IWD: Ushiriki wa siasa usisubiri nyakati za uchaguzi pekee

Na Fortunata Kitokesya

 

SIKU ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (International Women’s Day) ina mchango mkubwa kwa usawa na haki za wanawake wote duniani. Ni siku muhimu ya kutambua mapambano endelevu ya usawa wa kijinsia na kusherehekea mafanikio ya wanawake ulimwenguni kote.

 

Pia ni siku ambapo watu binafsi, mashirika, na jamii wanakusanyika kwa pamoja kutetea na kuchochea haki za wanawake, kuongeza uelewa kuhusu masuala yanayohusiana na jinsia, na kukuza mabadiliko chanya katika nyanja mbalimbali kama za kijamii, kiuchumi, utamaduni na siasa. Lakini pia kuikumbusha dunia kuwa haki za wanawake ni haki za binadamu kama alivopata kusema Waziri wa Mambo ya Nje wa wa zamani wa Marekani, Hillary Clinton.

 

Umoja wa Mataifa umetaja ‘Wekeza kwa Wanawake: Kuharakisha Maendeleo’ kuwa kaulimbiu ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake (SKW), ambayo husherehekewa kila mwaka tarehe 8 Machi. Kaulimbiu ya kampeni ya mwaka huu, “Ushirikishwaji” inasisitiza hatua thabiti za kukuza mazingira yasiyo na upendeleo, dhana potofu, na ubaguzi.

 

Vilevile mwanaharakati na mwandishi wa habari, Gloria Steinem, anaeleza kwa ufasaha dhima ya kuadhimisha siku hii kuwa ni mapambano ya usawa wa kijinsia hayawezi kuhusishwa na mtu au shirika mmoja bali ni juhudi za pamoja za wote wanaoamini katika haki za binadamu. Kila hatua, hata iwe ndogo kiasi gani, inachangia katika harakati kubwa kuelekea usawa na uwezeshaji. Hivyo basi, kila mtu ana mchango chanya katika kuhakikisha tunafikia usawa wa kijinsia katika dunia yetu.

Basi, kama ilivo ada, mwaka huu tena tarehe kama ya leo tunasherehekea hii siku muhimu ya kimataifa ya wanawake. Sisi kama wanawake wa Tanzania hatupo nyuma pia katika kusherehekea siku hii muhimu.Kwa kipekee kabisa serikali yetu inatambua siku hii muhimu na imekuwa ikisherehekewa kitaifa kila baada ya miaka minne. Lakini miaka mingine inasherehekewa Katika ngazi za kimikoa. Vileveile taasisi zisizo za kiserikali zimekuwa zikisherehekea siku hii kwa kuandaa makongamano au matamasha. Mfano leo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kitaadhimisha siku ya wanawake kimataifa kwa kujadili na wadau wa siasa kuhusu: Uchaguzi na Ushiriki wa kisiasa kwa Wanawake ni muhimu ili kuongeza idadi ya wanawake katika siasa na katika maamuzi.

 

Ushiriki wa wanawake katika siasa umekua ukiongezeka kwa kiasi duniani hasa katika bara la Ulaya ambapo tumeona kuna wimbi kubwa la viongozi wakubwa wa kisiasa wakiwa mawaziri wakuu na kushika nafasi mbalimbali za juu za kisiasa mfano ukiwa nchi kama vile Denmark, Finland, Sweden. Ushiriki wa wanawake katika siasa haukuanza kwa wepesi sana kutokana na mfumo uliokuwepo.

 

Lakini kidogo kidogo mambo yakaanza kubadilika na wanawake wakaanza kushiriki katika siasa kwa njia ya kupiga kura na baadaye hata kuingia katika vyama vya siasa na kuwa viongozi. Kitakwimu kufikia tarehe 10 Januari 2024, kuna nchi 26 ambapo wanawake 28 wanahudumu kama Wakuu wa Nchi na/au Serikali. Pamoja na kuwepo kwa mabadiliko kwa kiasi, usawa wa jinsia katika nyadhifa kuu za mamlaka hautafikiwa kwa miaka mingine 130!

 

Mjadala wa Kituo cha Haki cha Sheria na Haki za Binadamu ni mzuri sana kwa wakati huu ambapo tupo katika mchakato wa maboresho ya kisiasa lakini pia tukielekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

 

Swali kubwa la kujiuliza ni kwa kiasi gani wanawake tuna shiriki katika siasa zetu za ndani na pia tunatumiaje fursa hizi za ushiriki katika majukwaa yanayochochea kujadili mambo ya siasa?

 

Kwa uzoefu tu, mara nyingi tunasikia sana habari za siasa tukikaribia uchaguzi, baada ya hapo uchaguzi ukiisha tunafunga vitabu maisha yanaendelea mpaka tena awamu nyingine ya uchaguzi.  Jambo moja la muhimu la kuzingatia katika kuhakikisha wanawake wanashiriki katika siasa ni kuhakikisha kuwa kuna uendelevu wa kukumbushana mara kwa mara umuhimu wa kushiriki katika siasa katika maisha yetu ya kila siku. Siasa ni maisha yetu ya kila siku na si wakati wa uchaguzi pekee.

 

Ili wanawake wajijengee msingi mkubwa katika siasa na pia kushinda uchaguzi ni vizuri kuwajengea uwezo wa kuwa na ushawishi kwa jamii ambayo wanataka kuitumikia.  Siasa si tukio la siku moja au wakati wa uchaguzi na likaishia hapo la hasha!  Wanawake wanahitaji kujengewa uwezo wa kuwa na mbinu mbalimbali za ushawishi kwa jamii ili kujenga mahusiano mazuri na wapiga kura wao lakini pia kujua jamii inahitaji nini katika afya, elimu na mambo ya jamii kwa ujumla.  Bila ya kujenga ushawishi kwa ni ngumu sana kufanikisha adhma ya  ushindi.

 

Jambo lingine la muhimu kwa wanasiasa wanawake ni kuwa na maono yatakayoongoza ushawishi katika jamii. Ingawa kuwa na idadi kubwa ya wanawake katika siasa ni sehemu ya mafanikio muhimu kwa wanawake, lakini tusipotezwe na takwimu. Lengo kuu linapaswa kuwa na wanawake walio na uwezo wa kufanya siasa zenye tija kwa jamii na ndani ya vyama vyao na katika taswira pana ya kisiasa. Na mwisho wake ni kuhusu kuleta tofauti halisi katika maisha ya wanawake na katika sera zinazotungwa na kugusa maisha ya watu kila siku.

 

Pia wanawake wajengewe mazingira wezeshi, yanayo wahakikishia usalama wao wawapo katika majukwaa ya kisiasa yaani kupinga ukatili dhidi ya wanawake katika siasa. Inawezekana kuwa Wanawake wengi wanahisi kwamba majukwaa siasa sio mahali salama kwao.

 

Na inaweza kuwa ni sababu mojawapo inayorudisha nyuma ushiriki wa wanawake katika siasa. Ulinzi huu unatakiwa kuanzia ndani ya vyama vya siasa kwa kuwa na ulinzi wa kijinsia kwa wanachama wake wanawake. Mfano hivi karibuni tumeshuhudia chama cha ACT Wazalendo wamezindua sera ya kijinsia ndani ya chama chao, hii ni htaua nzuri yenye dhamira ya kuhakikisha usawa wa kijinsia unaoneka kwa matendo.

 

Hatimaye, Ni muhimu pia kutambua nafasi mbalimbali za wanawake walizo nazo katika siasa. Si lazima wanawake wote wajitokeze kwenye majukwaa. Kuna wengine wanafanya kazi nyuma ya pazia. Ni wahamasishaji, washauri waelekezi, watungaji na waboreshaji sera. Na hiyo ni sawa! Wote wana mchango chanya katika kukuza ushiriki wa wanawake katika siasa.

 

Na hii inaweza kuwa ni mbinu nzuri ya kujenga siasa ndani ya vyama vya siasa. Ukiwa na taasisi yenye wanawake wenye uwezo na ujuzi wa mambo ndani ya chama cha siasa basi matokeo chanya yataonekana  kupitia wale wanao kiwakilisha chama katika nafasi zao za uongozi.

 

Kuwekeza katika uongozi wa kisiasa wa mwanamke si sahihi tu bali ni hatua kubwa ya maendeleo. Hii inawatia moyo  kiujumla wanawake wanaoingia katika siasa, wakiwa na ujasiri na uwezo wa kufuta ile dhana ya kuwa na shaka  juu ya uwezo wao wa uongozi.

 

Mashaka haya yamefanya wanawake katika siasa kupata uchunguzi mkali zaidi kuliko wenzao wa kiume. Kwa hiyo vyama vya siasa viendelee kuhakikisha sera za wa usawa kijinsia zinafanya kazi lakini pia sera za nchi kwa ujumla zihakikishe kuwa wanawake wanashiriki vyema katika siasa zao kawa wanaume bila ya kubaguliwa na kubughudhiwa.

 

Mwisho, siku ya leo itukumbushe jamii kuwa siasa ni kila iitwapo leo na si wakati wa uchaguzi tu. Hivyo basi tukumbuke kuwa demokrasia haiimarishwi kwa kuchagua wanawake kwa msingi wa jinsia yao pekee tu, bali pia kwa kuwa na wanasiasa wanawake wanaoweza kuleta tija kwa jamii nzima lakini zaidi kuwa wawakilishi wazuri wa ajenda za wanawake katika vyombo vya kufanya maamuzi. Tusigubikwe na uhitaji idadi au kufikia idadi wanawake wengi kwenye siasa kama inavotakiwa na sheria bali vigezo vingine vitumike ili kupata wanasiasa bora wa jinsia ya kike.

 

Uchaguzi wa 2024 na 2025 utakuwa ni kipimo chetu kizuri cha maendeleo katika  kujenga mfumo wa kisiasa wenye kuwajumuisha na kuleta usawa na kupata idadi zaidi ya wanawake.

 

Mwandishi wa makala haya ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na  Mwanaharakati wa Masuala ya Utetezi wa Haki za Binadamu, Utawala wa Sheria na Utoaji Haki.

 

 

 

 

 

Top of Form