Mafunzo kutoka Zambia

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

OKTOBA mwaka huu, nilikuwa sehemu ya waandishi wa habari wa Tanzania waliokuwa kwenye ziara ya kitaifa ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Zambia. Ingawa vyombo vyetu vya habari viliandika kuhusu masuala makubwa yaliyotokea huko, jicho langu lilivutwa na jambo lingine dogo nililoshuhudia.

 

Oktoba 24, nilipata fursa ya kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa Zambia zilizofanyika katika Ikulu ya Lusaka. Kila kitu kilikuwa tofauti kwangu na nilijifunza mawili matatu kutoka pale na ndiyo msingi wa makala haya ya leo.

 

Muktadha ni muhimu. Mimi nimezaliwa na kukulia katika eneo la Kurasini, Temeke. Mojawapo ya kumbukumbu zangu kubwa za utotoni ni kuona msafara wa magari na pikipiki ukipita barabarani kumsindikiza Rais, kuanzia Rais Mwinyi – wakati wa Nyerere sikumbuki vizuri, na wengine waliomfuata.

 

Na kwa sababu nilisoma Shule ya Msingi Mgulani iliyo jirani na Uwanja wa Uhuru, mimi na wenzangu tulikuwa na utaratibu wa kwenda kutazama wanajeshi wakifanya mazoezi ya gwaride la Uhuru kabla ya siku yenyewe.

 

Kwa sababu hiyo, kwangu, kwa sababu ya usuli huo, maadhimisho ya Siku ya Uhuru yalikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na gwaride na ving’ora vya Rais. Katika Ikulu ya Zambia siku ile nikiwa pale, hakukuwa na ving’ora wala gwaride. Na bado shughuli ilifana sana.

Zambia walifanya nini? Kwenye siku yao ya Uhuru, wao huitumia kuwatuza watu waliofanya mambo ya kizalendo na yaliyolipa taifa lao heshima kimataifa. Ni siku ya kusherehekea Uzambia wao. Wale waliotunukiwa, walipewa vyeti maalumu na Rais mkononi.

 

Nakumbuka kumwona mmoja wa viongozi wa jadi – Chifu wa Kabila la Wazulu; mojawapo ya makabila yaliyo Zambia, akipewa zawadi kwa mchango wake kwenye kulinda utamaduni na umoja wa taifa hilo. Alikuwepo nesi aliyeokoa maisha ya mzazi kwa kumzalisha katika mazingira magumu.

 

Msanii wa Zambia aliyeshinda Tuzo ya Kimataifa ya Muziki na wengine walioshiriki katika filamu ya Wakanda nao walienziwa katika tukio hilo. Na ujumbe mkuu katika siku hiyo ni Uzalendo. Kwa hakika, niliamini palepale kwamba ile ndiyo namna inayofaa kusherehekea Uhuru wa taifa.

 

Mara kadhaa nimewahi kuandika kwamba sikubaliani na utamaduni ulioanza kujengeka kwenye miaka ya karibuni ya kuacha kufanya maadhimisho rasmi ya Uhuru wetu na badala yake kutumia fedha hizo kwenye mahitaji mengine ya kijamii.

 

Ingawa naamini kwamba taifa letu lina mahitaji mengi, na kila fedha inayoingia inaweza kutumika kufanya kitu kikubwa kwa wahitaji, ni jambo la hatari sana kusahau kwamba sisi hasa ni nani. Hili si jambo unaloweza kulichukulia kirahisi.

 

Tunaishi katika zama za kipekee wakati huu ambapo siasa za utaifa zinaanza kupata nguvu duniani kote. Tunashuhudia wanasiasa wanaozungumzia siasa za kibaguzi za kugawa watu kwa dini, rangi, maeneo na matabaka wakipanda chati.

 

Katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, hakuna wakati mgumu kwa nchi kama wakati huu. Hata hapa kwetu, ni rahisi kwa mwanasiasa au yeyote mwenye maslahi binafsi, kuzungumzia ubovu wa Muungano na kusema ni afadhali turudi kwenye Tanganyika na Zanzibar iondoke kwenye Muungano. Ni kama tunasema kila mmoja abaki na mbao zake.

 

Tunasahau jambo moja kubwa; kwamba tunaishi katika nchi tepetepe sana. Kimsingi, ni miujiza tu kuwa Tanzania haijaingia katika mizozo ya kikabila na kidini ambayo jirani zetu wanayo. Kwa kuangalia viashiria vya nchi zilizo hatarini kuingia kwenye migogoro, Tanzania tunavyo.

 

Tuna dini mbili kubwa; hili limewahi kuleta mpaka vita kati ya Uingereza na IRA wa Ireland na hadi leo Nigeria ina shida kubwa kwa sababu ya dini hizi mbili kubwa za Wakristo na Waislamu. Kuwa na dini mbili zenye uwiano unaokaribiana katika nchi si jambo la faida katika nchi nyingi.

 

Tuna makabila zaidi ya 120. Somalia na Rwanda ambako wana kabila moja tu la maana, wamewahi kupigana kwa sababu ya ukabila na mambo ya ukoo. Sisi – kwa maana hiyo, tuna sababu zaidi ya 120 za kugombana kwa sababu ya makabila tuliyonayo.

 

Jambo lingine linahusu umasikini wa kutupwa ambao bado tunao. Kuna msemo mmoja maarufu usemao mtu mwenye njaa ni mtu mwenye hasira. Kwa umasikini na changamoto ambazo watu wanazo hapa nchini, tatizo moja dogo linaweza kuleta shida kubwa.

 

Kwa nini haya mambo ya dini, makabila na ugumu wa maisha si mambo ya kuyadharau kwenye kulinda utaifa wetu? Nimepata elimu kubwa kwa kusoma kitabu cha Imagined Communities cha Benedict Anderson kilichoandikwa takribani miongo mitano iliyopita.

 

Anderson anasema nchi ni jamii ya watu wanaoamini au kuunganishwa na kitu au imani fulani. Kinaweza kuwa dini moja, kabila au stori fulani inayowaunganisha. Kwa sababu hiyo, kuna mataifa mengi ndani ya Tanzania yetu.

 

Siamini kwamba tumefikia hatua ya kuona hatuhitaji tena kukumbuka sisi ni nani na badala yake tunahitaji madarasa na barabara zaidi. Tunachotakiwa kufanya kama nchi, si kuachana na sherehe za siku ya Uhuru au magwaride, tunaweza kuwaza tofauti kama wenzetu.

 

La kwanza ni kuifanya siku yenyewe kuwa ya watu zaidi badala ya viongozi. Watu wanapumzika majumbani kwao siku hiyo lakini ni muhimu sana kufanya iwe na maana zaidi.

 

Kuna matukio mengi ya watu wanayofanya kwa nchi yao na kama yakithaminiwa, tutakuwa tunajenga taifa litakalodumu na kumudu mitikisiko ya sasa na inayokuja. Labda niweke mifano michache ya watu ambao wangeweza kupewa tuzo kwenye maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara au Muungano wa Tanzania.

 

Kwenye tukio la ajali ya ndege ya Precision mwaka jana, kijana kama Majaliwa na wenzake waliokuwa naye pale Mwaloni Mwanza na kusaidia kwenye uokoaji, wangeweza wote kuitwa Ikulu na kupewa vyeti na kushikwa mkono na Rais. Fikiria vijana wale kutoka Bukoba wajikute wako Ikulu ya Dodoma au Dar es Salaam!!

 

Kuna yule mama anayeitwa ‘Mama Kangaroo’ kwa namna alivyokuwa anakumbatia na kutunza watoto wanaozaliwa njiti katika mojawapo ya hospitali za Dar es Salaam. Kuna askari wetu wanaokesha baharini na mipakani wakitulinda. Tunajua kuna mengi tusiyoyajua yanaendelea kwenye mipaka yetu. Hiyo ndiyo siku yao.

 

Vijana wetu akina Diamond, Zuchu, Harmonize na wengine wanatwaa tuzo za muziki kimataifa. Wasomi wetu kwenye vyuo vikuu wanapata sifa kimataifa kwa kuandika miradi yenye akili na inayoweza kubadilisha maisha ya watu.

 

Fikiria kazi wanazofanya watu kama akina Dk. Frank Minja – daktari Mtanzania anayeishi Marekani ambaye ana miradi ya kusaidia Watanzania kiafya kwa kutumia muda na gharama zake binafsi. Kuna timu zetu za mpira na namna zinavyotuunganisha.

 

Badala ya Watanzania kukaa kwenye televisheni kuangalia Rais anaingia uwanjani na magari na pikipiki nyingi na kukagua gwaride, labda watu wanaweza kukaa kwenye televisheni zao kuangalia ni akina nani watatuzwa kwa matukio yasiyo ya kawaida.

 

Tutaanza kutengeneza mashujaa wetu wa kizazi chetu. Watoto wetu wanaokua sasa, watatamani nao siku moja kuingia Ikulu – si kwa sababu wanataka kuendeshwa kwa pikipiki nyingi na msafara mrefu wa magari, bali kwa sababu wanajua wakifanya kitu kwa ajili ya taifa lao, watafika Ikulu na kutangazwa nchi nzima.

 

Hatuna sababu ya kuacha kufanya maadhimisho kwa kisingizio cha gharama. Kuna ubaya gani kutumia shilingi bilioni kadhaa kwa ajili ya kutuza watu ambao wameokoa uhai wa watu, wanatulinda usiku na mchana, wanafanya vitu vitakavyoingizia taifa letu fedha nyingi zaidi na wanaofanya vitu visivyo vya kawaida.

 

Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu yalikuwa tofauti kidogo kwa Rais Samia kuitumia kufanya tafakuri  ya taifa letu kupitia kutangazwa kwa wajumbe wa timu itakayotengeneza Vision 2050. Ulikuwa ni ubunifu pia wa namna nyingine tunayoweza kuadhimisha siku hii kubwa kwa taifa letu.

 

Zambia wana mengi zaidi ya kujifunza kutoka kwetu. Yako mambo ambayo sisi tumewatangulia tayari. Lakini kuhusu hili la mada yangu ya leo, nadhani tunaweza kuchukua kitu kutoka kwao.