LEO Tanzania inatimiza miaka 30 tangu turejee rasmi katika siasa za mfumo wa vyama vingi. Katika kipindi hicho, taifa letu limepitia katika kipindi cha furaha, majonzi, misukusuko na changamoto zote wakati taifa linapoanza njia mpya. Jambo hili si jepesi kwa sababu nyakati hizo hazikuwa rahisi duniani kote.
Miaka ambayo Tanzania ilirejea katika mfumo huo ilikuwa miaka migumu. Miaka ya mwanzoni ya 1990, ndiyo ilishuhudia changamoto kama vile kuanguka kwa iliyokuwa Urusi, vita za wenyewe kwa wenyewe barani Afrika, mauaji ya kimbari na migogoro mingi ya kisiasa na kiuchumi katika nchi zinazoendelea kama yetu.
Lakini Watanzania walipita katika wakati wote huo wakiwa wamoja na tumeendeleza utamaduni huo miaka 30 baadaye. Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza wote na ni matumaini yangu makubwa kwamba viongozi watakaokuja miaka 50 hadi 100 baadaye, wataendelea kuongoza nchi iliyo moja na wananchi wasiobaguana na kupigana hata kama wanapingana kuhusu namna ya kuendesha nchi yao.
Ni vizuri kuzungumza kuhusu namna tulivyoingia katika mfumo huu. Rais Ali Hassan Mwinyi aliunda Tume ya Jaji Francis Nyalali iliyokuja na majibu kwamba ni asilimia 20 tu ya Watanzania ndiyo walitaka mfumo wa vyama vingi. Ni busara ya Mzee Mwinyi na viongozi wenzake wa wakati huo walioamua kusikiliza wachache. Kama wazee wetu wangesubiri mpaka asilimia 80 itake vyama vingi ndiyo tukubali, pengine leo tusingekuwa tulipo. Hili ni miongoni mwa mafunzo makubwa kwa wanasiasa wa kizazi changu na watakaokuja baadaye. Kwenye jambo la maslahi ya nchi, maarifa na busara ndiyo muhimu kuliko namba.
Kutoka kuwa na chama kimoja cha siasa – Chama Cha Mapinduzi (CCM), sasa tuna vyama vilivyosajiliwa takribani 20. Badala ya kusikia sauti moja na wakati mwingine tukisema “Zidumu Fikra za Mwenyekiti”, sasa Watanzania wanasikia kuhusu fikra za sauti tofauti. Kwa bahati nzuri, hata Mwenyekiti Mao alipata kusema “Acha maua 100 yamee kwa pamoja”.
Kipekee kabisa, nitumie nafasi hii kuwapongeza wote waliofanikisha safari hii. Viongozi wa CCM na Serikali walioona umuhimu wa kuruhusu vyama vingi kabla vita na vurugu havijatulazimisha na wanaharakati na wasomi waliokuwa wakisaidia kutuonyesha kuwa tunatakiwa kuingia katika mfumo wa vyama vingi.
Hata hivyo, yatakuwa makosa makubwa kama tutaona kuwa kazi ile imemalizika. Ninaamini, sasa tunapita katika mazingira yaleyale magumu yaliyokuwepo wakati tunaanza mfumo wa vyama vingi. Kuna vita katika maeneo mbalimbali duniani ikiwamo kwenye nchi zilizoendelea, mfumo wa kidemokrasia wa kiliberali unapitia katika changamoto na nchi kubwa zinapambana kuwania kutawala dunia. Ni changamoto ambazo viongozi wa kizazi chetu wanatakiwa kuzivuka kama walivyofanya watangulizi wangu.
Ndiyo sababu kwenye uongozi wangu ninaamini katika kile kinachojulikana kama 4R – ikiwa ni ufupisho wa maneno manne ya lugha ya Kiingereza; Reconcilation (Maridhiano), Resiliency (Ustahamivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuidlding ( Ukuaji).
Maridhiano
Katika tamthilia maarufu ya karne ya 19 ya Iolanthe, waandishi Gilbert na Sullivan walieleza jambo moja kuhusu taifa la Marekani wakati huo; ” Kila anayezaliwa ni ama mtoto mhafidhina au mtoto mliberali”. Mimi siamini kwenye misimamo ya namna hii. Kwamba mwanadamu, awe mwanasiasa, kiongozi au mwananchi wa kawaida, kuwa na msimamo usiobadilika kuhusu mambo yenye maslahi kwa taifa. Msimamo au hali fulani inaweza kueleweka au kukubalika wakati fulani lakini si wakati wote. Si wakati wakati wote ni wa kupongezana na si wakati wote ni wa kupingana.
Kwenye kujenga Tanzania bora ninatamani kujenga jamii yenye maridhiano na maelewano. Ninatamani kujenga umoja pasipo kujali tofauti zetu za kisiasa, kidini, kikabila na nyingine zote. Hili litawezekana kwa kujenga jamii inayopata haki sawa mbele ya sheria, isiyobaguana na inayotoa fursa sawa sawa za kiuchumi kwa wote. Ninaamini maridhiano hayawezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia.
Ustahamivu
Kama alivyopata kuasa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ujenzi wa taifa si kazi lelemama. Tanzania hii haiwezi kusonga mbele kama sisi wananchi na viongozi wenu tutakuwa legelege kulinda yaliyo yetu. Wahenga walisema Umoja ni Nguvu na namna pekee ya kupambana na changamoto zote zinazoikumba dunia kwa sasa ni kwetu sisi kufanya hivyo kwa Umoja na Mshikamano.
Huko tuendako tutatikiswa na kuyumbishwa. Iwe kiuchumi, kimazingira, kijamii na kisiasa lakini ni lazima tujenge ustahamivu. Hii ni kwa sababu hakuna nchi nyingine zaidi ya hii na hapa ndiyo kwetu. Nilitiwa nguvu sana na namna Watanzania walivyopokea tukio la Royal Tour kwa uzalendo wa kipekee.
Mabadiliko
Kuna msemo mmoja maarufu kwamba kitu pekee cha uhakika kwa mwanadamu ni mabadiliko. Nimedhamiria kwamba kwenye kuenzi miaka yetu ya demokrasia ya vyama vingi, serikali yangu itajitahidi kufanya mabadiliko katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi na katika sheria zetu za uchaguzi. Lengo ni kwamba Tanzania yetu iende na wakati na – kama ilivyokuwa wakati mwingine, tujue mapema ni wakati gani wa kufanya jambo hata kama si watu wanaliunga au hawaliungi mkono kwa wakati husika.
Mabadiliko katika sheria zetu za uchaguzi yataleta ushindani wa haki na kuwapa watu fursa ya kuwachagua wawatakao kuwaongoza. Kwenye uchumi, mabadiliko yatakuwa na lengo la kutoa fursa zaidi kwa watu wengi zaidi kunufaika kiuchumi badala ya wachache.
Ukuaji
Ninafahamu kwamba wananchi hawali maridhiano, ustahamivu wala mabadiliko. Mwisho wa siku – kama walivyofanya watangulizi wangu wengine kwenye karne hii; Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli, lengo kuu linatakiwa kuwa ukuaji wa uchumi wetu. Uchumi utakaoongeza ajira kwa vijana wetu na utakaofungua fursa kwa makundi yote ya kijamii yaliyo nchini.
Tayari tunaendeleza miradi mikubwa ya miundombinu na mengine kwenye sekta ya madini na nishati. Juhudi zilizofanywa kupitia kampeni ya Royal Tour zina lengo la kuzimua sekta muhimu ya utalii iliyoathiriwa sana na ugonjwa wa Covid 19. Katika kilimo tunakwenda kufanya mabadiliko mengine makubwa ili sekta hiyo muhimu ianze kuwa na mchango inaostahili kwenye uchumi wetu.
Ninaamini kwamba kwa jitihada zetu za R nne, tutaweza kutimiza malengo ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Lengo kuu halikuwa kuwa na vyama vingi vya siasa bali lengo lilikuwa kujenga jamii yenye uzalendo, maridhiano, ustahamivu na yenye uchumi unaokua kwa wote na endelevu. Hii ndiyo namna bora ya kuendeleza ndoto za wale waliopigania vyama vingi.
Kazi na Iendelee.