Na Ezekiel Kamwaga
TANGU aingie bungeni kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amekuwa na tabia moja inayomtofautisha na wabunge wengi – kwamba huwa haingii ndani ya viwanja vya Bunge jijini Dodoma kwa kutumia gari yake.
Badala yake huacha gari yake nje na kutembea kwa miguu kuingia ndani ya Bunge. Nimewahi kumwuliza wakati fulani kwa nini haingii ndani na gari na jibu lake lilionyesha busara kubwa; “Nataka kutumia dakika chache hizo kusalimiana na watu na kuzungumza na wale nitakaokutana nao njiani. Ukiingia na gari hadi ndani, unakosa muda – hata huo mdogo tu, wa kuzungumza na watu. Siasa ni watu”.
Ulega aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Februari mwaka huu, akipanda kutoka nafasi ya Unaibu Waziri wa wizara hiyo. Mtangulizi wake alikuwa ni Mashimba Ndani; ingawa pia alikuwa Naibu Waziri kwenye wizara hiyohiyo chini ya Luhaga Mpina kwenye utawala wa Rais John Magufuli.
Wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni wiki iliyopita, Mbunge huyu wa Jimbo la Mkuranga, tayari alikuwa mmoja wa mawaziri wanaozifahamu wizara zao vizuri kwani amekuwa wizarani hapo kwa takribani miaka saba sasa. Namna yake ya uwasilishaji bajeti na aina ya majibu ya maswali aliyojibu wabunge, ilionyesha pia kwamba anajua nini kinahitajika kufanywa kwenye eneo hilo.
Imesadifu pia kwamba Ulega ni mwanasayansi msomi wa masuala ya sayansi ya baharini aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ukiisoma bajeti ya wizara yake kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha wa 2023/2024, unaona namna sayansi na maarifa yanavyopewa nafasi ya kipekee.
Mifugo na Uvuvi Tanzania.
Kwa ujumla, sekta ya mifugo na uvuvi sasa inachangia asilimia 8.8 ya Pato la Taifa (GDP) la Tanzania. Katika asilimia hizo, mifugo inachangia asilimia saba huku uvuvi ukichangia asilimia 1.8. Kwa maana hiyo, kwa kutumia takwimu za mwaka jana za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umuhimu wa mifugo kwenye GDP unazidiwa na sekta za Ujenzi (16), Kilimo (14), Uzalishaji viwandani (9) na Uchuuzi wa bidhaa (9).
Kimsingi, mchango wa sekta ya mifugo kwenye uchumi wa Tanzania ulikuwa mkubwa zaidi kuliko hata madini yaliyokuwa yanachangia asilimia tano tu – ingawa, inasema BoT, katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2022, madini yalichangia asilimia 9.8 ya uchumi wa taifa letu.
Jambo ambalo mtu anaweza kuliona waziwazi kwenye takwimu zilizopo ni kwamba kama ilivyo kwa madini, mifugo na uvuvi pekee yake vinaweza kuchangia hadi kufikia asilimia 10 na kuzidi endapo mipango zaidi itawekwa kwenye kuboresha eneo hilo la kimkakati kiuchumi.
Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka huu imejikita katika mambo kadhaa ambayo kama yatafanyika, kuna uwezekano mkubwa kwamba ndoto za Serikali ya Rais Samia kuona sekta hizo mbili zinachangia zaidi kwenye GDP na kupambana na umasikini nchini zinafikiwa.
Katika mifugo, mkazo zaidi umewekwa kwenye kuongeza malisho ya wanyama (majani), huduma za kuboresha afya na ubora wa mifugo, kuchochea ufugaji wa kisasa na kutafuta zaidi masoko ya nyama na bidhaa za wanyama kama maziwa na ngozi katika nchi za nje.
Katika uvuvi, bajeti ya Ulega imejikita katika kusaidia wavuvi kupata zana za kisasa za uvuvi zikiwemo boti ili waweze kuongeza tija kwenye kazi zao, kuongeza udhibiti kwenye uvuvi hasa wa Bahari Kuu, kuimarisha uvuvi wa kwenye vizimba na kuboresha upatikanaji wa malisho ya samaki hapa nchini.
Kwa kuangalia uzoefu uliopatikana katika nchi nyingine, ni rahisi kufahamu kwa nini Ulega na wizara yake wameamua kufuata njia waliyofuata. Tatizo kubwa ambalo wachumi wengi wamekuwa wakilieleza kuhusu nchi nyingi za Afrika ni kuwa na uchumi usiofungamanishwa na shughuli nyingine za kiuchumi hasa zinazohusu wananchi wa kawaida.
Hili si tatizo la sekta ya uvuvi na mifugo. Katika bajeti iliyosomwa wiki iliyopita, Ulega alisema kwamba kiasi cha takribani shilingi trilioni 1.7 kilizungushwa kwenye mzunguko wa fedha wa ndani ya nchi kwenye sekta ya mifugo pekee – kuanzia mauzo ya wanyama halisi kama ng’ombe, mbuzi na kuku hadi kupitia katika mabucha na sehemu nyingine za biashara zinazohusu wala nyama. Hizi ni hela zinazozunguka ndani ya nchi.
Labda swali la kujiuliza ni nini kinaweza kutupa picha kwamba sasa wizara chini ya Ulega inaweza kuwa inakwenda njia sahihi. Mahali pazuri kuanzia ni kupitia ripoti mashuhuri ya mwaka 2020 iliyotolewa na taasisi ya Malabo Montpellier na kupewa jina la Meat, Milk and More. Ripoti hiyo ilichambua kwa kina sekta ya mifugo barani Afrika na namna inavyoweza kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye uchumi.
Ripoti hiyo ilitaja nchi nne barani Afrika kama kinara linapokuja suala la kuanza kufaidika na utajiri wa mifugo ilizonazo. Nchi zilizotajwa kama mfano kwenye ripoti hiyo ni Ethiopia, Mali, Uganda na Afrika. Hizi ni nchi zilizopiga hatua kubwa katika sekta hiyo na ripoti ilijikita katika kujua ni kwa vipi zimepiga hatua iliyopiga.
Kwa kifupi, ripoti inasema siri ya mafanikio ya Ethiopia – inayoongoza kwa wingi wa mifugo barani Afrika, Tanzania ikiwa ya pili, ni kujali zaidi afya ya mifugo yake na promosheni kubwa inayofanya kwa bidhaa zake. Mali inaelezwa kufanikiwa kwa kujali afya ya mifugo na kuweka nguvu kwenye suala la malisho ya wanyama. Uganda ni kwa sera za soko huria zilizofungua biashara ya maziwa na kuongeza uzalishaji huku Afrika Kusini ikipongezwa kwa kujali afya na kuongeza uwezo wa wafugaji kupata mikopo nafuu kusaidia biashara zao.
Kwa kufuata mfano wa wenzetu wa Afrika waliofanikiwa, inaonekana siri ya mafanikio iko kwenye mambo makubwa manne – afya njema ya mifugo, malisho ya uhakika, umuhimu wa promosheni kwa bidhaa za nchi husika na sera za nchi zinazotoa fursa kwa biashara kukua. Bajeti ya Ulega imejikita katika matatu kati ya hayo; pasi na shaka, hayo yakikaa vema, suala la promosheni litakuwa hatua kubwa inayofuata.
Afya njema ya mifugo itahakikisha mauzo ya bei nzuri zaidi kwa mifugo na kuaminika katika soko la nje ambako biashara haifanyiki pasipo kukidhi vigezo vya nyama vinavyokubalika. Hili litaweza kufanyika kwa kuchochea ufugaji wa kisasa na kuwa na vituo vya umahiri vya wafugaji vitakavyokuwa chachu kwa wafugaji wengine.
Ulega wa baharini
Waziri Ulega alikuwa sehemu ya utafiti wa karibuni zaidi wa masuala ya uvuvi ulioitwa; The Contribution of Marine Fisheries to Socio Economic Development in Mainland Tanzania uliochapishwa mwaka jana kwenye jarida la kisomi la Journal of Geographical Association of Tanzania (Vol 42). Utafiti huo uliangazia mchango wa sekta ya uvuvi kwenye maendeleo ya Tanzania na ulishirikisha wanasayansi wengine wa hapa nchini ambao ni maprofesa Yunus Mgaya, Reguli Mushy na Razack Lokina.
Pamoja na mambo mengine, utafiti huo ulibainisha kwamba wengi wa wavuvi wa Tanzania bado ni masikini na changamoto zao kubwa ni ukosefu wa mitaji na ukosefu wa zana za kisasa za uvuvi zikiwemo boti huku ikielezwa pia kwamba kunahitajika uvuvi na udhibiti zaidi kwenye maeneo ya Bahari Kuu ambako kuna nyakati kumegeuka kama shamba la bibi ambako meli kutoka mataifa makubwa zimekuwa zikija na kuvua pasipo udhibiti wa kutosha.
Ili kupambana na changamoto hizo, bajeti ya Ulega imeamua kuongeza mikopo kwa wavuvi wadogo ili wanunue vifaa vya kisasa vya uvuvi na serikali itanunua boti zaidi ya 100 ili kusaidia wavuvi kuvua kwenye maji ya kina kirefu. Serikali pia imetangaza nia ya kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Uvuvi ambayo itasimamia kwa kina sekta hiyo kama ambavyo EWURA inasimamia masuala ya mafuta au TANAPA na Hifadhi za Taifa.
Hata hivyo, ubunifu mkubwa zaidi katika bajeti ya uvuvi mwaka huu upo katika kuchochea uvuvi wa kutumia vizimba. Katika nyakati hizi ambapo teknolojia inaruhusu watu kufuga samaki badala ya kutegemea ratiba ya kuzaliana ya samaki, aina hii ya uvuvi inaweza kubadili kabisa sekta hii hapa nchini.
Tanzania ina vyanzo vingi zaidi vya maji kuliko Misri lakini taifa hilo la Afrika Kaskazini linaongoza Afrika nzima kwa kuzalisha tani za ujazo hadi milioni 1.8 kwa mwaka. Tanzania inazalisha wastani wa tani za ujazo 400,000 kwa mwaka. Ukubwa huu wa sekta umefanya uvuvi pekee kutoka ajira zaidi ya 800,000 nchini humo, kulinganisha na ajira 177, 000 kwenye sekta hiyohiyo nchini Tanzania – kwa mujibu wa mtandao wa WorldFish. Tunachovuna bado hakikidhi hata mahitaji ya ndani kwa vile mahitaji yetu ni tani walau 700, 000 kwa mujibu wa Ulega.
Ni muhimu kufahamu kwamba asilimia kubwa ya uvuvi nchini Misri, asilimia 80, hutegemea uvuvi wa kwenye vizimba. Msukumo mpya wa Ulega kwenye uvuvi wa vizimba unaweza kuwa mwokozi wa ajira kwa vijana wengi hapa nchini lakini pia kuongeza lishe bora kwa wananchi. Takwimu zinaonyesha kwamba Watanzania wengi hawali samaki kwa kiwango kinachotakiwa – karibu kilo 8.5 tu kwa mwaka, wakati wastani wa dunia ni walau kilo 20.5.
Ulaji wa samaki ni muhimu kwa protini na ukuaji wa afya ya mwili na akili. Katika nchi kama Korea Kusini, mtu mmoja hula wastani wa kilo 78 kwa mwaka. Pamoja na mambo mengine, utafiti wa akina Ulega na Mgaya ulibaini kuwa zipo familia za wavuvi ambazo umasikini unazifanya zishindwe kula samaki wanazovua na badala yake huuza tu.
Protini bungeni
Enzi za Urais wa Jakaya Kikwete, aliwahi kuibatiza wizara ya Ulega jina la Wizara ya Vitoweo ikimaanisha nyama na samaki. Siku moja wakiwa kwenye mazungumzo – wakati wa kuingia bungeni kama kawaida, Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, alipendekeza jambo moja kwa waziri huyo kijana; “Hivi kwa nini usiite wiki ya bajeti ya wizara yako – Wiki ya Protini?”.
Neno kitoweo humaanisha – kwa Waswahili wa pwani, kitu cha kutoezea chakula. Lakini, kwa mwanasayansi kama Ulega, protini iliyo ndani ya vitoweo ni neno pana na lenye maana zaidi kuliko kitoweo. Ushauri ule wa Shangazi ndiyo ukawa chanzo cha jina jipya la Wiki ya Protini.
Kama Ulega angetoka nyumbani kwake na kuingia na gari yake moja kwa moja bungeni, huenda asingekutana na Mbunge huyo wa Mlalo na kupata wazo hilo zuri kwa ajili ya kupromoti wizara yake. Hata hivyo, busara ya kuzungumza na watu ilimpa kauli mbiu nzuri ya kuanzia wiki iliyopita.
Na kama Ulega atabaki kuwa msikivu na muungwana – kama alivyojisema mwenyewe wakati wa hotuba yake ya kufunga bajeti, safari ya kubadili maisha ya wavuvi na wafugaji wa Tanzania itakuwa iko kwenye mikono salama. Na pengine maana halisi ya kaulimbiu yake ya #MifugoNaUvuviNiUtajiri itajidhidhiri.