TANESCO: Nyamo-Hanga, Ulanga, Makamba na wahanga

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika tukio la kuwaapisha viongozi wapya wa serikali wiki hii, Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha ya Ikulu
Na Ezekiel Kamwaga
KUELEWA uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumfanya Boniface Gissima Nyamo-Hanga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la TANESCO kunahitaji tafakuri ya mambo kadhaa yanayohusu shirika hilo na historia ya miaka ya karibuni ya mhusika.
Labda nianze na jambo ambalo halijasemwa sana. Kwamba katika uteuzi wa wiki iliyopita wa Rais Samia, watu watatu; Nyamo-Hanga, Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, Peter Ulanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felichesmi Mramba, walikuwa darasa moja wakati wakisomea Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katikati ya miaka ya 1990.
Hawa ni watu wanaojuana vema. Pacha wa Peter, Balozi John Ulanga, naye alikuwepo kwenye uteuzi ule – akihamishwa kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na kupelekwa kuratibu masuala ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje. Kwa sadfa tu, John na Nyamo-Hanga walisoma darasa moja wakati wakiwa wanasoma sekondari.
TANESCO ni shirika kubwa zaidi hapa Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa zilizo mtandaoni, kwa sasa lina zaidi ya wafanyakazi 10,300 nchini kote na thamani yake – kama mtu angetaka kulinunua leo, inakaribia shilingi trilioni nne za Tanzania.
Hata hivyo, Tanzania inapita katika wakati mgumu wa mgawo wa umeme ambapo yako maeneo yanayokosa umeme kwa walau saa 12 kila baada ya siku moja. Kilio kimekuwa kikubwa kutoka kwa wananchi na hasa wajasiriamali.
Na kama alivyosema Rais Samia, tatizo la ukosefu wa umeme hapa nchini si tatizo la mtu au wizara moja. Ni tatizo la serikali nzima na mfumo wote wa usambazaji umeme.
Walichofanya January na Maharage
Kuna nyakati, katika miezi ya karibuni, tatizo la kukatika kwa umeme lilihusishwa moja kwa moja na aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba. Baada yake, lawama pia zilikuwa zikielekezwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Maharage Chande.
Lawama kwa wawili hao ni jambo ambalo naweza kulielewa kutokana na aina ya majukumu waliyokuwa nayo. Hata hivyo, ilikuwa wazi pia kwa baadhi ya watu, lawama hizo zilikuwa binafsi na zinazoacha kusema au kuweka pembeni mazuri yaliyokuwa yakiendelea.
Labda nitatoa mifano. Wakati January akipewa wadhifa huo miaka takribani miaka miwili iliypita, TANESCO ilikuwa katika hali mbaya kifedha, ikiwa na madeni ya mabilioni ya shilingi. Huko nyuma, tangu enzi Zitto Kabwe akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Bunge liliwahi kupendekeza kuwa madeni hayo yafutwe na yatumike kama mtaji kwa serikali.
Kwa ushawishi wa January, na tayari akiwa amemshawishi Maharage akubali kurejea nchini kuongoza TANESCO, deni hilo hatimaye lilifutwa. Miezi miwili iliyopita, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, TANESCO ikatangaza kutengeneza faida ya zaidi ya shilingi bilioni 109.
Baadhi ya wateja wa TANESCO ni mashahidi kuwa huduma kwa wateja wa shirika hilo zimeimarika sana kwenye miaka ya karibuni na sina shaka kabisa kwamba miezi sita ijayo, mgawo huu wa sasa huenda ungekuwa umepungua au kuisha kabisa kama agizo la Rais Samia kwa Gissima lilivyotolewa wiki hii.
Kwa vyovyote vile, ukweli ni kwamba January na Maharage wasingeweza kumaliza shida ya umeme ndani ya miaka hii miwili. Mbinu zilizotumika enzi za utawala wa Rais John Magufuli kupunguza makali ya mgawo si aina ya mbinu ambazo wawili hao wangependa kuzitumia.
Chukulia suala la kuzima umeme kwa kampuni kubwa ili umeme ubaki kwa wananchi. Magufuli aliweza kufanya hivyo, lakini akina January na Maharage; wanaofahamu umuhimu wa umeme kwa sekta binafsi na kwa uchumi wetu na hasa katika hali hii ya sasa ya mdororo wa uchumi, wasingeweza kufanya hivyo.
Au kuacha mitambo ifanye kazi mfululizo bila kupumzishwa na kufanyiwa matengenezo madogo madogo. Wakati wa Magufuli iliwezekana, lakini kwa akina January na Maharage hilo si jambo la kitaalamu. Wasingeweza kufanya.
Kwao, namna njema ya kurudi katika hali njema ilikuwa ni kufuata maoni ya wataalamu, kutonyima umeme kundi moja kwa faida ya kundi jingine na pia kutangaza kuwa kuna mgawo – hadharani na mara kwa mara, wakati katika nyakati nyingine isingeruhusiwa kutoa matangazo ya aina hiyo.
Uongozi ni kuamua. Viongozi pia hawafanani. Kwa tabia, kwa makuzi, kwa elimu na kwa upeo wa uelewa. Uamuzi aliochukua Magufuli wakati wake, ulitoa picha ya kwamba ameondoa shida ya umeme. Uamuzi wa akina January – chini ya utawala wa Rais Samia, ulikuwa wa njia na namna nyingine. Kama wawili hawa wangekuwa enzi za utawala wa Jakaya Kikwete, Ali Hassan Mwinyi au Benjamin Mkapa, pengine wangekuwa wanaeleweka na umahiri wao ungeonekana.
Tatizo lao ni kuingia TANESCO mara tu baada ya uongozi wa mtu ambaye alibadili namna ya utendaji uliozoeleka wa taasisi hiyo. Na katika dunia ya sasa ambapo jambo dogo linafanywa kuwa kubwa mara mara elfu moja, huu si wakati rahisi sana.
Lakini, muda, ninatumai hivyo, utakuja kutuambia kile kizuri tulichopata kwenye miaka hii mwili ya January na Maharage. Lawama zote zilizokuwa juu yao zilikuwa ni lawama za nyakati. Haw a ni wahanga wa muda.
Boniface, Felichesmi na Peter
Bosi mpya wa TANESCO si mgeni wa maisha ya minyukano na mitafutano serikalini. Enzi za utawala wa Magufuli, alikuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA). Hakuna wakati ambapo REA ilipaa kimafanikio kuliko wakati wake.
Hata hivyo, alitolewa na kuwekwa benchi kwa kuhamishiwa TEMESA. Kwa nini Nyamo -Hanga alitolewa? Ni stori ambayo pengine naweza kuiweka hapa kwa mara ya kwanza.
Wakati ule nikiwa Mhariri wa Gazeti la kila wiki la Raia Mwema, tuliambiwa kuhusu mradi mmoja mkubwa ambapo zabuni ilitangazwa na REA. Wakala akampa mshindi mtu aliyekuwa na bei nzuri kwa serikali. Lakini aliyekuwa mshindi wa pili alikuwa na marafiki katika ngazi za juu za serikali. Akalazimisha sana apewe tenda yeye. Nyamo – Hanga akaweka mguu chini.
Jamaa akakata rufaa. Presha ikaongezwa kwa Nyamo – Hanga. Majibu ya rufaa yalipotoka, ikaonekana mshindi wa kwanza alikuwa na vigezo vyote. Na Nyamo – Hanga akaambiwa msimamo wake utamgharimu. Yeye akasema hawezi kutoa zabuni kwa asiye na sifa.
Matokeo yake ndiyo akajikuta yuko benchi TAMISEMI ingawa ni miongoni mwa Watanzania wenye uwezo na maarifa makubwa ya kikazi. Ni Mhandisi lakini amesomea masuala ya kifedha katika Chuo Kikuu cha Strathclyde nchini Scotland. Ni ‘mtu na nusu’ kama lilivyo umbo lake.
Gissima alikuwa mhanga wa msimamo wake wa kutaka kuona taratibu zinafuatwa. Hakuogopa kwamba kwa kufanya vile, anaweza kuwa anahatarisha riziki na pengine mustakabali wake mzima wa maisha.
Ni sawa na ilivyokuwa kwa Mramba. Huyu – kwa maoni ya watu wengi niliowahi kuzungumza nao, pengine ndiye mtu anayeifahamu TANESCO pengine kuliko wengine wote waliopo serikalini hivi sasa.
Yeye aliajiriwa TANESCO mara tu alipotoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1996. Alipanda vyeo taratibu kuanzia ngazi ya chini hadi kufikia kuwa Mkurugenzi Mkuu baadaye. Mramba anajulikana pia kwa kuwa mtu anayefuata maadili ya dini yake ya Kikristo.
Miaka michache iliyopita, kuna wakubwa wakataka kupindisha mambo TANESCO. Mramba akaweka mguu chini. Weledi wake, maadili yake na uelewa wake vikamkataza kufanya yasiyotakiwa. ‘Akatumbuliwa’.
Wala hakujali. Akapewa ‘kijiwe’ kule Chuo cha TANESCO ikisubiriwa muda wake wa kustaafu. Ilipoonekana mambo yanaanza kuharibika. Akarejeshwa na sasa yuko alipo. Huyu, alikuwa mhanga wa weledi na maadili yake.
Peter Ulanga ni hadithi nyingine ya Tanzania na wataalamu wake. Huyu ana wasifu wa kipekee. Ni yeye, miaka 20 iliyopita, ndiye aliyeandika andisho lililosababisha Watanzania tuanze kununua salio na kukwangua vocha kwa kutumia pesa za ‘madafu’. Kabla ya hapo, tulikuwa tunachajiwa kwa dola za Marekani. Kwa watu wa umri wangu, watakumbuka hizi vocha tukiziita dola miaka ile ya mwanzoni mwa 2000.
Ni Mhandisi Peter huyuhuyu ndiye aliyekuwa sehemu ya wataalamu wa kimataifa waliokuja na ubunifu wa chaja za simu ambazo sasa zinajulikana kwa jina la type c.
Ubunifu wake ndiyo umefanya leo watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro wafaidi huduma ya mtandao wa internet na sasa Tanzania ndiyo nchi ambayo mtu anaweza kupata internet akiwa mahali parefu zaidi kwenda juu.
Lakini juzi, Rais Samia akaeleza masikitiko yake kwamba kuna watu hawakumpa taarifa za kutosha wakati akitangaza uamuzi wa kumtoa TTCL. Binafsi, nilipokea simu mbili za wafanyakazi wa shirika hilo waliokuwa wakisikitika kwamba; “mbona mmetuondolea mtu wa maana aliyekuwa analifufua shirika?”.
Na hii haikuwa mara ya kwanza – na labda haitakuwa ya mwisho kwake, na kwa watu wa aina yake, kutafutiwa sababu ya kuwekwa ‘kijiweni’ kwa sababu za hila, fitna na ghilba. Lakini angalau Rais aliona tatizo na amelirekebisha.
Usiku wa juzi nilipata usingizi wa amani. Pamoja na changamoto zote ambazo inapitia hivi sasa, walau ninajua kwamba mashirika yetu makubwa mawili; TANESCO na TTCL yako kwenye mikono salama.
Ninafahamu kwamba Balozi John Ulanga na Balozi Saidi Othman Yakubu watafanya zaidi ya kile ambacho Rais Samia amepanga wakifanye. Nawajua wawili hawa vizuri kabisa.
Na January Makamba, kwa uhakika kabisa, atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa mfano. Hili, sina shaka nalo.
Mwandishi wa makala haya ni Msomi wa Masuala ya Siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS). Amewahi kuwa Mhariri wa magazeti kadhaa ya Tanzania. Anapatikana kupitia email: ekamwaga57@gmail.com.