Rais Samia Suluhu Hassan akimwapisha Ali Idi Siwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) wiki hii. Picha kwa Hisani ya Ikulu
Na Ezekiel Kamwaga
MARAIS huwa hawachagui siku au mazingira yatakayowafanya washike wadhifa huo katika wakati husika. Kama ungekutana na Ali Hassan Mwinyi mwaka 1983 na kumueleza angekuwa Rais wa Tanzania mwaka 1985, pengine angekushangaa. Hadi Januari mwaka 2015, wengi walidhani ni ndoto za mchana kwa John Magufuli kuwa Rais wa Tanzania. Lakini wote walikuja kuwa marais.
Rais Samia Suluhu Hassan hakupanga kuwa Rais wa Tanzania mnamo Machi mwaka 2021. Hakuchagua kuwa Rais kufuatia kifo cha mtangulizi wake, hakuchagua kuwa Rais katika wakati ambapo nchi yake na dunia kwa ujumla ilikuwa inazongwa na janga la Uviko-19 na kuanza kwa mporomoko wa uchumi wa dunia na, bila shaka, hakuchagua kuwa Rais katika wakati ambapo dunia inapita katika changamoto kubwa kwenye eneo la ulinzi na usalama.
Kadari ina namna yake ya kujionyesha kwa kila mmoja wetu.
Kwa sababu ya mazingira yake ya kuingia madarakani, Rais Samia hakupata nafasi ya kuingia na “mtu wake” kwa maana ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) – kama ambavyo Benjamin Mkapa alifanya kwa Cornel Apson, Jakaya Kikwete kwa Othman Rashid na Magufuli kwa Modestus Kipilimba. Alimkuta Diwani Athumani Msuya aliyeteuliwa kwenye nafasi hiyo na Magufuli.
Ilitazamiwa kwamba wakati fulani Samian aye angeteua mtu wake kushika wadhifa huo. Januari mwaka huu, akamteua Saidi Masoro kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TISS, miezi saba baadaye, amelazimika kufanya mabadiliko ya bosi wa taasisi hiyo – kama ambavyo Magufuli alilazimika kumbadili Kipilimba na kumpa Diwani.
Sifahamu sababu za mabadiliko haya. Na yalikuja ghafla hata kwa Masoro mwenyewe. Nimeambiwa kwamba wakati mabadiliko hayo yakitangazwa, Masoro alikuwa ziarani katika mojawapo ya mikoa ya Tanzania. Lakini lengo la uchambuzi huu ni kutaka kueleza kidogo kuhusu Siwa, siasa za uteuzi wa kachero namba moja na kadar katika maisha yetu.
Kwanza kabisa, ni nani huyu Ali Idi Siwa?
Kwa mara ya kwanza nilianza kumsikia Siwa miaka takribani 10 iliyopita. Wakati huo alikuwa na majukumu ya kidiplomasia nchini Ujerumani nami nilikuwa tayari Mhariri wa gazeti la Kiswahili la kila wiki la Raia Mwema. Mmoja wa waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Rais Kikwete alinisimulia kuhusu matukio yaliyotokea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ambapo jina la Siwa liliibuka.
Nikapata taarifa zake zaidi mwaka 2014 wakati nilipokwenda nchini Rwanda kwa kazi za kiuandishi huku yeye akiwa Balozi wa Tanzania katika taifa hilo. Sijui ni kiasi gani wasomaji wanajua hali ya kidiplomasia ilivyokuwa baina ya majirani hawa wakati huo lakini itoshe kusema tulivuka salama pasi na kuingia katika hatua mbaya ya kupigana vita.
Jambo moja ambalo wote wanaozungumzia Siwa wanakubaliana ni kwamba ni mmoja wa makachero waliopikwa na kuiva vizuri hapa Tanzania. Alijiunga na utumishi wa umma mwaka 1977 na ametumia sehemu kubwa ya maisha yake ya utu uzima akiwa mtumishi wa idara.
Kuna wengi wanaoamini kwamba pengine wakati wake wa kuwa kachero namba moja hapa Tanzania ulikuwa ni mwaka 2005 kuchukua nafasi ya Apson baada ya Mkapa kumaliza muda wake. Watu wanaofahamu siasa za ndani ya idara wanaamini kwamba kilichofanya asipewe wadhifa huo ni kuwa pengine hakuwa katika “upande sahihi” kisiasa wakati huo.
Badala yake, baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, alipewa majukumu ya nje ya nchi. Hadithi ya Siwa kupelekwa nje ya nchi kwa majukumu mengine si yak wake peke yake. Kulekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, supastaa wa tasnia ya ukachero hapa nchini alikuwa ni hayati Mahmoud Issa. Huyu ni kachero ambaye yeye na hayati Augustine Mahiga, ndiyo waliofanikishwa kukamatwa na kushitakiwa mahakamani kwa wanajeshi waliotaka kumpindua hayati Rais Julius Nyerere kwenye miaka ya 1980.
Issa na Mahiga walitoa mpaka ushahidi mahakamani kwenye kesi hiyo kwa kutumia lakabu za X na Y na mwishowe Jamhuri ikaibuka mshindi katika kesi hiyo ya uhaini dhidi ya akina hayati Zacharia Hans Poppe. Mahiga, nyota mwingine wa TISS nyakati hizo, alipanda na kufikia hadhi ya kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TISS na lilikuwa suala la wakati tu kabla zamu ya Issa haijafika. Kila mmoja alidhani atakuwa yeye mwaka 1995. Hata hivyo, Mkapa akaamua kwenda na Apson.
Kilichotokea ni kwamba Issa alipangiwa majukumu mengine nchini Russia alikokaa kwa zaidi ya miaka 10 hadi kustaafu kwake. Kama ilivyokuwa kwa mmoja wa walimu wake hao, Issa, Siwa naye alipangiwa majukumu mengine nje ya nchi mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi uliompa ukachero mkuu mtu mwingine.
Lakini, kadari ni kadari na ina namna yake ya kujionyesha kwa kila mmoja. Baada ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda mwaka 2014, ilionekana kwamba maisha yake kwenye dunia ya siri ya kikachero yalikuwa yamefikia mwisho. Lakini uteuzi huu umemrejesha pale ambapo wengine walidhani alistahili miongo miwili nyuma. Labda wakati wake ulikuwa bado.
Uteuzi wa Siwa unajibu maswali mengi ya changamoto za nyakati hizi. Kwanza kitendo cha mtu mahiri kupewa nafasi yake, kinamaanisha Rais Samia anajenga msingi wa meritocracy kwenye taasisi hiyo nyeti kwamba sasa watu watapewa vyeo na fursa kulingana na uwezo wao wa kazi na si vitu vingine.
Jambo lingine ni ukweli kwamba Siwa ni mtu anayeifahamu taasisi hiyo ndani na nje na hivyo ana sifa mbili kubwa; mosi kwamba anaijua vilivyo – mazuri na mabaya yake, lakini baada ya kukaa nje kwa takribani miongo miwili, anaweza pia kuja akiwa na mawazo mapya na mazuri zaidi kuliko kama angekuwa humohumo kwa tangu mwaka 2005.
Baadhi ya watu waliowahi kufanya naye kazi kwa karibu wanamuelezea kama mwalimu mzuri kwa watu walio chini yake. Faida ya mtu wa namna hii ni kuwa anaweza kusaidia kujenga kada mpya ya makachero wa Kitanzania wenye weledi, uwezo na ung’amuzi mzuri wa changamoto za kiusalama zilizopo sasa na za miaka ijayo.
Nauangalia uteuzi huu wa Siwa katika maeneo mawili makubwa zaidi; mosi ni kuhusu ni mwenendo wa kiusalama wa Tanzania katika nyakati hizi za ugaidi, mapinduzi ya kijeshi mfululizo barani Afrika na changamoto za kiusalama katika nchi jirani za Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika mataifa makubwa ambayo masuala ya usalama yanapewa nafasi kubwa; makachero viongozi wa nchi hizo huwa na sifa kubwa mbili – mosi ni utambuzi wa masuala ya nchi zinazowazunguka na pili ni uelewa mpana wa jumuiya ya kimataifa na namna inavyofanya kazi.
Chukulia mfano wa taifa la India. Mkuu wa Shirika la Ujasusi la India anayemaliza muda wake, Samant Goel, kwa muda mrefu alifanya kazi katika maeneo mawili; Dubai na London. Hivi ni vituo viwili vya kikachero ambapo masuala mengi ya dunia hupita hivi sasa. Siwa kakaa pia Dubai na Ujerumani – taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi barani Ulaya. Mambo yanayopita na kurudi ni mengi.
Aliyemrithi Goel, Ravi Sinha, ni mtaalamu wa masuala ya usalama baina ya India na jirani zake wa Pakistan. Kubwa zaidi, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Usalama wa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, Ajit Doval, si kwamba anaijua Pakistan vizuri – amewahi kuishi kwa jirani zake hao kwa takribani miaka saba akifanya ukachero.
Kachero Mkuu mpya wa Tanzania amefanya kazi ya kibalozi katika nchi jirani kwa takribani miaka minne. Kwa vyovyote vile, kwa maana ya dunia ya uhusiano wa kimataifa, hatari ya kwanza ya nchi kiusalama inatoka miongoni mwa jirani zake. Kama ambavyo India wanaona inafaa kuifahamu Pakistan na majirani wengine, ni muhimu kwa taifa letu kuwa na kachero namba moja ambaye anawafahamu vizuri majirani zetu.
Jambo la pili linahusu Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025. Mfuatiliaji yoyote wa siasa za Tanzania na Afrika anafahamu kwamba uchaguzi si jambo lelemama. Mjadala kuhusu suala la Bandari na kampuni ya DP World umetuweka ‘uchi’ kama taifa na kuonyesha nyufa tulizonazo. Ni wazi uchaguzi ujao, kama viongozi na wataalamu wa usalama hawatatekeleza majukumu yao ipasavyo, unaweza kutupasua zaidi kama taifa kuliko tulivyo sasa.
Kwenye mazingira ya namna hii, unamhitaji mtu anayejua namna ya kulinda amani na umoja wa kitaifa. Unamhitaji mtu ambaye uzalendo kwa taifa lake hauna shaka. Unahitaji mtu hodari.
Unamhitaji Ali Idi Siwa.