Na Ezekiel Kamwaga
MWAKA 2023 umeshuhudia Tanzania ikipewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yaliyopangwa kufanyika mnamo mwaka 2027. Tanzania itaandaa mashindano hayo kwa ushirikiano wa pamoja kati yake na jirani zake wa Kenya na Uganda.
Hata hivyo, hakuna shaka kwamba Tanzania ndiyo hasa ilifanikisha ushindi huo. Siri ya ushindi huo iko kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia. Chini ya uongozi wake, heshima ya soka la Tanzania imepaa katika kiwango ambacho hakikufikirika hata miaka 10 tu iliyopita.
Chini ya uongozi wake, Tanzania imeshiriki AFCON mara moja – baada ya miaka 40, na mwezi ujao itashiriki kwa mara ya pili. Chini ya uongozi wake, vilabu vya soka vya Tanzania vimepata udhamini mkubwa kiasi kwamba sasa vinashindana na vigogo wa asili wa bara hili kwenye kuwania wachezaji na uwanjani kwenye mashindano.
Yanga mwaka huu ilishiriki fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na inaonekana ni suala la muda tu kabla ya klabu ya Tanzania haijatwaa taji la ubingwa wa Afrika. Uongozi wa mhasibu huyu kitaaluma umeshuhudia Tanzania ikiwa na viwanja vizuri vya soka na timu nzuri za taifa za vijana na wanawake.
Kwa sababu ya kazi yake inayoonekana, sasa Karia ametengeneza mtandao mzuri wa marafiki katika kabumbu ndani na nje ya bara la Afrika. Sasa si ajabu kuona viongozi wa kiwango cha Rais wa FIFA, Gianni Infantino, wakija Tanzania kwa ajili ya matukio ya kikanda na mengine kwa sababu ya heshima ambayo kiongozi huyu ameijenga.
Kama unazungumzia mafanikio ya Tanzania kimichezo, kupata AFCON kwa 2027 ni mafanikio makubwa na uwepo wa Wallace Karia umefanikisha hilo.