Kipi kimeipa China ukubwa wake wa sasa?

 

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

WIKI iliyopita nilikuwa nchini China kwenye ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, kufuatia mwaliko wa mwenzake wa China, Wang Yi. Ilisadifu kwamba ziara hiyo iliendana na maadhimisho ya miaka 60 ya nchi hizi mbili lakini pia miaka 75 ya uhusiano baina ya China na Russia.

 

January na Putin walipishana kwa takribani siku mbili – Putin akiandaliwa dhifa na mwenyeji wake, Rais Xi Jin Ping huku January akiandaliwa na mwenyeji wake Wang – na katika matukio yote mawili; ujumbe ulikuwa ni namna ya kutengeneza mfumo mpya wa uendeshaji wa dunia unaojali usawa, haki na maendeleo kwa wote.

 

Na kuna jambo la muhimu kulitaja hapa. Kwamba mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2013, Rais Xi alitembelea Russia na Tanzania kama nchi zake za kwanza. Putin pia alikuwa China ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu ashinde uchaguzi mkuu wa taifa wiki chache zilizopita.

 

Inawezekana China ina marafiki wengine duniani, lakini kuna kila sababu ya kuamini kwamba Tanzania na Russia zina upekee kwa taifa hilo. Itahitaji Makala nzima kueleza kwa nini naamini hivi. Hilo naliweza kulifanya siku nyingine lakini leo natamani kuandika kuhusu swali ambalo nilijiuliza sana kabla sijafika China.

Kwamba imekuwaje China ambayo miongo saba tu iliyopita ilikuwa imetoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe iliyofuatia kukaliwa na Japan na Vita ya Kasumba (Opium War), leo liwe taifa Pato la Taifa la kiasi cha dola trilioni 18? Nini kimeifanya China kuwa hapa ilipo leo?

 

Kwa wiki moja niliyokaa China – na kwa kusoma na kutazama vitu mbalimbali katika takribani miaka 10 iliyopita, nimepata walau pa kuanzia kwenye kujibu swali hili. Na ilikuwa vema kujionea kwa macho yangu yale ambayo pengine ningeandika ingekuwa ni maneno matupu. Kuona ni kuamini.

 

Uongozi imara

 

Kuilewa China ni kuulewa mfumo wake wa uongozi. Tangu enzi za wafalme, Wachina wamekuwa na utamaduni wa kuwa na watu wao bora serikalini. Katika zama za Kifalme, kulikuwa na mitihani kabisa ambayo mtu alitakiwa kufanya kuingia serikalini.

 

Hadi leo, China inahakikisha viongozi wake wanaopewa madaraka ni watu wenye uwezo usio wa kawaida. Rais Xi alipewa nafasi ya kuongoza China kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata wakati akiongoza jimbo la Fujian.

 

Kwa mujibu wa takwimu za sensa, Fujian inakadiriwa kuwa na watu takribani milioni 40 hivi sasa. Hii ni idadi kubwa ya watu kuliko nchi nyingi duniani. Kwa hiyo, kipimo kilichompa urais ni mafanikio ya kupambana na umasikini, rushwa, ubunifu na uimara wakati akiongoza Fujian.

Ukiwasoma Henry Kissinger na Lee Kuan Yew kwenye vitabu vyao, utaona wanasema aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa China, Chou En Lai ni mtu mahiri zaidi waliyewahi kukutana naye. Nikiwa China, nilimwona kwa karibu Wang Yi na kwa kuangalia wasifu wake, maneno yake na namna anavyosikiliza wanaozungumza, unaona maarifa makubwa aliyonayo.

 

Kitu kikubwa zaidi nilichojifunza kwenye ziara hii – na kwa sababu ya kukutana na watu na kuzungumza nao baada ya saa za kazi, ni kwamba hakuna uwezekano wa mtu mwenye rekodi mbaya, asiye mweledi na mwenye maarifa kupewa nafasi ya kuongoza China.

 

Nilikutana na kijana mmoja mdogo, Luo Yingzhan, ambaye ni ofisa kwenye wizara ya mambo ya nje ya China. Tulikuwa naye muda wote wa safari. Alikuwa hazungumzi bila ya kuulizwa lakini katika umri wake mdogo wa chini ya miaka 35, anazungumza Kichina, Kiingereza lakini amebobea katika lugha ya Kifaransa.

 

Yeye ndiye mtu aliyenipa darasa la kutosha kuhusu China kuanzia kwenye Nyakati za Vita (Warring Period) mpaka wakati utawala wa Qin unafikia tamati. Kwa kila swali, alikuwa ananichorea ramani ya China kwenye karatasi – iwe kuanzia ilipopita The Long March au ulipojengwa Ukuta Mkuu wa China. Sina shaka kwamba kijana huyu atakuja kuwa mtu mkubwa kwenye uga wa diplomasia wa taifa lake.

 

Na kuna maelfu ya akina Luo Yingzhan ndani ya China. Wazazi wao na jamii yao inajua kwamba ili hatimaye uwe kiongozi wao, unahitaji kupitia hatua nyingi za kupikwa na kupikika. Kama uongozi uko imara, ni lazima nchi itapiga hatua.

 

Watu wanataka nini?

 

China inaongozwa na Chama cha Kikomunisti (CPC) tangu Mapinduzi ya mwaka 1949. Baada ya mapinduzi, CPC ilisema kwamba malengo yake makubwa ni mawili tu; Kuwapa Wachina maisha bora na kurejesha heshima ya China duniani.

 

Kwenye kuwapa Wachina maisha bora kanuni kuu inahusu kuwapa watu kile wanachohitaji ili waendelee. Hakuna mfano mzuri wa kueleza hili kuliko hatua ya Rais Xi mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2013 ambako aliagiza makada zaidi ya 200,000 wa chama waende vijijini kuuliza watu wa huko wanataka nini ili CPC ijipange kutatua changamoto hizo.

 

Tatizo kubwa la nchi zetu nyingi ni kwamba mara nyingi mipango ya maendeleo huwa inapangwa kuanzia juu kwenda chini na wakati mwingine mipango yetu huwa inapangwa na wageni.

 

Nakumbuka sana kuhusu hadithi moja ambayo mwanazuoni Profesa Issa Shivji, amewahi kusimulia kuhusu mipango yetu. Alisema aliwahi kualikwa kuchangia mawazo yake kuhusu Mpango wa Vision 2025 lakini alipoingia kwenye ukumbi, alishangaa kukuta watu kutoka Ulaya, Marekani na mabara mengine wakiwa sehemu ya watungaji wa mpango huo.

Nini hasara ya mipango ya namna hii? Hasara kubwa ni kuwa wakati mwingine wananchi wanapelekewa mradi ambao ingawa gharama zake ni kubwa, halikuwa hitaji la wale waliopaswa kusaidiwa na mradi huo. Yaani kama watu wanahitaji hospitali, wanapelekewa maji, wanahitaji soko la mazao, wanajengewa zahanati nk.

 

Kwa kuangalia nini wananchi wanataka, China imeweza kupunguza umasikini kwa watu wake takribani miaka 10 kabla ya muda uliokuwa umewekwa na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia malengo ya milenia. Lakini tangu ianze mabadiliko ya uchumi, mamilioni ya Wachina wameondolewa kwenye umasikini.

 

Beijing ndiyo mji pekee mkubwa miongoni mwa majiji makubwa ambayo nimewahi kufika ambako sikukutana hata na mtu mmoja aliyelala mtaani (homeless). Inawezekana katika majiji mengine wapo lakini si kawaida kuona nilichokiona China kwenye majiji makuu.

 

Kama Tanzania inataka kuiga kitu, mojawapo ya mambo tunayoweza kuiga ni kuuliza wananchi wetu wanataka nini ili wakwamuliwe kutoka walipo. Wakati mwingine washauri wa sera ni watu wanaoishi mbali kabisa na uhalisia wanaokutana nao wananchi wa kawaida.

 

Tukiwa China ndiyo nilikumbuka tukio moja lililotokea miaka michache hapa nchini. Kiongozi mmoja wa serikali alilalamika kwamba watu wa kabila la wafugaji wamehama Kijiji wakati serikali imewajengea shule ili waishi pale. Nikajiuliza, hao wafugaji waliulizwa kama wanataka shule au shida yao ilikuwa ni malisho ya mifugo. Kwamba kama wangepewa mradi wa uhakika wa malisho, pengine shule wangejenga wenyewe.

 

Falsafa moja

 

Awali, katika ratiba rasmi ya Waziri Makamba kutembelea China, hakukuwepo na nafasi ya kutembelea Chuo cha Kikada cha CCP kilichopo Beijing. Lakini kwa sababu za kutaka kujifunza, Waziri huyo alibananisha ratiba yake na kupata fursa ya kutembelea chuo hicho.

 

Chuo hicho kina umri wa takribani miaka 100 na ndiyo tanuru la ujenzi wa kifikra wa viongozi wa China. Chuo tulichotembelea ni miongoni mwa vyuo takribani 2000 vilivyoko nchini kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa Chuo hicho, Chen Xi.

 

Kujua umuhimu wa chuo hicho ni kufahamu kwamba miongoni mwa wakuu waliowahi kupita hapo ni Mwenyekiti Mao Zedong n ahata Rais Xi aliwahi kuongoza chuo hicho kati yam waka 2007 hadi 2013. Huwezi kuwa mkurugenzi wa shirika, meya, Waziri au kiongozi yeyote wa maana ndani ya China kama hujapikwa kwenye vyuo hivi.

 

Maana yake ni kwamba viongozi wote wa China wanajua falsafa yao, mwongozo wao na matarajio yao. Hii ni namna pekee ya kuhakikisha viongozi au taifa kwa ujumla haliendi nje ya mstari uliokubalika. Tanzania tumeanzisha pia chuo cha namna hiyo kilichopo Kibaha lakini safari bado ni ndefu kufikia uwekezaji na heshima ya hivyo vya China.

Huko nyuma Tanzania ilikuwa ikifundisha viongozi wake lakini sasa naamini tumeingia katika zama ambazo tunaamini mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi. Labda kwa sababu ana followers wengi mitandaoni, ana sura nzuri au anachekesha na kufurahisha watu wakati anazungumza.

 

Funzo nililopata China ni kuwa uongozi si kitu lelemama. Ni wajibu na majukumu mazito yanayohitaji watu waliolelewa vema, walio kwenye mstari mmoja na wanaojua kuhusu mahitaji ya watu wao na taifa lao. Katika hotuba yake ya shukurani, Makamba alisema jambo la kufunza viongozi ni la muhimu hasa kwa mataifa yaliyo katika hali ilipo Tanzania hivi sasa.

 

Soko la kwanza ni la ndani

 

Sijui ni mara ngapi nimesikia msemo huu lakini inasemwa kwamba nchi za Afrika zinazalisha zisichokula na zinakula zisichozalisha. China ina watu zaidi ya bilioni 1.4 na wameamua kwamba wateja wao wa kwanza ni wa ndani.

 

Nilifika kiwanda cha Huawei na nikaona takwimu zilizoonyesha kwamba zaidi ya nusu ya mauzo yake kidunia ni China. Hali ilikuwa hivyo karibu katika sehemu nyingine nilizotembelea. Kwa kuzalisha bidhaa za kutosheleza soko la ndani, uchumi wa China unafanya vizuri.

 

Tanzania tuna watu takribani milioni 60. Idadi ya watu wa China imetuacha mbali sana. Lakini bado watu milioni 60 ni wengi. Ukizungumza na wafanyabiashara, watakuambia ziko fursa nyingine katika soko pana zaidi kupitia eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) lenye watu zaidi ya milioni 200.

 

Ni kwa kiasi gani tumefanya jitihada za kuzalisha kwa wingi na kuhakikisha watumiaji wake ni wa soko la ndani kabla ya kufikiria AGOA na masoko mengine? Soko la ndani likikua, uchumi nao utakua. Lakini kama hatuwezi kukidhi mahitaji ya soko la ndani, tutawezaje kukidhi mahitaji ya soko la China, India au Marekani?

 

Maono ya Kitaifa

 

Tukiwa China, nilipata fursa ya kuzungumza na Waziri Makamba na tulijadiliana kwa kina kuhusu suala la viongozi kutoa maono na kuzalisha fikra zitakazofanya taifa lisonge mbele.

 

Ni Deng Xiaoping ndiye aliyeamua China ijenge mji wa Shenzhen ili ushindane na Hong Kong kwa uzuri, fursa na uzalishaji. Kwenye safari hii, nimepata fursa ya kufika kwenye miji ya Shenzhen na Hong Kong na kwa maoni yangu, mji wa Deng ni mzuri kuliko Hong Kong.

 

Nchi ni muhimu ikawa na maono ya kitaifa yatakayowafanya watu wake kufanya hata yale ambayo awali yalikuwa hayawezekani. Kupitia Azimio la Arusha, Tanzania iliweka malengo ya aina ya taifa ambalo waasisi wetu walitaka kulijenga.

 

Ni muhimu kwa viongozi wetu kuendelea kuwaza na kuwazua kuhusu aina ya nchi ambayo tunaitaka na namna gani tutafika huko wanakotaka twende. Ni jukumu la viongozi kufanya Watanzania wote waote na wawe tayari kutoka jasho linalotakiwa – na wakati mwingine machozi na damu kufika tunapotaka kwenda.

 

Kuna vitu vingine vya Kichina ambavyo vinaendana na utamaduni wao wa kuthamini kazi na uhusiano na watu wengine. Lakini kwenye makala haya, nimeamua kuangalia mambo ambayo Wachina wameyatumia kupanda ambayo nasi tunaweza kuyaiga – kivyetu.