Tatizo la Dk. Slaa

Picha: Dk. Wilbrod Slaa. Kwa hisani ya The Citizen

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

MWAKA 2015, akiwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika sana nchini Tanzania, Dk. Wilbrod Slaa, alitangaza kupingana na hatua ya chama chake kumkaribisha Edward Lowassa kwenye chama hicho na kumfanya kuwa mgombea urais kwenye uchaguzi wa mwaka huo.

 

Katika hotuba ambayo baadaye ilikuja kujulikana kwa jina la “Asset au Liability”, Dk. Slaa alihoji kama ujio huo wa Lowassa ni faida au hasara kwa chama hicho na kwamba kwa kuzingatia rekodi ya nyuma ya Waziri Mkuu huyo wa zamani, isingekuwa vema kwa Chadema kumpa nafasi ya kuwania urais.

 

Huo, hatimaye, ndiyo ulikuwa mgogoro uliofanya Slaa aondoke Chadema na kuamua kwenda kuishi uhamishoni nchini Canada kabla ya baadaye kutumikia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama Balozi nchini Sweden enzi za utawala wa Rais John Magufuli.

 

Hata hivyo, ingawa hotuba ile ya Slaa ilikuwa na maelezo yanayoweza kuingia akilini, kulikuwa na jambo moja lililoshangaza viongozi na rafiki zake wa karibu; kwamba yeye binafsi alikuwa mmoja wa watu wachache walioshiriki katika mpango wa kumtongoza Lowassa aondoke CCM na kuingia Chadema. Marafiki zake walisema Slaa hakuwa na tatizo kwa Lowassa kuingia Chadema. Kwamba mbunge huyo za zamani wa Karatu alijua kuhusu mbunge huyo wa zamani wa Monduli kuingia kwenye chama chao mapema kuliko wengi wa Watanzania – hasa wanasiasa wa Chadema, kwa muktadha wa makala haya.

 

Kulitengenezwa hitimisho moja kuhusu tabia hiyo ya kushangaza ya Slaa – kuwa alijua mgombea urais wa Chadema atakuwa yeye. Kwenye mawazo ya Slaa, ilikuwa kwamba yeye ndiye aliyetakiwa kuwa mgombea urais wa Chadema; kama ilivyokuwa mwaka 2010 aliposhindana na Jakaya Kikwete wa CCM.

 

Wakati wote wakati Lowassa anatongozwa aende Chadema, kichwani kwa Slaa ilikuwa kwamba mgeni huyo ataleta pesa, ushawishi na wagombea wa ngazi za ubunge na udiwani wa kutosha na kumpa yeye nafasi kubwa zaidi ya kushindana na Magufuli ambaye ikijulikana tayari ndiye atakuwa mgombea wa CCM.

 

Hivyo, alichokataa – kwa mujibu wa tafsiri ya rafiki na waliokuwa viongozi wa Chadema waliozungumza na vyombo vya habari wakati ule, tatizo la Slaa halikuwa tabia na mwenendo wa Lowassa kwa miaka mingi ya nyuma kama ambavyo hotuba yake ya “Asset au Liability” ilivyotaka kuonyesha.  Wala Slaa hakuwa na tatizo kwa Lowassa kuhamia Chadema. Tatizo kubwa la Slaa lilikuwa kwamba Lowassa alikuwa ameingia Chadema kula ‘kitumbua’ chake. Kwa maneno mengine, ujio wa Lowassa ulikuwa sawa na kutia mchanga kitumbua binafsi cha Slaa.

 

Nafikiri udhaifu mkubwa kuliko yote wa Dk. Wilbrod Slaa ni ule wa kuona kwamba maslahi yake binafsi yana maana kubwa kuliko maslahi ya taasisi yake, imani yake, rafiki zake na wakati mwingine nchi yake. Slaa, kwa maneno mengine, hana urafiki na mtu au taasisi. Yeye huwa ana maslahi yake binafsi na ni maslahi hayo ndiyo atayasimamia kwa gharama yoyote.

Chukulia mfano wa Lowassa. Bila Slaa na mtikisiko na fadhaa yoyote waliyopata washabiki wake na wapiga kura kwa ujumla, Lowassa alipata takribani asilimia 40 ya kura na Chadema ilipata kura nyingi na kushinda viti vingi vya ubunge kuliko katika wakati mwingine wowote kwenye historia ya uchaguzi wa vyama vingi tangu virejeshwe mwaka 1992.

 

Kama Slaa asingekimbia Chadema kwa sababu ya hasira ya kunyimwa kugombea urais, na Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF) asingetupa taulo ulingoni kuelekea uchaguzi huo – kiasi kwamba ule muungano wa Ukawa ukafanya kazi ukiwa na vinara wao wote, nina imani kura za upinzani zingevuka asilimia 40. Pamoja na kutovuka asilimia 40, namba zinatuonyesha kwamba ujio wa Lowasa ulikuwa ni faida kwa Chadema na si hasara kama ambavyo Slaa angetaka kuaminisha umma wa Watanzania. Kama kuna mtu alipata hasara kwa nafsi na matamanio yake kutokana na ujio huo wa Lowassa, mtu huyo alikuwa ni Slaa na familia yake.

 

Kama tulivyo sisi wengine sote, Slaa ni mwanadamu na si malaika. Anafanya makosa kama sisi wengine sote na namna tunavyomhukumu inatakiwa ahukumiwe kama mwanadamu pia. Pmaoja na hayo, kuna mlolongo wa tabia za kutojali taasisi na badala yake kujitazama binafsi katika maisha ya mwanasiasa huyo wa aina yake kwenye siasa zetu.

 

Kabla ya kuingia kwenye siasa, Dk. Slaa alikuwa Kasisi wa Kanisa Katoliki. Kwenye miaka ya 1990 alikuwa miongoni mwa nyota vijana wa Kanisa hilo kiasi cha kufikia kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Baraza la Maaskofu wa Tanzania (TEC). Wengi walitaraji kumwona kwenye ngazi za juu zaidi za utumishi ndani ya Kanisa hilo.

 

Lakini Slaa aliacha kiapo chake cha ukasisi na kuamua kuwa muumini wa kawaida. Katika historia ya Kanisa Katoliki la Tanzania, mapadri wawili; Slaa na rafiki yangu hayati Privatus Karugendo, ndiyo mapadri wawili ambao kuondoka kwao kwenye utumishi kunajulikana na wengi kuliko wengi wengine waliofanya hivyo.

 

Baada ya kuachana na Upadri na kuingia uraiani, Slaa alifunga ndoa na Rosemary Kamili – aliyekuja kuwa mmoja wa wanasiasa machachari wanawake nchini Tanzania. Kwa mujibu wa desturi za Kikatoliki, ndoa ni kiapo ambacho walichoingia wanatakiwa kuishi pamoja – kwenye shida na raha, mpaka pale kifo kitakapowatenganisha.

 

Lakini, kama ilivyokuwa kwa kiapo cha upadri, Slaa alikipiga teke kiapo hicho – na inajulikana kuwa alikuja kufunga ndoa na Josephine Mushumbusi ambaye ndiye alikuwa mkewe kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Sijawahi kuingia undani kujua ni nini kilisababisha aache upadri na aachane na mkewe wa ndoa – maana hayo ni masuala yake binafsi, lakini hitimisho langu ni kuwa ilifikia kipindi ambacho viapo vyake na taasisi ya Kanisa na ile Ndoa havikuendana na matamanio yake binafsi na huo ndiyo ukawa mwisho wa viapo hivyo.

 

Alipoamua kuingia kwenye siasa, Slaa alijiunga na CCM na akaaminika na wafuasi wa chama hicho tawala kiasi cha kufikiria kuwania ubunge wa Jimbo la Karatu kupitia chama hicho. CCM Karatu walimfanyia figisu na akapitishwa mtu mwingine kuwania ubunge badala yake. Slaa, kama ilivyo utaratibu wake, akaondoka CCM na kujiunga Chadema na ‘kamari’ yake aliyocheza wakati huo ikalipa kwani alishinda ubunge.

 

Hivyo Chadema ndiyo iliyomsitiri baada ya CCM kujaribu kuzima ndoto yake. Siyo tu kwamba Chadema ilimpa fursa ya ubunge na jukwaa la kufanya aina ya siasa alizozipenda, lakini ilimpa nafasi ya kuwa Katibu Mkuu wake na kumfanya kuwa mmoja wa wanasiasa maarufu na wenye ushawishi zaidi nchini Tanzania.

 

Mwaka 2010 wakati Chadema ikimtaka aache ubunge wake na kuwa mgombea urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka huo, Slaa aliweka masharti kwamba ili awanie nafasi hiyo, chama hicho kinatakiwa kiahidi kumlipa mshahara sawa na ule aliokuwa anaupata wakati akiwa mbunge – endapo atakosa Urais.

 

Hilo halikuwa ombi la kawaida kufanywa na kiongozi wa upinzani katika historia ya Tanzania ya vyama vingi. Augustine Mrema hakuwahi kutoa sharti hilo kwa NCCR Mageuzi wakati alipojiunga nacho akitoka kuwa mbunge na waziri kwenye Serikali ya CCM. Kama Mrema angetaka mshahara, angerudi kwao Kiraracha na kuwania ubunge wa Moshi Vijijini ambako bila angeshinda na kubaki na mshahara wake.

 

Lakini Mrema hakutaka mshahara wala marupurupu ya ubunge wakati alipoamua kwenda NCCR. Alitaka Urais wa Tanzania na pengine sharti pekee alilowapa NCCR lilikuwa ni kumruhusu awe mgombea urais wa chama hicho. Lakini Slaa, katika namna ambayo ni Slaa pekee ndiye huifahamu, alikubali kuwania urais na pia kulipwa mshahara kama mbunge kwa miaka walau mitano inayofuata baada ya uchaguzi wa 2010. Akili kubwa, nikitumia maneno ya mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Peter Msigwa.

 

Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF alipewa nafasi ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 akiwa mmoja wa wachumi mashuhuri si Tanzania pekee bali katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Umahiri wake katika uchumi ulivuka mipaka kiasi cha kuwahi kutumiwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kama mshauri wake wa uchumi. Nimewahi kuzungumza na Lipumba na akanieleza gharama za kijamii alizolipa kufuatia kukubali kwake kuwa mgombea urais wa CUF wakati ule; kuanzia kuanza kunyimwa kazi za kitaalamu na taasisi zilizo ndani na nje ya Tanzania kwa kuhofia kukorofishana na serikali ya CCM na kuanza kukimbiwa na baadhi ya marafiki zake. Profesa Lipumba aliomba nini kwa kupewa nafasi ya kugombea urais na CUF mwaka 1995, 2000 na 2005? Hakuomba chochote. Zero. Sifuri. Zilch.

 

Lakini Slaa alichukua nafasi ya kuwania urais kwa mikono miwili na mshahara kama mbunge juu. Kama nataka kutumia maneno ya mwana masumbwi Karim Mandonga ningesema kwenye uchaguzi wa 2010, Slaa angeshinda urais angekuwa ameshinda na angekosa urais angekuwa ameshinda pia. Kipato chake kingebaki kuwa kilekile pasipo ‘vurugu’ za kuwa na jimbo na wapiga kura.

 

Pamoja na Chadema kukubali maombi yake na kuendelea kumlea kama Prince wa chama hicho, Slaa hakusita kukihama chama hicho na baadaye kutimkia kwenye kuhudumia serikali ya CCM mara baada ya kukataa kumpa heshima ya kuwania tena urais – na bila shaka kumhakikishia mshahara wa kibunge endapo angeshindwa tena kwenye uchaguzi huo. Sina hakika kama Lowassa naye aliwapa Chadema masharti ya kumlipa mshahara wa ubunge au wa aina yoyote endapo asingeshinda kwenye uchaguzi wa urais.

 

Kitendo cha Rais Magufuli kumsitiri Slaa kilizingatia kwamba wakati huo mwanasiasa huyo – pengine kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya utu uzima, hakuwa tena na kipato rasmi cha kuendesha maisha yake. Uteuzi wa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden ulimpa riziki, ushawishi na heshima aliyoanza kuikosa tangu aondoke Chadema.

 

Kwenye utawala wa Magufuli, Slaa hakuwa yule aliyezoeleka wa kukemea na kufichua maovu. Hakuwa Slaa yule aliyezungumza pasi na kuogopa mamlaka. Hakuwa Slaa aliyejulikana kwa kuzungumza kwa kuchanganya ushahidi na hoja zenye mashiko. Akawa mtetezi wa dola iliyokuwa ikihangaisha na wakati mwingine kudhuru wale aliokuwa nao pamoja kwenye mapambano ya kudai Tanzania iliyo bora zaidi.

 

Hivi sasa, Slaa si balozi tena. Rais Samia Suluhu Hassan hakumuongezea muda wake wa ubalozi ikizingatiwa kwamba hivi sasa umri wa Slaa umezidi umri wa kawaida wa watumishi wa umma. Uamuzi huo pengine ulizingatia zaidi maslahi ya umma kuliko maslahi ya Slaa na wale wanaofaidika na hali yake ya kipato. Kwa mara nyingine hivi sasa, Slaa yuko katika hali ambayo hana tena kipato cha uhakika wala hadhi ya kisiasa ya kuheshimiwa. Kitendo cha kukosa kipato na cheo cha kumfanya awe na hadhi fulani kwenye jamii ni kitendo ambacho hakikubaliki katika saikolojia ya Slaa kama ambavyo tumeona katika historia yake ya miaka 30 iliyopita.

 

Hili ndilo tatizo la Slaa. Hana urafiki wala maslahi ya pamoja na watu au taasisi. Kama jambo lina maslahi yake binafsi, atalipigania kwa kichwa na kucha – na kama halina, hilo litakuwa tatizo la watu wengine. Bila shaka, tutasikia mengi kutoka kwake katika nyakati hizi.