Maelezo ya Picha: Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, akiongoza kikao cha mazungumzo ya Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar kilichofanyika Ikulu ya Zanzibar hivi karibuni. Picha kwa Hisani ya Ikulu ya Zanzibar
Na Ezekiel Kamwaga
WAKATI Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ikiwa inatimiza nusu muhula tangu iundwe baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, bado kuna sura ya mkanganyiko na kutoaminiana miongoni mwa vyama viwili vinavyounda serikali hiyo – ingawa uwepo wake peke yake unatoa matumaini ya kufikiwa kwa maridhiano ya kitaifa visiwani Zanzibar.
Miaka miwili iliyopita, SUK ilipata pigo kutokana na kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Serikali hiyo, Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye alikuwa akichukuliwa kama mojawapo ya nguzo ambazo serikali hiyo ilikuwa imezisimamia. Kuliko mwanasiasa mwingine yeyote visiwani humo, yeye ndiye aliyehusika zaidi na kuwapo kwa serikali hiyo. Sioni uwezekano wa SUK kuwepo endapo Maalim Seif angewaambia wafuasi wake kuwa wasusie.
Hata hivyo, kifo cha mkongwe huyo wa siasa za Zanzibar, kilitoa fursa kwa Othman Masoud Othman, kushika wadhifa wake huo ndani ya SUK. Kitabia, kihistoria na kiushawishi, Othman na Maalim ni watu wawili tofauti. Lakini tofauti zao zinaishia hapo kwani linapokuja suala la kudai haki na maslahi ya Wazanzibari, inawezekana Makamu wa Rais huyo ana mrengo mkali zaidi pengine kumzidi mtangulizi na mwalimu wake huyo wa siasa.
Kuingia kwa Othman kumetoa fursa ya kuingiza sura, historia na msukumo mpya kwenye uendeshaji wa SUK na suala zima la maridhiano ya kitaifa visiwani humo. Kuna nyakati katika siasa kuna dhana kwamba fagio jipya linaweza kufanya kazi vizuri zaidi kuliko lile la zamani, ingawa la zamani linajua pembe zote za nyumba na pengine hata yale yaliyo uvunguni mwa vitanda.
Hadi sasa, kwa bahati mbaya, hakuna kitu cha muhimu kushika mkononi kuhusu mafanikio ya SUK katika muda huu wa nusu muhula kulinganisha na ilivyokuwa mwaka 2020 wakati inaundwa. Ukiondoa ukweli kwamba kuwepo kwa SUK pekee ni hatua nzuri kwenye kufikia maridhiano, lakini hakuna kitu kingine kikubwa kilichotokea kwenye miaka hii miwili na nusu ya kwanza kuonyesha kwamba mwafaka wa kisiasa kweli uko njiani.
Mkanganyiko
Msingi wa dhana ya kuanzishwa kwa Serikali za Umoja wa Kitaifa popote duniani ni kwa jamii husika kukubali kwamba kwanza kuna matatizo kwenye jamii yao yanayohitaji kumalizwa, pili umuhimu wa uwajibikaji kwa waliohusika na vitendo vibaya vya miaka ya nyuma, tatu kukubali kusameheana kwa vile kujenga taifa ni kitu kikubwa zaidi kuliko madhila au tofauti za mtu mmoja mmoja na mwisho kabisa uwezekano wa fidia kwa wale walioumizwa.
Nilianza kupatwa na wasiwasi kuhusu mwelekeo wa SUK ya Zanzibar mara tu baada ya kusikiliza hotuba ya Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyoitoa Desemba 8, mwaka 2020 aliposema; “ Maridhiano ya kweli yanajengwa kwa kuvumiliana, kustahamiliana na kusahau yaliyopita. Ujasiri wa maridhiano ni kusahau yaliyopita na kutotonesha vidonda”.
Kama msomi wa masuala ya maridhiano, kauli hiyo ya Mwinyi ilinipa picha kwamba kuna mkanganyiko au kutoelewa kuhusu dhana hii ya maridhiano. Katika kitabu chake maarufu cha La Memoire, l’histoire, l’Memoire, l’Oubli (2002), mwanafalsafa wa Kifaransa, Paul Ricoeur, alionya kwamba katika suala la maridhiano, kuna hatari pale endapo wahusika hawatachukua hatua ngumu zaidi.
Ricoeur alitumia muda mwingi kueleza kwamba ni hatari kuweka nguvu katika maneno matupu ya kukumbuka na kukumbushana tu (le devoir de memoire) na badala yake nguvu kubwa itumike katika kufanya yale mambo yanayoumiza kuyafanya na kuyazungumza lakini yenye faida za muda mrefu (Le travail de memoire).
Kinyume kabisa na maelezo ya Rais Mwinyi, kinachotakiwa kufanyika Zanzibar ni ‘kumla jongoo kwa meno’. Maana ya msemo huu ni kuhakikisha kwamba mabadiliko yanayohitajika kufanyika Zanzibar kuanzia kwenye mifumo ya uchaguzi, uteuzi wa viongozi katika taasisi za serikali na dola, suala zima la ajira kwa Wazanzibari, tofauti ya kimaendeleo baina ya Unguja na Pemba ni miongoni mwa masuala yanayotakiwa kufanyiwa kazi.
Msomi maarufu wa masuala ya maridhiano nchini Afrika Kusini, Dk. Tshepo Madlingozi, huwa anatumia msemo mmoja maarufu kwamba katika maridhiano, kama wewe ulichukua ng’ombe wangu, inatakiwa kwanza unirudishie ng’ombe huyo halafu ndiyo tukae mezani tuzungumze. Hakuwezi kuwa na maridhiano endapo utabaki na ng’ombe wa mwenzako uliyemchukua pasipo halali kabla ya kuridhiana.
Katika siasa za Zanzibar, inawezekana watu hawakuchukuliana ng’ombe huko nyuma lakini kuna walionyang’anywa mali zao, waliouliwa ndugu zao, waliodhalilishwa na mambo mengine. Kwenye kutafuta mwafaka wa kitaifa, ni muhimu ikatafutwa namna iwe ya kuombwa msamaha, kurudisha kinachowezekana na kuapizana kwamba yaliyopita katika kipindi cha takribani miaka 60 iliyopita, hakitatokea tena.
Ninajua kwamba ni lazima watu wasameheane ili kuwepo na maridhiano kwa sababu hata Askofu Desmond Tutu alipata kusema “hakutakuwa na maisha pasipo kusameheana” lakini ni lazima – nikirudi kwa Ricoeur, kukubali kufanya mambo yanayoumiza na kuonyesha vitendo kama kweli tunataka kujenga mwafaka.
Wazanzibari, hasa wale wanaodhani historia ya miaka 60 iliyopita ya visiwa hivyo haijawatendea haki, wanaweza vipi kuacha kukumbushia yaliyopita na kutonesha vidonda, pale wanapoona Rais Mwinyi anamteua Thabit Idarous Faina, kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wakati mbia muhimu katika SUK, Chama cha ACT Wazalendo, kimetangaza kutokuwa na imani naye?
Kwa wanaofuatilia siasa za Zanzibar, wanaona dalili za viongozi wa CCM Zanzibar kutofurahishwa na ukosoaji wa hadharani unaofanywa na viongozi wa ACT kwenye masuala ya uendeshaji wa serikali ya Zanzibar. Wengi wa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inaonekana wanaona kuwa si sahihi kwa wenzao wanaounda serikali ya pamoja kwenda nje na kuwakosoa.
Hii inaonyesha kwamba majukumu ya nini chama kilichoshindwa uchaguzi kinatakiwa kufanya ndani ya SUK hayafahamiki vizuri kwa wengi. Sijasikia viongozi wa CCM wakitoa lawama za moja kwa moja kwa wizara mbili zinazoongozwa na mawaziri kutoka ACT Wazalendo. Watu wanajiuliza, kama ikitokea tatizo kwenye Wizara ya Afya, Rais Mwinyi anaweza kwenda hadharani na kusema tatizo ni ACT na si wao?
Kama Mwinyi hawezi kuwasema vibaya ACT hadharani kwa sababu kimsingi serikali ni ya CCM na inatekeleza ilani ya chama hicho, je mbia huyo kwenye SUK ana nguvu gani ya kumsema vibaya mwenzake wakati wote wanakaa kwenye Baraza la Mawaziri na kupanga mipango ya kuendesha nchi pamoja?
Nina uhakika kwamba wengi wa wanachama na wafuasi wa vyama vya CCM na ACT Wazalendo hawajui ni wakati gani wawili hao wanakuwa kitu kimoja na wakati gani wanakuwa tofauti. Kwa wengi, kuna mkanganyiko kuhusu nini hasa majukumu ya upinzani kwenye SUK.
Katika mahojiano niliyofanya na Tendai Biti aliyepata kuwa Waziri wa Fedha kwenye SUK ya Zimbabwe baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008, alinieleza kwamba alipewa wizara hiyo na Mugabe kwa sababu kubwa moja; kama angefanya vizuri, Mugabe angechukua sifa ya kurejesha uchumi wa Zimbabwe kwenye mstari sahihi lakini kama angeharibu, Mugabe angesema wapinzani hawana jipya. Huu ndiyo mkanganyiko ninaozungumzia kwenye suala hili la SUK si Zanzibar pekee bali Afrika kwa ujumla.
Kutoaminiana
Kwa nini SUK ni muhimu katika maridhiano? Ni kwa sababu ndiyo namna rahisi zaidi ya kuwakutanisha mahasimu wa kisiasa na kufanya wafanye kazi pamoja. Tafiti mbalimbali za wasomi wa siasa za Kiafrika ikiwemo ule wa Nic Cheeseman na Blessing-Miles Tendi, zinaonyesha kwamba uwezekano wa kumwagika damu ni mdogo pale tabaka la watawala kwenye nchi husika linapofanya kazi kwa karibu na kuaminiana.
Kwa hiyo, Kenya kwa mfano, ni vigumu kumwagika damu sasa kwa vile akina William Ruto, Raila Odinga, Uhuru Kenyatta, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na wengine wanafahamiana na wanahusiana kwa karibu na hivyo ni vigumu kuamua kuingia vitani na kuharibu maslahi yao ya kibiashara na kisiasa.
Angola, Msumbiji na Rwanda walipigana vita na kumwaga damu nyingi kwa sababu tabaka la watawala halikuwa likiaminiana vya kutosha katika nchi zao. Wakati akina Maalim Seif wakitoka jela na kuanzisha upinzani mwanzoni mwa miaka ya 1990, kutoaminiana baina ya upinzani na chama tawala cha CCM kulikuwa kwa kiwango cha juu. Kufikia mwaka 2010 – baada ya jitihada za sirini na hadharani na marais Mkapa, Kikwete na Amani Karume, kuaminiana kulianza kutokea na ndiyo sababu SUK ikaundwa mwaka 2010.
Kwa mfuatiliaji wa siasa za Zanzibar, ni wazi unaona bado tabaka la watawala wa Zanzibar halijafikia kiwango cha juu cha kuaminiana kama ambavyo wengi wangedhani. Mikutano ya karibuni ya viongozi wa ACT Wazalendo inayoendelea visiwani humo inatoa picha ya msuguano ndani ya tabaka la watawala ambayo haijapunguzwa nguvu na uwepo wa SUK.
Kuna picha nyingi zinazoonyesha mikutano ya Rais Mwinyi na viongozi wa ACT Wazalendo. Hata hivyo, maoni yangu binafsi ni kwamba sijaona kama mawazo ya vigogo wa CCM Zanzibar yamebadilika sana kuhusu maridhiano visiwani humo. Ikumbukwe kwamba karibu katika maeneo yote yanakojulikana kama ngome ya CCM Zanzibar, matokeo ya kura ya maoni ya mwaka 2010 yalionyesha wengi wao hawakuwa wakitaka SUK iwepo.
Kuna wakati Napata picha kwamba huenda suala la SUK na maridhiano ya kitaifa visiwani humo ni suala binafsi la Rais Mwinyi na halina baraka zote za chama hicho. Vigogo waliokuwa wakitajwa kumpinga Rais Karume wakati akipambania SUK mwaka 2010, bado wapo na hawatoi kauli zozote za kuunga mkono SUK.
Kutoaminiana huku kunatiwa nguvu zaidi na ukweli kwamba hakuna mabadiliko yoyote makubwa yanayoweza kutoa picha kwamba sasa CCM Zanzibar na ACT Wazalendo zimeamua kufuata le travail de memoire kwa kung’ata jongoo na kufuata njia mpya. Hadi sasa, sina jibu la uhakika kama ni wahafidhina ndani ya CCM Zanzibar ndiyo wanamfunga breki Mwinyi au Rais huyo mwenyewe anashindwa kuchukua hatua nzito kwa sababu ACT hawajamwonyesha dalili kuwa wanataka maridhiano kwa gharama yoyote.
Andishi langu la Shahada ya Uzamili kuhusu Siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS), lilikuwa na kichwa cha habari kisemacho Power Sharing Without Power na hitimisho langu lilikuwa kwamba SUK za Afrika hazizai matunda kwa sababu kimsingi hakuna madaraka yanayogawanywa baina ya wabia bali chama kimoja hubaki na madaraka yote.
Kwa hali ilivyo sasa Zanzibar, ingawa kuna SUK, CCM ndiyo inadhibiti Hazina, Vikosi vya SMZ na Rais wa SMZ ndiye mwenye mamlaka ya peke yake ya kuteua wakuu wa mikoa, wakurugenzi wa mashirika, mabalozi wanaowakilisha Zanzibar nje ya nchi na fursa nyingine za kiuchumi. ACT ni wabia tu kwenye serikali lakini si zaidi ya hapo. Ni wazi kwamba nikunukuu andishi la Minde na wenzake, kinachotokea Zanzibar ni kugawana vyeo na si madaraka.
Matumaini
Kuna msemo wa Kiswahili unaosema kwamba ndugu wanaokaa pamoja hawagombani. Ukweli kwamba vyama vya ACT Wazalendo na CCM vimekubali kuunda SUK na kufanya kazi pamoja kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa, ni jambo la kutia moyo. Ziko nchi kadhaa Afrika ambazo zingetamani kufikia walau hatua hii lakini hali ni ngumu zaidi.
Ni jambo zuri pia kwamba tayari kuna Tume ya Maridhiano inayoundwa na wajumbe kutoka vyama hivyo viwili inayofuatilia masuala muhimu kwenye kuelekea maridhiano kamili. Jambo kubwa kuliko yote linaloweza kufanyika sasa ni kutokea au kufanyika kwa kitu kitakachoonyesha kwamba wadau hao wa SUK wanafanya wanachokisema midomoni mwao.
Rais Ali Mohamed Shein aliunda SUK na ikafanya kazi kuanzia mwaka 2010 hadi 2015. Kwa sababu hiyo, mafanikio ya SUK hii hayawezi kupimwa kwa kustahamili miaka mitano. Mafanikio makubwa kwa SUK ya Dk. Mwinyi yatakuwa ni kuivusha Zanzibar salama baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwani huo ndiyo mfupa uliomshinda Shein mwaka 2015.
Itawezekanaje kwa Dk. Mwinyi kutafuna mfupa uliomshinda Shein? Ni kwa kuweka mazingira ambapo mshindi atayetangazwa atakuwa ni mshindi aliyechaguliwa na Wazanzibari wenyewe. Mfumo wa kuhesabu kura kama uliotumika nchini Kenya mwaka jana, unafaa kutumika Zanzibar huku wananchi wakiona matokeo halisi kadri yanavyoletwa.
Kazi kubwa ya Tume ya Maridhiano inayoendelea na kazi huko Zanzibar ni kuhakikisha kwamba baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, hakutakuwa na chama kitakachosusa kuingia kwenye SUK kwa sababu hakikubaliana na matokeo ya uchaguzi huo. Tukipita mwaka 2025 salama, nina matumaini kwamba maisha yatakayofuata, hayatakuwa na changamoto wala kuaminiana tunakokuona sasa.
Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha SOAS nchini Uingereza.