Niger: Sababu za Tinubu kuja matao ya chini  

Picha: Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria. Picha kwa Hisani ya mtandao wa Business NG. 

 

 Na Ahmed Rajab

 

SIKU zinaingia na siku zinatoka lakini Afrika Magharibi haziingii tena kwa vishindo.  Hatuyasikii magoma yakipigwa kunadi vita.  Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) na mwenyekiti wake wa sasa, Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria, wanaonesha kama wamekwama.

 

Tinubu na Ecowas wanashikilia kuwa wapinduzi wa Niger wamrejeshe madarakani Rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum lakini vitisho vyao kwa sasa ni sawa na nguvu za povu.  Rais Alassane Ouattara wa Côte d’Ivoire ndiye aliyebeba bendera ya kutaka ‘demokrasia’ irejeshwe Niger.

 

Ouattara huyuhuyu anayeyalaani mapinduzi ya kijeshi ya Niger ndiye huyuhuyu ambaye Desemba 24, 1999 alishangilia pale jeshi la Côte d’Ivoire lilipompindua hasimu yake, Rais Henri Konan Bédié.  Ouattara aliyaelezea mapinduzi hayo kuwa ni yenye kuungwa mkono na wananchi wote wa nchi yake. Leo hii anayaelezea mapinduzi ya Niger kuwa ni kitendo cha ugaidi.

 

Anautaka ulimwengu usahau kwamba yeye aliifinya demokrasia mwaka 2020 kwa kujiongezea muhula mwingine wa kutawala.  Katiba ya nchi yake inaruhusu mihula miwili tu lakini yeye alijiongezea wa tatu.

 

Rais Macky Sall wa Senegal naye pia alijaribu kubadili katiba ajipe muda zaidi wa kutawala lakini nguvu za umma zilimshinda. Kwa hamaki zake wiki iliyopita tu alikipiga marufuku na kukivunja chama cha upinzani cha Wazalendo wa Senegal (PASTEF) na amemkamata kiongozi wake Ousmane Sonko kwa mashitaka ya kupindua serikali.

 

Viongozi sampuli ya Ouattara na Sall ndio wenye kupigania demokrasia ya Niger na ndo maana wenye akili zao timamu hawawatii maanani. Ouattara bado anaibeba bendera ya nchi zenye kutaka kutumia nguvu dhidi ya Niger. Ajabu ya mambo ni kwamba nchi nyingine zilizokuwa nyuma yake zinaonesha ishara za kulegeza misimamo yao. Cape Verde, kwa mfano, imeshasema kwamba haitopeleka wanajeshi wake kuivamia Niger.

 

Hisia za wananchi katika nchi nyingine kama Ghana, Gambia, Liberia na Sierra Leone zinaonesha kupinga uvamizi huo. Upinzani huo dhidi ya uvamizi wa Niger unaonesha wazi kwamba Jumuiya ya Ecowas imeingia nyufa kubwa na huenda ikapasuka. Tunayakumbuka ya mwaka 2000 pale Mauritania ilipojitoa kwenye jumuiya hiyo.  Mauritania ilikuwa mojawapo ya nchi zilizoiasisi Ecowas 1975. Ilikaa nje kwa miaka hadi 2017 iliporudi tena kwa makubaliano ya kuwa mwanachama-mshiriki.

 

Mauritania nayo pia inaelekea kupinga matumizi ya nguvu dhidi ya Niger.  Hisia kubwa iliyopo ndani ya nchi za Ecowas ni kwamba damu ya Mwafrika isimwagike ili kuyatekeleza matakwa ya Marekani na Ufaransa. Watu wamechoka kutumiwa kwa faida ya wakoloni wa zamani au wakoloni mamboleo.

 

Sasa Ecowas badala ya kupeleka majeshi Niger imekubali kupeleka kamati ya Bunge lake kwenda Niamey kuzungumza na wapinduzi wa kijeshi. Juu ya yote hayo, bado upo uwezekano wa kuzuka mapigano ya maangamizi nchini Niger. Uwezekano huo upo kwa sababu Ufaransa, ikiungwa mkono na Marekani na Muungano wa Ulaya (EU), bado inalipiga baragumu la vita.  Inawataka marais wa Kiafrika walio chini ya mbawa zake wawatose wanajeshi wao Niger.

 

Marekani, Ufaransa pamoja na nchi za EU zimezoea kufanya utundu Afrika, kuwaua viongozi na kuziparaganya nchi zao. Mfano mzuri ni njama walizozila dhidi ya Muammar Qadhafi wa Libya waliyemuua na kuifanya nchi yake isijijue, isijitambue.

 

Nchi hizo za Magharibi zina uwezo wa kuivuruga vibaya Niger na kuusambaratisha ukanda mzima wa nchi za Sahel. Kwanza, zinaweza kuyachochea makundi ya kigaidi kuishambulia Niger. Maslahi ya kiuchumi yaliyo katika eneo zima la Sahara na Sahel ndiyo sababu kubwa iliyozifanya Marekani na Ufaransa ziwe na kambi za kijeshi, pamoja na wanajeshi wao, katika eneo hilo. Niger tu Marekani ina wanajeshi 1,500 na kambi mbili za kijeshi — moja ni ile kubwa kabisa yenye madroni yanayoweza kurushwa kwenda takriban nchi zote za eneo hilo na zilizo nje ya mipaka ya eneo hilo.

 

Ufaransa nayo ina kambi zake na wanajeshi 1,100; Italia ina wanajeshi 300 na Ujerumani kama mia moja hivi. Yote hayo yamo kwenye hesabu za Tinubu, mwenyekiti wa Ecowas.  Na kuna yanayomhusu yeye mwenyewe binafsi ambayo lazima anayaingiza kwenye hesabu zake za iwapo nchi yake ishiriki kuivamia kijeshi Niger.

 

Tinubu aliingia matatani hata kabla ya kuapishwa awe Rais wa 16 wa shirikisho la Nigeria mnamo Mei 29 mwaka huu.  Uhalali wa urais wake ulikuwa mashakani na kesi ilifunguliwa kwenye mahakama kuu kupinga uchaguzi wake.

 

Pili, ameingia katika Ikulu ya Aso Rock, Abuja, wakati wananchi wenzake wakiwa taabani. Wengi wao wana njaa, hawana fedha za kununulia mafuta ya kupikia seuze ya petroli ya kuendeshea magari. Mamilioni ya vijana wanazurura majiani wakiwa hawana ajira, hawana mbele hawana nyuma.

 

Hali zikiwa hivyo, Tinubu aliwajibika kwanza kutafuta, kwa haraka, ufumbuzi wa matatizo yanayowakumba wananchi wenzake kabla ya kujiingiza katika mgogoro wowote ule nje ya Nigeria.  Alizidi kukosea alipojifanya mbabe kwa kujaribu kuwatisha wapinduzi wa Niger.

 

Kuna wasemao, hasa ndani ya duru zake, kwamba alilazimishwa na Ufaransa awe na msimamo mkali. Hakuweza kuwavunja Wafaransa kwa sababu ndio waliomfadhili, waliowekeza juu yake wakati wa uchaguzi na sasa ni wakati wao wa kuvuna matunda ya fadhila zao.

 

Wafaransa waliwatumia wafanyabiashara wao wakuu Nigeria wakiwa pamoja na wale wenye asili ya Lebanon na wenye ushawishi mkubwa nchini humo kama vile Gilbert Chougory, aliyewahi pia kuwa sahibu mkubwa wa dikteta Jenerali Sani Abacha.

 

Inasemekana kwamba vyombo vya usalama vya Ufaransa vilipoona jinsi nchi yao inavyochukiwa katika makoloni yake ya zamani ya Afrika Magharibi vilipendekeza kwamba Ufaransa ibadili mkakati na iwekeze kwa kiongozi atayeiliongoza taifa kubwa lisemalo Kiingereza katika ukanda huo.

 

Taifa hilo ni Nigeria.  Na kiongozi ambaye Wafaransa walimlenga alikuwa Tinubu tangu alipoanza kuonesha dalili kuwa atagombea urais wa Nigeria. Hatua ya kuivamia kijeshi nchi yoyote ni hatua ya nguvu lakini pia inahitaji busara na fedha. Wakati Nigeria ilipokuwa na uchumi imara na uwezo mkubwa wa kifedha, yenyewe, peke yake ndiyo iliyokuwa ikigharimia operesheni za kijeshi za Ecowas. Leo uchumi wake Nigeria ni dhaifu kidogo.

 

Tusisahau kwamba Mali na Burkina Faso nazo zimeshasema kwamba zitapigana ubavu kwa ubavu na Niger kuisaidia kupambana na wavamizi wa Ecowas, wakiongozwa na Nigeria. Hivyo vitakuwa vita kamili. Hautokuwa uvamizi wa kuingia na kutoka Niger.

 

Mnamo 1990 nchi za Ecowas zenye kuzungumza Kiingereza ziliunda lile liitwalo Kundi la ECOMOG, likiwa kama chombo cha kuingilia kati na kuvizuia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia, vilivyoanza mwaka 1989.  Nasema ‘chombo’ kwa sababu kiliyawezesha majeshi ya mataifa tofauti yafanye kazi pamoja.

 

Wanajeshi wengi wa Ecomog walitoka Nigeria. Vikosi vya batalioni ndogo vilitoka Gambia, Ghana na Sierra Leone.  Burkina Faso, Mali na Niger, zinazozungumza Kifaransa, zilipeleka wanajeshi wachache.

 

Nigeria ndiyo iliyotoa fedha nyingi kugharimia harakati hizo.  Rais wa Nigeria wa wakati huo Jenerali Ibrahim Babangida alianza kwa kuwapeleka wanajeshi 3,000 huko Monrovia, mji mkuu wa Liberia, Agosti 24, 1990. Hata yeye akifikiri kwamba wanajeshi hao watamaliza shughuli zao kwa miezi sita. Miezi sita iligeuka ikawa miaka saba.

 

Inakisiwa kwamba Nigeria ilitumia fedha zipatazo dola za Marekani bilioni 8 kuvizima vita hivyo na kurejesha amani katika Liberia. Kichekesho ni kwamba walipokwenda mwanzo Liberia, wanajeshi wa Ecomog hawakuwa hata na ramani za Liberia.  Wanajeshi hao walitoswa bila ya nyenzo muhimu za kivita.

 

Niliyashuhudia mengi ya Liberia vita hivyo vilipomalizika mwaka 1997.  Nilikwenda huko nikiwa mmoja wa wakufunzi wa kuwafunza waandishi wa habari na watendaji wengine wa vyombo vya habari juu ya namna ya kuuripoti uchaguzi mkuu uliokuwa unakaribia kufanywa nchini humo.

 

Nilikoshukia, kwenye hoteli ya Mamba Point, ndio mahala pekee palipokuwa pa nadhifu na palipokuwa na nidhamu katika jiji zima la Monrovia.  Kwengineko kulihanikiza uvundo na baadhi ya wanajeshi wa Ecomog wasiokuwa na nidhamu walihusika na vitendo visivyo vya kiungwana kama ubakaji na ufisadi.

 

Walio karibu na duru za Tinubu wanasema kwamba juu ya matatizo aliyonayo kuna jambo jengine litalozidi kumla roho.  Nalo ni vita vya chinichini, vya kimya kimya, anavyopigwa na baadhi ya waliomzunguka.  Shutuma zinawaangukia watu wawili: mkuu wa ofisi yake, Femi Gbajabiamila na Mshauri wa Usalama wa Taifa, Mallam Nuhu Ribadu.

 

Hawa wanashutumiwa kuwa wanazidhibiti shughuli za serikali na kwamba wanamficha Tinubu mambo mengi yanayoendelea serikalini mwake.  Wanapiga mbali — kwenye uchaguzi ujao wa 2027.

 

Uvumi uliopo ni kuwa Gbajabiamila anaamini kwamba Tinubu, kwa sababu ya ugonjwa, hatokuwa na nguvu za kugombea tena urais mwaka 2027. Kwa hivyo, Gbajabiamila amepanga mkakati wa kuzikata mbawa za wale anaohisi watajaribu kupaa na kuushika urais baada ya Tinubu. Kwa hilo anashirikiana na Ribabu.

 

Inasemekana pia kwamba Gbajabiamila ameamua kwamba endapo Tinubu hatoweza kuwa rais kwa mihula miwili ya jumla ya miaka minane basi atamfanya Ribadu awe mwenza wake.  Lakini endapo Tinubu atamaliza miaka yake minane na madaraka yabidi kurudi kaskazini mwa nchi hiyo basi atamuachia Ribabu agombee urais na yeye awe mwenza wake.

 

Gbajabiamila atabidi azicheze karata zake vizuri ili aupate muradi wake.  Hatua yake ya mwanzo ni kuwazuia watu walio karibu na Tinubu, wasiwe mawaziri.  Mfano mzuri ni Mallam Nassir Mohamed El-Rufai, aliyewahi kuwa waziri na Gavana wa Kaduna. Tinubu anamtaka awe waziri wake lakini El-Rufai ametiliwa guu na Idara ya Usalama wa Taifa ya Nigeria, State Security Service (SSS).

 

Gazeti la Dunia limepewa orodha refu ya washirika na marafiki wakubwa wa Tinubu waliompigia kampeni na ambao sasa wamejikuta patupu. Mambo yote hayo yameikoroga akili ya Tinubu kiasi cha kwamba hana hila ila aache kuyapiga magoma ya vita.

 

Inaonesha pia kuwa ameanza kuwasikiliza wale wasemao kwamba majeshi ya Ecowas yakijaribu kuivamia Niger yatakumbana na ‘Waterloo’ yao. Yaani yatashindwa vibaya kama yalivyoshindwa majeshi ya Napoléon Bonaparte yalipopambana na majeshi ya Uingereza na ya Prussia katika mapigano ya Waterloo Juni 18, mwaka 1815. Zama hizo Prussia ilikuwa ni tawala kamili ya kifalme lakini sasa imegawika vipande vipande. Viko katika nchi za Ujerumani, Poland, Denmark, Ubelgiji, Jamhuri ya Czech, Urusi na Lithuania.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; X: @ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.