Shajara yangu inanieleza kuwa nilikuwa na mazungumzo na Prof. Haroub Othman na akanieleza kuwa Dr. John Sivalon alikuwa anataka kufanya semina kuhusu ‘’Dini na Siasa’’ kwa kuwa Uchaguzi Mkuu utatawaliwa na udini. Semina hii haikuweza kufanyika kwa kuwa wahisani hawakupendezewa nayo lakini walikuwa tayari kutoa fedha kiandikwe kitabu.
Prof. Haroub Othman akaniambia kuwa yeye amewaomba Dr. Khalfan na Dr. Sivalon wote kutoka Chuo Kikuu Cha Dar-es-Salaam kuratibu mradi huo na mimi niandike moja ya sura katika kitabu hicho.
Haya ndiyo niliyoandika tarehe 1 Machi.
Machi 2 sentensi ya kwanza niliyoandika ni Adam Lusekelo akitangaza kupitia BBC Idhaa ya Kiswahili kuwa Augustino Mrema amejitoa CCM. Machi 3 Rais Mwinyi akizungumza katika Eid Baraza iliyoandaliwa na BAKWATA Ukumbi wa Diamond Jubilee aliwaonya Waislam kutosababisha kuvunjika kwa amani. Mwinyi, kwa bahati mbaya sana, kwa kutoijua historia ya uhuru wa Tanganyika alidhani kuwa kwa kuwafokea Waislamu yeye atapendeza na kupendwa.
Haikuwa hivyo.
Augustino Mrema kwa mambo aliyokuwa akifanya alionekana ana nguvu kumshinda Rais Mwinyi. Siku tatu kabla ya Mrema hajajitoa CCM, John Bwire mmoja wa wahariri wa Rai akihojiwa na BBC Idhaa ya Kiswahili alisema kuwa Mrema alikuwa kipenzi cha wananchi wa mji huo na wakimzunguka kwa mapenzi makubwa kila alipojitokeza hadharani.
Haya hayakuwa bure kulikuwa na ujumbe maalum katika yote haya na wenye macho waliona na wenye masikio walisikia. Katika Sala ya Ijumaa Msikiti wa Mtoro siku hiyo hiyo Sheikh Khalifa Khamis alimshambulia sana Augustino Mrema. Kila kukicha asubuhi kuna jipya.
Machi 4, gazeti la Nipashe likaandika katika ukurasa wa mbele kuwa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Sheikh Hemed bin Jumaa amewaonya Waislam wasiwapigie kura Waislam wenzao katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba.
Hii ndiyo hali ya siasa iliyokuwapo wakati nilipokutana na wazee wangu wale nyumbani kwa Balozi Abbas Sykes wakaniuliza Waislamu wana lipi katika uchaguzi unaokuja mwezi October 1995.
Mazungumzo yetu yalikuwa marefu na nakumbuka Mzee Rashaad mbele yao alikuwa akiniambia, “Mohamed hapa uko ndani ya kambi ya adui haya yote unayowaeleza yatafika Makao Makuu Dodoma.” Si kama sikuyajua hayo lakini nilitaka kufikisha ujumbe.
Nilipomaliza kumsoma Dk. Salim nikajiuliza kwa nini ilikuwa lazima ielezwe au ienezwe na Rai kuwa Salim Ahmed Salim si mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM?
Je, hii ilikuwa moja ya njia ya kumsafishia njia Benjamin Mkapa?
Ieleweke kuwa Mkapa na Jenerali Ulimwengu walipata kuwa marafiki wakubwa.
Nikajiuliza tena kuna uwezekano kuwa yale ambayo niliwaeleza wazee wangu siku ile pale nyumbani kwa Balozi Sykes ndiyo huu ujumbe uliotoka kwa Balozi Khamis Suedi Genava kwenda kwa Dk. Salim Ahmed Salim Addis Ababa?
Salim hakusema ule ujumbe ulikuwa wa nini. Kilichobakia ni dhana tu. Labda ilikuwa kuhusu Uchaguzi Mkuu. Kavazi la Dk. Salim lina mambo hapana mchezo.
Allah Ndiye Mjuzi.