Kwa nini tatizo la Burundi ni tatizo letu?

Picha: Picha ya pamoja kati ya Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye na kiongozi wa chama cha upinzani cha CNL, Agathon Rwasa (kulia). Picha ya Al Jazeera:
Ezekiel Kamwaga
RIPOTI maarufu ya Taasisi ya Kimataifa ya ACCORD ya mwaka 2016 iliyoitwa Conflict in the Great Lakes Region, ilieleza kwa kifupi kwamba vita na migogoro isiyokwisha katika eneo la Maziwa Makuu vinasababishwa na uwezo mdogo wa serikali za nchi hizo kudhibiti misuguano ya kijamii inayosababishwa na tofauti za kikabila, ugawaji mbaya wa rasilimali ardhi na kutengwa kisiasa kwa makundi fulani ya kijamii.
Katika eneo hili la Nchi za Maziwa Makuu, hakuna nchi iliyoumizwa kwa vita na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kuliko taifa la Burundi. Tangu ipate Uhuru mwaka 1962, Burundi imeshuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe mara sita, mapinduzi saba ya kijeshi – sita yaliyopindua nchi na kubadili viongozi na mawili yaliyoshindwa.
Vita na mapinduzi hayo ya kijeshi yamesababisha madhila makubwa kwa nchi hiyo, wananchi wake na nchi jirani. Zaidi ya Warundi milioni 1.5 wamewahi kukimbia nchi yao na kuishi ukimbizini – Tanzania ikiwa imepokea wakimbizi wengi zaidi – takribani nusu ya hao, kuliko majirani wengine.
Hali hii imeifanya Burundi kuwa nchi tepetepe kiusalama kulinganisha na nchi nyingi za Afrika. Kama kuna mfano mzuri zaidi wa kueleza hali hii ya taifa hili, tukio la mauaji ya Rais Melchior Ndadaye mwaka 1993 linaweza kutumika kama mfano mzuri.
Mauaji ya Ndadaye aliyekuwa Rais wa kwanza wa Burundi kuchaguliwa kidemokrasia kwa njia ya kupigiwa kura, yalisababisha vita ya hasara kubwa ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takribani miaka 10.
Wakati huohuo, nchi kama Burkina Fasso na Niger zilipoteza viongozi wake wawili waliokuwa wakipendwa na wananchi wao kwenye miaka ya 1980 na 1990; Thomas Sankara na Ibrahim Bare Mainasara, lakini hazikuingia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe kama jirani zetu hawa wa Afrika Mashariki.
Mazungumzo niliyofanya jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita na Kiongozi wa Upinzani nchini Burundi, Agathon Rwasa, yamenipa picha ya uhusiano usioridhisha baina yake na Rais Evariste Ndayishimiye.
Ripoti ya mwaka jana ya Shirika la Kimataifa la Human Right Watch (HRW) imetoa picha ya kuzorota kwa karibu vigezo vyote vya utawala bora – ikiwemo utawala wa kisheria, uhuru wa vyombo vya habari na uimara wa vyombo vya utoaji haki. HRW imeeleza kuongezeka kwa ushawishi wa kundi la mgambo wa Imbonerakure – kikundi cha kijeshi cha vijana wa chama tawala cha CNDD-FDD, kinachotishia wapinzani wa chama tawala na wakati mwingine kujichukulia sheria mkononi.
Chama tawala cha CNDD kimekitenga chama kikuu cha upinzani cha CNL kwenye kuendesha serikali kama ambavyo makubaliano ya Arusha yalivyopendekeza kwenye kuhakikisha kwamba vyama vikuu vya kisiasa vinashirikiana kwa kufanya kazi pamoja ili kujenga umoja wa kitaifa wa nchi hiyo.
Katika mazingira ambayo chama tawala kimeamua kushirikiana na vyama vidogo badala ya mshindani mkuu baada ya uchaguzi uliodaiwa kutokidhi vigezo vya kidemokrasia, ni wazi Burundi inaselelea -japo taratibu, katika shimo linaloweza kuleta madhara makubwa.
Kuliko nchi nyingine zote katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla, Tanzania ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kulegalega huko kwa uhusiano baina ya chama tawala na chama kikuu cha upinzani nchini Burundi kunazuiwa.
Kwa nini Tanzania na Afrika Mashariki zinawajibika?
Mateso na maisha ya maumivu kwa wananchi wa taifa lolote la Afrika Mashariki ni jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa na wapenda amani duniani kote. Lakini, hali ikichafuka Burundi, kuna nchi zinaumia zaidi kuliko nyingine.
Chukulia mfano wa Tanzania. Tangu kuimarika kwa amani ya Burundi kufuatia mazungumzo ya Arusha, biashara baina ya nchi hizi mbili imekuwa kwa wastani wa takribani asilimia 11 kwa mwaka.
Mwaka jana pekee, Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 109 nchini Burundi. Kenya, kwa upande mwingine, ambayo ndiyo taifa lenye uchumi mkubwa zaidi kwenye ukanda huu, biashara yake kwa jirani zetu hao ilikuwa dola milioni 67.9 tu.
Takwimu rasmi za Wizara ya Fedha zinaonyesha kwamba kwa kiasi kikubwa Burundi hununua mbolea, saruji na mchele kutoka kwetu. Hizi ni aina ya bidhaa ambazo Tanzania inatarajiwa kuongeza uzalishaji zaidi katika miaka ijayo na amani kwa nchi hiyo jirani inamaanisha biashara zaidi.
Kwa sababu ya uzoefu wa miaka 50 iliyopita, amani inapotoweka Burundi, Tanzania ndiyo hubeba mzigo mkubwa wa wakimbizi. Dunia ya sasa ni tofauti na miaka 30 au 50 iliyopita na changamoto ya kuwa na mamilioni ya wakimbizi – katika dunia yenye mivutano ya kimazingira, uchumi mbovu na siasa za kitaifa zinazochukia wakimbizi, hili si jambo la kuliombea.
Na kwa sababu ya udugu – Tanganyika na Burundi ziliwahi kuwa taifa moja enzi za ukoloni wa Ujerumani, na uswahiba baina ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere, na Baba wa Taifa la Burundi, Louis Rwagasore, Tanzania ina wajibu mahususi wa kuhakikisha wenzetu hawa hawaharibikiwi.
Hatua ya kwanza ambayo viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakiongozwa na Tanzania wanatakiwa kufanya kwa sasa ni kuhakikisha Rais Ndayishimiye na Rwasa wanarejea mezani na kuzungumza.
Ni muhimu kumshawishi Ndayishimiye kwamba mustakabali wa Burundi unaanzia kwanza kwenye uhusiano wa kuaminiana na kushiriki kwenye uongozi wa taifa hilo. Pengine kuliko hata sisi wan je, Rais huyo anafahamu kwamba pengine kwa sasa kunahitajika kutokea tatizo dogo kabisa na nchi hiyo ikalipuka tena.
Alama zilizo ukutani zinaonyesha kwamba hali si shwari. Hata hivyo, mazungumzo yangu na Rwasa yamenionyesha kwamba hadi sasa maji hayajamwagika.
Wakati wa kuzungumza na kuchukua hatua ni sasa. Mchezo wenu, unaweza kuja kuwa mauti ya wengi.
Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.