Mwisho wa fungate ya Rais Samia

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

MWANAFALSAFA wa Ufaransa, Alexis de Tocqueville, alipata kunukuliwa akisema; “the most dangerous moment for a bad government is when it begins to reform itself” (wakati wa hatari zaidi kwa serikali isiyo ya kidemokrasia ni wakati ikianza kujirekebisha). Msomi huyo alikuwa anafanya uchambuzi wa nini kilisababisha Mapinduzi ya Ufaransa (1789 -1799) lakini kauli yake hiyo ina mantiki hadi leo.

 

Usemi huo ndiyo msingi wa dhana ya revolution of rising expectation (mapinduzi kutokana na matarajio yaliyoongezeka) inayotumiwa sana na wataalamu wa sayansi ya siasa. Wakati fulani nilimsikia mbunge na waziri mstaafu, Profesa Anna Tibaijuka, akiizungumzia bungeni kwa kutumia msemo wa “kila unavyozidi kupanua, inabidi upanue zaidi”. Wakati ule ilichekesha baadhi ya wabunge kwa sababu ya tafsiri yao ya lugha ya Kiswahili lakini alichosema ndiyo halisi ilivyo.

 

Muktadha huo ndiyo unaakisi mahali ulipo utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan hivi sasa. Kwa vigezo vyote vya kidemokrasia na utawala bora, urais wa Samia ni bora kulinganisha na ule wa mtangulizi wake, hayati Dk. John Magufuli. Lakini, ni ukweli pia kwamba chama kilicho madarakani ni kilekile, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mifumo yote ya utawala imebaki ileile.

 

Kwa kufuata nadharia ya Tocqueville, kitendo cha Rais Samia kutaka kufanya marekebisho ya kile kilichokuwa kinafanyika wakati wa utawala wa Rais Magufuli – wakati chama ni kilekile na serikali ni ileile, ni jambo la kijasiri kwake binafsi na kwa chama chake kufanya kwa sababu matarajio ya wananchi yameongezeka na hamu ya watu waliozibwa pumzi kwa muda mrefu kutaka kuzungumza imerejea.

 

Kama kuna kitu kimeonyesha wazi mahali nchi yetu ilipo sasa ni suala la mkataba wa bandari uliowasilishwa bungeni wiki iliyopita kwa ajili ya kuridhiwa. Tangu Rais Samia aingie madarakani, pengine hili ndilo suala kubwa zaidi la kwanza kuhusu utawala wake ambalo limezua mijadala hasi iliyo mizito mitandaoni, kwenye vyombo rasmi vya habari na miongoni mwa wananchi.

 

Bila kuingia katika kilichomo ndani ya mkataba huo, kuna mambo mawili ambayo ni muhimu kuyasema kuhusu suala hilo. Mosi ni ukweli kwamba jambo hili linajadiliwa kwa uwazi na watu wengi zaidi  kwa sababu – pamoja na mambo mengine, Rais ameamua kufuata sheria inavyotaka ya kulipeleka jambo hili bungeni ili lijadiliwe. Njia rahisi – ambayo haina maslahi ya taifa, ilikuwa ni kuvunja sheria na kulipitisha jambo hili kimyakimya.

Jambo la pili ni uhuru wa kutoa maoni uliosababisha watu wengi zaidi kuchangia kwa uwazi zaidi hilo kuanzia mitandaoni na kwingineko. Wakati wa utawala wa Magufuli – pia mwana CCM kama alivyo Samia, kulianza kujengeka woga ndani ya jamii kwenye kujadili masuala ambayo serikali haikupenda kusikia. Kwa hiyo uhuru huu wa kutoa maoni umesababisha pia mjadala kuwa mkubwa kuliko ambavyo ingekuwa kama wananchi wangekuwa waoga kuchangia.

 

Kwa maana hiyo, upinzani huu mkubwa ulioonekana kuhusu suala hilo la bandari na mtikisiko ambao umeikumba serikali ya Samia kwa kiasi fulani ni zao la aina ya utawala ambayo ameamua kuifuata tangu aingie madarakani. Kwa maneno mengine, kama Samia angeamua kufuata njia na staili ya mtangulizi wake, pengine hali iliyopo sasa isingekuwepo au isingekuwa kwa ukubwa iliyoupata sasa hivi.

 

Kama kuna kitu ninakiona katika sakata hili la bandari, ni matukio mawili makubwa katika utawala wa Rais Samia kuangukia katika wakati mmoja; kuongezeka kwa matarajio ya wananchi kwa utawala wake na kufikia mwisho kwa bando la fungate la kisiasa alilokuwa nalo tangu aingie madarakani.

Ninaposema fungate ninamaanisha kipindi ambacho Rais aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza hupewa na wananchi wae kuweka mambo yake sawa. Huu ni wakati ambapo hana baya alilofanya kwa wananchi wake na kama kuna mapungufu yoyote, karibu yote yataelekezwa moja kwa moja kwa mtangulizi wake.

 

Fungate za marais wa Tanzania

 

Kihistoria, tangu Uhuru wa Tanganyika na Muungano na Zanzibar, marais wa Tanzania wamekuwa na wastani wa kipindi cha fungate ya kisiasa (political honeymoon) na wananchi wao kwa kipindi cha kati ya miaka miwili hadi mitatu kabla mambo hayabadilika na kipindi chao cha urais kuanza rasmi.

 

Fungate ya Mwalimu Nyerere iliisha Januari mwaka 1964 wakati wa Maasi ya Jeshi la Tanganyika yaliyosababisha achukue uamuzi mgumu ikiwamo kulivunja na kuanzisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuingia kwenye mfumo wa siasa wa chama kimoja mwaka 1965 na baadaye Azimio la Arusha la mwaka 1967.

 

Fungate ya Benjamin Mkapa iliisha wakati wa kashfa ya minofu ya samaki na mafuta ya kula iliyosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Profesa Simon Mbilinyi na Naibu wake, Kilontsi Mporogomyi. Kama utafuatilia urais wa Mkapa, utabaini mengi ya mambo yanayoutambulisha urais wake sasa yalianza baada ya tukio hilo kubwa kisiasa kwake.

 

Rais Jakaya Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005 kwa kura nyingi pengine kuliko mgombea mwingine yeyote wa urais katika historia ya uchaguzi wa vyama vingi hapa nchini. Hata hivyo, fungate yake ya kisiasa ilimalizika rasmi baada ya tukio la kashfa ya Richmond lililosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

 

Sina hakika sana kama utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi ulimaliza fungate lake katika mabadiliko yaliyomwingiza Kikwete kwenye baraza la mawaziri kwa mara ya kwanza mwaka 1988 na kumwondoa mwanasiasa mkongwe Al Noor Kassum na Magufuli kwa tukio la Operesheni Ukuta iliyopangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia maandamano yasiyo ya kikomo. Hata hivyo, nadhani matukio hayo mawili yaliashiria rasmi kuanza rasmi kwa urais wa wawili hao.

 

Tukio hili la mkataba wa bandari baina ya Tanzania na Dubai, halijasababisha waziri yeyote kung’oka madarakani au Samia kuonyesha nguvu yake ya kijeshi kama Amiri Jeshi kuzuia watu wasiandamane kama alivyofanya Magufuli wakati wa Operesheni Ukuta, lakini naliona likiwa linahitimisha fungate yake ya kisiasa kwa Watanzania.

 

Urais wa Samia Suluhu Hassan ‘unaanza’ rasmi baada ya tukio hili la bandari. Kuanzia sasa, makosa yake na mazuri yake yataanza kuhesabika kwa kutumia matendo yake akiwa madarakani na si kabla ya hapo. Maadui na marafiki aliowatengeneza katika suala hili la bandari, ndiyo watabaki kuwa hivyo katika siku zake za urais zilizobaki.

 

CCM na Ancien Regime

 

Katika uchambuzi wake wa utawala wa kifalme wa Ufaransa uliotangulia Mapinduzi (Ancien Regime), Tocqueville alijenga hoja kwamba kilichotokea ni kwamba wananchi walichoka na kila kitu kuhusu utawala huo – kuanzia Mfalme na wale wote waliokuwa wakiutetea; wakiwemo viongozi wa Kanisa. Walichotaka wananchi ni mabadiliko ya mfumo mzima.

 

Uchambuzi wangu ni kwamba Tanzania bado haijafikia kiwango hicho, tipping point, ambapo wananchi kwa ujumla wao, wanahitaji mabadiliko ya mfumo mzima wa utawala. Kama nataka kuwaza suala la tipping point kwa mfumo wa mimba, ni kuwa ujauzito bado haujafikia miezi tisa.

 

Jambo ambalo Rais anapaswa kulifanya kuanzia sasa na kuendelea na kubaki kuwa Rais wa Mabadiliko na Mwendelezo. (Continuity and Change). Kuna mambo mazuri ambayo watangulizi wake – Nyerere, Mwinyi, Mkapa, Kikwete na Magufuli waliyafanya anatakiwa kuyaendeleza lakini wakati huohuo akiendelea kufanya mabadiliko kwa mambo ambayo wananchi na mwenendo wa dunia hivi sasa unataka.

 

Wafaransa waliamua kujenga jamii ya watu walio sawa na wanaoheshimiana baada ya kuondoa ancient regime. Watanzania tulifundishwa kujenga taifa lenye Umoja na Mshikamano. Kila Rais wa Tanzania ana jambo la kufaa kwenye utawala wake – Mwinyi alitoa uhuru kwa watu, Mkapa alijenga taasisi, Kikwete aliimarisha uchumi na demokrasia na Magufuli alijenga vitu vinavyoonekana kwa wananchi.

 

Kazi ambayo Rais Samia atakuwa nayo kuanzia sasa ni kufuata nyayo za watangulizi wake kwenye nafasi hiyo kwa kufanya yafuatayo; kujenga uchumi, kufanya siasa za mambo yanayoonekana kwa macho na wananchi, kujenga taasisi imara zitakazodumu miaka mingi baada ya urais wake, kujenga uchumi imara wa taifa letu na wakati huohuo, kuendelea kuachia watu watoe maoni kuhusu mwelekeo wa taifa lao.

 

Bahati nzuri, mwisho wa fungate huwa haumaanishi mwisho wa kipindi cha Rais kubaki madarakani. Badala yake, mwisho wa fungate humaanisha kuanza rasmi kwa kipindi cha Urais kwa yule aliyepewa nafasi hiyo wakati huo.

 

Sasa, ndiyo urais wa Samia Suluhu Hassan ‘umeanza’ rasmi.

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha SOAS nchini Uingereza.