Katika hili, Rais asiyumbe

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

MWAKA 1978, Rais Julius Nyerere, alilazimika kufanya uamuzi mzito wa kuiingiza Tanzania vitani dhidi ya Uganda. Majeshi ya Nduli Idi Amin yalikuwa yameivamia ardhi ya Tanzania na kama Amiri Jeshi Mkuu, Baba wa Taifa hakuwa na namna zaidi ya kupeleka majeshi yetu yaende vitani akijua kuna watu wanakwenda kupoteza maisha yao kwa sababu hiyo. Huo ndiyo mzigo wa uongozi.

 

Nimeisoma na kusikiliza mara kadhaa hotuba yake ya kutangaza vita hiyo aliyoitoa Novemba 2, 1978 na kumbukumbu ya kudumu ya vita ile inahusu maneno haya maarufu; “Uwezo wa Kumpiga Tunao, Sababu ya Kumpiga Tunayo na Nia ya Kumpiga Tunayo.” Hotuba ile ilikuwa na maneno takribani 910, lakini watu wanakumbuka zaidi hiyo nukuu niliyoichukua.

 

Ni sawa na hotuba ya Juni 4, mwaka 1940, iliyotolewa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, Winston Churchill, alipohutubia raia wake na kuwaambia kwamba taifa lao kamwe halitafyata mkia kwenye vita hiyo. Hotuba ile inakumbukwa zaidi kwa maneno; “We shall fight on the beaches, we shall fight on the landing grounds, we shall fight in the fields and in the streets, we shall fight in the hills; we shall never surrender.”

 

Nimetumia nukuu hizi muhimu za viongozi wawili maarufu duniani walizotumia wakati wa mojawapo ya nyakati ngumu kwao kuweka msingi wa jambo moja; kwamba kuliko kitu kingine chochote, wananchi wanatarajia jambo moja kubwa zaidi kutoka kwa viongozi wao; Uongozi (Leadership). Kama kiongozi wa juu wa nchi ataonyesha uthabiti na kutotetereka katika jambo, ni rahisi kwa wananchi wake kumwamini.

 

Huo ndiyo msimamo wangu kuhusu suala hili la uwekezaji unaotarajiwa kufanyika katika Bandari ya Dar es Salaam na kampuni ya DP World kutoka Dubai, Falme za Kiarabu (UAE). Wanachotaka wananchi, pengine kuliko jambo lingine lolote, ni uongozi na sura ya uthabiti kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwamba jambo linalokwenda kufanyika ni la msingi na linabeba maslahi ya taifa.

 

Ninafahamu kwamba kwa sababu tofauti, kuna kelele nyingi za kupinga uwekezaji huo. Wapo wanaopiga kelele kwa kutoa mawazo ambayo wanaona yakifuatwa na serikali, nchi itafaidika zaidi na suala hilo. Wapo wanaopiga kelele kwa sababu uwekezaji huo utawanyima fursa za kiuchumi walizonazo sasa kwa sababu ya mapungufu yaliyopo. Kuna kundi la tatu la watu wanaopiga kelele kwa sababu hilo linawasaidia kisiasa kuonyesha kwamba serikali iliyo madarakani ina mapungufu na wao ndiyo mbadala sahihi.

 

Ninafahamu pia kwamba hata wakati wa Vita ya Kagera, kuna waliokuwa hawaungi mkono Tanzania kwenda vitani. Nakumbuka mahojiano niliyowahi kufanya na Mnadhimu wa zamani wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hayati Kanali Ameen Kashmiri, aliyenieleza kwamba anadhani vita ile haikuwa na maana na ndiyo chanzo cha matatizo makubwa ya kiuchumi yaliyolikumba taifa letu baada ya vita.

 

Taarifa zilizotolewa baadaye na taasisi za kijasusi za Uingereza, zinaeleza pia kwamba walikuwepo Waingereza wenye ushawishi mkubwa waliokuwa wakimshawishi Churchill aachane na msimamo wake mkali na afanye makubaliano na Adolf Hitler wa Ujerumani kuiepusha nchi yake na adha ya vita. Kwa vyovyote vile, huo pia haukuwa ushauri mbaya lakini Churchill – kama ilivyokuwa kwa Nyerere baadaye, alibaki na msimamo wake hadi ushindi ulipopatikana upande wake.

 

Wakati naandika makala haya, sijaona dalili za Rais Samia kuyumba katika dhamira yake ya kutaka uwekezaji ufanyike katika Bandari ya Dar es Salaam. Hata hivyo, kwa wiki walau tatu za kwanza tangu suala hili lijadiliwe na Mapatano ya Tanzania na Dubai kuridhiwa na Bunge, kulikuwa na hali ya suitafahamu na kwa hakika sauti za kupinga zilikuwa kubwa zaidi huku serikali ikionekana kama haina hamu wala ari ya kupigania suala hilo.

 

Angalau katika wiki za karibuni, Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeanza kufanya jitihada kubwa zaidi za kueleza, kufafanua na kutetea uwekezaji huo. Angalau wananchi wanaanza kuona ari na nishati – walau kwa kuchelewa, inayoonyesha kwamba kimsingi uwekezaji huo utakuwa na manufaa kwa taifa letu.

 

Ni muhimu sana kufahamu kuhusu saikolojia ya Watanzania linapokuja suala la uwekezaji hasa kutoka kwa mataifa ya kigeni. Kwa sababu ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyotawala kwa takribani miongo mitatu ya kwanza ya Uhuru wetu, watu wetu wengi wamekuwa na dhana hasi kuhusu masuala ya uwekezaji. Lakini, ni ukweli pia kwamba hatuna historia nzuri sana katika eneo la ubinafsishaji na uwekezaji. Msemo wa Kiswahili wa aliyegongwa na nyoka hushtuka akiguswa na majani unaisibu tabia hii.

 

Kama ripoti tofauti za kitafiti zinaonyesha kwamba Bandari yetu inaweza kutusaidia kuongeza mapato yetu kufikia asilimia 67 kutoka 37 za sasa, ni muhimu uamuzi ukachukuliwa wa kutufanya tufike hapo panapowezekana – walau kukaribia au kuzidi kabisa. Kwangu mimi, tatizo kubwa zaidi ni kutofanya uamuzi wa kuboresha hali na si kuacha hali iliyopo iendelee hivyohivyo kwa sababu ya kuogopa lawama.

 

Faida mojawapo ya kuongozwa kwa misingi ya kidemokrasia ni kwamba upo wakati wa kufanya marekebisho. Serikali zilizochaguliwa na watu zina uwezo wa kujirekebisha zenyewe na wakati mwingine kurekebishwa kwa kushindwa kwenye uchaguzi kutokana na makosa zilizofanya wakati zikitawala. Kama Rais Samia na Serikali yake ya CCM wanaamini kwamba uwekezaji huu wa DP World utaleta mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo, hakuna sababu ya kuhofia au kusikiliza wale wanaopinga kwa sababu kazi yao ndiyo hiyo.

 

Nionavyo mimi, kama Rais Samia akiyumba na kufanya kitu kitakachoonyesha yeye kukosa uthabiti au kujiamini kwenye hili, muda wake wote wa Urais uliobakia utakuwa ni wa wasiwasi, shaka na kutoaminika. Kama kuna watu ambao tangu mwanzo walikuwa wanataka aonekane hafai kwa nafasi hiyo, watakuwa wamepata jambo la kuithibitisha hoja yao.

 

Mwanasayansi ya siasa, Karl Popper, alipata kueleza kuhusu umuhimu wa kuhakikisha jamii nzima inabadilika kwa kuchukua hatua ndogo na zenye manufaa. Kama uwekezaji huu wa DP World ukifanikiwa kama Rais Samia anavyoamini, Watanzania watamwamini zaidi pale atakapokuja na mradi mwingine wenye ukubwa wa aina hii. Ni kwa mafanikio madogo madogo ya uwekezaji na ubinafsishaji wa hapa na pale, ndipo saikolojia hii ya Watanzania kuhusu wageni na uwekezaji itakapoanza kubadilika taratibu.

 

Na kama uwekezaji wenyewe hautafaa, Rais Samia, nikimnukuu Churchill kutoka katika hotuba yake nyingine, itabidi ajiandae na majibu ya kwa nini jambo hili halikufanikiwa na lipi litakuwa funzo kubwa tulilolipata kupitia uwekezaji huo. Labda wananchi watamwelewa. Na kama hawatamwelewa, watampa nafasi mtu mwingine watakayeona ataweza kubeba matamanio yao. Huo ndiyo utamu wa mfumo wa kidemokrasia.

 

Lakini, hadi wakati huo utakapofika, jambo moja Rais Samia Suluhu Hassan hatakiwi kulifanya sasa ni kuonyesha udhaifu au uwezekano wa yeye kubadili mawazo. Akifanya hivyo, atakuwa ameweka rehani muda wake uliobakia wa Urais.

 

Kwa sasa, anatakiwa kubaki thabiti kwenye msimamo wake na kutuonyesha uongozi imara kwenye jambo hili.

 

Mwisho