Putin na Prighozin: Mafunzo  

Picha: Putin na Rasputin. Picha ya Washington Times

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

TUKIO la mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo vikosi vya majeshi ya mamluki wa Wagner Group vinavyoongozwa na Yevgeny Prigozhin kusogea hadi takribani kilometa 400 kutoka Mji Mkuu wa Urussi katika kilichoonekana kama mwanzo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, liliwashangaza wengi.

 

Inajulikana kwamba Prigozhin ni swahiba wa muda mrefu wa Rais Vladimir Putin na mambo yote yanayofanywa naye na mamluki wake yana baraka za mtawala huyo wa Urusi kwa takribani miongo mitatu. Swali ambalo wengi walikuwa wakijiuliza ni kwamba nini kimesababisha wawili hao kukorofishana kiasi cha kufikia Wagner kuonyesha uasi huo wa hadharani?

 

Ni muhimu nikaeleza mapema pia kwamba angalau sasa tunafahamu Putin na Prigozhin wameelewana kiasi kwamba vikosi vya Wagner vimeachana na uasi wake baada ya mazungumzo yaliyoratibiwa na Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko. Lakini nini hasa tunaweza kujifunza kutoka katika kadhia hii ya karibuni nchini Urussi?

 

Jambo la kwanza kabisa linahusu siasa. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanafahamu kwamba kiongozi yeyote anayekaa madarakani kwa muda mrefu – yeye au chama chake, wanaanza kupoteza mvuto kwa watu wa kada ya chini. Hii ni kwa sababu kuwa kwao madarakani taratibu kunawafanya wapoteze sifa zilizowaingiza madarakani awali.

 

Ni mgogoro unaovikumba vyama na viongozi wengi walio madarakani. Rais Yoweri Museveni wa Uganda leo hasisimui vijana na watu wa kada ya chini kama alivyokuwa miaka 40 iliyopita. Juhudi zozote atakazotaka kufanya sasa kuunganisha au kupata wafuasi inabidi zitumie ama rasilimaliza fedha au nguvu ya kumiliki dola.

 

Hata hapa nyumbani kwetu leo, nguvu na ushawishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokuwa nayo wakati ikianzishwa mwaka 1977, haifanani na hali ilivyo leo. Ni vigumu kwake leo kufanya aina yoyote ya mapinduzi kupitia kada za watu wa kawaida kwa sababu muda wake mrefu kumeifanya ipoteze ushawishi na kada hiyo.

 

Huo ndiyo mtihani mkubwa alionao Putin hivi sasa. Kwamba baada ya takribani miaka 25 madarakani, nguvu na ushawishi wake kwa wananchi wa Urussi haifanani na ilivyokuwa miaka 15 hadi 10 iliyopita. Pamoja na yote aliyoyafanya kwa taifa na watu wake, ukweli kwamba amekaa madarakani kwa muda mrefu – hata katika kipindi kile kidogo alichomwachia Dmitry Medvedev, kunafanya baadhi ya watu kuanza kumchoka.

 

Inapofika katika mazingira haya, kiongozi au utawala wake, hutafuta mtu au kikundi cha kuiunga mkono ambacho kitaleta muunganiko kati ya dola/kiongozi na watu wa kada ya chini. Urussi ina historia na jambo hili. Utawala wa mwisho wa kifalme wa Urusi ya zamani – The Romanovs, ulikuwa katika mazingira ya namna hii kabla ya Mapinduzi ya Ki-Bolsheviki ya mwaka 1997.

 

Wakati huo, mtu aliyefanya kazi ya kuwa kiungo kati ya watu wa chini na Ufalme aliitwa Grigor Rasputin – wengi wakimwita kwa jina la Kasisi Kichaa. Rasputin alijisogeza karibu na Ufalme kiasi cha kuaminika na kuheshimika, akikemea maovu, kuponya wagonjwa na kuzungumza lugha inayoeleweka kwa watu wa daraja la chini.

 

Ndiyo kazi anayofanya Prigozhin sasa. Ukisikiliza kwa makini mazungumzo yake, hajawahi kumsema Putin hadharani. Vita yake kubwa huwa ni dhidi ya Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu na viongozi wengine wa jeshi rasmi la taifa hilo. Anawaponda kwa kusababisha mikakati ya kijeshi ya Russia kwenye vita dhidi ya Ukraine kwenda mrama hadi sasa.

 

Anakemea ufisadi wa watu wa tabaka lao na kuunga kwao mkono “kwa wasiwasi” vita inayoendelea sasa Ukraine. Maneno yake ndiyo hasa maneno ambayo watu wa kada ya chini wanataka kuyasikia. Yeye – kwa sasa, anaonekana kama shujaa wa watu wa chini na Putin anahitaji mtu wa aina hiyo pembeni yake kwa sababu kukaa kwake madarakani muda mrefu kunamnyima sifa hiyo.

 

Mwisho wa maisha ya Rasputin haukuwa mzuri na natabiri kuwa hata mwisho wa Prigozhin nao hautakuwa mzuri. Itafikia wakati ambapo nguvu ya Prigozhin itakuwa kubwa au sawa na ile ya Putin na huo ndiyo utakuwa wakati ambapo jasusi huyo wa zamani KGB atamalizana naye.

 

Jambo la pili kulifahamu kuhusu kinachoendelea Urussi sasa kimeelezwa vizuri sana na Profesa Nina Khruscheva, mjukuu wa Rais wa zamani wa Urusi, Nikita Khruschev, ambaye kwangu ndiye mchambuzi mahiri zaidi ninayemfahamu kuhusu masuala ya Urusi. Katika uchambuzi aliouandika Aprili mwaka huu kwenye jarida la Project Syndicate, Nina aliandika kifalsafa kuhusu ni kwa vipi Warussi wanapigana vita dhidi ya Ukraine.

 

Nina alisema nchini Urussi, anayepinga vita dhidi ya Ukraine anaonekana kama msaliti na hivyo watu wengi ‘hupigana’ vita hii kimyakimya. Pasipo kupinga au kuonyesha hadharani kupinga vita isiyo na maana, wengi wao wameamua kukaa kimya. Namna ambavyo vikosi vya Wagner vilipasua katikati ya Urussi – huku vikishangiliwa katika baadhi ya maeneo, bila kupata upinzani wowote wa maana wa kijeshi, kunaeleza tabia hii ya Kirussi.

 

Kama wangekuwa wanaunga mkono vita au serikali inakubalika, tungeona hadharani namna vikosi vya Urussi vinavyopambana na mamluki hao au wananchi kuweka aina fulani ya vikwazo barabarani. Vyote hivyo hatukuviona wikiendi iliyopita na hii ni ishara mbaya kwa Putin.

 

Vitu vingi havifahamiki sana kuhusu nini hasa kilisababisha Prigozhin na vikosi vyake vioneshe uasi huu wa waziwazi ulioshtua dunia. Kadri muda unavyokwenda, tutazidi kupata taarifa na maarifa zaidi kuhusu nini hasa kimetokea. Lakini, kwa sasa, inaonekana nyakati za giza (Smuta) haziko mbali sana na utawala wa Vladimir Vladimirovich Putin.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.