Israeli: Demokrasia yenye dosari na ubaguzi uliozagaa

Picha: Kiongozi wa zamani wa Wapalestina, Yasser Arafat, kwenye picha na Mwalimu Nyerere.

Na Ezekiel Kamwaga
Katika moja ya hotuba zake maarufu za zamani, Baba wa Taifa la Zambia, Dk. Kenneth Kaunda, alipata kuelezea uhusiano baina ya taifa lake na Tanzania kuwa sawa na ule wa pacha walioungana. Hakuna kilichokuwa kinaeleza uhusiano huo kama uhusiano baina yake na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Wawili hawa walipendana kiasi kwamba Kaunda aliamua kumpa mmoja wa watoto zake jina la Kambarage – ambalo ni moja ya majina ya Mwalimu Nyerere.
Na hata wakati alipokuwa akipita katika wakati mgumu kwenye utawala wa mbadala wake, Frederick Chiluba, kiasi cha kususa kula, ni Mwalimu ndiye aliyekwenda Zambia kumbembeleza aache mgomo huo wa kula.
Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akianza ziara yake ya kitaifa ya siku tatu nchini Zambia leo, ni muhimu kutumia muktadha huu kumtazama yeye na Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema.
Wanafanana nini? Nyerere na Kaunda waliunganishwa na itikadi ya Ujamaa wa Kiafrika (Ubuntu). Samia na Hakainde ni waamini wa mfumo wa soko huria. Nyerere na Kaunda walikuwa wamepishana miaka miwili – Julius akiwa mkubwa kwa Keneth, na Samia na Hakainde pia wamepishana miaka miwili; wa Tanzania akiwa mkubwa kwa wa Zambia.
Wote wameingia madarakani wakati dunia ikiwa inapambana na janga la Uviko 19 huku wanasiasa wa siasa za kidikteta wakipanda chati na mfumo wa dunia ukibadilika kutoka ule unaoongozwa na nchi za Magharibi na kuwa wa pande tatu – China na India kwa upande mmoja na Russia kwa upande mwingine.
Wanafanana pia kwa mazingira yao ya kuongoza vyama vyao vya siasa. Hakainde alianza kuongoza chama chake cha UPND mwaka 2006 kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wake, Anderson Mazoka huku Samia akipata Uenyekiti kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.
Wanatofautiana nini wawili hawa?  Mambo makubwa mawili – kwanza ni ukweli kuwa Hakainde ni mfanyabiashara aliyeingia kwenye siasa wakati Samia ni mwanasiasa ambaye hajawahi kuwa mfanyabiashara. La pili, na hili ni kubwa, ni kuwa Hakainde amewahi kuwa mwanasiasa wa upinzani wakati Samia ameishi katika nchi ambayo kwa muda wote imetawaliwa na chama kimoja cha siasa.
Samia na Hichilema kwenye macho ya dunia
Wakati likifanya uchambuzi wa mwaka mmoja madarakani wa Rais Hichilema, taasisi ya Chatham House ya Uingereza; ilimwita Rais huyo kwa jina la Meneja Masoko wa Zambia. Lakabu hiyo ilikuwa ikiakisi juhudi za kiongozi huyo kwenye kuhakikisha taifa lake linavutia wawekezaji na mitaji kutoka nje.
Hiyo pia ni lakabu aliyopewa Rais Samia wakati alipoamua yeye binafsi kutumia filamu ya Royal Tour kutangaza utalii wa Tanzania uliokuwa umeumizwa sana na changamoto ya Uviko 19.
Wawili hawa pia wanafahamika kwa kuelekeza sera za mambo ya nje ya mataifa yao kwenye kutofungamana na upande wowote na diplomasia ya uchumi. Wote wanavutia mitaji kutoka China, Marekani na kote kwingine kwenye fursa.
Wote wawili waliingia madarakania wakiwarithi viongozi ambao maridhiano ya kisiasa hayakuwa ajenda kuu kisiasa. Hakainde aliwahi kufunguliwa kesi ya uhaini na mara kadhaa kuwekwa ndani na mtangulizi wake, Edgar Lungu.
Samia kwa upande wake, alirithi nchi iliyogawanyika kutokana na utawala wa Magufuli na aliamua suala la maridhiano liwe ajenda kuu ya Urais wake mara tu alipoingia madarakani.
Wote wawili wanachukuliwa kuwa ni miongoni mwa viongozi wanaofanya mabadiliko makubwa ya kimifumo kuzifanya nchi zao za kidemokrasia zaidi katika bara ambalo udikteta na mapinduzi ya kijeshi vinaanza kupanda chati.
Fursa
Pengine kuliko marais wengine wa Afrika, Samia na Hakainde wana fursa ya kusimika zaidi uhusiano wa nchi zao kwa sababu misingi tayari ipo. Reli ya Tazara na Bomba la Mafuta la Tazama ni ushahidi wa msingi ambao tayari umewekwa.
Miundombinu na nishati ni masuala mawili ambayo yanaunganisha nchi na watu kwa namna ya kipekee. Reli ya Tazara si tu inasafirisha mizigo, lakini ni jukwaa la kipekee kwa raia wa nchi hizi mbili kuchangamana, kutembelea na kukutana.
Bomba la mafuta linamaanisha nchi hizi zimeunganishwa kiunoni- nikiazima maneno ya hayati Kaunda wakati akifananisha Tanzania na Zambia na mapacha walioungana, na jambo ambalo wote wana maslahi ya pamoja ya kudumu.
Kinachotakiwa sasa ni kuambizana kuhusu ni kwa vipi Zambia itaendelea kutumia bandari ya Dar kwa miaka mingi zaidi, wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizi mbili wataunganishwa kifursa ili waweze kuwekeza miongoni mwao na kuruhusu watu na mitaji wahame kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Biashara baina ya Zambia na Tanzania bado haijafika katika kiwango cha kuridhisha. Kiwango cha chini ya shilingi bilioni 300 ni kidogo kulinganishwa na umuhimu na ukaribu uliopo baina ya nchi hizi mbili.

 

Na Ahmed Rajab

 

‘Je, Israeli ni dola la ubaguzi wa kikabila?’ Nilimuuliza mwandishi habari maarufu wa Israeli Gideon Spiro kwenye mkahawa wa Bookworm Café jijini Tel Aviv, Mei 2009. Bookworm ni duka la vitabu lakini lina mkahawa na ni mahali ambapo Waisraeli wa mrengo wa kushoto hukutana.

Sijui kwa nini nilimuuliza Spiro swali hilo kwani nikijua kwamba Israeli ni nchi ya kibaguzi yenye utawala wa kikaburu. Labda nikitaka kushangazwa. Labda nikitaka kumsikia Mwisraeli wa mrengo wa kushoto akikana, kama inavyokana serikali yao, kwamba nchi hiyo si ya kibaguzi.

Siku chache kabla nilimuuliza swali hilo hilo mwandishi mwengine Wakiisraeli mwenye mawazo ya wastani. Alinijibu, kinaga ubaga, kwamba Israel ni dola la kibaguzi.

Lakini Spiro, aliyekuwa na umri wa miaka 77, hakukurukupa. Niliiona tabasamu yake iliyokunjika ikichezacheza kwenye ndimi zake na macho yake yakimetameta.  Alilipima jibu lake kabla ya kufungua mdomo wake na alipoufungua alisema haya: ‘Ni mfumo wa utawala wa kimbari (ethnocracy)’.

 

Baada ya kusema hayo alisita, akapiga fundo la kahawa aipendayo, iliyojaa povu la maziwa — aina ya Cappuccino — na akaendelea kunieleza hivi:

‘Kwa Wayahudi ni utawala wa demokrasia yenye mipaka, kwa Wapalestina walio kwenye maeneo yanayokaliwa na Israeli ni utawala wa udikteta wa kijeshi na kwa Waarabu wa Israeli ni utawala wa demokrasia yenye ubaguzi. Lakini kwa Wayahudi na Waarabu kwa pamoja utawala huo si wa demokrasia,’ alisema.

 

Ingawa Wapalestina wana utambulisho mmoja, kuna aina tano za Wapalestina. Kuna Wapalestina wa Gaza walio chini ya utawala wa Hamas, kuna wa Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan walio chini ya Mamlaka ya Palestina, kuna wa Jerusalem ya Mashariki wenye ukaazi wa kudumu, kuna Waarabu wa Israeli wenye uraia wa Israeli na kuna Wapalestina walio uhamishoni, wasioruhusiwa kurudi kwao.

 

Wapalestina wa sampuli zote hizo hawasalimiki na makucha ya chuma ya Israeli.  Walio Gaza, mara kwa mara, hutwangwa kwa mabomu ya Israeli.

 

Wa Ufukwe wa Magharibi wanaishi katika eneo linalokaliwa kijeshi na Israeli.  Wanajeshi wa Israeli huingia katika eneo hilo saa yoyote waitakayo, huzivamia nyumba na kuzipekua juu chini.  Huwakamata au kuwaua Wapalestina wa huko.

 

Maisha ya Wapalestina wa Ufukwe wa Magharibi ni magumu katika miji yake yote ikiwa pamoja na Ramallah, Nablus, Hebron, Bathlehem, Qalqilya, Jenin na Tulkarm.  Wanashambuliwa na walowezi wa Kiyahudi wenye silaha na wanaolindwa na wanajeshi wa Israeli ili waweze kuiba ardhi za Wapalestina.

 

Wapalestina wa Jerusalem ya Mashariki wanatolewa kwa nguvu majumbani mwao na nyumba zao wanapewa Wayahudi kutoka Marekani.  Na Waarabu wa Israeli daima hubaguliwa.  Ni marufuku Waarabu wa Israeli kuoa wanawake wa Kiyahudi. Siku hizi ni nadra kuwaona Waarabu wa Israeli wakitoka nje saa za usiku; wanaogopa.  Hofu yao ni magenge ya wahalifu wenye silaha wenye kuwashambulia.

 

Kuna sheria 65 zenye kuwabagua Waarabu wenye uraia wa Israeli. Waarabu hao hawaruhusiwi kununua ardhi katika maeneo mengi ya Israeli.  Vijiji vingi vya Waarabu vimetengwa mbali na miji ya Wayahudi.  Katika Israeli nzima kuna miji kama minane tu ambamo Waarabu na Wayahudi wanaruhusiwa kuishi pamoja.  Kila mji wa Waarabu umezungukwa na makazi ya Wayahudi kuwazuia Waarabu wasijitanue.

Spiro aliongeza kwamba, hata wenyewe kwa wenyewe, Wayahudi wanabaguana. Wayahudi wenye asili za kizungu ndio walio tabaka la juu lenye kutawala na Wayahudi waliosalia, hasa walio weusi, wako chini, fungu la Mungu.

 

Ikiwa hivyo ndivyo watendewavyo Wayahudi Weusi, kefu Wapalestina Weusi wenye asili ya Kiafrika na walio Waislamu? Kama nilivyogusia wiki iliyopita nilikutana nao katika jangwa la Negev walikonialika chakula cha mchana.

 

Wapalestina hao wa Kiafrika wameshiriki katika harakati za ukombozi.  Aliye maarufu na ambaye sikujaaliwa kukutana naye, alikuwa Fatima Mohamed Bernawi, aliyefariki Cairo, Misri, Novemba mwaka jana na kuzikwa Gaza.

 

Fatima alizaliwa Jerusalem mwaka 1939.  Baba yake, aliyetoka Nigeria, alishiriki katika mapigano ya Wapalestina ya 1936 dhidi ya Waingereza. Mama yake alikuwa Mpalestina.  Alipokuwa na miaka tisa wakati wa ‘Nakba’ (Maafa) ya 1948 Wayahudi walipokuwa wakiwafukuza Wapalestina kutoka kwenye nyumba zao na kuyapora mashamba yao, Fatima alimfuata mama yake aliyekimbilia kambi ya wakimbizi karibu na Amman, mji mkuu wa Jordan.  Baba yake alibakia Palestina.  Baadaye, Fatima na mama yake walirudi Jerusalem kuishi naye.

 

Alipokuwa anakua, Fatima alijiunga na mvuvumko wa ukombozi wa Palestina. Alikuwa miongoni mwa Wapalestina waliopatiwa mafunzo ya kijeshi ili wapambane na Israeli. Yeye alikuwa mwanamke wa kwanza wa Kipalestina aliyeandaa shambulizi dhidi ya Israeli.

 

Oktoba 1967 alitega bomu ndani ya sinema katika Jerusalem ya Magharibi.  Ingawa bomu hilo halikuripuka wanajeshi wa Israeli walimkamata, akiwa Mpalestina wa kwanza wa kike kutiwa nguvuni na vyombo vya ulinzi vya Israeli. Fatima alihukumiwa kifungo cha maisha.  Alikaa jela kwa miaka kumi.  Aliachiwa kwa maafikiano ya Israeli na Wapalestina ya kubadilishana wafungwa.

 

Yasser Arafat, aliyekuwa kiongozi wa Chama Kikuu cha Ukombozi wa Palestina (PLO), alikawia sana kuoa.  Alioa akiwa na miaka 61.  Kabla hajaoa akisema kwamba kama ataoa, atamuoa Fatima Bernawi.  Fatima hakuwa riziki yake Arafat kwani aliolewa na Mpalestina mwengine aliyewahi kuwa mfungwa wa Waisraeli, Fawzi al-Nimr, aliyeachiwa huru Mei 1985.

 

Kufikia 1996 Fatima alikuwa mwanamke wa ngazi ya juu kabisa katika jeshi la mgambo la chama cha Fateh na mkuu wa polisi wa kike katika serikali ya Gaza na Jericho.

 

Wiki iliyopita nilieleza kwamba kabla ya kuingia Gaza nilikaa Israeli kwa siku kadhaa.  Nilipata fursa ya kuingia Ufukwe wa Magharibi na kushinda, kwa siku nzima, Ramallah, makao ya Rais Mahmoud Abbas, mrithi wa Arafat.

 

Arafat akiipenda Afrika na alikuwa na mshauri wake muhtasi kuhusu Afrika, Salman al-Hirif.  Kadhalika, alikuwa na usuhuba na viongozi kadhaa wa Kiafrika.  Akisikilizana na Nelson Mandela, Mwalimu Julius Nyerere pamoja na mrithi wake Rais Ali Hassan Mwinyi na pia Ahmed Abdallah, aliyekuwa Rais wa Comoro.

 

Arafat aliwahi kuzizuru Afrika Kusini, Tanzania na Comoro, ingawa Comoro hakulala kwa sababu ya usalama wake.  Wakati huo, Comoro ilikuwa ikidhibitiwa na mamluki wa Kizungu waliomrejesha madarakani Abdallah ambaye baadaye walimuua.

 

Nilipokuwa Ramallah nililizuru kaburi lake Arafat.  Kuvuka Ufukwe wa Magharibi na kuingia Israel si rahisi kwa Wapalestina.  Kuna vizuizi vingi vya barabarani na wanajeshi wa Israeli wanaovisimamia hawana huruma na Wapalestina.  Kazi yao kubwa ni kuwanyanyasa.

 

Wanyanyasaji ni vitoto vidogo utafikiri vina umri wa miaka 16. Lakini wana silaha nzito na ndimi zao zimejaa kiburi na ufedhuli. Kwa hivyo, ‘vijanajeshi’ hivyo vinakuwa mabwana — ingawa wengine ni wasichana — na ukiwa Mpalestina hukuona kinyangarika tu.

Niliyaona mengi Israeli. Nilizifuata nyayo za Nabii Issa (Yesu Kristo), nikatembea kwenye Mji Mkongwe wa Quds (Jerusalem), nikasali Ijumaa mbili kwenye msikiti wa Al Aqsa. Kiguu na njia nikaizuru miji ya Tel Aviv, Jaffa, Sderot na Be’er Sheva ulio katika Jangwa la Negev.

Israeli ni nchi ya kuta, vizuizi, vikwazo, vipingamizi na vikaratasi vya ruhusa na vibali vya kila aina wanavyotakiwa Wapalestina wawe navyo.  Daima wanadhalilishwa kwa kila namna ya idhilali. Nyumba zao zinabomolewa, wanafukuzwa makwao na lengo la Wazayoni jijini Jerusalem ni kuufanya mji mzima uwe na sura ya Kiyahudi.

Waarabu hawaruhusiwi kujenga katika Jerusalem ya Magharibi kwa Wayahudi lakini Wayahudi wanaruhusiwa kujenga Jerusalem ya Mashariki kwa Waarabu.

Siku moja nilialikwa kwenye Bunge la Israel, Knesset, na Dakta Dov Khenin, aliyekuwa Mbunge wa chama cha Hadash, chama pekee cha Wayahudi na Waarabu na ambacho ni cha mrengo wa kushoto. Khenin alikuwa pia mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Israeli, Maki.

Ofisini mwake Khenin alitundika picha ya Che Guevara, mwanamapinduzi mzalia wa Argentina aliyeshiriki kwenye mapinduzi ya Cuba. Nilipomwambia kwamba tathmini yake ya mustakbali wa mgogoro wa Israeli na Wapalestina inakosa rajua, kwa vile inayaona mambo yote kuwa yasiyo na mbele wala nyuma, alinijibu kwa kumnukuu mwanafalsafa wa Kimarx wa Kitaliana, Antonio Gramsci.

Alinikumbusha kwamba Gramsci aliwahi kuandika kwamba alikuwa hana ‘rajua ya akili, lakini alikuwa na dhamira ya kutegemea mema’ (pessimist of the intellect, optimist of the will). Ukosefu wa rajua ni kichocheo cha kuchukuwa hatua, na msimamo wa kutarajia mazuri ni ukakamavu wa kuamini kwamba hatua hiyo italeta mageuzi ya maana hata pakiwa na nakama.

Khenin alinisikitikia kwamba ubovu wa Israeli ni kuwa Waarabu na Wayahudi hawalingani kwa lolote. Jamii zao zimegawika vibaya. Hajakusudia Wapalestina na Wayahudi lakini Waarabu wa Israel na Wayahudi wao.

Si tu kwamba Waarabu na Wayahudi wanazungumza lugha tofauti lakini hata misamiati yao ni tofauti na dhana (concepts) zao ni tofauti — katika siasa, utamaduni, na katika maingiliano yao ya kijamii ambayo ni madogo mno na kwa namna wanavyoangaliana, kwa kuchujana.

Jamii zote mbili zinaogopana. Wayahudi wana hofu na Waarabu; Waarabu nao wanawaogopa Wayahudi. Lakini alitaka nitambuwe kwamba ‘Israeli sio tu pahala ambapo matatizo hukutana lakini pia ni pahala penye uwezekano mwingi,’ yaani mengi yanaweza kufanywa.

 

Hamna shaka kwamba hii ni saa ya giza katika Israeli.  Ni wakati ambapo mengi yanaweza kufanywa, na lazima yafanywe, ili eneo zima la Mashariki ya Kati liwe na amani. La kwanza ni kuufumua mfumo mzima wa kikabila na ubaguzi uliotamalaki katika taifa hilo.

 

Dhana kama ‘demokrasia’ na ‘uhuru’ au ‘ukombozi’ zimekuwa zikitumiwa vibaya na wanasiasa wa Kizayoni.  Wanazitumia kwa maslahi ya kikabila — kabila la Wayahudi.  Lakini kuna tatizo: Wayahudi wengi wanazidi kupaza sauti zao kuwapinga Wazayoni, wakihoji kwamba imani za Kizayoni, zikiwa pamoja na kuundwa kwa dola la Israeli na misingi yake ya kikaburu, zinakwenda kinyume na dini yao na ni ukoloni wa Kizayoni.  Uzayoni wenyewe nao ni itikadi ya ubaguzi wa kikabila.

 

Sauti hizo za Wayahudi zinapazwa sambamba na zile zinazotaka Wapalestina warejeshewe haki zao na demokrasia halisi isimamishwe Israel.

 

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com/X:@ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. §§§§§§§§§London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.