Muungano @59: Israel ilihusika mwaka 1964?

Picha: Marais Julius Nyerere wa Tanganyika na Abeid Amani Karume wakitia saini Hati za Muungano.

Na Ezekiel Kamwaga

MARA ya kwanza kusikia jina la Misha Feinsilber ilikuwa wakati niliposoma – kwa mara ya kwanza pia, kitabu adhimu cha Harith Ghassany “Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru (2010) ” takribani muongo mmoja uliopita.

Mara ya pili ikawa kwenye mahojiano niliyowahi kuyafanya jijini Dar es Salaam na aliyekuwa mke wa mwanasiasa na mwanazuoni nguli wa Kizanzibari, hayati Abdulrahman Omar Babu, Bi Ashura, ambapo jina hilo liliibuka pia.

Huyu Misha – wengine wakimwita Mischa, alikuwa nani? Kwa Ghassany alitambulishwa kama mfanyabiashara aliyetoa boti iliyowarejesha Zanzibar akina Babu kutoka Dar es Salaam walikokuja kujificha mara baada ya Mapinduzi. Kwa Bi. Ashura, alitajwa kama mmoja wa marafiki wa wana mapinduzi wa wakati huo.

Kuna utambulisho mwingine muhimu kumhusu Misha. Huu ulifanywa kupitia makala iliyochapwa kwenye gazeti la Oman Observer la Februari 5 mwaka huu na mwandishi Nasser Bin Abdul Al Riyami (https://www.omanobserver.om/article/1132280/features/oman-in-fact/remembering-a-dawn-that-changed-fate-of-zanzibar-part-4). Humu, Misha anatambulishwa kama “Balozi asiye rasmi wa Israel nchini Tanzania). Ghassanny na Ashura wote walimtaja kama “Myahudi” ikimaanisha uhusiano na taifa la Israel.

Rekodi rasmi za kibalozi zinaonyesha kuwa Balozi wa Kwanza wa Israel nchini Tanganyika alikuwa ni Joseph Ruppin aliyekuja mwaka 1962 na akafuatiwa na Yitzhak Pundak, aliyekuja Novemba 1965. Hata hivyo, Riyami anasema hapa nchini, Misha alikuwa na ushawishi unaofanana na wa balozi wake.

Ilikuwa ni bahati tu kwa Misha kutoa boti yake kuwarejesha akina Babu Zanzibar? Ilikuwaje akajikuta kuwa katikati ya tukio kubwa zaidi katika historia ya miaka ya karibuni ya visiwa hivyo?

Kumwelewa Misha ni kuelewa historia ya uhusiano wa Tanzania na Israel. Kuelewa historia hii, ni kuelewa pia sababu kwa nini taifa hilo la Mashariki ya Kati huenda lilikuwa na mkono katika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na pengine Muungano na Tanganyika uliofuata miezi mitatu baadaye.

Akindika katika Journal of African Modern Studies mwezi Agosti mwaka 1971, Dk. Abel Jacob wa Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza, aliandika kwamba chanzo cha uhusiano wa kiserikali kilianza mwaka 1959 wakati wa ziara ya aliyekuwa Kiongozi wa Umoja wa Vijana wa TANU, Joseph Nyerere – mdogo wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kwenye mkutano wa vijana.

Uhusiano ulikuwa kuwa mzuri kiasi kwamba kufikia mwaka 1964, anaandika Jacob, Tanzania ilikuwa nchi ya tatu kwa kupokea misaada mingi ya kijeshi na kiuchumi kutoka Israel.

Andishi hilo la Jacob limezitaja nchi nyingine zilizokuwa zinapata misaada kwa wingi kutoka Israel kuwa ni Ethiopia, Kenya, Ghana, Uganda, Zambia na Sierra Leone.

Kwa nini Israel, ambayo haikuwa na uchumi mkubwa kama Marekani, Uingereza, Ufaransa au yenyewe ilivyo sasa, ilikuwa inatoa msaada mkubwa kwa nchi za Kiafrika? Jibu hilo limejibiwa na Jacob – kwa sehemu, lakini Profesa wa Historia katika Chuo Kikuu cha Regis kilichopo Denver, Colorado, Ethan Sanders, amelijibu kwa kina zaidi.

Katika andishi lake; A Small Stage for Global Conflict: Decolonization, the Cold War and Revolution in Zanzibar, Profesa Sanders anasema lengo la Israel lilikuwa ni kuhakikisha nchi za Afrika haziungi mkono Misri na Wapalestina kwenye mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Ni kwenye chapisho hilo la Sanders ndipo jina la Misha linapoibuka kwa mara nyingine. Sanders anasema misaada mingi ya masuala “nyeti” ya Israel kwa Tanganyika na Zanzibar ilikuwa inapitia mikononi mwa Misha.

Ni rahisi, kwa kufuata mstari huu, kuona kwamba katika masuala nyeti kama ya kuwaficha au kuwasafirisha akina Babu kurudi kwao, ni lazima Misha alikuwa na kibali cha taifa lake kufanya jambo hilo.

Nikiiba nukuu kutoka kwenye andiko la Jacob, “tusipofanya sisi, Sadat atakuja hapa”, akili ya Israel ilikuwa kwamba namna ya kuwa salama pale ilipo ni kuhakikisha jirani zake hawapati msaada kutoka majirani zao.

Uhusiano wa Israel na Tanganyika ulikuwa mkubwa kufikia 1964. Ni Israel ndiyo ilikuwa imetoa mafunzo kwa askari Polisi wa Tanganyika kiasi kwamba tukawa taifa la kwanza lenye Polisi wa Kikosi Miavuli barani Afrika.

Ni kutokana na uhusiano wetu na Israel ndiko tulikopata wazo la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Andiko la Jacob lina maelezo mazuri sana kuhusu kilichotokea baada ya uasi wa Jeshi la Tanganyika mwaka 1964.

Kilichotokea, ameandika Jacob, ni kwamba Serikali ya Tanganyika iliamua kuchukua vijana waliokuwa kwenye mafunzo ya JKT chini ya Israel na kuwageuza kuwa wanajeshi wa kwanza wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika korido za utawala nchini Israel, kulikuwa na furaha kwamba jeshi lililoanza lina askari wengi waliofunzwa nao. Baadaye Ujerumani ilikuja kutoa mafunzo pia kwa Jeshi la Tanzania.

Ni Jacob pia aliyeandika kwamba mgogoro wa awali wa Tanzania na Israel ulianza baada ya serikali ya Nyerere kuachia wakufunzi wa kijeshi kutoka Canada kuvaa sare zao za kijeshi hadharani – ilhali ikikataza wale wa Israel kufanya hivyo “isipokuwa katika matukio muhimu”.

Hivyo, wakati Tanganyika na Zanzibar zinaungana mwaka 1964, Polisi waliofuzu zaidi walikuwa wale waliokwenda Israel na vijana kutoka JKT iliyofunzwa na israel ndiyo walikuwa uti wa mgongo wa jeshi la kizalendo.

Kwa nini Israel ilikuwa na maslahi na Muungano wa Tanzania? Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilikuwa na wanasiasa wa aina ya Babu, Badawi Quillatein na wengine ambao ilijulikana kwamba wasingekubaliana na vitendo vya Israel kwa Wapalestina.

Ikumbukwe kwamba katika teuzi za awali kabisa za SMZ ilikuwa ni kumpeleka Salim Ahmed Salim kuwa balozi nchini Misri. Ni Misri pia ndiko yalikokuwa Makao Makuu ya iliyokuwa Radio maarufu kwenye harakati za Ukombozi wa Afrika, Radio Free Africa.

Mtangazaji kinara wa redio hiyo alikuwa ni Mzanzibari, Ahmad Rashad Ally, na alikuwa akifahamika hata kwa aliyekuwa akionekana kama adui namba moja wa Israel, Rais Gamal Abdel Nasser wa Misri.

Zanzibar ya namna ile isingekuwa nzuri kwa Israel. Kwa upande mwingine, walau katika siku za awali za Uhuru, Tanganyika ilionekana kama ingeweza kuwa rafiki mzuri wa taifa hilo linaloongozwa na Benjamin Netanyahu hivi sasa.

Nionavyo ni kwamba msaada wa Misha kwa akina Babu ulitokana zaidi na msukumo kutoka kwa rafiki zao waliokuwa Tanganyika kuliko Wazanzibari.

Nionavyo ni kwamba kabla boti ya akina Babu haijatia nanga Unguja, inawezekana tayari mipango ya kufanikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tayari ilikuwa mezani.

Na hata kama wanahistoria kama Joseph Mihangwa wamekuwa wakieleza mchango wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na aliyekuwa Balozi mdogo wa taifa hilo hapa nchini, Frank Charles Carlucci III, kwenye kufanikisha jambo hili kubwa, nafikiri Waisraeli hawakuwa mbali.

Muungano wa Tanzania ulikuwa na maslahi kwao pia.

Mwandishi wa makala haya ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi aliyefanya kazi hiyo ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 20. Ndiye Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Dunia.