KC Dorothy Semu: Kupanda, sababu na changamoto  

 

Ezekiel Kamwaga

 

MIAKA michache iliyopita, Dorothy Semu – wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, alianza kupokea simu; za kushawishi na kumtisha, kutaka akihame chama chake na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakati wa wimbi kubwa lililokuja kufahamika baadaye kama “kuunga mkono juhudi”.

 

Waliokuwa wakiwasiliana naye, walimuahidi vyeo na mambo mengine. Wakati huo, Dorothy – sasa Kiongozi wa Chama (KC) cha ACT Wazalendo, alikuwa ameacha ajira ya utaalamu aliyosomea ya tiba ya viungo vya mwili (physiotherapy) na kujiingiza kindakindaki katika siasa. Ahadi ya vyeo, mamlaka na fedha, havikumbadilisha mawazo wala akili yake; katika mazingira ambayo walioonekana wagumu, mahiri na wazoefu zaidi yake walitepeta.

 

Wakati Dorothy Semu alipotangazwa kuwa KC wa ACT Wazalendo akichukua nafasi ya Zitto Kabwe, sehemu kubwa ya maswali yaliyoelekezwa kwangu yalikuwa yanataka jibu moja; Kwa nini Dorothy? Kwa nini kwa maana ya kumfahamu zaidi na pia kueleza ilikuwaje wanachama wa chama hicho wakampa madaraka ya kubeba mikoba hiyo.

 

Mfano nilioanza nao awali unaeleza vitu viwili katika hoja moja – kwanza si mtu rahisi kushawishiwa kubadili mawazo au ndoto zake na pili, na la muhimu zaidi katika mazingira haya, ni ukweli kuwa huyu ni aina ya wanasiasa wa kizazi cha sasa walioamua kuacha kazi na uhakika wa maisha kwa ajili ya kujiunga katika safari ambayo haina uhakika wa kipato wala pensheni.

 

Labda tuanze na jibu la swali la kwanza, kwa nini Dorothy Semu?

 

Mtu wa chama

 

Tangu chama cha ACT Wazalendo kianzishwe takribani miaka 10 iliyopita, Dorothy ni miongoni mwa viongozi wa chama hicho unaoweza kusema wanakijua ndani nje. Ni mtu ambaye ameanza kufanya kazi ndani ya chama katika ngazi kuanzia kwenye Kurugenzi za Sera na Fedha, Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti na sasa KC.

 

Kama ACT ilikuwa inatafuta KC ambaye anakijua chama kilivyo, misingi yake na changamoto zake, ni wachache wana wasifu, muda na uelewa wa kutosha wa chama kumzidi KC huyu mpya. Kama chama kilikuwa kinahitaji mwendelezo wa hali halisi iliyopo sasa, ni wazi Dorothy alikuwa mbele kidogo ya watu wengine waliokuwa na nia ya kutaka nafasi hiyo.

 

Katika vyama vya siasa – hasa vile vya upinzani, tatizo la kuendeleza kinachojengwa kupitia kwa kiongozi mpya baada ya kuondoka wa zamani ni kubwa. Na hili huwa ni tatizo zaidi kwa sababu mara nyingi ubadilishanaji wa madaraka huwa si wa hiyari kama ilivyotokea kati ya Zitto na Semu na ndiyo sababu kinachoendelea kwa ACT sasa kitakuwa darasa zuri – endapo litaenda vizuri au vibaya.

 

Kwa kumchagua Dorothy kuwa KC, ACT Wazalendo imeamua kufuata njia ya kurithishana madaraka ambayo si ya kawaida – si Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla, lakini ni kamari thabiti (calculated risk) kwa sababu walau mtu aliyechukua nafasi anakifahamu chama na wanachama hawana wasiwasi naye.

 

Ingekuwa hatari zaidi kwa ACT Wazalendo endapo ingemchagua kuwa KC mtu ambaye si mtu wa ndani na madhubuti wa chama na hajawahi kujaribiwa na mtihani wowote wa kisiasa kama ilivyomtokea Dorothy huko nyuma. Kama ingekuwa naandika kwa lugha ya Kiingereza, ningesema KC mpya ni “tried and tested”.

 

Hali halisi ya ACT kwa sasa

 

ACT ya sasa si ile iliyokuwepo kabla ya tukio lile la Shusha Tanga, Pandisha Tanga ambapo karibu viongozi wote wa juu wa Chama cha Wananchi (CUF) akiwemo marehemu Seif Shariff Hamad, walitangaza kukihama chama chao na kuhamia ACT Wazalendo.

 

Historia ya namna ambavyo Maalim Seif na akina Juma Duni Haji, Ismail Jussa na wengine walihama CUF na kuhamia ACT Wazalendo, bado haijaandikwa na kuelezwa vya kutosha. Lakini kuna mambo mawili matatu ambayo walau yanafahamika.

 

Kwa mfano, inajulikana kwamba wakati akina Maalim Seif wakihamia ACT, Dorothy ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama walichohamia. Ninafahamu, walau kidogo, safari za mara kwa mara, alizokuwa akifanya kwenda na kurudi Zbar – kabla ya Shusha Tanga, na baada ya kukamilika kwa tukio hilo.

 

Kwa waandishi wa habari tuliokuwa tunafuatilia tukio hilo kwa karibu, inajulikana kwamba siku za awali hazikuwa rahisi. Wapo wana CUF waliokuwa wakiamini kwamba wangekuwa wakubwa zaidi endapo wangeungana na CHADEMA kuliko ACT. Wapo waliokuwa wakiamini – upande wa Bara, kwamba chama chao sasa kitamezwa na “Wazanzibari”. Ulikuwa ni mchanyato wa kisiasa iliobidi Dorothy na viongozi wengine wa chama hicho waupitie na kuuvuka ili hatimaye chama kisimame.

 

Uchaguzi wa Dorothy kuwa KC unamaanisha chama kimemchagua mtu ambaye anajua siasa za ndani za chama hicho, hofu na mashaka ya pande zote na kwa nini Zitto na Maalim Seif walichukua uamuzi mzito kuunganisha chama hicho wakati mwingine kinyume cha matakwa ya baadhi ya watu wao wa karibu.

 

Hakutakuwa na upande au watu ambao kwa sababu yoyote wataogopa kumwambia Dorothy kuhusu kinachoendelea au hofu na mashaka yao. Ana faida ya kuwa anawajua wanachama wake, anajua hoja kinzani za ndani ya chama na majibu yake, kama ambavyo yamekuwa yakitolewa katika vikao vya siri na hadharani alivyowahi kushiriki.

 

 

Mwanasiasa Mtendaji

 

Mtangulizi wa Dorothy, Zitto Kabwe, ni mwanasiasa wa kuzaliwa. Tangu aingie kwenye balehe, siasa na harakati zimekuwa sehemu ya maisha yake. Dorothy, kwa upande mwingine, ni mwanataalamu ya tiba ambaye aliingia kwenye siasa baadaye kidogo.

 

Katika masuala ambayo Zitto angeyafanya kwa sababu ya hisia pekee, Dorothy – kwa sababu ya usuli wake katika sayansi, angeweza kuweka pozi kidogo na kufikiri kuona kama mambo yataoana au yatafikia katika hitimisho lisilo na madhara kwa chama au taasisi.

 

Kama Zitto ni Silvio Berlusconi, Dorothy ni Mario Draghi. Kama Zitto ni Helmut Kohl, Dorothy ni Angela Merkel. Katika utelezaji wao wa majukumu, Zitto ni mwanasiasa kwanza halafu mtendaji baadaye lakini Semu ni kinyume chake.

 

Zitto alikuwa KC wa kwanza wa ACT Wazalendo. Uchaguzi wa Dorothy umekipa chama hicho fursa ya kuwa na mtu tofauti ambaye anaweza kuja na staili tofauti ya uongozi tofauti na mtangulizi wake. Wakati utakapofika wa kumaliza muda wake, chama hicho kitajua ni mtu wa aina gani kitamhitaji kwenda mbele zaidi.

 

Kivuli cha Zitto

 

Mtangulizi wa Dorothy alikuwa na maisha marefu na yenye mivutano kisiasa kuliko KC mpya. Kwa mfano, ilikuwa rahisi kwa hoja au suala kukataliwa na baadhi ya vyama kwa sababu ya migogoro au uhasama wa kisiasa uliopo baina ya Zitto na CHADEMA kwa mfano.

 

Katika zama ambazo ushindi katika uchaguzi unaweza kusababishwa na ushirikiano wa vyama, wakati mwingine kuwa na Zitto kama alama ya chama kulikuwa ni kikwazo. Kwa bahati nzuri, Dorothy hajawahi kuwa CHADEMA na hakuna historia yoyote ya uhasama baina yake na chama hicho.

 

Kwa vyovyote vile, kuchaguliwa kwa Dorothy kuwa KC kunaweza kufungua milango ya ushirikiano ambayo pengine ilikuwa imefungwa kwa Zitto. Wakati mwingine hoja ilikuwa sahihi, wakati sahihi na mahali sahihi lakini ilikuwa inaweza kukataliwa au kupingwa kwa sababu ya mtoa ujumbe. Labda ACT imeona huu unaweza kuwa wakati sahihi kufungua milango iliyofungwa kwa kuwa na mtu asiye na historia mbaya ya nyuma na wengine.

 

 

Changamoto kwa KC mpya

 

Changamoto ya kwanza ya Dorothy ni kwamba anarithi nafasi ya mwanasiasa na kiongozi wa kipekee. Kumrithi Zitto kwenye nafasi yoyote ya uongozi ni “viatu vikubwa” kwa yeyote anayetaka kuvivaa. Iwe kuongoza Wanafunzi wa Chuo Kikuu, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na kwingine kokote.

 

Ni changamoto ambayo wanasiasa kama Merkel walikutana nayo kwa kushika madaraka baada ya viongozi wa aina ya Kohl. Naweza kusema kwamba Zitto ni kiongozi wa kipekee miongoni mwa viongozi wa upinzani kutokana na uwezo wa kuibua hoja mpya, kujenga hoja na kufuatilia chanzo na suluhu za matatizo lukuki yanayowakabili Watanzania.

 

Bahato nzuri Dorothy ana vitendea kazi mkononi vya kumsaidia kupunguza nakisi ya kiuongozi kati yake na mtangulizi wake na pengine kupiga hatua zaidi. Kwa mfano, wakati ACT ikianza kupata hati safi za ukaguzi kutoka kwa CAG, ni Dorothy ndiye – kama Ofisa Masuuli wa Chama (Katibu Mkuu), aliyeweka misingi ya kiutendaji kufika hapo.

 

Kwa sababu hiyo, hakutakuwa na sababu ya ACT kama chama kuanza kupata hati chafu za ukaguzi wa CAG – ikizingatiwa ripoti za ukaguzi ni eneo muhimu kisiasa kwa ACT, kwa sababu KC wa sasa ndiye mtu aliyesimamisha nguzo zilizokifanya chama hicho kupata hati safi.

 

Jambo la muhimu kwa Dorothy ni kutumia katika maeneo ya na majukwaa ya kimkakati, watu wanaopenda na kuinjoi kufanya siasa. Kwa sababu ya usuli wake kama mwanasayansi, anaweza kuibakisha ACT kama chama cha hoja kwa sababu hilo tayari amelisimamia.

 

Jambo la kwanza ambalo ningetamani Dorothy alitilie maanani ni kuonyesha kwa vitendo kwamba yeye si “KC nusu”. Ni muhimu sana kwake kuonyesha nguvu na uimara wake ndani na nje ya chama. Ninasema hivi nikijua wapo watakaojaribu kuona kama “kibiriti kimejaa” na kuonyesha kwake udhaifu kwa aina yoyote, kunaweza kumletea shida kwenda mbele.

 

Kuanzia kwenye kuunda Baraza Kivuli la Mawaziri na majukumu yake mengine, Dorothy anapaswa kuwaonyesha wanachama wake, na Watanzania kwa ujumla, kwamba yeye ndiye KC wa ACT Wazalendo. Na hahitaji kuonyesha hilo kama mwanasiasa, bali kama mtendaji.

 

Dorothy ni mama mwenye watoto watatu, ameolewa na umri wake sasa ni miaka 48.