Pitio la Kitabu: ‘’Survived and Thriving cha Madiha Tubman

Picha: Ukurasa wa mbele wa kitabu cha Survived and Thriving. Picha kwa hisani ya Mohamed Said

 

Na Mohamed Said

 

KUANZIA  mwanzo wa kitabu ukurasa wa kwanza akili yako itakuambia kuwa mkononi kwako umeshika kitabu ambacho si cha kawaida; si kitabu utakachosoma na kikombe cha kahawa mkononi.

 

Kitabu kinaanza katika hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Liberia na simulizi za watu kuuliwa na majumba kuchomwa moto.

 

Kitabu kama hiki hakikupi nafasi ya kunyanyua kikombe cha kahawa au glasi ya maji ya matunda kwa kuwa mwendo ni wa kasi kinywaji ulichoshika mkononi kitakumwagikia na kuchafua nguo zako.

 

Kitabu hiki kinaanza na kisa cha kutisha cha mwandishi wakati huo msichana mdogo aliyemaliza shahada yake New York Marekani na kuolewa na kijana mwenzake wanahama Marekani kuhamia Liberia kuanza maisha ya ndoa yaliyojaa furaha na mapenzi.

 

Haupiti muda wanabarikiwa mtoto wa kiume.

 

Vijana hawa wanaanza maisha na mwandishi anajikuta katika jukumu gumu la kumsaidia mumewe kufufua shamba la mpira la familia yake.

 

Hili jukumu ni gumu linalohitaji kwanza fedha, muda na mke kujitolea kwa mapenzi aliyokuwanayo kwa mumewe.

 

Kazi hii inamfanya mwandishi wakati mwingine aishi mbali na mumewe anaekuwa shamba porini mbali na mkewe na mtoto.

 

Lakini mwandishi hakuwa peke yake katika juhudi hii ya kumsaidia mumewe.

 

Anawaleta kaka zake pia kuja kusaidia juhudi hizi za kulifufua shamba la shemeji yao.

 

Wakiwa katika hali hii vita vya wenyewe kwa wenyewe vinazuka Liberia.

 

Huu ulikuwa mwaka wa 1989.

 

Raia wengi wa Liberia wanafanya jitihada ya kukimbia nchi kunusuru maisha yao.

 

Mumewe mwandishi anamshauri mkewe wabakie Liberia kwani vita vitapita na wao wataendelea na maisha yao.

 

Hili halikuwa na vita vitakwenda kwa miaka 15 na damu nyingi kumwagika ikifuatiwa na mateso ambayo hayaelezeki wala hayafikiriki kwa yule ambae hakupitia maisha yale.

 

Katika hali kama hii ya vurugu la vita mwandishi na mumewe na mtoto wao mdogo wa umri wa miaka mitatu na watu wengine wanajikuta wamesimamishwa kwenye mstari wakisubiri kuuliwa kwa kupigwa risasi.

 

Hali hii ya watu kuuliwa ovyo pasi na sababu ilikuwa jambo la kawada.

 

Siku yao ya arobaini ya wao kuuliwa ilikuwa imewadia.

 

Wamesimamishwa wao kuuliwa kwa kupigwa risasi kama walivyouliwa wenzao wengi kwa ujumla wao na wengine jamaa zao wa karibu.

 

Kitabu hiki kinampitisha msomaji katika barabara ambayo hajapata kupita, inamuingiza msomaji katika maisha ambayo hajapata kuwaza hata kwa mbali kuwa yalikuwapo na yapo katika dunia hii.

 

Kwako wewe kuamini kuwa maisha hayo yalikuwapo ni kuzama ndani ya kitabu hiki ukawa mmoja wa wale waliofikwa na janga linalohadithiwa na mwandishi, janga lililowakumba watu kama wewe na kwenye nchi kama yako ambayo wewe leo hii unaishi kwa salama.

 

Kila unapofunua ukurasa mpya kuendelea kusoma kitabu hiki akili yako inajipiga maswali yenyewe.

 

Liberia ilifikaje pale na nini sababu yake?

 

Akili inataka kujua inawezekanaje binadamu kumfanyia binadamu mwenzake unyama kama ule?

 

Akili inataka kujua nguvu gani kubwa ilikuwa juu ya mwandishi na mumewe na mtoto wao mdogo ninaowasoma katika kitabu hiki kiasi wakaweza kuishi katika dhiki ile siku baada ya siku wakiwa hawana chakula cha kutosha wala maji si ya kunywa wala fundo la kusukutua baada ya kupiga mswaki asubuhi?

 

Leo mwandishi akiwa hapa pamoja nasi swali kubwa ni kuwa kaweza vipi kuviruka viunzi vyote vilivyomkabili na akatoka salama?

 

Msomaji naamini utapenda kusoma ilikuwaje askari wale wauaji waliolewa damu hakuwamiminia risasi hawa raia waliokuwa hawana kosa lolote.

 

Hili sitakuambia kwani nitakuondolea msisimko utakaopata kwa kusoma kisa kizima kwa macho yako mwenyewe ndani ya kitabu tena ukihadithiwa na muhisika mwenyewe.

 

Ila kwa ufupi ni kuwa Mungu alishusha muujuza kupitia malaika wake mmoja.

 

Msomaji usishtuke kwa mimi kukutajia malaika ukasema labda nataka kukupeleka kwengine.

 

Huyu malaika ni yule mtoto mdogo wa kiume wa miaka mitatu ndiye aliyefanya muujiza uliomnusuru mama na baba yake na kundi lile kubwa la watu kunusurika na kifo.

 

Hakika watoto wadogo ni malaika na ushahidi ni huu.

 

Baada ya kunusurika katika balaa hili mwandishi anasema hapakuwa na cha kuwabakiza Liberia juhudi za kukimbia Liberia zilianza.

 

Mwandishi anaeleza vipi yeye na mumewe na mtoto wao walivyoweza kuondoka Liberia na kuhamia Kenya akidhani kuwa atapata amani aliyokuwa anaitafuta kwa familia yake.

 

Walifanikiwa kuingia Kenya lakini sheria za uhamiaji za Kenya zilimzuia mwandishi kuwa mdhamini wa mumewe kuishi Kenya kama mkimbizi kwa hiyo ikabidi mumewe aondoke aende Ivory Coast kutafuta hifadhi.
Mwandishi akabaki Kenya peke yake na mwanae mdogo.

 

Kutengana na mumewe kipenzi hili lilikuwa pigo kubwa ambalo hakulitegemea.

 

Kufika hapa mwandishi anabadilisha uandishi wake wa mpiga hadithi mahiri aelezae historia ya kutisha anageuka na kuwa mshauri nasaha, mtoa ushauri wa ndoa, na mwanasaikolojia wa maisha ya binadamu kwa ujumla wake.

 

Kitu gani mwandishi kilichomsababisha ageuke na kuwa haya yote?

 

Hili mwandishi kalieleza vizuri katika utanguliza wa kitabu na amerejea tena na tena ndani ya kitabu kulieleza hili kila ilipopatikana nafasi kwa nia ya kusisitiza kuwa binadamu asikate tamaa kwa lolote zito litakalomfika kwani matatizo na mateso ni sehemu ya maisha ya kila binadamu.

 

Mimi najizuia kueleza yale yaliyomkuta mwandishi akiwa Kenya mpweke.

 

Nataka watu wasome wenyewe katika kitabu wapate kufaidi.

 

Nitakachosema hapa kwa maneno mafupi sana ni kuwa mwandishi alitendwa na dhoruba hii haikuwa ndogo.

 

Mwandishi alifikwa na usaliti ulio furtu ada.

 

Alisalitiwa na yule aliyempa nafasi ya kuishi ndani ya moyo wake kwa jua na mvua kitu ambacho hakukitegemea.

 

Waswahili tuna msemo, ‘’Funika kombe mwanaharamu apite.’’

 

Haya yanatosha mkasa kamili tuusome kitabuni.

 

Katika shari hii mwandishi akaitafuta kheri na akaipata ingawa ilimfikia polepole na kwa yeye kutia bidii na ustahamilivu mkubwa.

 

Mwandishi anasema marafiki zake waliokuwa karibu walikuwa na mchango mkubwa sana kwake kuweza kuyashinda yote na kupata faraja.

 

Ushindi huu ndiyo uliosababisha yeye kunyanyua kalamu na kutuandikia kitabu hiki.

 

Mwandishi katambua kuwa yaliyomfika yeye yanawafika wanawake wengi akaamua akae kitako atazame nyuma na katika yale aliyopitia na kuyashinda ayaeleze ili wanawake wengine watakaojikuta katika matatizo kama haya wajue nini la kufanya kujinasua pindi watakapofikwa na yale yaliyomfika yeye.

 

Mwandishi anasema tatizo lolote linalomfika binadamu katika maisha asichukulie kama ni balaa bali ayaangalie hayo matatizo kuwa ni sura kama sura ya kitabu katika maisha na atambue kuwa kuna mafunzo ndani yake.

 

Mwandishi katika kueleza yaliyomfika na kuyashinda kuna maneno anayatumia ambayo yanaweza kumliza hata yule mwenye moyo mgumu.

 

Mwandishi anaeleza mapenzi yake kwa yule aliyemjaza moyoni kwake.

 

Anaeleza jinsi alivyojitolea kwake ambayo na tuzo aliyopokea kama ijaza yake ilikuwa kusalitiwa.

 

Mwandishi anauliza, ‘’Kwa nini mambo mabaya huwafika waja wema?

 

Kuanzia hapa mwandishi sasa anamuingiza msomaji darasani kumsomesha nini akifanye mtu anapokumbwa na balaa lama lile lililomfika yeye.

 

Mwandishi kaandika mengi kuanzia kuishi kwa matumaini badala ya kukubali kuelemewa na matatizo mwishowe yamwangushe chini.

 

Mwandishi baada ya kuweka msingi huu kitabu kinaingia katika sura fupi lakini zimejaa nasaha akieleza tatizo na namna ya kukabiliana nalo.

 

Kuna mengi sana ya manufaa katika hili darsa.

 

Mwandishi anaeleza kuanzia namna ya kujiepusha na watu waovu hadi umuhimu wa kuwa na subra pale mtu anapovamiwa na matatizo.

 

Mwandishi anasema ili kuweza kunyanyuka unahitaji kujua kuanguka kukoje.

 

Hili mwandishi anasema ni somo muhimu.

 

Hiki ni kitabu cha kipekee sana hakipo katika orodha ya vitabu vilivyozoeleka kwani kimejipambanua katika kila nyanja.

 

Kitabu hiki ni rejea tosha kwa jamii kujifunza kuwa panapo nia ipo njia.

 

Hakuna kubwa la kumshinda yule aliyedhamiria kushinda.

 

Hii ndiyo sababu leo tunae miongoni mwetu mtu aliyepitia mazito ya kutisha na kukatisha tamaa na akaibuka mshindi; na baada ya ushindi akatuandikia kitabu ili jamii ijifunze kutoka kwake kuwa inawezekana kuhimili na hatimaye kushinda.