Namna ya kukabili hoja za dunia mpya anayoitaka Rais XI Jinping

Picha ya Xi: Kwa hisani ya AP/Andy Wong. 

Na Mark Leonard

KATIKA siku za karibuni, Rais Xi Jinping wa China ametawala vichwa vya habari katika vyombo vya Magharibi kwa matukio makubwa mawili. Mosi ni kwa namna alivyofanikisha mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia na pili ziara yake nchini Russia ambako alitoa mawazo yake kuhusu namna ya kumaliza vita vya Ukraine.

Jarida mashuhuri la The Economist limeeleza matukio haya kuwa yamefungua ukurasa mpya kwa watu kuanza kuifikiria dunia kwa kutumia jicho la Rais huyo wa China. Maneno hayo ya Xi yameleta mtikisiko na fadhaa – Wajerumani wangesema Sturm und Drang, katika nchi za Magharibi ambako hamkani hali si shwari hivi sasa.

Kwa muda mrefu sasa, dunia imeendeshwa kutokana na mfumo wa dunia uliowekwa na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani – mfumo uliojengwa kwa dhana ya kuendesha dunia kwa kufuata kanuni fulanifulani zilizowekwa na jamii ya kimataifa.

Maneno kutoka kwa baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi ni kwamba sasa kuna mvutano baina ya makundi ya aina mbili ya utawala; wale wanaopenda demokrasia na wale wanaopenda utawala wa kiimla.

Lakini mtazamo wa aina hii ni fyongo kwa sababu – kwa hakika kabisa, haujibu inavyopaswa kuhusu changamoto za uhakika ambazo kuinuka kwa China kumezileta kwenye mfumo wa dunia.

Kwanza, dhana kwamba nchi za Magharibi zinasimamia utawala wa sheria na kufuata makubaliano ya jamii ya kimataifa inapingwa na matukio kadhaa yaliyofanywa na nchi kama Marekani kwenye masuala tofauti.

Wakosoaji wa nchi za Magharibi wanatumia mifano kama vile namna suala la Kosovo na Vita vya Irak vilivyoshughulikiwa na Marekani pasipo kupata ridhaa ya jamii ya kimataifa. Na wakati mwingine, hata bila kutumia majeshi na mabomu, Marekani na washirika wamekuwa wakitumia vikwazo vya kiuchumi kuziumiza nchi kama Iran.

Suala la pili ni kuhusu huo mgawanyiko ambao Rais Joe Biden wa Marekani ameueleza baina ya tawala zinazofuata sheria na zile zisizofuata sheria. Kwa hali inavyoonekana, nchi nyingi sasa hazitaki kuongozwa kwa imani kwamba inachopenda Marekani au nchi za Magharibi ndiyo namna pekee ya kuongoza dunia.

Nchi kama vile Brazil, Uturuki, India na nyingine zinaamini kwamba zenyewe zina changamoto zake binafsi ambazo hazihitaji kufuata mfumo unaopendekezwa na mataifa mengine bali kwa namna zenyewe zinaona kwa muktadha wa kwao.

Jambo la tatu ambalo ni muhimu kulisema ni kwamba si kweli kwamba wale wanaokataa kukemea uvamizi wa Russia nchini Ukraine hawaamini katika utawala wa haki. Kilichopo ni kwamba nchi nyingine zina maslahi tofauti kwenye suala hili na kwamba vita hii kwao haihatarishi chochote kwao.

Kwa mfano, kama unaishi nchini Mali, taifa kubwa linalokusumbua mara kwa mara ni Ufaransa. Kuingia kwa Russia kwenye siasa zako inamaanisha kunapunguza nguvu na ushawishi wa Ufaransa – ambalo ni jambo zuri. India pia ina hofu na China na hivyo uhusiano wake na Russia ni wa kimkakati zaidi.

Matatizo hayo ya dhana za ki-Magharibi ndiyo yamesababisha China ianze kuwa na ushawishi zaidi duniani katika miaka ya karibuni. Kwa China, changamoto kubwa zaidi kwa sasa si baina ya tawala za kidemokrasia na za kiimla bali tafsiri ya nini maana ya demokrasia katika nchi husika.

Kwa Biden na viongozi wenzake wa Magharibi wenye hofu kwamba China inataka ‘kupindua meza’ na kutengeneza dunia yenye kanuni tofauti, suluhisho lao ni kujenga mfumo wa dunia unaoundwa na nchi zinazoamini katika demokrasia, zinazofanya biashara pamoja, kubadilishana teknolojia na kupeana ulinzi wa kiusalama.

Kwa upande wake, mkakati wa China unajengwa kwenye dhana ya kutofungamana na upande wowote – na wakati huohuo kutoa nafasi kwa kila nchi kuwa na uhuru wa kufanya mambo yake yenyewe bila kuingiliwa na wengine. Huu ndiyo ulikuwa ujumbe wake alipokuwa Russia.

Ushindani huu wa kimaono baina ya pande hizi mbili uko wazi sasa. Marekani inataka kuendeleza mfumo wa dunia ambao yeye ndiye kinara na China inajiweka kama taifa ambalo halitaki lenyewe kuwa kinara bali kujenga dunia yenye vinara wengi.

Zipo sababu kadhaa zinazoleta shaka kama China itafanikiwa katika dhamira yake hii. Katika maeneo yote ambako ushawishi wa taifa hilo umekua – Kusini Mashariki mwa Asia na Afrika, kuna mizozo. Hata hivyo, hoja ya nchi kuwa na maamuzi yao inapokewa vema.

Kutokana na mkakati huu wa China, watunga sera wa Magharibi wanatakiwa kuangalia upya namna ya kushughulika na nguvu hii ya China. Badala ya kutumia muda mrefu kuhubiria nchi nyingine kuhusu mazuri ya mfumo wa sasa, wanatakiwa kuelewa kuwa kila nchi ina maslahi yake binafsi ambayo wakati mwingine hayafanani na wanachotaka Marekani na washirika wake.

Kwa vyovyote vile, ni lazima nchi za Magharibi zifahamu kuwa suala la nchi kujiamulia mambo yake na kufuata mfumo wenye maslahi kwa nchi husika ndiyo ukweli halisi wa sasa na si tatizo linalohitaji kutafutiwa dawa.

Kwa kupunguza tabia ya u-kiranja dhidi ya nchi nyingine na kuzitendea kama nchi huru zenye uwezo wa kufanya maamuzi yake zenyewe, nchi za Magharibi zinaweza kuwa na ushawishi zaidi duniani kuliko ilivyo sasa.

Badala ya kutumia muda na rasilimali kushawishi nchi nyingine kulinda mfumo wa dunia uliopo sasa, nchi za Magharibi zinatakiwa kuanza kutafuta washirika wake kutengeneza dunia mpya ambayo sote tutakubaliana.

Mwandishi wa makala haya ni Mkurugenzi wa Umoja wa Ulaya anayehusika na Masuala ya Nje. Makala ilichapwa kwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kiiingereza katika tovuti ya Project Syndicate mnamo Machi 30, 2023. https://www.project-syndicate.org/commentary/xi-jinping-idea-of-world-order-fragmented-sovereign-interests-over-western-domination-by-mark-leonard-2023-03