Picha: Sehemu ya matukio yaliyotokea nchini Tanzania kama yalivyoripotiwa kwenye magazeti ya Agosti 16, 2023. Picha kwa hisani ya mtandao wa Millard Ayo.
Na Ezekiel Kamwaga
KUTOKANA na hali ya Tanzania inayoendelea hivi sasa – hasa katika medani ya siasa, jambo moja ambalo nimelibaini ni kuwa ni kwa kiasi gani umoja wetu kama taifa bado ni nyondenyonde na unahitaji kufanyiwa kazi. Ni rahisi kuona kwa nje taifa lenye amani na utulivu kwa takribani miaka 60 sasa, lakini kwa ndani, nimeanza kuona nyufa za taifa lililo hatarini.
Ni muhimu nikakiri kwamba kwa mara ya kwanza katika maisha yangu ya utu uzima, nimeanza kuhofu kuhusu mwenendo wa taifa letu. Suala la uwekezaji katika bandari za Tanzania kupitia kampuni ya DP World kutoka Dubai limeibua hoja za kidini, Muungano wetu, lugha za kutwezana utu, kukamatwa kwa watu ambako hakujaoneka katika miaka ya karibuni, mijadala yenye hoja za nguvu badala ya nguvu za hoja na vitendo vya kihalifu.
Ninaamini huu ni wakati ambapo viongozi wetu – wa kisiasa na kidini, wanaharakati na wasio wanaharakati, wananchi wa kawaida na kila mwenye maslahi ya taifa letu anahitaji kupiga hatua moja na kuwaza picha kubwa katika haya yanayoendelea. Tunahitaji kutulia na kuwaza.
Mimi ni shabiki wa mchezo wa mpira wa miguu. Katika mchezo huo, kuna kitu huwa kinaitwa La Pausa (The Pause). Huu ni uwezo wa mchezaji mmoja au timu kutulia na mpira kwa muda kidogo na kufanya uamuzi sahihi. Huyu ni mchezaji ambaye huwa akiwa na mpira, utaona kama ana sekunde chache zaidi kuliko wachezaji wengine.
Klabu yangu ya Simba ina mchezaji wa aina hiyo. Anaitwa Clatous Chama. Akiwa kwenye eneo la hatari la adui, unaweza kuona kachelewa na mpira, akiyumba huku au kule, akitisha kama anapiga lakini hapigi, na mwishowe huachia mpira kwa kufunga au kumpa pasi yule ambaye ni rahisi zaidi kufunga kuliko mchezaji mwingine yeyote yule. Utulivu huo wa Chama ndiyo humfanya aamue ni wakati gani timu iongeze spidi au ishushe pumzi.
Kama taifa, huu ni wakati ambao tunahitaji jambo moja kuliko lingine lolote. Tunahitaji La Pausa.
Niliandika kupitia mtandao wa twita (X) mapema wiki hii kwamba ujenzi wa taifa lolote unafanana na safari ya gari. Kwenye magari, kuna wakati wa kukanyaga mafuta na wakati wa kukanyaga breki. Nchi inasogea na kupiga hatua pale ambapo wahusika wakuu wanajua ni wakati gani wa kukanyaga mafuta na wakati gani wa kushika breki.
Mtazamo wangu wa nini hasa kinaikuta Tanzania kwa sasa ni kwamba pande zote mbili zimeamua kukanyaga mafuta na hakuna anayetaka kushika breki na kujipa muda wa kutafakari na kutazama fursa nyingine muhimu au namna tofauti zinazofaa kwenda kutuondoa kwenye mkwamo tulionao sasa.
Nimeishi Tanzania maisha yangu yote. Kusema kweli siifahamu chuki ya mtu wa CCM, ACT Wazalendo au Chadema inayoweza kumfanya aende kuchoma gari au kumuumiza mwenzake ambaye hawajawahi kukosana wala kupishana zaidi ya tofauti za mwelekeo wa chama kipi kinataka kuipeleka Tanzania kwenye njia ipi.
Lakini nafahamu pia mazingira yetu. Hii ni nchi ambayo ina dini mbili kubwa, ina makabila zaidi ya 120 yenye mil ana utamaduni tofauti, yenye wafuasi wa vyama tofauti vya siasa, yenye watu wa jinsia tofauti na tukiwa tumezungukwa na nchi jirani ambazo ama zimewahi kuingia kwenye machafuko mabaya, ziko kwenye machafuko na zenye migawanyiko ya wazi ya ukabila.
Tatizo kubwa zaidi la kidunia
Kizazi chetu kinaishi katika nyakati tofauti hapa duniani. Kwa takribani miaka 100 iliyopita, amani na utulivu wa kidunia ulijengwa katika mifumo ya demokrasia ya kiliberali iliyokuwa na vyama vilivyosimamia itikadi fulani zilizoeleweka. Tatizo lililojitokeza, hasa katika takribani miaka 10 iliyopita, ni kuibuka kwa viongozi na wanasiasa ambao hawaamini au wanapindisha misingi iliyoleta utulivu na amani duniani.
Hakuna mfano mzuri kueleza hili kuliko taifa la Uingereza. Kule kuna chama kinaitwa Conservatives. Maana hasa ya chama hicho inatokana na neno la lugha ya Kiingereza; to conserve, yaani kuhifadhi au kutunza. Ukiwa chama hicho kulikuwa na misingi kama vile kuamini katika Ufalme ambao ndiyo unaongoza taifa hilo, kuamini kwenye biashara, mil ana desturi za watu wao, kuenzi dini yao ya Anglikana na miiko yake na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Miaka michache ijayo, wakaja kuongozwa na mtu anayeitwa Boris Johnson. Huyu ni mtu ambaye hana maadini yoyote yanayofanana na dhana ya kutunza. Haamini sana katika Ufalme, katika dini, katika mila na desturi za taifa hilo. Kitu pekee ambacho alikifahamu ni namna gani ya kutumia migawanyiko iliyopo kushinda uchaguzi.
Hata hapa kwetu tulipita katika mtihani wa aina hiyohiyo. CCM ilimpitisha John Magufuli kuwa mgombea wake na urais wake haukufanana na mwingine yeyote aliyepita kabla yake. Tangu angali ikiwa TANU na baadaye CCM, chama hicho kilijijenga kuwa kinachojali mijadala, cha kidemokrasia, cha Kimajui ya Afrika, Kisichofungamana na upande wowote na kinachojenga umoja na mshikamano na kinachopinga ukabila.
Mojawapo ya urathi (legacy) wa Magufuli ni kwamba alimaliza ule ushindani uliozoeleka wa hoja baina ya vyama vya siasa. Kutokana na woga na mazingira magumu ya kufanya siasa kwa wanasiasa na kubanwa kwa uhuru wa vyombo vya siasa, likaibuka kundi la wanaharakati walioongoza upinzani dhidi ya utawala wa Magufuli.
Matokeo yake ni kwamba hapa Tanzania, taratibu, wanaharakati – hasa wale wa mitandaoni na kwingineko, wameanza kuchukua jukumu ambalo huko nyuma lilikuwa likifanywa na viongozi wa kisiasa na vyombo vya habari. Tatizo la wanaharakati ni moja; kama alivyopata kusema msomi wa Israel, Yuval Noah Harari, ni kwamba shughuli zao kwa asili si za kujenga au kuhifadhi.
Kwa miaka mingi, wao kazi yao kubwa ni kukosoa na kuonyesha wapi pana mapungufu ili yarekebishwe. Wao si watawala wazuri au watu wa kufanya mambo ya kujenga umoja, utaifa na kutoa mwongozo wa jumla wa namna ya kuendesha nchi. Kwao, kama mtawala au mpinzani wao amekanyaga mafuta, nao watakanyaga mafuta mpaka “kieleweke”. Hiyo ndiyo hali halisi ilivyo.
Naamini huu ni wakati wa viongozi wetu wa kisiasa, kijamii na kidini – maana tafiti zinaonyesha viongozi wa kidini ndiyo wanaoaminika zaidi na watu wetu kuliko viongozi wengine wowote, kukaa chini na kuchukua nafasi yao katika kulinusuru taifa letu na mserereko mbaya ambao nimeanza kuuona. Huu ni mserereko ambao kama haujadakwa mapema, maumivu yake yanaweza kuwa makubwa.
Kama kuna jambo la kujivunia kwetu kwa sasa ni kwamba hii ni nchi ya kidemokrasia hata kama si kwa asilimia 100. Na kama alivyopata kusema mwandishi na msomi wa sayansi ya siasa mashuhuri wa Marekani, Fareed Zakaria, kwenye demokrasia inaruhusiwa kuosha nguo za ndani hadharani. Kwamba haya mapungufu na migawanyiko iliyoletwa na sakata la DP World, ni nguo zetu za ndani zilizofuliwa zikiwa nje na zikikauka, zinaweza kurejeshwa ndani na maisha yakaendelea kama kawaida.
Nakumbuka mazungumzo niliyowahi kufanya miaka 20 iliyopita na mmoja wa watu waliowahi kushitakiwa kwa uhaini, hayati Eugene Maganga. Mazungumzo hayo nayaunganisha na yale niliyowahi pia kufanya na hayati Zacharia Hans Poppe takribani miaka minane iliyopita. Wawili hao walishitakiwa na kuhukumiwa katika kesi ya uhaini kwenye miaka ya 1980 enzi za utawala wa Julius Nyerere.
Walinieleza jambo moja linalofanana; kwamba mabadiliko ya kisera na kiutendaji yaliyofanywa na utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, kwa kiasi kikubwa yalijibu masuala ambayo wao walitaka yafanywe na serikali ya Nyerere kiasi cha kufikia kutaka kufanya mapinduzi. Kwangu, huo ulikuwa ni ushindi mkubwa wa utawala wa kidemokrasia, kwamba ndiyo mfumo pekee ambao unaweza kujigeuza na kujirekebisha kupitia mabadiliko ya viongozi na uongozi. Kwamba ni muhimu tukaendelea kuamini katika mfumo wetu wa kidemokrasia.
Jambo pekee linalohitajika ni kwa wanasiasa kuchukua nafasi zao. Ukiangalia Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995, Watanzania hawakuvutiwa na harakati au ajenda zenye migawanyiko. Walivutiwa na sera mbadala na maneno matamu ya akina Dk. Masumbuko Lamwai, Dk. Ringo Tenga, Mabere Marando, Ndimara Tegambwage, Mashaka Nindi Chimoto na wanasiasa wakongwe waliokuwa na heshima kubwa katika jamii kama akina Chifu Abdallah Saidi Fundikira.
Matokeo mazuri ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hayakusababishwa na hadaa, vitisho au hoja zenye kugawa na kutweza utu wa washindani – kimsingi, kwenye uchaguzi ule, hakukuwa hata na risasi moja wala bomu la machozi lililopigwa ingawa ulikuwa mkali kuliko mwingine wowote kwenye historia ya taifa letu. Lakini tulifikaje hapo?
Ni kwa sababu wanasiasa wenye uwezo mkubwa wa kushindana kwa hoja walijenga msingi huo kwa takribani miaka 10 nyuma. Nazungumzia wanasiasa wa upinzani kama vile Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Kitila Mkumbo, Zitto Kabwe, Freeman Mbowe, James Mbatia, Profesa Ibrahim Lipumba, Marando na wengine walioshiriki katika vuguvugu la kuleta mabadiliko kwa njia ya demokrasia. Hawa ndiyo waliongoza harakati za kuleta mageuzi kwa njia ya siasa lakini wao wakiwa wameshika hatma hiyo mikononi mwao.
Kama taifa, tunachohitaji sasa ni pause kidogo. Wale wenye mamlaka waangalie na kuona kwamba huu ni wakati wa kushika breki hata kama kuna kundi limeamua kukanyaga mafuta. Bado naamini tuna kazi kubwa ya kujenga nchi yetu na umoja wetu kabla ya vitu vingine.
Bila umoja. Bila amani na utulivu. Bila viongozi kuamua kuchukua dhamana yao ya uongozi kwa mikono miwili na kubaini dhamana hiyo ni mtihani na fursa kwa wakati mmoja, kuna hatari nchi ikaangukia kubaya. Huu ni wakati mwafaka kufanya jambo moja la muhimu. Kutulia na kutafakari.
Kama ambavyo La Pausa angefanya kwenye uwanja wa mpira.