Lowassa apigania uhai Afrika Kusini

HALI ya kiafya ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa, inaelezwa kuwa ya kutoridhisha katika siku za karibuni na kwamba sasa “anapigania uhai wake”, Gazeti la Dunia linaweza kuthibitisha.

Lowassa anayetarajiwa kutimiza umri wa miaka 70 Agosti 26 mwaka huu, amelazwa nchini Afrika Kusini alikopelekwa mwanzoni mwa mwaka jana kwa matibabu zaidi baada ya awali kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Taarifa za karibuni kutoka kwa wanafamilia na marafiki wa karibu zimeeleza kwamba kwa sasa mwanasiasa huyo mashuhuri yuko hospitalini katika uangalizi maalumu kwenye Wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU) huko Afrika Kusini .

“Mimi sina cha kukwambia kwa sasa. Kitu pekee ninachoweza kusema ni kuwaomba Watanzania waendelee kumwombea. Madaktari wanaendelea na juhudi zao lakini kwa hapa tulipofika rehema za Mwenyezi Mungu zinahitajika,” chanzo cha habari kinachofuatilia afya ya Lowassa kwa ukaribu kimeniambia.

Serikali na familia yake hazijatoa taarifa rasmi kuhusu kuugua kwake lakini mwishoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikwenda Afrika Kusini kumjulia hali na ofisi yake ilitoa taarifa rasmi kwamba alikuwa amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, picha zilizopigwa na wasaidizi wake hazikumwonyesha Lowassa – tofauti na ilivyokuwa wakati alipomtembelea Waziri Mkuu mstaafu mwingine, Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye naye anaugua kwa sasa.

Picha zilizopigwa Afrika Kusini zilimwonyesha Majaliwa akiwa na wanafamilia ya mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Monduli – mkewe, Regina, mtoto wake mkubwa wa kiume, Frederick na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi.

Akizungumza nami kutoka Afrika Kusini, Balozi wa Tanzania nchini humo, Meja Jenerali, Gaudence Milanzi, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na akashauri familia itafutwe kuzungumzia jambo hilo.

“Mimi siwezi kuzungumzia suala la mgonjwa. Nashauri muwatafute watu wa familia yake au serikali huko nyumbani. Kama kutakuwa na cha kuzungumza, nitaelekezwa na mamlaka husika lakini siwezi kuzungumza chochote kabla ya hapo,” alisema Milanzi ambaye ni mmoja wa mabalozi wanaosifika kwa ufanisi katika duru za kidiplomasia.

Ingawa hakuna aliyekuwa tayari kuzungumzia kuhusu suala hilo na kukubali kunukuliwa na tovuti hii, mmoja wa wanafamilia ya Lowassa aliniambia kiongozi huyo mstaafu alianza kupata maumivu makali ya tumbo mwanzoni mwa mwaka jana.

“Nafahamu kwamba ilianza kama maumivu makali ya tumbo. Alipopelekwa Muhimbili kwa vipimo, ilibainika kwamba alikuwa na shida ya shinikizo kali la damu ambalo baadaye lilikuja kumletea shida kichwani.

“Tangu alipohamishwa kutoka Muhimbili kwenda Afrika Kusini hajarejea tena nchini. Kwa sasa nafahamu kwamba yuko katika chumba cha uangalizi maalumu ambako anapigania uhai wake,” alisema rafiki huyo ambaye hata hivyo hakuwa tayari kunukuliwa.

Juhudi za kumpata Frederick ilia toe taarifa rasmi kama kiongozi wa familia hazikufanikiwa hadi kuchapwa kwa habari hii. Juhudi za kumpata kupitia njia ya simu yake ya mkononi au ujumbe mfupi wa maneno zote hazikuzaa matunda.

Frederick ambaye ndiye mbunge wa sasa wa Monduli na anayejulikana zaidi kwa jina la Freddy, ndiye anayefahamika sasa kama msemaji rasmi wa familia hiyo na karibu watu wote waliofuatwa kutoa taarifa walisisitiza mtu anayepaswa kuzungumzia suala hilo ni yeye.

Historia ya afya ya Lowassa

Kuelekea mwaka 2005, Lowassa alikuwa miongoni mwa wanasiasa mashuhuri wa Tanzania waliokuwa wakijulikana kwa afya njema na stamina kubwa ya kufanya kazi.

Lowassa ndiye alikuwa kama kiongozi wa mtandao wa aina yake wa kisiasaulioanzishwa kwa lengo la kufanikisha kuingia madarakani kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005. Vinara wa mtandao huo walikuwa yeye, Samuel Sitta aliyekuja kuwa Spika wa Bunge baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 na mfanyabiashara mashuhuri, Rostam Aziz.

Mgombea urais huyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alikuwa akijulikana kwa uwezo wake wa kufanya kazi hadi usiku wa manane – akikutana na watu mbalimbali kwenye mtandao wake wa kisiasa.

Taarifa za kuanza kudorora kwa afya ya Lowassa zilianza kusikika miaka michache baada ya kujiuzulu kwake nafasi ya Waziri Mkuu kutokana na kile kilichokuja kujulikana baadaye kama kashfa ya Richmond.

Minong’ono ilikuwa mingi kiasi kwamba Lowassa mwenyewe alilazimika kuzungumza na kusema alikuwa akisumbuliwa na tatizo la macho na ndilo lililomfanya aende kutibiwa nchini Ujerumani.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, suala la afya yake lilikuwa miongoni mwa ajenda kuu za uchaguzi huo – baadhi ya wapinzani wake kisiasa wakiitumia kama kete kwa kuwataka watu wasimchague mgombea ambaye ni mgonjwa.

Kimsingi, hata hatua ya aliyekuwa mshindani wake kwenye uchaguzi huo, John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupiga ‘pushapu’ kwenye jukwaa la kampeni ilikuwa na nia ya kuwaonyesha Watanzania kwamba yeye yuko fiti tofauti na mshindani wake huyo.

Taswira ya kampeni zile ilikuwa ni ya Lowassa aliyekuwa akizungumza kwa taratibu na chini ya dakika 10 kwenye mkutano mmoja – ingawa wafuasi wake waliamini katika kauli mbiu yake ya Mabadiliko na kampeni yake ilikaribia kukiondoa madarakani chama tawala.

Lowassa alirejea CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na alionekana hadharani mara chache baada ya mkutano wake na Magufuli – akiwa amesindikizwa na Rostam, uliotangaza kurejea kwenye chama kilichomlea na kukitumikia karibu katika maisha yake yote kisiasa.