Kadinali Pengo angesemaje kuhusu Waraka wa Maaskofu?

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

KUELEKEA kipindi cha Kwaresma na Sikukuu ya Pasaka ya mwaka 2018, Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) lilitoa waraka ambao kimsingi ulikosoa vitendo vya uminyaji wa demokrasia na uhuru wa watu kujieleza uliokuwepo wakati wa utawala wa hayati Rais John Magufuli.

 

Waraka ule ulikuwa na sehemu nne lakini sehemu iliyozua mjadala zaidi ilikuwa ni sehemu ya tatu iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho; “Dalili za Nyakati Zetu Tanzania” ambapo pamoja na mambo mengine, Maaskofu walieleza kutofurahishwa kwao na maandamano na mikutano ya kisiasa kuzuiwa na vyombo vya dola huku vyombo vya habari vikifungiwa.

 

Siku chache baadaye, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, alizungumza na vyombo vya habari na kutoa maelezo yaliyokuwa na sura ya kutokubaliana na waraka ule. Kwanza alisema kwamba hakuwa anajua chochote kilichoandikwa ndani ya waraka ule na kwamba jina lake alilikuta tu kwenye lile tamko. Na pili, Pengo ambaye pengine alikuwa ndiye Mkatoliki mashuhuri na anayeheshimika zaidi nchini, alieleza kutokubaliana na yaliyomo kwenye waraka ule – hasa masuala yasiyo ya kidini yaliyojumuishwa humo.

 

Kuna mambo makubwa mawili ambayo tunaweza kujifunza kutoka kwenye maelezo hayo ya Pengo wakati tukianza kudadavua waraka wa hivi karibuni uliotolewa na TEC kuhusu suala zima la mkataba wa uendeshaji wa bandari za hapa nchini baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai.

 

La kwanza ni kwamba waraka wa TEC si neno la Mungu. Kama ingekuwa waraka huo ni neno, mtu wa hadhi ya Kadinali Pengo asingeweza kutoka hadharani na kueleza mapungufu ya waraka wa mwaka 2018. Mwadhama Pengo ni mlinzi wa imani ya Kikatoliki na kwa vyovyote vile asingeweza kupingana na jambo lenye kulinda imani au la maelekezo ya Kimungu.

 

Jambo la pili linahusu wanaosaini waraka. Maelezo ya Pengo yalitufundisha kwamba unapoona waraka umesainiwa na Maaskofu 37 – kama ilivyokuwa kwa waraka uliosomwa kwa waumini Wakatoliki kwenye makanisa ya Tanzania Jumapili iliyopita, si lazima Maaskofu wote wawe wanajua kilichomo. Inawezekana kazi hiyo imefanywa na Maaskofu wachache tu – na wengine hawakujua chochote hadi waraka huo ulipojitokeza; kwanza kwenye vyombo vya habari na pili makanisani.

 

Na Mwadhama alikuwa na swali moja muhimu alilouliza TEC baada ya waraka ule wa mwaka 2018; kwamba Maaskofu wanajua nini kuhusu haki za kidemokrasia na kubana uhuru wa watu kujieleza? Pengo aliwaambia waandishi wa habari kwamba hayo si maeneo ambayo viongozi wa dini wanayajua zaidi kuliko wanasiasa na vyama vya siasa.

 

Ndilo swali ambalo pia nadhani Kadinali Pengo angeuliza kuhusu waraka huu wa TEC wa wiki iliyopita. Kwamba Maaskofu wanajua nini kuhusu masuala ya uendeshaji wa bandari? Wanajua nini kuhusu masuala ya haki za kibiashara za Tanzania na nchi nyingine kwenye uwekezaji?

 

Hili ni swali muhimu kwa sababu; kama Maaskofu wakianza kuhoji kuhusu uwekezaji bandarini, mpaka wa kuhoji utaishia wapi? Nini kitawafanya wasihoji kuhusu gharama za ujenzi wa Reli ya SGR au Bwawa la Mwalimu Nyerere? Kama wanaruhusiwa kuhoji uwekezaji bandarini, nini kitawazuia wasihoji kuhusu bei za korosho na kahawa kwa wakulima?

 

Hofu kubwa ya Pengo wakati ule – na naamini ndiyo hofu kubwa ya baadhi yetu kwenye waraka huu wa Maaskofu ni kwamba, Tanzania imebaki kuwa nchi ya mfano kwa Umoja na Amani yetu kwa sababu ya mgawanyo mzuri wa majukumu baina ya masuala ya kiserikali na yale ya kidini.

 

Kama Serikali ingekuwa imetangaza Jumapili kuwa siku ya kazi na watu hawataruhusiwa kwenda kanisani, waraka wa TEC kupinga hilo na kuusambaza na kusomwa makanisani lingekuwa jambo linaloingia kichwani. Kama Serikali ingelazimisha watu kufanya mambo ambayo ni kinyume cha misingi na imani ya kidini, waraka ungekuwa na maana kubwa.

 

Lakini suala la uwekezaji tayari lina mijadala yake kupitia itikadi za vyama. Ziko itikadi zinazoamini kwamba uchumi wa unatakiwa kumilikiwa na dola na watu wake na ziko itikadi za kisiasa zinazoamini uchumi unatakiwa kuamuliwa na nguvu ya soko. Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin Mkapa, aliliweka hili vema kwa kutumia mfano wa paka.

 

Akimnukuu Kiongozi wa zamani wa China, Deng Xiaoping, Mkapa alisema yeye ni mfuasi wa kuamini kwamba cha msingi ni kuona paka anakamata panya na si paka ni wa rangi gani. Kuna wengine, wanaamini kwamba rangi ya paka ni muhimu kwenye kukamata panya. Ukisoma tamko la TEC, utaona kwamba wao wanaamini katika rangi ya paka. Lakini, hili ni jambo ambalo vyama vinatakiwa kushindana na wapiga kura kuamua. Si jambo ambalo Kanisa linatakiwa kutoa maelekezo – nikimnukuu Pengo; “wanajua nini” kuhusu paka au rangi yake?

 

Hekima ya Kidini

 

Wakati TEC ikitoa tamko lake, kulikuwa na dalili ya mgawanyiko wa kidini kuhusu jambo hili la uwekezaji kwenye bandari kupitia kampuni ya DP World kutoka Dubai. Busara ya kawaida kabisa, ilihitaji TEC kufanya tafakuri jadidi kuhusu ni wakati gani na namna gani wangeweza kutoa waraka wao.

 

Kwa mfano, wapo Waislamu wanaoamini kwamba Kanisa Katoliki limekuwa na utaratibu wa kuwa “wakali” zaidi wakati Rais anapokuwa Mwislamu kuliko Rais anapokuwa Mkristo. Kwamba Rais Samia Suluhu Hassan anakosolewa na kuandikiwa waraka kwa sababu za kidini zaidi kuliko suala lenyewe la uwekezaji.

 

Na wanatumia mifano kadhaa. Kwamba wakati wa utawala wa Mkapa – aliyekuwa Mkatoliki, Kanisa halikuwahi kutoa waraka wa kusomwa makanisani kuhusu kupinga ubinafsishaji wa viwanda, mabenki na mali nyingine za umma uliofanyika wakati wa utawala wake. Mkapa ndiye Rais aliyebinafsisha mali nyingi za umma kuliko mwingine yeyote.

 

Hata uwekezaji wa kwanza binafsi kufanywa kwenye Bandari ya Dar es Salaam kupitia kampuni ya TICTS ulifanyika wakati wa utawala wa Mkapa. Wanaoamini kuhusu ukali wa Maaskofu kwa marais Waislamu wanatoa pia mfano wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete ambapo matamko ya namna hii takribani matatu yalitolewa wakati wake. Enzi za Magufuli, waraka ulitoka mmoja – na bado Mkatoliki anayesheshimika na maarufu zaidi alikwenda hadharani kuukosoa.

 

Kwenye mazingira ya namna hii, kulikuwa na namna bora zaidi ya kuwasilisha waraka huu. Namna hiyo ilikuwa ni kushirikisha wadau wengine kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) . Na hili liliwezekana kwa sababu TEC wenyewe kwenye waraka wao wameonyesha kwamba wamewahi kukutana na Rais Samia kwa umoja wao kujadili kuhusu suala hili Juni mwaka huu.

 

Sasa, kama TEC, CCT na Bakwata walikutana na Rais kwa umoja wao na kuna mambo ya msingi walikubaliana naye – ilikuwaje waraka huo ukatoka wa dhehebu moja katika mazingira ambayo infahamika kuna kundi linaamini Wakatoliki huwa hawatendi haki kwa Rais Mwislamu? Siku chache baada ya waraka kusomwa kwenye makanisa ya Wakatoliki, Mkuu wa KKKT, Askofu Frederick Shoo, alizungumza hadharani kueleza kuwa bado wana imani kuwa Rais atatekeleza yale waliyokubaliana.

 

Inawezekana Askofu Shoo pia hakubaliani na spidi ya serikali kwenye utekelezaji wa masuala waliyokubaliana lakini pengine busara ilimfanya ajiepushe na kuweka msimamo mkali wa kanisa lake wakati huu – au akijua kwamba jambo hilo linaweza kuwagawa zaidi wananchi kuliko kupata kile wanachotarajia kukipata.

 

Bakwata – kwa upande wao, hawajasema chochote, kama ambavyo hakukuwa na taarifa iliyotolewa mara baada ya mkutano baina ya Rais Samia na wawakilishi wa TEC, KKKT na Bakwata. Labda kauli ya Bakwata kuunga mkono wakati huu ingeonekana kama kumuunga mkono Rais Mwislamu dhidi ya Kanisa, au pengine wakati sahihi wa kutoa matamko haujafika.

 

Kwa bahati nzuri, wenzetu Waislamu wana msemo mmoja maarufu kuhusu tabia ya kusubiri; Innallaha Ma Sabireen (Wamejaaliwa wale wenye Subra). Pengine subra, si jambo jepesi kwa kila mtu – na labda kwa kila dhehebu la dini.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kupitia email: ekamwaga57@gmail.com