Picha: Mwandishi wa taabini hii, Mohamed Said, akizungumza na swahiba yake, Sheikh Aly Basaleh, enzi za uhai wake, katika moja ya mazungumzo waliyofanya nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Picha kwa hisani ya Mohamed Said
Na Mohamed Said
Nimepata taarifa ya kifo cha Sheikh Aly Basaleh msikitini petu Masjid Nur baada ya Sala ya Maghrib. Nilipofika nyumbani kitu cha kwanza nilichofanya ni kuingia Maktaba kutafuta kitabu alichoandika, ‘’Kwa Nini Waislamu Walalamika,’’ kilichotolewa na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania. Nimekifunua kitabu na kusoma, ‘’Yaliyomo.’’
Kitabu hiki kina mengi yanayomfaa kila Muislam kuyajua, mambo ambayo kwa hakika ni mazito kupita kiasi na si ajabu kuwa aliyekuwa na ushujaa wa kuyasema alikuwa6 marehemu Sheikh Aly Basaleh. Hawezi mtu kuisoma dhulma iliyoelezwa katika kitabu hiki ila moyo wake utahuzunika. Kwa lugha nyepesi sana Maalim Aly Basaleh katika kitabu hiki anawapitisha Waislam katika yote yaliyowasibu kuanzia uhuru upatikane mwaka wa 1961 na bado yanaendela hadi hivi sasa.
Katika kitabu hiki Maalim Aly Basaleh kama ilivyokuwa taaluma yake ya ualimu sheikh anasomesha kwa rejea ya vitabu vilivyoandikwa na watu maarufu wanaojua mambo mfano wa Dr. John Sivalon mwandishi wa kitabu, ‘’Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985,” (1992). Kitabu hiki kwa uzito wa yale yaliyomo kimetolewa katika soko kimyakimya kunusuru umoja wa taifa letu.
Maalim Aly Basaleh akitoka hapo katika kitabu hicho anakuingiza katika kitabu cha Aboud Jumbe, ‘’The Partner-Ship,’’ (1994).
Sheikh Aly Basaleh kwa ushahidi wa waandishi hawa wawili ambao kauli zao zinajitosheleza anaeleza hali na matatizo waliyonayo Waislam na vikwazo vinavyowakabili katika kujiletea maendeleo na kueleza wepesi waliokuwanao wenzao kusonga mbele katika maendeleo yao wakitumia nafasi zao katika serikali.
Maalim Basaleh katufanyia wema mkubwa kwa kuandika na kutuachia kitabu hiki. Maalim Aly Basaleh kafariki katika kipindi nchi yetu imegubikwa na sakata la bandari.
Naamini Sheikh Aly Basaleh kama si maradhi kumweka kitandani hadi umauti wake asingekosa la kusema kuhusu kadhia hii na kama mwenyewe alivyopenda kusema kila alipohadhiri kuwa yeye hasemi jambo ila kwa ushahidi wa nukuu kiasi wanafunzi wake wakampa jina, ‘’Mzee wa Kunukuu.’’
Katika suala la bandari kelele nyingi zinapigwa kuhusu kinachdaiwa yamo ndani ya mkataba wa Serikali na Waarabu. Neno, ‘’Waarabu,’’ halijapata kupewa uzito kama linavyopewa hivi sasa katika suala la bandari. Hata pale wanaolitumia neno hili wanapoonywa kuwa wanajipiga risasi ya mguu wenyewe kwa kutumia neno hili, akili imewaruka wanashindwa kuliacha limekuwa neno muhimu kati ya msamiati wao wa kibaguzi.
Msome Sheikh Aly Basaleh anavyozungumza katika kitabu chake, ‘’Kwa Nini Waislamu Walalamika,’’ kuhusu mkataba wa Maelewano ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mabaraza ya Makanisa (Christian Council of Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC).
Sheikh Aly Basaleh anaandika katika kitabu hicho kuwa, ‘’Serikali ya Tanzania ilikubali kuwarejeshea Wakristo shule za sekondari na hospitali zilizotaifishwa mwaka wa 1970 na pia kuahidi kutozitaifisha tena shule na hospitali hizo au zile zitakazojengwa na makanisa kutoka kwa wahisani wa nje, na hasa serikali ya Ujerumani, kwa ajili ya kuendeleza huduma za kijamii zinazotolewa na Makanisa.
Chini ya muafaka huo Serikali ilipaswa kutenga nafasi maalumu katika vyuo vyake vya ualimu kwa ajili ya waalimu na makanisa kwenda kusomea ualimu kwa lengo la kuimarisha ubora wa shule za Kikristo.’’ Hiki ni kipande tu katika mkataba wa Serikali na Makanisa. Kalamu ya Maalim Aly Basaleh naisoma na kama vile namuona katika uhai wake anazungumza au namsikiliza Radio Kheri. Kitabu hiki kina hoja, simulizi, takwimu na mengi muhimu kufahamika na wananchi.
Allah kwa mapenzi yake amemchukua Maalim Aly Basaleh katika kipindi hiki ambacho serikali ya Tanzania inashutumiwa kwa kile kinachoeleza ‘’kuridhia mkataba mbovu na kuuza bandari kwa Waarabu. Kama hili halitoshi serikali imesimamishwa kizimbani kujitetea.
Allah kamchukua Sheikh Aly Basaleh katika majira haya kukiwa na shutuma kuwa Waarabu hawa kutoka Dubai wameingia Tanzania kwa malengo ya kuunufaisha Uislam na Waislam wa Tanzania.
Namsoma Maalim Aly Basaleh kisha najiuliza hawa wanaotoa shutuma hizi hawajui kuwa Kanisa lifaidi mabilioni ya fedha kutoka Hazina ya Taifa sasa miaka 30? Namsoma Sheikh Aly Basaleh najiuliza hawa wanaotoa shutuma hizi wanajua kuwa wengine hawana haya waliyonayo wao na wametulia tuli?
Ali Basaleh alikuwa mzungumzaji wangu na kila tukikutana tutakuwa na mengi ya kujadili. Namkumbuka Maalim alipokuwa na duka lake Mtaa wa Tandamti karibu na Soko la Kariakoo nikipita mitaa ile nitampitia kumsalimu na hapo tutazungumza mengi.
Laiti Maalim Aly Basaleh angekuwa hai na tukatana wakati huu wa hili joto kali la Waarabu kuuziwa bandari na Serikali kusimamishwa kizimbani mahakamani bila shaka tungelizungumza mengi moja likiwa kwa nini Waislam hawajafikisha madai yao mahakamani kupinga mkataba wa
Serikali na Makanisa?
Hapa nimesimama kuandika. Nimekaa nafikiria na fikra nyingi zinanipita kichwani kwangu. Namuona kama vile sheikh yuko hai na naisikia sauti yake Maalim Aly Basaleh akinipa nasaha ya faida gani itapatikana kwetu sisi wakati kama huu kufanya jambo kubwa kama hilo? Kama vile namuona Maalim Aly Basaleh na namsikia akiniuliza, ‘’Hebu niambie Sheikh Mohamed tija gani itapatikana? Tutakuwa tunajenga udugu baina ya wananchi au tunaiamsha fitna iliyokuwa imelala?
Haiwi kwa kuwa wao wamefanya nasi tufanye. Sisi Allah katusifia kasema ni “watu wenye akili.’’ Maalim Aly Basaleh alikuwa mtu fasaha kwa lugha zote Kiswahili, Kiarabu na Kiingereza. Nimejiinamia najiuliza nazungumza na nafsi yangu huku nikimkumbuka Sheikh Aly Basaleh, kuna ukimya ambao si wa kawaida kama vile Waislam hawapo. Hali hii imeleta utulivu mkubwa nchini na imeondoa taharuki katika jamii.
Nakumbuka mengi katika kesi za Waislam Mahakamani Kisutu miaka mingi iliyopita. Kulikuwa na kesi ya Mwembechai na kesi ya Dibagula. Ulinzi mkali na barabara kufungwa kwa muda mrefu. Kesi kama hiyo wakati huu hakika ingezua taharuki kubwa. Kuwa Allah kamchukua Sheikh Aly Basaleh katika majira haya yanayohanikiza nchi yetu ni ibra tosha ya kutufanya tufikiri mengi na kumshukuru Allah kwa subra aliyotujaalia, subra iliyoleta utulivu na kudumisha amani nchini petu.
Tunakuomba Mola Wetu umsamehe dhambi zake Maalim na Sheikh wetu na umtie peponi.
Amin.