“Sit down and talk”: Uchambuzi wangu

Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume (kushoto) katika mojawapo ya mazungumzo ya faragha aliyowahi kuyafanya na aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, marehemu Seif Shariff Hamad, kisiwani Unguja. Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

BAADA ya maneno ya kujibizana baina ya viongozi wa vyama viwili vikuu vya siasa visiwani Zanzibar – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo, kuhusu mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUKI), hatimaye Rais mstaafu, Amani Karume, ametoa kauli yake akizitaka pande hizo kuacha kuoneshana ubabe na badala yake wakae chini na kuzungumza.

 

Kwenye eneo la SUKI, maneno ya Karume yanachukuliwa kwa uzito mkubwa. Yeye anaweza, bila ubishi wowote, kuitwa ndiye mlinzi au mwangalizi wa Maridhiano ya kisiasa ya Zanzibar, hasa baada ya kifo cha Seif Shariff Hamad. Wawili hao, pengine kuliko mtu mwingine yeyote, ndiyo walisimamia na kufanikisha uundwaji wa SUKI ya kwanza mnamo mwaka 2010.

 

Katika mahojiano alofanya jana Machi 12, 2024 na mwenzangu Yusuf Khamis wa Azam TV Zanzibar, Karume alitumia lugha ya Kiingereza kutoa kauli yake. “Sit down and talk” na kueleza kwa urefu kuwa suala la SUKI lina manufaa kwa Wazanzibari wote na kwamba suala la jeuri na kiburi halina maana kwa sababu hakuna anayemiliki visiwa hivyo.

 

Suala la SUKI na maridhiano ya kisiasa Zanzibar ni suala ninalolifuatilia kwa karibu. Mapema sana, ninapenda kutangaza maslahi mapema kwamba mimi ni muumini wa SUKI na naamini kwa maslahi ya visiwa hivyo, hilo ni suala lenye tija. Ninalotaka kufanya kwenye uchambuzi huu ni kuangalia kiundani kidogo nini kilichosemwa na Karume na kuweka maoni yangu kuhusu akina nani wanatakiwa ku “sit down na talk”.

 

 

Kuhusu SUKI na udhaifu wake

 

Rafiki yangu Dk. Nico Minde jana kafanya uchambuzi mzuri kwenye tovuti ya The Chanzo kwa kuandika kwa nini SUKI Zanzibar inashindwa kutimiza kile kilichotakiwa kufanyika. Kuna matatizo yanayofanana kuhusu nchi tofauti ambazo ziliamua kufuata njia ya kuunda serikali za maridhiani kutokana na matatizo yaliyojitokeza.

 

Nakubaliana na Minde kuhusu kwamba tatizo la SUKI ni kuwa CCM na ACT wamegawana vyeo kwenye SUKI lakini hawajagawana mamlaka kama ambavyo ingetakiwa kufanyika. Lakini amezungumzia pia udhaifu wa kimsingi wa serikali za aina ya SUKI ambapo kunakuwa kama hakuna chama cha upinzani na hivyo uwajibikaji unakuwa tatizo.

 

Mimi naamini kwamba tatizo kubwa la SUKI ya Zanzibar na serikali nyingine za maridhiano zilizowahi kufanyika Afrika haliko kwenye SUKI yenyewe. Tatizo kubwa liko kwenye dhamira za wale waliounda serikali hizo. Ni kama vile hawakuwa wanaamini kwenye roho ya kuwa na utawala wa aina hiyo – iwe Umoja wa Kitaifa, Mseto au vinginevyo.

 

Kwa mfano, Robert Mugabe wa Zimbabwe alikubali kuunda serikali na MDC ya Morgan Tsvangirai si kwa sababu aliamini katika maridhiano bali kwa sababu ndiyo ilikuwa njia yake ya kubaki madarakani. Ukiangalia ya Mwai Kibaki na Raila Odinga kule Kenya mwaka 2008, utaona tatizo lilikuwa hilohilo kwamba baada ya kushindwa uchaguzi, namna pekee ya Kibaki kuendelea kubaki madarakani ilikuwa ni kuongoza kupitia maridhiano na mpinzani wake.

 

Ni kwa sababu hiyo, ndiyo sababu mara wanaporejea kwenye viti vya enzi, watawala wanaweza kutoa kauli zinazoonyesha kwamba kimsingi walilotaka limefanikiwa. Na namna ya kwanza, ni kuhakikisha wapinzani hawashiki madaraka katika vyombo ambavyo kweli vingewapa nguvu ya kufanya kitu.

 

Sehemu nyeti kama vyombo vya ulinzi na usalama, fedha, mambo ya nje na tawala za mikoa na serikali za mitaa hubaki kwenye mikono ya chama kilichokuwa madarakani. Wale wanaoingia, huishia kubaki kwenye wizara na idara ama zenye changamoto nyingi au zisizo na mamlaka au nguvu ya kufanya kitu cha maana.

 

Chukulia mfano wa Zanzibar. Katika hali ya kawaida, kama SUKI ingekuwa imetengenezwa kwa nia njema, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar angepewa mamlaka fulani ambayo yangempa majukumu. Kwa mfano, kuwa Kiongozi wa Shughuli za Baraza la Wawakilishi. Lakini kwenye SUKI ya Zanzibar, Makamu wa Kwanza hana majukumu yoyote zaidi ya kuwa na cheo alichonacho.

 

Kwenye uchaguzi uliopita, zilikuwepo taarifa za viongozi wa ACT Wazalendo kutekwa na kuumizwa na watu waliohusishwa na vyombo vya dola. Kama SUKI ingekuwa na nia njema na kufuata ile raisson d’etre ya uwepo wake, ungetarajia wizara ya Vikosi vya SMZ kupewa mtu wa ACT ili aweze kuifanyia marekebisho na maboresho. Lakini hilo halikufanyika.

 

Katika mahojiano aliyofanya jana na Azam TV, Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto, alimweleza mwandishi kwamba makubaliano yaliyofikiwa baina ya Rais Hussein Mwinyi na Maalim Seif hayakuwa ya kisheria na kimsingi hayakuwahi kufikishwa CCM na pengine ndiyo sababu utekelezaji wake unakwama. Kauli hii ina viashiria vyote vya kuonyesha kwamba hakukuwa na maridhiano baada ya uchaguzi wa 2020.

 

Mmoja wa wasomi nguli wa masuala ya maridhiano katika nchi zilizokuwa na migogoro, Dk. Tshepo Madlingozi, aliwahi kufanya uchambuzi maridhawa kuhusu maridhiano yaliyopo Afrika na kukosoa kwamba tatizo kubwa liko kwenye ukweli kwamba waliotengeneza dhana hiyo walikuwa watu wa magharibi wenye mila na desturi tofauti kuanzia kwenye kuzungumza ukweli, dini na mazingira na watu wa maeneo kama Afrika.

 

Kwenye sit down na talk ya Karume, naamini – kwa kuangalia changamoto ya Madlingozi, kuangalia ni akina nani na kwa vipi wanatakiwa kukaa chini na kuzungumza ili mwafaka wa kweli wa kisiasa wa Zanzibar upatikane.

 

Napendekeza kwamba kwa sababu Zanzibar ni taifa ambalo karibu watu wake wote ni Waislamu na Uislamu una athari zaidi katika jamii yake, ni muhimu viongozi wa dini wakahusishwa katika aina yoyote ya mazungumzo kuanzia sasa. Siyo tu viongozi, lakini ikiwezekana wanasiasa watakaohusika, wanatakiwa kushikishwa kitabu kitakatifu cha Kurani na kusema kwamba kile kitakachokubaliwa, ndicho hasa kitakachofanyika.

 

Kama mtu ataweza kuapa kwa kutumia Kurani na kisha akashindwa kufuata kile alichoahidi kutekeleza, jambo hilo sasa itabidi liachwe kwa Allah mwenyewe alimalize kwa namna yake. Maridhiano ya Afrika Kusini yaliongozwa na Askofu Desmond Tutu kwa sababu ya hadhi yake kama mtetezi na dini ya Kikristo ina ushawishi zaidi huko. Badala ya mazungumzo ya Rais Mwinyi na Makamu Othman Masoud, pengine Mufti au Sheikh anayeheshimika zaidi visiwani humo anaweza kuwemo kwenye mazungumzo yanayofuata.

 

Naamini pia kwamba ni lazima watu wa vyombo vya ulinzi na usalama washiriki kwenye mazungumzo hayo. Hakuna uchaguzi wa Zanzibar uliowahi kufanywa ambako hutasikia hili au lile kuhusu vikosi na masuala ya Janjaweed. Ni muhimu wadau wa vikosi hivyo wakawepo ili kuondoa kutoaminiana na kuwa katika mstari mmoja kwa wahusika wote.

 

Kundi lingine ambalo ningetamani lishiriki katika “sit down and talk” linatakiwa kuwa wadau wa maendeleo kutoka jumuiya ya kimataifa. Ninaamini kabisa kwamba endapo nchi kama Marekani, Uingereza na nyingine za namna hiyo zikiahidi kuweka vikwazo dhidi ya wale wote watakaokiuka mwafaka na kuvuruga hali ya Zanzibar kuelekea 2025 na baada ya hapo, hilo linaweza kuwa ni kitisho cha kutosha kwa wahusika wa maridhiano ya Zanzibar.

 

Kuna asasi za kiraia zenye nguvu na zinazofanya kazi na wananchi wa Zanzibar, pomoja na wawakilishi wa makundi ya wananchi ambao wanastahili kuwa sehemu ya maridhiano. Haitakuwa rahisi kwa CCM au ACT kudai kwamba mazungumzo baina ya viongozi wao hayakuwa ya kisheria au hayajafikishwa kwenye chama, endapo watu wa makundi tofauti watakuwa pia walihusika na kushuhudia kilichozungumzwa na kutolewa viapo.

 

Ni kwa kufuata njia ambayo inahusisha watu wengi zaidi, ya kuaminiana zaidi na yenye kufuata mila na desturi za Wazanzibari kama watu na jamii, ndiyo SUKI itaweza kushika mizizi na hatimaye kuchanua, na kuwa mfano wa kuigwa na wengine.

 

Na wala haitakuwa ajabu kwa Zanzibar kuwa ya kwanza kufanya kitu na kikaigwa na wengine. Fursa ipo. Naunga mkono “Sit down and talk”, lakini natamani hao watakaokaa, wasiwe watu wawili waliojifungia wenyewe.

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.