Ni nguvu ya kisiasa au nguvu ya rushwa?  

Picha: Wananchi wa Afrika Kusini wakiandamana kupinga vitendo vya rushwa vinavyofanywa na viongozi wa kisiasa wa taifa hilo.

 

Na Godfrey Dilunga

 

ILIKUWA mwaka 1962, jijini Dar es Salaam, Rais Julius Nyerere, wakati huo, alifungua Mkutano wa Vijana Duniani. Katika hotuba yake ya ufunguzi iliyopewa jina la The Second Scramble, alitetea ujamaa akisema utajiri wa nchi unapaswa kutatua kero za wananchi kwa usawa na pia kero za wachache.

 

Kwa wakati huo, miaka 51 iliyopita, Tanzania Bara haikuwa imebobea katika dhana ya matajiri kushindana kuhodhi hadhi, siasa na madaraka ingawa pia Mwalimu aliona dalili hizo. Katika hotuba yake hiyo ya Kiingereza, Mwalimu alisema; “There is then ruthless competition between individual-not to get wealth to feed themselves, or to clothe themselves, or to house themselves-but to seize enough wealth to give themselves more power, more prestige than their fellows.

 

“That is, wealth which exceeds their real need and which will enable them to dominate other individuals. When that stage is reached, one millionaire is prepared to spend millions simply in order to destroy another millionaire.” Kimantiki, anazungumzia ushindani usio wa kiutu katika kujilimbikizia mali ili kuhodhi mamlaka, hadhi au ufahari. Kwamba milionea mmoja anaweza kutumia mamilioni yake kumshughulikia milionea mwingine.

 

Kwa kuzingatia mantiki hiyo, wanaoshangaa rushwa kustawi katika chaguzi za CCM wasidhani hilo ni suala la ghafla. Wasidhani rushwa hiyo ni upepo wa kupita tu, iwe kwa CCM au vyama vingine. Rushwa nchini si upepo wa kupita. Ni makosa kuitazama rushwa kwa kuwatazama wanasiasa pekee.

 

Inawezekana baadhi ya vyama kwa sasa vimekuwa mawakala wa rushwa, lakini ni muhimu zaidi kutazama na kushughulikia chimbuko la mfumo huu wa rushwa. Mbali na wanasiasa, mfumo wa rushwa kwa sasa unapaswa kutazamwa kwa kuwahusisha wafanyabiashara au wawekezaji wakubwa. Tunapaswa sasa kujadiliana kuhusu mifumo ya uendeshaji biashara nchini, mifumo ya kodi na hata mifumo ya kufikia uamuzi kiutawala au kisiasa.

 

Mifumo ni viwanda vya kuzalisha watoaji, mawakala na madalali wa rushwa katika sekta zote, ikiwamo siasa. Kwa bahati mbaya, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wanapotoshwa na kujikuta wakipambana na matokeo. Hawapambani na viwanda vya kutengeneza mawakala na madalali wa rushwa.

 

Zingatia maneno haya ya Mwalimu; “That is, wealth which exceeds their real need and which will enable them to dominate other individuals.When that stage is reached, one millionaire is prepared to spend millions simply in order to destroy another millionaire.” Hapo haina maana wafanyabiashara waache kushindana kutafuta faida ya kupindukia.

 

Tatizo ni namna gani wanapata faida ya kupindukia? Kama mwekezaji au mfanyabiashara amekwepa mabilioni ya kodi ni dhahiri atakuwa na mabilioni ya ziada yanayomshawishi kufikiri namna ya kukwepa kodi siku zijazo. Katika kufikiri, atatumia nusu ya mabilioni hayo kuhodhi mifumo ya uamuzi ambayo msingi wake ni siasa. Atatengeneza wanasiasa wake ndani ya chama tawala na upinzani. Ataamua waseme nini, wafanye nini na kwa wakati gani.

 

Mabilioni yaliyotokana na kukwepa kodi yataingilia mfumo huru wa kisiasa, mfumo wa kuchagua na kuchaguliwa. Genge lake litang’ara katika soko la ununuzi wa kura ndani ya CCM au chama kingine chochote. Mwanasiasa anayetokana na genge hilo sifa yake kubwa ni kujitengenezea uhalali kwa kuegemea matumizi ya fedha, iwe michango kanisani au misikitini.

 

Mipango ya kisiasa ya genge la namna hiyo itaongozwa kwa nguvu ya rushwa. Hoja ya msingi kwao ni kuhodhi madaraka, hadhi na ufahari na si namna madaraka wanayopigania yatanufaisha chama au taasisi husika. Kwa nguvu za rushwa (si nguvu za mipango ya maendeleo), watajipenyeza miongoni mwa vijana, wanawake na wazee.

 

Wataimba jina moja teule la mgombea mtarajiwa wa ubunge au urais. Mtego mkubwa watakaoutumia ni kauli mbiu kwamba mteule wao anazo nguvu za kisiasa. Kauli mbiu hiyo italenga kuua hoja sahihi kwamba hizo si nguvu za kisiasa bali ni nguvu za rushwa.

 

Wanaweza kufanikiwa kupata mgombea ubunge au urais. Hata hivyo, ni vigumu kwao kupata mshindi wa kiti cha ubunge au urais. Kuwa mgombea ni suala moja na kuwa mshindi wa unachogombea ni suala pana zaidi na sababu ni nyingi. Kati ya sababu hizo ni ukweli kwamba, kwa kadiri mipango yao inavyotekelezwa kwa msukumo wa rushwa ndivyo wapiga kura halisi mitaani wanavyoungana kifikra kumkabili mgombea ambaye ni zao la mfumo huo dhalimu.

 

Haya yametokea nchini. Katika baadhi ya majimbo, nguvu ya rushwa zilitengeneza wagombea, wananchi waliwakabiliana wagombea hao. Ushauri kwa magenge ya namna hii ni kutambua, kwa mfano, nguvu za Nelson Mandela au Mwalimu Nyerere kisiasa hazikutokana na kugawa rushwa.

 

Rushwa hainunui fikra huru, wapiganaji wanaounganishwa kwa nguvu ya rushwa ni mateka wa baadaye katika jeshi linaloangamiza rushwa. Ni mateka wa baadaye mbele ya majemedari wa haki. Zamu itafika waliosimama upande wa haki kushuhudia mateka hao wakijisalimisha.

 

Tujifunze kwamba, haitoshi kuimarisha sheria ya TAKUKURU pekee wakati sheria nyingine za kudhibiti nidhamu katika shughuli za kiuchumi ni dhaifu. Nihitimishe kwa sawali, hawa wanaotajwa kuwa na nguvu katika CCM; je, hizo ni nguvu za kisiasa au nguvu za rushwa?

 

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

 

Mwandishi wa makala haya alipata kuwa Mhariri wa magazeti kadhaa hapa nchini yakiwemo Raia Mwema na JAMHURI. Makala hii ilichapwa kwa mara ya kwanza kwenye Raia Mwema mnamo mwaka 2012.