Na Ezekiel Kamwaga
MWISHONI mwa wiki hii, nilikuwa na mjadala mzuri katika mojawapo ya makundi sogozi niliyopo. Rafiki yangu mmoja alijenga hoja kwamba tatizo la akinamama kujifungulia sakafuni lililotawala sana katika vyombo vya habari na mitandaoni hapa nchini au mwenendo wa suala la Naibu Waziri wa zamani wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul, yasingetokea endapo hayati John Magufuli angekuwa bado Rais wa Tanzania. Kauli aliyotumia ilikuwa “Tutamkumbuka Magufuli”.
Kauli ile ilinirudisha nyuma kidogo. Sikutaraji kwamba mtu wa aina ya huyo rafiki yangu angeweza kutoa sentensi nyepesi ya aina ile. Kuna sababu kubwa mbili za mimi kusema hivyo. Moja ni kwamba si kweli kwamba hakukuwa na akinamama waliokuwa wanajifungulia sakafuni enzi za Rais Magufuli. Walikuwepo na ushahidi upo.
La pili, ni ukweli kuhusu uvumilivu wa Rais kwa watendaji wake wanaokutwa na makosa. Ambalo rafiki yangu hakulisema ni kwamba Rais kwa mamlaka yake tayari amemvua Gekul nafasi yake ya Naibu Waziri hata kabla vyombo vya haki havijachukua hatua.
Enzi za Magufuli, kuna wakuu wa mikoa na wilaya waliokuwa na tuhuma mbaya kabisa kuliko hata hizi za Gekul ambao walidunda na wanaendelea kudunda mitaani hata leo. Hawakuchukuliwa hatua yoyote wala kufikishwa mahakamani kwa vitendo vyao. Kusema kwamba kitendo kama cha Gekul – na niseme hili ni suala ambalo uchunguzi wake unaendelea kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali (DPP), kisingeweza kuvumiliwa wakati wa Magufuli ni usahaulifu wa makusudi – nikitumia lugha ya kiungwana kabisa.
Swali la kujiuliza ni kwamba kwa sababu gani Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ambaye ni mmoja wa mawaziri wachapa kazi katika Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ghafla anaonekana hatimizi majukumu yake au watu wanasahau matukio ya kutisha na ya hovyo zaidi yaliyowahi kutokea wakati wa mtangulizi wa Rais Samia? Jibu ni moja tu; Uhuru wa kujieleza.
Mimi nakumbuka kwamba enzi za utawala wa Magufuli, shida ya kwanza ilikuwa ni kueleza matatizo au kasoro zilizokuwepo serikalini wakati ule. Nakumbuka wakati fulani kuna mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipiga picha zilizoonyesha nyufa katika majengo ya Hosteli za Magufuli na kilichompata baadaye kilikuwa ni funzo kuwa yeye na wenzake walipaswa kuwa kimya. Kuna mengi hayajulikani ya enzi za Magufuli kwa sababu hakukuwa na wa ya kuyapiga picha na kusambaza mitandaoni. Wote tuliufyata.
Mtihani ambao Waziri Ummy na wenzake – na mtihani wa Serikali ya Rais Samia, inao ni kuwa sasa wananchi wako huru kupiga picha na kueleza kasoro zote wanazoziona kuanzia kwenye huduma za serikali na changamoto nyingine za maisha wanazokutana nazo.
Tanzania bado ni nchi inayoendelea na changamoto ziko nyingi. Uwepo wa mitandao ya kijamii na uhuru wa kujieleza ulioongezeka sasa unamaanisha kwamba kila kasoro na kila tatizo vitakuzwa mara kumi au zaidi kulingana na ukubwa wake. Huu ni mtihani ambao haukuwepo wakati wa Awamu ya kwanza mpaka walau Awamu ya Tatu. Mtihani mkubwa zaidi ni kwamba baada ya mwaka 2010, mitandao imekuwa na nguvu zaidi katika siasa kuliko wakati mwingine wowote kwenye historia ya mwanadamu.
Nchi yetu haina huduma za kutosha za afya kwa watu wake. Lakini miaka michache iliyopita, ndiyo nchi iliyoanzisha Bima ya Afya kwa wananchi iliyowezesha ongezeko kubwa la upatikanaji wa huduma za afya. Mjadala unaoendelea sasa wa Bima ya Afya unatokana zaidi na mafanikio na uelewa ambao Watanzania wameanza kuwa nao kuhusu bima. Kama Bima ya Afya hatimaye itafikia kiwango cha wananchi wengi zaidi kufaidika nayo kwa gharama nafuu – nchi yetu itakuwa imepiga hatua kubwa sana.
Wiki hii nilikuwa nasikiliza mazungumzo ya Balozi wa Tanzania nchini Cuba na Jenerali Ulimwengu na akazungumzia ukweli kwamba Tanzania tayari ina huduma za kimatibabu za mifupa na moyo ambazo haziko katika nchi za Afrika. Kama Mtanzania ana ugonjwa wa moyo, uwezekano wa kupata huduma kwa gharama nafuu ni mkubwa kuliko katika nchi nyingi za Afrika. Somo kubwa lilikuwa kwamba kulinganisha na wenzetu wengi, Tanzania walau inaanza kupiga hatua.
Lakini bado idadi ya akinamama wanaokufa wakati wanajifungua ni kubwa. Lakini ni bahati pia kwamba huu ni wakati pekee katika historia ya nchi yetu ambapo Rais aliye madarakani amezungumza waziwazi kuwa jambo la kuzuia wazazi wasife wakati wa kujifungua na vifo vya watoto wachanga ni masuala yaliyo karibu zaidi na moyo wake kuliko mengine. Kama kuna wakati suala hili linafanyiwa kazi kwa kina, basi wakati huo ni huu.
Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka huu pekee inafikia kiasi cha shilingi trilioni 1.2 na kuna kiasi kikubwa cha fedha kimetengwa kwa ajili ya eneo hilo. Hata hivyo, changamoto za namna hii – kama lile tukio la mkoani Geita lililoleta tafrani mitandaoni yataendelea kuwepo.
Namna pekee ya kushughulika na masuala ya namna hii ni kuzidi kuongeza fedha kwenye eneo hilo la huduma kwa wazazi na kuhakikisha hata pale ambapo rasilimali hazijafika za kutosha, kunakuwa walau na kiwango cha chini kabisa cha utu ambacho hospitali na vituo vya afya vinaweza kufanya ili wahusika waone wamesitirika. Njia rahisi kuliko zote ilikuwa ni kuanza upya kubana watu na taarifa lakini hiyo si namna endelevu.
Namna endelevu – kwa sasa, ni kuhakikisha changamoto hizo zinamalizwa lakini wakati huohuo, kutengeneza mazingira ambayo wahusika wa kada ya afya na nyingine za namna hiyo wanajua wajibu wao na kuweka mazingira ya stara kwa akinamama na akinababa ambao aina ya magonjwa yao yanaweza kuwaondolea stara.
Ni mtihani lakini ni muhimu zaidi kuachia watu uhuru wa kuzungumza na kuonyesha kero zilipo. Huo ndiyo msingi wa demokrasia.