Na Ezekiel Kamwaga
RAIS Yoweri Museveni wa Uganda alipata kuulizwa wakati mmoja kuwa ni jambo gani kubwa analodhani Baba wa Taifa la Tanzania, Julius Nyerere, alilifanya kiasi cha kubaki madarakani kwa muda mrefu? Pasi na kufikiri sana, Museveni alijibu; “He tamed the army” Kwa tafsiri ya haraka ya lugha ya Kiswahili, alimaanisha alilidhibiti Jeshi.
Wakati tukiadhimisha Kumbukizi ya Baba wa Taifa hii leo, jibu hilo la Museveni limerudi tena kichwani kwangu. Na limerudi kwa sababu kuliko katika wakati mwingine wowote tangu nimekuwa mtu mzima, Afrika inapitia katika kipindi ambacho Mapinduzi ya Kijeshi yameanza tena kuwa fasheni.
Na hili ni jambo ninalolifuatilia kwa karibu sana. Kadri hali ngumu ya maisha inavyozidi kwa wananchi na kero kuonekana kutotatuliwa, kuna ombwe ambalo linaweza kuzibwa na yeyote – likiwemo jeshi katika taifa lolote.
Chukulia mfano wa Afrika Kusini. Utafiti uliofanywa na taasisi ya Afrobarometer mwaka huu na kunukuliwa na toleo la wiki hii la jarida la The Economist, asilimia 72 ya waliohojiwa wanasema akitokea kiongozi ambaye ataondosha uhalifu, rushwa na kero ya kukosa umeme, watakuwa tayari nchi kuendeshwa pasipo uchaguzi.
Hata hivyo, kuna kitu kuhusu Tanzania kinachoniambia kwamba uwezekano wa kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi ni mgumu kuliko nchi nyingi barani Afrika. Na kwa kutazama utawala wa Mwalimu Nyerere, naamini kwamba msingi wa hili ulitokana na maono na mbinu za medani za Baba wa Taifa.
Sisemi kwamba haiwezekani kwa Tanzania kutokea kwa mapinduzi, ninachosema ni kwamba ni vigumu kutokea na yote hiyo ni kwa sababu ya Baba wa Taifa. Kama alivyosema Museveni, siri iko katika namna alivyoweza kulifuma Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Tukio la Uasi la Januari 1964
Nyerere alinusurika kupinduliwa na askari wake mnamo Januari mwaka 1964. Kufeli kwa Mapinduzi hayo, ndiko kulikofanya avunje lililokuwa Jeshi la wakati huo la KAR na kuunda JWTZ.
Kulikuwa na tofauti gani baina ya JWTZ na King’s African Rifles (KAR)? Zilikuwepo nyingi. Lakini kwa sababu ya nafasi, nitajikita kwenye eneo moja pekee; utaifa na majukumu yake.
Mpaka wakati wa uasi wa mwaka 1964, kulikuwa na vigogo wa Jeshi waliokuwa si raia wa Tanzania. Kwa baadhi ya askari, hiyo ilikuwa ni dalili ya kuendelea kuongozwa na wakoloni. Kuundwa kwa JWTZ kulitoa nafasi kwa Mtanzania, Mirisho Sarakikya, kuwa Mkuu wa JWTZ.
Lakini Nyerere alifanya kitu kingine kikubwa. Kuna tukio moja maarufu jeshini mwaka 1963 ambapo vigogo wa jeshi walikataa askari kufanyishwa kazi za ujenzi wa barabara na kusema kazi hiyo ifanywe na watumishi wa Wizara ya Ujenzi.
Baada ya 1964, Nyerere alihakikisha kwamba askari wa JWTZ wanafanya kazi na majukumu ambayo hufanywa pia na raia. Ni kama vile Ahmed Sekou Toure wa Guinea alivyowapa majukumu askari wake kwenda kuchuma pamba shambani au Fidel Castro wa Cuba na askari wake kuvuna miwa na kufanya shughuli nyingine kama raia wa kawaida.
Jeshi linaposhirikiana na raia wa kawaida kwenye shughuli za ujenzi wa taifa – linakuwa halina tofauti na watumishi wengine wa serikali; ingawa lenyewe lina silaha. Lakini kingine kikubwa kilikuwa ni kufungamanisha Jeshi na chama kimoja kilichokuwa madarakani wakati wote wa Nyerere – Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Busara ya Nyerere ilikuwa kuhakikisha kwamba Jeshi lenyewe lilikuwa na askari ambao ni makada wa CCM. Makada wa chama walikuwa ni wanachama waliopitia hadi mafunzo ya kijeshi na kiitikadi kuhakikisha uhai wa chama.
Kwa maana hiyo, chama kilikuwa juu ya jeshi. Kama ingetokea jeshi lenyewe kuasi, humo ndani yake kulikuwa na makada ambao wangeweza kuondoka jeshini, kuingia msituni na kupambana hadi kukirejesha chama madarakani.
Kwa lugha rahisi, jeshi na chama vilikuwa vimefumwa katika namna ambayo kupindua kimojawapo ilikuwa sawa na kupindua kingine.
Jeshi baada ya Nyerere
Baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi, ilibidi JWTZ na CCM vitenganishwe. Hii ndiyo namna watu kama akina Kikwete, Abdulrahman Kinana, Edward Lowassa, John Komba, Yusuf Makamba, Moses Nnauye na wengine waliamua kuvua magwanda na kuingia kwenye siasa moja kwa moja – wakiacha ajira zao jeshini.
Lakini, hata hivyo, JWTZ bado inafanya kazi za kiraia kila wakati inapobidi. Mara nyingi tunaona askari wetu wakifanya shughuli za ujenzi wa taifa kwa namna zaidi ya moja.
Mojawapo ya urathi tulioachiwa na Baba wa Taifa hadi leo ni mazoea ya kuwapa askari majukumu ya kufanya kazi katika taasisi za kiraia. Kuna wanajeshi ni wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, makatibu wakuu wa wizara na wengine mabalozi.
Na jeshi lenyewe limebaki kuwa lisilotegemea misaada ya kivifaa na kimafunzo kutoka nchi moja. Askari wa JWTZ wanapewa mafunzo kutoka pande zote za dunia na huwezi kusema jeshi limelowea Uingereza, Marekani, India au China, kama katika nchi ambazo unaweza kuona ushawishi wa nchi moja katika jeshi.
Wakati wa Vita ya Kagera, ulikuwepo ushahidi kuwa JWTZ ilikuwa nyuma ya Amiri Jeshi wake. Ushindi wa Tanzania kwenye vita ile ni ushahidi wa mapenzi ya askari kwa Amiri wao.
Nyerere pia alilijali Jeshi. Nakumbuka katika moja ya mazungumzo niliyowahi kufanya na Zakaria Hans Poppe, alipata kuniambia kwamba hata katika nyakati ambazo nchi ilikuwa inapita katika wakati mgumu, jeshini hali haikuwa mbaya kama uraiani.
Mwalimu alijua namna ya kuishi na askari. Na waliomfuata, walau mpaka sasa, wanapita katika njia ileile aliyopita, walau katika mazingira, muktadha na nyakati tofauti.
Uteuzi wa Wakuu wa Majeshi
Eneo lingine nyeti ambalo Baba wa Taifa inaonekana alilitilia maanani lilihusu aina ya watu aliowapa majukumu ya kuongoza JWTZ. Kuondoa uwezo wa kijeshi, inafahamika kuwa Mwalimu alipenda jeshi liongozwe na watu wanaoaminika, wazalendo na walioamini katika falsafa ya JWTZ.
Miaka mingi nyuma, niliwahi kuzungumza na mmoja wa vigogo wastaafu wa JWTZ waliosoma katika chuo maarufu cha Sandhurst nchini Uingereza na jambo moja nililoliona mwanzo ni kuwa hakuwa akikubaliana na Nyerere kwenye mambo mengi.
Kwa mfano, yeye hakutaka JWTZ ishiriki katika vita vya ukombozi wa nchi za Afrika, hakutaka Vita ya Kagera na hakuwa akipenda askari kupewa majukumu nje ya jeshi. Askari wa aina hii hawakuwahi kupewa nafasi ya kuongoza JWTZ, akiwemo huyu niliyezungumza naye ambaye sasa amefariki dunia.
Ukiangalia katika nchi nyingi zinazoandamwa na mapinduzi, sura moja inayojirudia mara kwa mara ni askari waliofundwa nje ya nchi na wenye mahusiano mazuri na wakoloni wa zamani. Haw ani askari waliokuwa wanataka jeshi la taifa lao lifanane na la Ufaransa, Uingereza au Ubelgiji. Hili, kwa Nyerere, halikuwa linakubalika. Kwake, askari wa Tanzania ndoto yake ilikuwa ni JWTZ na si Jeshi la Mwingereza.
Labda Mwalimu alikuwa na bahati ya kuokoka kwenye mapinduzi ya 1964. Hii ni kwa sababu, kama maasi yale yangefanikiwa, huenda leo nisingekuwa naandika makala haya.
Mwandishi ni msomi wa masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kwa email ya; ekamwaga57@gmail.com