Mkama Ndume na ukarimu wa Wapemba

Picha: Mwandishi wa makala haya, Mohamed Said, akishiriki chakula na wenyeji wake kisiwani Pemba hivi karibuni. Picha kwa hisani ya Mohamed Said

 

Na Mohamed Said

 

 

Wenyeji wangu wananitembeza kila sehemu Pemba. Ndani ya gari yetu kumetiwa maji ya kunywa, majamvi na viti vya kukunja ikiwa vitahitajika. Maji ya kunywa kuchukuliwa nimeelewa ila kilichonishangaza ni majamvi na viti. Sikuwa na ujasiri wa kuuliza. Nimebakia kimya.

 

Baadae nilijua kwa nini vitu hivyo vimebebwa. Wananipeleka Makumbusho kwa kupata utambulisho (induction) wa historia ya Pemba. Nimepitishwa archives (makavazini) kwa kuwa wananipeleka Pujini kwenye Ngome ya Mkama Ndume. Kwa kupitishwa Makumbusho nitaelewa vizuri nyakati, maisha na historia ya Mkama Ndume.

 

Wafanyakazi wa Makumbusho wametupokea vizuri sana. Jengo la Makumbusho ni kivutio tosha kwani msingi  ulijengwa na Wareno lakini hakuwapata kumaliza ujenzi baada ya Waomani kuingia na kuwashambulia kuwatoa Zanzibar yote. Waomani ndiyo wakaja kujenga hiyo ngome ambayo sasa ni jengo linalohifadhi historia ya Pemba.

 

Vitu vingi vimehifadhiwa hapa na kijana anayetupitisha katika historia ya Pemba hakika ni mweledi kwani anaeleza historia ya uchimbwaji wa eneo lile na majina ya wachimbaji hawa na paper walizoandika na “citation,” zake yaani rejea. Huyu ni kijana aliyesoma vizuri hapana shaka.

 

Vitu vilivyopatikana katika uchimbaji vyote viko hapo na maelezo yake. Idara ni nyingi na ya kuona ni mengi pia.

Huwezi kuchoka kutazama na kusikiliza. Historia ya kupigania Uhuru wa Zanzibar ni kivutio cha kutosha katika Makumbusho.

 

Picha za Kisima na Jogoo alama za uchaguzi za vyama vikubwa viwili vya siasa Zanzibar, Afro-Shirazi Party (ASP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP) zinakumbusha historia ya ushindani mkubwa wa siasa katika zama zile. Picha za wazalendo wa nyakati zile miaka ya 1950 zilizopo zinavutia sana kuziangalia. Unawaona wanasiasa hawa katika kilele cha ujana wao.

 

Kwangu mimi baadhi nimejaliwa kukutana nao na wengine kujuana kwa karibu lakini tayari walikuwa wameshaondoka Zanzibar wengi wao baada ya kifungo kirefu wako nchi za nje, Uingereza, Oman, Dubai na kwingineko. Namwangalia katika picha zile Juma Aley mwalimu wa Kiingereza na bingwa wa lugha hiyo akiwa kijana sana.

 

Nawaona Dr. Baalawy daktari wa meno niliyefahamiana naye Dubai, Ali Muhsin niliyekutana naye Muscat na Abdulrahman Babu niliyemjua Uingereza. Mwalimu Juma Aley nilimfahamu Tanga. Nilinunua kitabu chake Tanga na nikaelekezwa alipokuwa akifanya kazi mwandishi ikiwa nitapenda kumsalimu. Nilikwenda ofisini kwake na akanitilia saini kitabu changu. Kitabu hiki kilikuwa Maktaba kwa miaka mingi kisha kikatoweka.

 

Picha za wazalendo hawa wapigania uhuru wa Zanzibar zinasema maneno elfu moja. Historia ya Mkama Ndume ambaye jina lake khasa ni Mohamed bin Abdulrahman iko Pujini na ni kisa cha kipekee sana kinachoeleza ukomo wa juu wa ukarimu wa watu wa Pemba.

 

Mkama Ndume nimesoma habari zake Makumbusho na tukawaomba wenyeji watupe mwanahistoria atusindikize kwenye  ngome yake ili atupe maelezo ya kiongozi huyu ambae anaingia katika historia ya Zanzibar kama kiongozi wa jadi ingawa alitokea Uajemi (Persia).

 

Niliuliza swali hili na nikajibiwa kuwa Mohamed bin Abdulrahman kwa jina lingine alilopewa, “Mkama Ndume,” anahesabiwa kama ni kiongozi wa jadi. Nimetangulia kusema kuwa kupokelewa kwa Mohamed bin Abdulrahman Pemba akapewa ardhi na kufanywa mtawala ni ushahidi tosha wa kielelezo cha ukarimu wa watu wa Pemba.

 

Mtaalamu wa historia ya Pemba akawa anatutembeza ndani ya ngome ya Mkama Ndumbe huku akitupa mhadhara uliokuwa ukimmwagika kama maji. Anaeleza mwanahistoria kuwa Mohamed bin Abdulrahman alipendeza kwa wenyeji wake wa Pemba kwa kuwa alikuwa alim, mwanazuoni wa dini ya Kiislam na kutokana na ukoo wa Kisharif.

 

Mkama Ndume akawa Imam wa kuongoza sala na khatibu wa sala ya Ijumaa. Waislamu kutoka sehemu mbalimbali wakihudhuria sala ya Ijumaa msikitini kwake ndani ya ngome. Katika ngome ya Mkama Ndume kulikuwa na nyumba nyingi za ghorofa moja moja wakiishi watu.

 

Nyumba hizi kwa sasa hazipo lakini baadhi ya magofu yake yapo na nyumba zilijengwa kwa mawe. Ndani ya eneo hili kulikuwa na sehemu ya kufua chuma na kisima cha maji kinachojulikana kama, “Kisima Cha Wivu.” Hiki kisima kingali kipo hadi hivi sasa na inabidi ushuke chini ardhini kwa ngazi kukifikia.

 

Jina hilo la “Kisima Cha Wivu,” limetokana na sababu ya kuwa Mkama Ndume alikuwa na wake wawili ambao hawakupata kuonana na aliwawekea sehemu mbili za kuteka maji kila mtu kutumia sehemu yake ili wasionane.

 

Mkama Ndume alijenga gati lake alipokuwa anaegesha vyombo vyake akiteremkia hapo na kuingia kwake kila alipotoka safarini Mombasa alipokwenda kwa shughuli za serikali. Mfereji huu na mnara aliojenga upo hadi leo na wakati wa bamvua bahari inapojaa mawimbi yanapiga mabaki ya ngome iliyopo.

 

Ukisimama olipokuwa ngome gati unaitazama kwa chini. Yapo mengi sana ya kueleza kuhusu Mkama Ndume na wanawe ambao na wao walitawala sehemu ya Pemba. Wareno wakaingia Pemba. Mkama Ndume aliposikia taarifa hii kuwa meli za Wareno zimeingia na kutia nanga aliamua kuondoka Pemba kwa haraka yeye na wake zake wawili.

 

Hakutaka kukutana na Wareno.

 

Wanasema hakuna aliyejua Mkama Ndume alikwenda wapi. Hivi ndivyo ulivyokuwa mwisho wa utawala wa Mohamed bin Abdulrahman ambae anajulikana zaidi kwa lakabu ya Mkama Ndume aliyopewa na Wapemba. Tulipomaliza kuisikia historia hii tukatoka nje ya ngome.

 

Haraka wenyeji wangu wakatoa mikeka na viti wakaweka chini ya kivuli cha mwembe. Tulipokuwa njiani tulisimama nje ya hoteli moja nikaona vyakula vinatiwa katika gari. Haikunipitikia kuwa vyakula hivi vitaliwa katika staili hiyo unayoiona katika picha mfano wa chakula cha “picnic.”

 

Ngome ya Mkama Ndume inalindwa na jeshi na kuna wafanyakazi wengi pia. Wenyeji wangu wakatuma mtu kwenda kuwakaribisha waje tule chakula pamoja nasi wageni wao chini ya mwembe. Hawa ndiyo Wapemba ambao babu zao walimkaribisha Mkama Ndume Pemba miaka mingi sana iliyopita.

 

Wapemba hakika ni watu wakarimu wa kupigiwa mfano.

 

Mwandishi wa makala haya ni mwanahistoria na mwandishi wa vitabu mashuhuri hapa nchini. Kitabu chake Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes ni miongoni mwa vitabu vilivyosomwa zaidi nchini Tanzania