Mara hii nina hofu na Sudan

Picha kwa hisani ya mtandao wa Africanintelligence. 

MACHAFUKO yameanza upya nchini Sudan. Mgogoro wa sasa ni mbaya kwa sababu unahusisha watu wawili wenye silaha – Mkuu wa Majeshi, Jenerali Abdel Fatah al Burhan na Kiongozi wa Vikosi vya Mgambo, Jenerali Mohamed Hamdani Dagalo maarufu kwa jina la Hemedti.

Kwangu, huu unaweza kugeuka kuwa mgogoro mbaya zaidi kwa Sudan katika kipindi cha miongo minne iliyopita. Katika siasa za bara la Afrika, migogoro iliyofanya uharibifu mkubwa wa mali na uhai wa watu ni migogoro iliyohusu viongozi wenye majeshi.

Majenerali hawa awali walikuwa maswahiba wakubwa kisiasa. Uhusiano wao ulianza mwanzoni mwa miaka ya 2000 wakati Hemedti alipounda vikosi vya mgambo kukabiliana na vikundi vilivyokuwa vikipinga utawala wa Rais Omar Hassan al Bashir. Wakati huo, Burhan alikuwa anaongoza vikosi rasmi vya Jeshi la Sudan vilivyotumwa Darfur.

Mwaka 2019 wawili hawa walikuwa kitu kimoja walipoamua kuwa muda wa Bashir kuwa madarakani umekwisha. Waliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyochochewa na maadamano ya wananchi kupinga hali ngumu ya uchumi ya taifa hilo.

Wachambuzi wa siasa za Sudan wanaona chanzo cha mgogoro huu kuwa ni mambo mawili; Mosi hatua ya kutaka vikosi vya Hemedti vinavyojulikana kwa jina la Rapid Support Force (RSF) kuingizwa kwenye Jeshi la Sudan. Ni vigumu kwa Hemedt kukubali hilo kwa sababu litamwondolea kete yake muhimu kwenye ushawishi ndani ya Baraza la Utawala linaloongoza Sudan kwa sasa.

Jambo la pili ni malalamiko kutoka kwa watu wa Hemedt kwamba Burhan ameanza kurejesha watu waliokuwa karibu na Bashir kinyume cha makubaliano yao wakati wanampindua. Tayari mdogo wa Hemedt, Abdul Rahim Dagalo, ametangaza kwamba vikosi vyake sasa havitakamata wala kuua waandamanaji.

Tangu ipate Uhuru wake mwaka 1956 kutoka kwa Uingereza na Misri, Sudan imekuwa ikiongozwa kwa muda mrefu na wanajeshi kwa njia ya mapinduzi. Katika uchambuzi wake kuhusu siasa za Sudan; More Turbulence in Sudan: A New Politics This Time? , Peter Bechtold, alieleza kwamba tatizo la nchi hiyo ni ukosefu wa mshikamano wakati serikali za kiraia zinapoingia madarakani.

Kwa nini serikali za kiraia na asasi za kiraia za Sudan ni dhaifu? Kiini chake ni asili ya taifa lenyewe. Sudan ni nchi kubwa. Kabla ya kumeguka kwa Sudan Kusini mwaka 2011, Sudan ndiyo ilikuwa nchi yenye eneo kubwa zaidi barani Afrika.

Sasa ina eneo la takribani kilometa za mraba 1,861,484. Kulinganisha na Tanzania yenye ukubwa wa kilometa za mraba 947,300 – maana yake ukubwa wake ni mara mbili ya Tanzania. Kwa wasiofahamu, Tanzania ni nchi yenye ukubwa sana na kuunganisha nchi tatu tofauti; Kenya, Uganda na Malawi.

Kuna mchanganyiko wa watu weusi, wenye asili ya kiarabu na machotara. Ndani ya watu weusi, kuna walau aina zote tofauti za kundi hilo, kuanzia wabantu, wanailoti, wahamitiki na makundi mengine. Kuna Wakristo, Waislamu na wale wanaoamini dini za ajabu.

Kwa sababu ya ukubwa wa Sudan, kwa muda mrefu watu walizoea kujiendeshea maisha yao kwa namna yao pasipo kutegemea chochote kutoka Khartoum. Wakati wa kupinga utawala wa kijeshi, makundi haya huwa kitu kimoja lakini wakati yenyewe yanapoingia madarakani au kukaribia kushika madaraka, kutoamiana kwao huanza kujitokeza.

Wanasiasa wawili wametawala Sudan kwa muda mrefu kuliko wengine; Jaafar Numeiry kwenye miaka ya 1970 mpaka 1985 na Bashir kati ya mwaka 1989 hadi 2019. Kuna sifa moja kubwa waliyokuwa nayo kuwatofautisha na wengine waliokaa madarakani muda mchache; namna walivyotumia dini kubaki madarakani.

Numeiry ambaye binafsi hakuwa mtu wa dini na akijulikana kwa kunywa pombe na kula vinavyokataliwa kwenye Uislamu, ndiye aliyeamua Sudan ianze kutumia sheria za dini ya Kiislamu (Shariah) kwenye utawala. Alichofanya ni kuwapa nguvu viongozi wa kidini kwenye masuala ya watu na jeshi kubaki kuwa nguzo ya utawala.

Ndivyo hivyo ambavyo Bashir alimtumia Hassan al Turabi kuongoza Sudan hadi walipokorofishani baadaye. Kwa sababu ya kuwa na Waislamu wengi Khartoum na kwenye maeneo yenye Waislamu wengi, kutumia Shariah kulirahisisha utawala na imani ya watu kwa watawala.

Ugomvi wake na Turabi na hatua ya Bashir kutaka kuungwa mkono na nchi za Magharibi kwa kukataa kufuata njia alizotaka mwanasiasa huyo aliyekuwa na ushawishi kwa Waislamu, kulimpunguzia nguvu iliyofanya iwe rahisi kupinduliwa mwaka 2019.

Inaonekana Burhan anataka kuelewana na wafuasi wa Bashir – hasa kundi la viongozi wa kidini ili awe na nguvu ya kutosha kubaki madarakani. Kama akiweza kufanikisha hilo, hatahitaji kuungwa mkono na Hemedt.

Uzoefu katika nchi za Afrika ni kwamba wakati mgogoro unapohusu mahasimu wenye silaha, suluhisho huwa ni kupigana mpaka apatikane mshindi mmoja vitani. Ukubwa wa Sudan unamaanisha uwezo wa kupigana vita kwa muda mrefu ni mkubwa.

Ugomvi huu utakuwa sawa na ule wa vikosi vya RPA dhidi ya majeshi ya Rwanda, vita ya Jonas Savimbi wa UNITA dhidi ya vikosi vya MPLA ya Agostinho Neto na baadaye Eduardo dos Santos au Renamo ya Alfonso Dhlakama na Frelimo ya Samora Machel.

Nina wasiwasi kwamba mgogoro wa Sudan sasa utakuwa mbaya zaidi. Huko nyuma, raia ndiyo walikuwa wakiumizwa kwa sababu jeshi lilikuwa kitu kimoja na mgogoro ulikuwa baina ya jeshi na raia. Mgogoro wa Burhan na Hemedt unaonyesha kuwa sasa kibao kimegeuka.

Ninaihofia Sudan.