Namna Rais Samia ‘alivyoiteka’ India

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

NIANZE kwa kutumia takwimu kueleza kile nilichopanga kuandika kwenye makala haya.

 

Katika siku nne ambazo Rais Samia Suluhu Hassan alikaa nchini India, Oktoba 8 mpaka 11 mwaka huu, kuna siku mbili ambazo jina lake liliongoza kwa kusakwa kupitia mitandaoni na raia wa taifa hilo.

 

Siku ya kwanza ilikuwa Oktoba 9 na kisha Oktoba 10 hali ikawa hivyo. Kama isingekuwa kuwepo kwa mechi ya mchezo wa Kriketi baina ya Pakistan na Sri Lanka Oktoba 8, kuna kila dalili kwamba huenda Rais Samia angekuwa namba moja. Nchini India, kriketi inapendwa pengine kuliko hata Watanzania wanavyopenda Simba na Yanga.

 

Ilikuwaje mitandaoni, magazeti na kwenye vituo vya televisheni Rais wa Tanzania ali trend kuliko kawaida? Nilikuwa India wakati wote wa ziara hiyo ya Samia na nadhani nina nafasi nzuri ya kuweka muktadha wa hali hiyo.

 

Muktadha

 

Ni muhimu kufahamu muktadha wa hali hii. India imetoka kuandaa mkutano wa mataifa tajiri duniani wa G20 ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo. Pia, sasa inajulikana kuwa India ni ya tano kwa uchumi mkubwa duniani; ikiwa imezidiwa na Marekani, China, Japan na Ujerumani tu.

Hata hivyo, viongozi wa India wanaamini kuwa kufikia mwaka 2027 – kama uchumi wake utaendelea kukua kwa spidi ya sasa, taifa hilo litazipiku Japan na Ujerumani. Propaganda, rekodi na siasa za India za sasa chini ya Waziri Mkuu, Narendra Modi, zimewatia shime viongozi na raia wa kawaida wa taifa hilo.

 

Ziara ya Rais Samia ilikuwa ya kwanza kufanywa na kiongozi kutoka Afrika mara baada ya mkutano huo. Imefanywa katika wakati ambapo India inajiona kuwa sasa ni taifa kubwa na lenye nguvu. Ilikuwa vizuri kwamba Samia aliingia India katika wakati ambapo taifa zima linajisikia fahari na kiongozi miongoni mwa nchi zinazotafuta maendeleo kama Tanzania.

 

Lakini Samia naye alifanya kitu kilichosababisha vyombo vya habari vidake ujio wake kwa mikono miwili; jambo hilo ni kutoa hotuba iliyoipongeza India kwa maandalizi mazuri na yenye mafanikio ya mkutano wa G20. Pengine, Rais huyo wa Tanzania ndiye alikuwa kiongozi wa kwanza nje ya wale waliohudhuria G20 aliyetoa pongezi hizo. Huo ulikuwa sawa na muziki kwenye masikio ya vyombo vya habari na raia wa India.

 

Tanzania si taifa kubwa na lenye nguvu duniani. Tanzania si Ukraine au Israel/Palestina zinazoandikwa sana kwenye vyombo vya India hivi sasa. Tanzania haiuzi vifaru au ndege za kijeshi kwa India. Wala si China wala Pakistan ambazo India ina uhasimu nazo. Ili ziara ya Rais Samia ipate umuhimu kwenye vyombo hivyo, ilitakiwa aseme kitu kitakachokonga mioyo na fahari yao. Hotuba ya Rais Samia ilipiga kunako.

 

Rais Samia si tu aliishia kwenye kuisifu India kwa kuandaa mkutano vema lakini aliitaja India kama taifa lililo rafiki wa kweli wa Afrika, akieleza kuhusu namna ilivyopambana kuhakikisha bara hili la weusi linawakilishwa kwenye G20 kupitia Umoja wa Afrika (AU).

 

Nikune, nikukune

 

India sasa inatamani kuwa kinara kwenye teknolojia ya sasa. Katika vitu ambavyo vinaumiza vichwa vya India vinahusu ni namna gani wataweza kupata madini yatakayosaidia kutengeneza betri za magari ya kisasa. Hadi sasa, India inaagiza kwa asilimia 100 madini ya Lithium yanayotumiwa kutengeneza betri hizo.

 

Ujumbe wa Rais Samia kwenye ziara hii ulikuwa kwamba Tanzania ina madini na malighafi za kutosha kwa ajili ya kusaidia India kuwa vinara katika teknolojia za kileo.

 

Ombi la Tanzania kwa India lilikuwa kwamba badala ya kuhangaika kuagiza Lithium ghafi, India inatakiwa kuja kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza nchini Tanzania kwa kutumia malighafi iliyopo nchini.

 

India inahitaji malighafi kwa ajili ya viwanda vyake vikubwa na wakati huohuo, Tanzania ina madini na malighafi nyingine na inachohitaji sasa ni mitaji kwa ajili ya kuvuna rasimali hizo.

 

Ni vigumu sana kuona ni namna gani Wahindi wangekuwa na mshawasha na safari ya Rais Samia endapo angekuwa hana kitu mkononi cha kuwaambia “ninacho mnachotaka, mnipe ninachotaka na sote tufaidi”. Tanzania pia ina utajiri wa makaa ya mawe na gesi ambavyo ni muhimu kwa uchumi wa taifa lolote linalotaka kupiga kasi katika uzalishaji kama India.

 

Ushawishi wa Makamba na Jainshankar

 

Kuna siri huwa haisemwi sana kuhusu nini has ani thamani ya Waziri wa Mambo ya Nje au balozi katika nchi husika. Katika duru za kidiplomasia, inafahamika kwamba thamani ya waziri au balozi ni ukaribu wake na Rais wa taifa analowakilisha.

 

Nchi husika zinafahamu kwamba endapo waziri wa mambo ya kigeni ana ukaribu na rais husika, ina maana hakuhitajiki njia nyingi kufikisha jambo katika ofisi kubwa.

 

Kama kuna kitu kilikuwa wazi katika ziara hii ni ukaribu baina ya kwanza; Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, January Makamba, mwenzake wa India, Subramahyan Jainshankar na pili ushawishi walionao kwa mabosi wao; Rais Samia na Waziri Mkuu Modi.

 

Wawili hawa wanafahamika kwamba wana masikio ya mabosi wao. January na Jainshankar walikutana na kufanya mazungumzo kabla ya viongozi wao kukutana. Ni wazi walikubaliana kuhusu namna iliyofaa kuipa ziara hiyo ukubwa iliostahili.

 

Ndiyo sababu dhumuni kubwa la ziara lile; la kupandisha hadhi ya uhusiano kuwa ya kimkakati, iliyoruhusu faida nyingine zote kufuatia, lilifanikiwa.

 

Katika taifa lenye migawanyiko kuanzia ya kidini, kikanda, kisiasa, kifamilia, kitabaka na hata kivyama, ulimi wa Rais Samia ungeweza kuteleza kwa dakika moja kwenye tukio moja na kuleta vichwa vya habari visivyofaa. Lakini maandalizi ya mapema ya mawaziri wa mambo ya nje yalizuia kutokea kwa hilo.

 

Marais wanawake

 

Sami ani Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania. Rais wa sasa wa India, Droupadi Murmu, ndiye mwanamke wa pili kushika wadhifa huo nchini humo. Kwa baadhi ya vyombo vya habari na mitandao, kuwa na marais wawili wanawake kwenye tukio moja lilikuwa tukio adhimu.

 

Ni muhimu pia kufahamu historia ya Murmu. Huyu ni Rais anayetoka katika makabila ya pembezoni ambayo zamani hayakuwa yakipewa nafasi za uongozi. Ukimtazama kwa rangi, Murmu ni mweusi.

 

Lakini kuna historia nyingine inayofanya vyombo vya habari vya India view na upendeleo wa kipekee kwa Rais Droupadi; na hiyo ni historia. Huyu ni mwanamke ambaye amekumbwa na masahibu makubwa kwenye maisha yake.

 

Aliolewa kwenye miaka ya 1980 na kubahatika kupata watoto watatu; wawili wa kiume na mmoja wa kike. Hata hivyo, amepata bahati mbaya ya kufiwa na mume na watoto wake wawili wa kiume na hivyo sasa ni mjane mwenye mtoto mmoja.

 

Kwenye siasa za India, anaonekana kama mama aliyejitolea maisha yake yaliyobakia kwa ajili ya kutetea watu wa makundi maalumu, wanawake na taifa lake. Nafasi ya Urais nchini India haina nguvu kama ilivyo Tanzania lakini bado Rais ndiye Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu.

 

Kwa Murmu mwenyewe, ilikuwa jambo zuri kumpokea mwanamke mwenzake. Kwa wanawake wa India ambako mfume dume bado umetamalaki na kusimika mizizi, picha ya wanawake wawili wenye madaraka ya juu ilikuwa na umuhimu mkubwa.

 

Ujumbe ulioonyesha umuhimu wa ziara

 

Kidiplomasia, ziara ya Samia nchini India ilikuwa kwenye hadhi ya ziara ya kitaifa. Maana yake ni kwamba ilitarajiwa ujumbe utakuwa mkubwa kulingana na hadhi hiyo. Ingawa mitandaoni kulikuwa na maneno mengi kuhusu ukubwa wa ujumbe wa Tanzania, lakini taarifa rasmi ya serikali ilionyesha wajumbe rasmi wa serikali walikuwa 32.

 

Kati ya hao, kupitia utaratibu wa kidiplomasia wa 15+1, Tanzania ilikuwa inaruhusiwa kuja na watu 16 – Rais na watu wake 15 ambao wangehudumiwa na serikali ya India, kama ambavyo Tanzania ingehudumia kwa kiwango hichohicho ujumbe wa India kama Modi au Murmu angekuwa amefanya ziara ya kitaifa hapa nchini.

 

Msafara ulionekana mkubwa pia kwa sababu kulikuwa na wafanyabiashara takribani 100 ambao walikwenda India kwa gharama zao kwa lengo la kutafuta fursa za kibiashara. Na kwa hakika, hakukuwa na wachekeshaji au wasanii wa Bongo Movie/Bongo Flavour waliojumuika katika ziara hiyo kama ambavyo ilidaiwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

 

Ujumbe huu wa Tanzania, kibiashara na kiserikali, ulikuwa na lengo la kukamilisha mazungumzo na kujenga mahusiano ya kudumu katika maeneo makubwa manne ambayo uhusiano wa India na Tanzania utajikita kuanzia sasa.

 

Maeneo hayo ni Usalama Majini, Ulinzi, Ushirikiano wa Maendeleo na Biashara na Uwekezaji. Wengi wa watu wa serikali waliokuwepo kwenye ziara hiyo walikwenda kupitia vyeo vyao, majukumu yao, muktadha wa ziara yenyewe na utaalamu wao katika maeneo ya kimkakati.

 

Ni ujumbe huu wa Tanzania ndiyo uliosababisha vyombo vya habari vya India – ambako sasa vimejigawanya hadi katika maeneo maalumu ya kuripoti, kupata hamu ya kujua, hawa ni akina nani na wamekuja kufuata nini.

 

Kwa bendera zilizokuwa zimetamalaki India, kwa Watanzania wa diaspora wanaoishi India walivyojitokeza kulaki na kusindikiza ujumbe wa Tanzania, vyombo vya habari vya India vililazimika kuandika kuhusu ziara ya Rais Samia kwao.