Siku Membe aliponieleza kuhusu Miungu Watu

MWAKA 2017, utawala wa Rais John Magufuli ulikuwa umeanza kushika kasi. Wakati huo nilikuwa Mhariri wa gazeti la Kiswahili la kila wiki la Raia Mwema na uchambuzi wangu kuhusu uteuzi wa baraza lake la kwanza la mawaziri – ambapo nilihoji uchache wa Wazanzibari, Waislamu na Wanawake kwenye baraza hilo, ulikuwa tayari umevuruga uhusiano wangu naye.

Kwa kifupi, uchambuzi wangu ulieleza kwamba haikuwa sahihi kuwa na baraza la mawaziri lenye wanawake wawili na Wazanzibari wa idadi hiyo katika nyakati hizi ambazo usawa wa kijinsia na kelele kuhusu Muungano  hasa kutoka upande wa Zanzibar, yalikuwa ni masuala tete.

Hitimisho langu kuhusu baraza la kwanza la Magufuli lilikuwa kwamba katika historia ya Tanzania, hasa baada ya kuungana kwa vyama vya TANU na ASP na kuundwa kwa CCM mwaka 1977, baraza hilo ndilo lililokuwa na uwiano  mbovu zaidi wa masuala ya kidini, kikanda, kijinsia na kwa kuzingatia Muungano.

Nakumbuka mmoja wa mawaziri wa Magufuli alinifuata na kunieleza namna uchambuzi wangu ule ulimvyomkera Rais. Akaniambia kwamba kwenye jicho la Magufuli, masuala ya usawa wa kijinsia, kuangalia uteuzi kwa jicho la Muungano au usawa wa kidini ni mambo yaliyosababisha nchi irudi nyuma. Kwa maneno mengine, akanieleza waziri yule, kama unaweza kuunda baraza la mawaziri lenye Wakristo, wanaume au Waislamu watupu lakini wakafanya kazi inayotakiwa, ni vizuri kuliko kuwa na usawa wa kidini na kijinsia lakini kuweka wasiofaa.

Nilimweleza waziri yule kwamba mimi siamini kwamba ukijali usawa maana yake utaharibu ubora wa wanaoteuliwa. Unaweza kuwa na uwiano mzuri na bado ukapata watu bora wa kukufanyia kazi zako. Nikampa ofa waziri yule kwamba kama wana mtu anaweza kuandika mawazo ya Rais yanayopingana na makala yangu, ningewapa kurasa mbili za kati waandike.

Kwa bahati mbaya, hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kuandika makala ya kueleza hayo aliyonieleza mheshimiwa yule na mwaka huo ndiyo ulikuwa mwaka wangu wa mwisho kuhariri gazeti hilo kwani lilifungiwa kutokana na mahojiano niliyofanya na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye wakati huo alikuwa mwanachama wa CHADEMA.

Lakini hiyo ni stori ya siku nyingine. Leo tuzungumze kuhusu miungu watu.

Miungu Watu ni akina nani?

Sasa katika nyakati hizo, nilikuwa nainjoi sana kuzungumza na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Benard Membe. Nikiwa na wazo au kazi za kichambuzi kuhusu siasa na masuala ya mambo ya nje ya Tanzania, mtu mmoja wa kumwona alikuwa Membe.

Katika siku hizo za mwaka 2017, nilikwenda ilipokuwa ofisi binafsi ya Membe jirani na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika iliyoko Oysterbay, kwa ajili ya mazungumzo. Tulipozungumza kuhusu nini kilichokuwa kinaendelea, Membe alinifungua macho na masikio kwa mtazamo wake kuhusu utawala wa Magufuli.

 

Alinieleza kwamba tatizo moja kubwa la Magufuli lilikuwa kwamba alikuwa akijiona kwamba kwenye utawala wake, baada ya yeye ni Mungu. Kwamba kuna Watawaliwa, Rais na halafu Mungu. Mwanasiasa huyo ambaye wakati huo tayari alikuwa akionekana kama mkosoaji wa utawala wa Magufuli na mmoja wa wale waliokuwa wamewekwa kando, ndiyo akanipa msamiati mpya kisiasa.

“ Ukweli ni kuwa kati ya Magufuli na Mungu kuna kundi lipo hapo katikati linaitwa Miungu Watu. Hao ni haya mataifa makubwa duniani kama vile Marekani, Uingereza, China na Russia. Hawa, kama wakiamua jambo lao kuhusu wewe, uongozi wako utakuwa wa taabu. Ni muhimu sana kukaa vizuri na hawa miungu watu”, alinieleza.

Membe alikuwa akinieleza kuhusu namna Tanzania ilivyofanikiwa kuwa rafiki wa Marekani, China na Russia kwa wakati mmoja. Kimsingi, wakati nikiwa na Membe siku hiyo, alikuwa amemaliza kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, kuhusu masuala ya uhusiano wa Russia na Afrika.

Membe alinieleza namna alivyosikitika kuona utawala wa Muammar Gaddafi ukiangushwa kwa sababu hao Miungu Watu waliamua hivyo. Akanieleza namna mtawala huyo wa zamani wa Libya alivyokuwa na ukwasi uliowafanya hata marais wa nchi tajiri wamtafute kuwasaidia fedha za kampeni zao na biashara za maswahiba wao.

Akanieleza namna Cuba ilivyobanwa na vikwazo na Saddam Hussein alivyokamatwa “kama panya” baada ya Marekani – sehemu ya hao Miungu Watu, kuibua tuhuma kwamba anahifadhi silaha za maangamizi ambazo hazikukutwa hadi wakati kiongozi huyo wa Irak aliponyongwa.

Somo kubwa katika mazungumzo yetu lilikuwa hilo la kuishi vizuri na Miungu Watu. Ukiishi nao vizuri utapata fursa ya kujenga taifa lako bila vikwazo vingi kama Julius Nyerere lakini ukigombana nao unaweza kuondoka duniani ukiwa kijana kama Patrice Lumumba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ukiwa Rais wa nchi za dunia ya tatu, ni muhimu sana kufahamu kuwa kati yako na Mwenyezi Mungu kuna hao wanaoitwa Miungu Watu