na maji. Namuona John Heche Suguta kama mtu anayeweza kukabiliana na changamoto hii uso kwa uso. Heche ana sifa kadhaa zinazofanya nimwone anafaa kwa jukumu hili; ni mwanasiasa anayejulikana ambaye vyombo vya habari vinalazimika kumsikiliza anapozungumza, amewahi kuwa bungeni na hivyo anajua vitu vingi vya kiutawala na yeye binafsi anaweza kuitisha mikutano ya hadhara na akavuta watu – kama chama kitampa nguvu inavyotakiwa.

 

Kwenye nyakati hizi za posverdad, ni muhimu kuwa na wanasiasa ambao wanaweza kupokea ngumi ya pua na kutoka damu kidogo. Jambo la msingi ni kuwa nao wanaweza kusababisha majeraha ya namna hiyo kwa wapinzani wao. Ningeweza pia kupendekeza jina la Tundu Lissu kama mtu anayefaa kwa nafasi hiyo lakini tayari ana cheo kikubwa na Heche angalau ni wa kizazi cha kisiasa kinachofanana na cha mwenezi mpya wa CCM.

 

Na Heche ana jambo lingine ambalo ingawa haliendani na nyakati hizi za posverdad, lakini ndiyo dawa pekee ya kupambana na political charlatans, na jambo hilo ni ukweli kuwa mbunge huyu wa zamani wa Tarime huzungumza kwa kutumia takwimu na taarifa rasmi. Yeye si mtu wa fake news. Kuna nyakati kutatokea mikutano ambayo vyama vitatakiwa kuwakilishwa walau na makatibu wenezi na ni muhimu chama kikuu cha upinzani kikawa na mtu ambaye anaonekana ana uzito na hadhi sawa – pengine kuzidi, ya yule wa chama tawala.

 

Sisemi kwamba Mrema hafai lakini ninachosema hapa ni kwamba fundemantals ala Kasparov, zimebadilika. Mkulima mzuri wa mchele wa kondeni, wakati mwingine anaweza kupata taabu kulima mchele uleule ulimwapo milimani. Kwenye soka – ukitazama Simba na Yanga, kwa kiasi wamejua namna ya kuwatumia wasemaji wao. Msemaji mmoja akiwa na makali zaidi kuliko mwingine, wakati mwingine hilo huashiria unyonge kwa timu pinzani.

 

Na kama aimbavyo mwanamuziki mmoja wa muziki wa kizazi kipya, Lavalava, alivyosema kwenye wimbo maarufu wa Tajiri; “Tulikaa kinyonge sana”, katika siasa hizi za ushindani, upande mmoja hautakiwi kuishi kinyonge wakati mwingine ukitamba.

 

Huu ni wakati wa Chadema kumtumia ipasavyo John Heche, mbunge wa zamani wa Tarime Mjini. Fungulia John Heche Suguta.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.