Pumba na mchele kwenye maandamano ya Kenya

Na Willy Mutunga

IBARA ya 37 ya Katiba ya Kenya inampa Raila Odinga na Wakenya wengine haki ya kuandamana, kufanya kusanyiko na kufanya shinikizo kwa njia ya amani, bila vurugu au kubeba silaha.

 

Kwenye mazingira ya namna hii, wajibu wa kikatiba wa vyombo vya dola wakati wa maandamano ni kuhakikisha kuwa haki hiyo ya Raila na Wakenya wote “inatimizwa, kulindwa na kuheshimiwa”.

 

Hii maana yake ni kwamba kazi ya Polisi, kwa mfano, ni kutoa ulinzi kwa waandamanaji “kwa usalama na bila kutumia silaha” kama ilivyo kwa watu wengine ili Wakenya wafurahie haki yao hiyo ya kikatiba.

 

Ni muhimu kufahamu kwamba Katiba inawapa nguvu Polisi kuhakikisha kwamba pale inapotokea kuna watu wanapingana na maandamano hayo, wale wanaotaka kuandamana inabidi ndiyo walindwe.

 

Kazi ya Polisi ni kuhakikisha maandamano yanakuwa ya amani. Jambo pekee lililo kwenye mamlaka ya Polisi ni kuhusu kupanga yatakapofanyikia nan jia zitakazotumika.

 

Suala la Polisi kutaka wao ndiyo watoe kibali ili watu waandamane si la kikatiba na ni matokeo tu ya urathi wa Jeshi la Polisi la enzi za mkoloni. Kwenye utata wowote kuhusu hili, Katiba ya Kenya mwaka 2010 ina majibu yote.

 

Jeshi la Polisi limekuwa likitumika na dola na viongozi tofauti walio madarakani kwa nyakati tofauti kama chombo cha kufanya ukatili dhidi ya raia na kuwanyima haki zao.

 

Zipo hadithi nyingi zinazohusu askari kupiga wananchi, kuwatia vilema vya maisha, kuwaua, kuwapiga mabomu ya machozi, maji yenye kuwasha na virungu katika nyakati tofauti hapa kwetu.

 

Ziko nyakati ukiwatazama Polisi wakiwa wanapambana na waandamanaji unaweza kudhani labda wao ni maroboti tu na si wanadamu wenye hisia, familia na watu wanaowapenda.

 

Mara nyingi ukatili unaofanywa na Polisi huwa una kiwango cha juu cha ukosefu wa ubinadamu. Akiandika katika mtandao wa twitter mara baada ya siku ya kwanza ya maandamano ya Azimio Kwanza kupinga kupanda kwa gharama za maisha, Shailja Patel aliandika; Katika wakati ambapo taifa la Kenya linapita kwenye ukame mkali, na jiji la Nairobi likiwa na shida ya maji, Polisi inatumia maji ya kuwasha kutawanya waandamanaji.”

Kuiangusha serikali

 

Katiba ya Kenya iko wazi kwenye hili. Sehemu ya Kwanza ya Katiba inasema; “Mamlaka yote iko kwa wananchi wa Kenya wenyewe na itatumika kwa mujibu wa Katiba. Wananchi wanaweza kuitumia mamlaka hiyo wao wenyewe au kupitia kwa wawakilishi waliowachagua”.

 

Ibara ya Tatu ya Katiba ya Kenya inaelekeza kwamba kila raia ana wajibu wa kuheshimu, kutekeleza na kuilinda Katiba ya Kenya na zaidi inaongeza; “Jaribio lolote la kutaka kuingiza serikali kinyume cha matakwa ya Katiba ni kinyume cha sheria”.

 

Kwa muktadha huu, ni wazi kuwa Katiba imewapa nguvu Wakenya ya kuiondoa serikali yoyote madarakani pale wanapotaka kufanya hivyo – ali mradi wafuate maelekezo ya Katiba ya mwaka 2010.

 

Ziko namna tofauti ambazo Wakenya wanaweza kufanya kuondoa madarakani serikali ambazo hawaridhiki nazo. Kwa mfano wanaweza kufungua kesi mahakamani kudai kwamba serikali iliyo madarakani si halali na endapo Mahakama itakubaliana nao, serikali itaondoka.

 

Serikali za Kenya zilizofuata baada ya kupatikana kwa Katiba ya 2010 zimefanya mambo kadhaa yaliyoonyesha kutoheshimu amri za Mahakama kwa ulevi wa madaraka na kuoona kwamba hakuna wa kuwafanya kitu.

 

Ni bahati yao tu kwamba hakuna mwananchi walau mmoja aliyekwenda mahakamani na kufungua kesi kwa hoja kwamba kutosikilizwa kwa amri ya Mahakama ya uvunjaji wa Katiba unaoweza kabisa kuitoa serikali madarakani. Hivyo hakuna aliyetumia njia hii.

 

Kama Raila ameamua kufuata njia hii ya kikatiba, anapaswa kubaki kwenye njia hiyo. Ameshiriki kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita na taasisi zote zilizowekwa kikatiba zimeonyesha kwamba alishindwa kwenye huo uchaguzi.

 

Ninaamini kwamba Raila ana wajibu mkubwa wa kuilinda Katiba ya Kenya. Baadhi ya mambo anayofanya sasa yanapingana moja kwa moja na uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya uliomtangaza Ruto mshindi. Hawezi kumwambia mtu aliyeshinda uchaguzi kuondoka Ikulu bila kufuata vigezo na masharti vilivyowekwa kwenye Katiba.

 

Tabaka la Watawala dhidi ya Raia wa Kawaida

 

Kinachoendelea sasa nchini Kenya ni mapambano miongoni mwa tabaka la watawala wa Kenya kimsingi ni mkakati uliotengenezwa kiufundi wenye lengo la kutaka kundi moja la kijamii – tabaka la watawala, kuhodhi mijadala kwa kuwaweka pembeni wale wenye mawazo tofauti kuhusu mwelekeo wa taifa letu.

 

Inanihuzunisha mno kwamba kwenye fursa hii kubwa ya kuwaunganisha na kuwaandaa Wakenya kwenye njia tofauti ya kisiasa inayoweza kufuatwa na taifa lao, hakuna mbadala wa uongozi wa kisiasa unaoweza kuonekana.

 

Kuna wakati gani mzuri wa kuwaweka Wakenya chini kuzungumzia mambo ya msingi yanayowaumiza kuliko wakati huu? Masuala kama ufisadi, madeni ya nchi, kukosekana kwa vyama vya kisiasa ambavyo ni taasisi, umasikini, ukabila, ukosefu wa ardhi, ushirikishwaji wa makundi yote ya kijamii kwenye masuala ya jamii na ujenzi wa taifa letu la Kenya?

 

Na hapo wala sijazungumzia mambo mengi yanayowasibu watu wetu. Kitu cha kuumiza ni kwamba kwenye hayo matatizo niliyoyazungumza, vyama vyetu vya kisiasa vilivyopo kama vile Azimio na Kenya Kwanza – na hata vile vilivyokuwepo zamani kama vile CORD, NASA, Jubilee, havijawahi kuja na suluhisho la matatizo hayo.

 

Nikiri kwamba mara zote nimevutiwa sana na uwezo mkubwa sana wa kiakili wa wanasiasa wetu watawala kwa namna wanavyoweza migawanyiko yetu kama nyenzo yao ya kisiasa na kuweka kando siasa za masuala.

 

Sasa, kwa mtu yeyote mwenye macho na masikio, anaweza kufahamu kwamba siasa zile za kupambana na tabaka la watawala au kuwa Rais wa Wanyonge zilikuwa ni tambo tu za kisiasa. Wakenya ambao hadi sasa wanashindwa kuliona hili katika mapana yake, macho yao yamefunikwa na ukungu wa siasa za makundi zilizoifunika nchi yetu. We now know what the hue and cry about dynasties and hustlers were all about.

 

Nini kinahitaji kufanyika?

 

Kwa mara nyingine, ninatoa wito wa kuitishwa kwa Kongamano la Kitaifa la Wakenya kwa ajili yetu tunaoamini kwamba kitu kinachoitafuna Kenya kwa sasa ni ukosefu wa uongozi wa kisiasa unaohitajika.

 

Mkutano huo utakuwa ni hatua ya kwanza kwenye kutengeneza mbadala wa siasa za sasa za Kenya ambao kwa kweli utafumua kabisa mfumo wa sasa wa tabaka la watawala walio serikalini na kwenye vyama vya upinzani.

 

Mapambano ya Tano ya Ukombozi wa Kenya yamechelewa sana kuanza. Wakati wake ni huu.

 

Ni wazi kabisa kwamba miongoni mwa wanasiasa wa tabaka la watawala walioko sasa, hakuna yeyote mwenye uwezo wa kuongoza Ukombozi huo wa Wakenya unaohitajika sana wakati huu.

 

Kwa miaka yote, ni sisi Wakenya wenyewe ndiyo ambao tulifanya vitu vilivyoleta mabadiliko hapa kwetu, hata wakati ambapo kufanya hivyo ilikuwa hatari.

 

Tuendelea na Mapambano kwani safari yetu bado haijafika tunapotaka. Tutumie maadhimisho ya siku ya SABA SABA mwaka huu kwa ajili ya kufanya mkutano huu muhimu. Haya mengine yanayoendelea ni pumba tu, mchele ni huu.

 

Mwandishi wa makala haya ni Jaji Mkuu mstaafu na Rais wa Mahakama ya Juu ya Kenya (2011 -2016). Makala hii ilichapwa kwa lugha ya Kiingereza kwenye gazeti la The Star la Kenya la Machi 21 mwaka huu. Hii ni tafsiri isiyo rasmi ya lugha ya Kiswahili. https://www.the-star.co.ke/opinion/leader/2023-03-21-willy-mutunga-separating-political-wheat-from-chaff-in-azimio-demos/