KARATA za kisiasa anazozicheza William Ruto, Rais wa Kenya, katika jukwaa la kimataifa zinamfanya aonekane kuwa ama ni mwerevu au ni fala. Kuna wasemao kwamba hana uwerevu wowote lakini si mjinga wala zuzu kwani anajua akifanyacho — amejitolea kuitumikia Marekani na kuwa askari wake katika ukanda wa Afrika Mashariki na katika nchi zinazoendelea, kwa jumla. Kwa ufupi, wanasema kuwa yeye ni kibaraka mwenye kucheza ngoma ipigwayo na Marekani.
Tunaifanya tathmini hii ya haraka haraka wakati ambapo Ruto amejitolea kupeleka askari wa Kenya kwenda kutuliza hali tete ya usalama huko Haiti, nchi iliyo takriban kilometa 12, 300 kutoka Kenya, ukivuka misitu ya Afrika, jangwa na bahari ya Atlantiki. Wiki iliyopita, Ruto alipokewa kwa mbwembwe na Rais Joe Biden wa Marekani alipofanya ziara ya kitaifa nchini humo.
Ruto alialikwa Washington kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano madhubuti baina ya Marekani na Kenya.
Hizi ni nyakati za kusisimua katika siasa za kimataifa. Pia ni nyakati za kutisha na kuhuzunisha tukiangalia yanayojiri Gaza, Ukraine na katika sehemu nyingine za dunia.
Tukiuangaza ulimwengu tunayaona madola makuu yakiwa yanaurejelea ukorofi wa vile viitwavyo “Vita Baridi.” Hivi si vita vya kupigana lakini zaidi ni ushindani mkali, wa kufa au kupona, baina ya Marekani na washirika wake wakuu wa Ulaya ya Magharibi, kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, Urussi na China.
Hata hivyo, kuna dalili kwamba Marekani, Uingereza na Umoja wa Kujihami wa NATO, zimekaa mkao wa vita halisi dhidi ya Urussi. Hata Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban ameonya kwamba Umoja wa Ulaya unajiandaa kuanzisha vita dhidi ya Urussi. Pande hizo mbili zinayarandia mataifa ya Kiafrika. Tukiupiga macho ulimwengu tunaziona nchi za Kiafrika, za Amerika ya Kusini na za barani Asia zinaelemea upande wa Urussi.
Hali hiyo imeishtua Marekani na washirika wake. Katika miezi ya hivi karibuni Marekani na Ufaransa zimepata mapigo makubwa katika ukanda wa magharibi mwa Afrika.
Mwaka jana, baada ya mapinduzi ya kijeshi huko Niger serikali mpya iliwatimua wanajeshi wa Marekani waliopindukia elfu moja waliokuwa kwenye kambi mbili nchini humo. Wanajeshi hao walikuwa huko kuyasaidia majeshi ya Niger kupambana na magaidi wa Kiislamu katika eneo la Sahel.
Katika wiki za hivi karibuni Chad nayo iliiambia Marekani iwaondoshe wanajeshi wake waliokuwa huko. Hali kadhalika, serikali za Burkina Faso, Mali na Niger zimewafukuza wanajeshi wa Kifaransa kutoka nchi zao. Mtindo uliopo ni wa nchi hizo zilizo katika Ukanda wa Afrika Magharibi kuzipa kisogo Marekani na Ufaransa na badala yake kukuza ushirikiano na nchi za Urussi, China na Iran.
Marekani, kwa upande wake, haikulala na imekuwa mbioni kuzitia kwapani nchi zitazokuwa tayari kufuata maamrisho yake. Na huo ndio umuhimu kwa Marekani wa nchi kama Kenya.
Tangu ipewe uhuru na Uingereza Desemba 1963, Kenya imekuwa ikipakatwa na Marekani. Ni miongoni mwa nchi za Kiafrika ambazo Marekani inaziona kuwa ni muhimu kwa mikakati yake. Ndio maana Kenya imekuwa ikiengwaengwa na Marekani katika muda wote huu wa miaka 60. Hakuna hata mara moja ambapo Kenya iliikosea Marekani kiasi cha kuifanya itengwe na hilo dola kubwa kiuchumi lenye nguvu kuu za kijeshi duniani na ushawishi wa kisiasa usio kifani.
Kumekuwako na mikwaruzano ya hapa na pale kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utawala wa Rais wa pili wa nchi hiyo, Daniel arap Moi. Lakini, kwa jumla, Marekani na Kenya zimekuwa chanda na pete.
Kwa namna uhusiano wa nchi hizo mbili ulivyopea hutolaumiwa ukisema kwamba Kenya imekuwa kama himaya ya Marekani na Uingereza tangu enzi za Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Mzee Jomo Kenyatta. Hakuna Rais yeyote wa Kenya aliyethubutu kuisusa Marekani, si Kenyatta, si Moi, si Mwai Kibaki, si Uhuru Kenyatta (mtoto wa Jomo) na wala si huyu wa sasa, William Ruto.
Novemba mwaka jana Ruto na serikali yake walikubali kupeleka askari polisi 1,000 katika nchi ya Haiti ili kuyashinda nguvu magenge yaliyotamalaki huko na kuisambaratisha hata serikali.
Haiti ni taifa lililoshindwa kujikimu kwa kila hali. Ni taifa lililofeli ambalo, kwa miongo mingi, limekuwa likidhibitiwa na Marekani na Ufaransa. Kuna nchi tatu duniani zilizojitangazia uhuru wa kisiasa kutoka Ufaransa na zote hazijatulia, zimekuwa na migogoro isiyokwisha na zimekumbwa na ufukara usiosemeka. Nchi zenyewe ni Comoro (Julai 6, 1975), Guinea (Oktoba 2, 1958) na Haiti (Januari 1, 1804).
Ruto ameshindwa kuzuia uhalifu unaofanywa na magenge na majambazi nchini Kenya kwenyewe, na hasa Nairobi. Na sasa anawapeleka polisi wa Kenya nchini Haiti kuyazuia magenge ya huko ambayo pengine ni ya hatari kubwa zaidi kushinda yale ya Kenya. Mpango huo hauingi akilini lakini unawafanya wengi waamini kwamba ni mpango wa Ruto kujipendekeza kwa Marekani.
Wenye kuamini hivyo wanasema kwamba mpango huo ni sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kuwa madarakani. Ruto amekwama na anaonekana kuwa tayari kufanya kila analoweza kulifanya ili endelee kubaki Ikulu ya Nairobi.
Wiki iliyopita katibu mkuu wa chama chake cha United Democratic Alliance (UDA), Cleophas Malala, alikuwa Beijing akijaribu kujifunza mawili matatu kutoka Chama cha Kikomunisti cha China (CCP), chama chenye umri wa miaka 103 kilichoundwa na Mao Zedong mwaka 1921. Ukivilinganisha vyama hivyo vya UDA na CCP, UDA cha Ruto ni kichanga mno.
Chama hicho kiliundwa Desemba 2020 na kauli mbiu yake ni “Kazi ni Kazi” na, kwa kweli, kina kazi kubwa ya kuuangalia uzima na uhai wake. Vyama vya siasa nchini Kenya huwa havidumu kwa muda mrefu, mara hufa. Hakuna hata kimoja kinachoweza kulinganishwa, kwa mfano, na Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Tanzania seuze hicho cha Kikomunisti cha China. Hata CCM nacho hujifunza kutoka kwa Wachina.
Kwa hivyo, inaeleweka kwa nini Ruto akataka chama chake nacho kitabaruku kwa mafunzo ya Wachina juu ya namna ya kukifanya kiendelee kuwa na afya njema.
Bahati mbaya, ukabila haujatoweka katika siasa za Kenya na kuna mpasuko baina ya Ruto na kaimu wake Rigathi Gachagua pamoja na wanasiasa waroho kutoka eneo la Mlima Kenya. Wao wanayapinga maridhiano ya Ruto na Raila Odinga.
Ruto ameuweka mbele mustakbali wake wa kisiasa na ziara ya kitaifa aliyoifanya Marekani wiki iliyopita ilitokea katika wakati muwafaka kwa mustakbali huo. Bila ya shaka, ni sadfa kwamba Ruto ndiye Rais wa Kenya, Biden alipotangaza kwamba Marekani inaipa Kenya hadhi ya kuwa mshirika wake mkuu asiye mwanachama wa Umoja wa Kujihami wa NATO.
Swali la kujiuliza ni hili: Ina maana gani Kenya kupewa hadhi ya kuwa mshirika mkuu wa Marekani asiye mwanachama wa Umoja wa Kujihami wa NATO? Wengi wanaiona hadhi hiyo kuwa kama bahashishi ambayo Marekani inaipa Kenya kwa kukubali kuyasimamia maslahi ya Marekani katika mataifa ya ulimwengu wa tatu, iwe Somalia au Haiti.
Nchi inayokuwa na hadhi hiyo inakuwa na uhusiano wa kina wa kimkakati na wa usalama pamoja na Marekani. Kwa kupewa hadhi hiyo, Kenya itapata manufaa ya kiuchumi na kijeshi. Kwa mfano, itakuwa rahisi kwa nchi hiyo kununua teknolojia za kijeshi kutoka Marekani kushinda nchi nyingine zisizo na hadhi hiyo.
Kenya ni nchi ya kwanza ya Kiafrika iliyo kusini mwa jangwa la Sahara kutunukiwa hadhi hiyo. Kuna nchi tatu nyingine za Kiafrika zenye hadhi hiyo lakini zote ziko Afrika Kaskazini — Misri, Morocco na Tunisia.
Kwa Ruto kupewa bendera hiyo ya kuitetea Marekani kunatoa tafsiri hasi kwa bara la Afrika. Tukio hilo linatisha kwa kuwa katika mkutano mkuu uliopita wa Umoja wa Afrika, Rais huyo wa Kenya alichaguliwa awe mwenyekiti wa Kamati ya Mageuzi ya Umoja huo. Hiyo ni dhima kubwa aliyotwikwa Ruto.
Swali jengine linaloibuka hapo ni hili: ikiwa Ruto atakuwa anabeba bendera ya kuitetea Marekani atawezaje wakati huo huo kubeba bendera ya kiitikadi ya Umajumui wa Afrika? Si kuna mgongano wa maslahi hapo?
Inasikitisha kwamba baada ya miaka 60 tangu nchi nyingi za Afrika zipate uhuru, bado kuna majaribio ya mataifa ya nje kulichezea bara letu, kutugonganisha vichwa wenyewe kwa wenyewe na kutufanya tuwe kama vikaragosi.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.