Uchaguzi Uturuki: Mafunzo kwa vyama vya upinzani

Maelezo ya picha:

Mgombea wa upinzani katika uchaguzi wa Uturuki, Kemal Kılıçdaroğlu (kushoto), akitembea kwenye mitaa ya Ankara Mei 19 mwaka huu. 

 

Na Murat Sommer na Jennifer McCoy

 

Uchaguzi wa Rais na Wabunge nchini Uturuki uliofanyika Mei 14 mwaka huu ulikuwa mkali huku ukiweka rekodi ya watu kujitokeza kwa wingi kupiga kura. Asilimia 88.9 ya waliojiandikisha walijitokeza kupiga kura; ikimaanisha watu tisa katika kila watu 10 walioandikishwa, walipiga kura.

 

Katika siku za mwisho kuelekea uchaguzi huo, kura za maoni zilikuwa zikimpa ushindi mgombea wa upinzani, Kemal Kılıçdaroğlu, aliyeshindana na Rais wa sasa wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan. Rais huyo aliyeitawala Uturuki kwa miongo miwili alikuwa na wakati mgumu kwenye uchaguzi huu kuliko wakati mwingine wowote kwenye utawala wake.

 

Hata hivyo, matokeo yalipotangazwa, Erdoğan aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 49.5, akikosa asilimia 0.5 tu kutangazwa mshindi wa moja kwa moja kwenye uchaguzi huo. Katiba ya Uturuki inataka mshindi apate walau asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa na kwa matokeo hayo, itabidi uchaguzi huo urudiwe Mei 28 mwaka huu.

 

Katika uchaguzi huo, Kılıçdaroğlu alipata asilimia 44.9 ya kura zote zilizopigwa. Mgombea mwingine kutoka chama chenye mrengo mkali, Sinan Oğan, alipata asilimia 5.2 ya kura zote zilizopigwa. Kwa sasa, chama tawala cha Justice and Development Party (AKP) kimeendelea kuwa na viti vingi bungeni.

 

Matokeo ya uchaguzi huu yamewashangaza na kuwavunja nguvu wengi waliodhani huu ndiyo ungekuwa mwisho wa utawala wa Erdoğan. Kuna mafunzo yapi ambayo vyama vya upinzani duniani kote vinaweza kujifunza kupitia uchaguzi huu wa Uturuki? Kuna mambo saba ambayo yana mafunzo makubwa kutoka uchaguzi wa Uturuki.

 

Kuungana Vyama vya Upinzani

 

Vyama vya upinzani vya Uturuki vilifahamu kwamba haviwezi kushindana na chama tawala chenye kiongozi anayetumia madaraka yake kuwagawa, kuwadhalilisha na kusambaza uongo dhidi yao. Kwa hiyo waliunganisha nguvu.

 

Waliungana kwa kutengeneza muungano wa aina mbili. Miungano hiyo hatimaye ilimpendekeza Kılıçdaroğlu kuwa mgombea wake dhidi ya Rais aliye madarakani. Katika uchaguzi wa Mei 28, inaonekana kuwa mgombea atayeungwa mkono na Oğan ndiye atashinda.

 

Hata hivyo, bado upinzani haukuweza kuungana kwa ujumla wao kwani vilikuwemo vingine vidogo ambavyo viliwekwa pembeni na mwishoni Erdoğan’s akavisogeza kwake. Kilicho wazi ni kuwa kama kusingekuwa na muungano wa wapinzani walioungana, chama tawala kingeibuka na ushindi mkubwa na kusingekuwa na sababu ya uchaguzi wa marudio.

 

Kupunguza makali ya mashambulizi

 

Silaha kubwa ya watawala wenye mrengo wa kidikteta kama Erdoğan ni kufanya siasa zenye kuleta mgawanyiko kwa kuwapa wapinzani wake majina mabaya na kuwapa wananchi sababu ya kutowaamini.

 

Ili kujilinda dhidi ya mashambulizi hayo, vyama vya upinzani vilitengeneza aina ya muungano ambao ilikuwa vigumu kuwapa jina moja – liwe la vibaraka, mafisadi, watetea ushoga au wasio wazalendo. Karibu kila kundi liliingia ndani ya umoja huo na ikawa vigumu kwa chama tawala kutumia hoja moja kuviharibia vyote.

 

Mbinu hii ilifanikiwa sana kiasi kwamba ilibidi Rais Erdogan na timu yake ya kampeni ianze kutumia mbinu zisizo za kawaida – ikiwamo teknolojia za mtandao za kutengeneza taarifa feki alizosaidiwa na maswahiba wake wa kisiasa kutoka Russia.

 

Jambo la kuvutia ni kwamba vyama vya upinzani vilijizuia kujibu mapigo kwa kufanya alivyofanya mshindani wao. Badala yake vilitumia muda mrefu zaidi kushawishi wapiga kura kwa kutumia ujumbe uliokuwa unajenga umoja wa kitaifa.

 

Kuwa na ajenda inayoeleweka

 

Kwa kawaida, vyama vya upinzani kwenye nchi zinazoongozwa na mtawala wa aina ya Erdogan hutafuta mwanasiasa mwingine mwenye sifa na tabia zinazofanana naye ili washindanishwe.

 

Washindani wa Erdogan walikuja kitofauti. Wao walitengeneza mpango kazi wa makubaliano wenye kurasa 244 ulioeleza nini wanataka kuifanyia Uturuki na Waturuki endapo watafanikiwa kuingia madarakani. Hoja yao haikuwa kumwondoa tu madarakani mtawala wa sasa.

 

Matokeo ya uamuzi huo wa wapinzani ni kwamba kwa mara ya kwanza kampeni za uchaguzi wa mwaka huu zilitawaliwa zaidi na hoja kuhusu mustakabali wa taifa hilo badala ya kutaka tu kubadilisha chama kilicho madarakani.

 

Kukubaliana kutokubaliana

 

Tofauti na miaka ya nyuma, vyama vya upinzani vya Uturuki safari hii vilionyesha uvumilivu mkubwa miongoni mwao kwa wakati mwingine kuwa pamoja hata kulipotokea kutokubaliana miongoni mwao kwenye masuala fulani.

 

Kwa mfano, kulitokea mgogoro ambao ulisababisha wakati kujiondoa kwenye muungano huo kwa kiongozi wa Good Party, Meral Akşener, ambaye hata hivyo alirejea tena siku mbili baadaye. Hii ilionyesha ukomavu mkubwa na picha kwamba viongozi hao wanaweza kufanya kazi pamoja hata wakiwa madarakani.

 

Mbinu mpya kupambana na mtawala wa kiimla

 

Wapinzani walitumia ubunifu na ucheshi wa kipekee kwenye matangazo yao ya kampeni dhidi ya chama tawala. Kwa mfano, wakifahamu mtindo wa Erdoğan’s wa majidai na kutumia majengo makubwa ya Ikulu, wao walifanya tofauti.

 

Kupitia mitandao ya kijamii, wapinzani kupitia mgombea wao walianza kutengeneza video fupi za jioni wakati akiwa anaandaa chakula au kuzungumza na familia yake kama walivyo Waturuki wengi.

 

Matendo na maneno kufanana

 

Wakiwa wanaomba kura kwa wananchi, watawala wenye tabia za kiimla huwa wanaahidi wananchi wao mambo makubwa watakayofanya kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili endapo watawachagua.

 

Lakini wakiingia madarakani, kazi yao kubwa huwa ni kunyima uhuru wa watu kujieleza na kupambana na wale wote wanaojitambulisha kama wapinzani wao. Kwenye kampeni za vyama vya upinzani Uturuki, walikuwa wakiahidi kwamba wakiingia madarakani watafanya wanayoahidi.

 

Kutawala kwa umoja

 

Muungano wa upinzani nchini Uturuki pia ulifanya jambo moja lisilo la kawaida kwa kutangaza timu ya uongozi itayotawala kwa pamoja. Katika uongozi huo wa pamoja, viongozi kutoka vyama vilivyoungana walikuwa wakitangazwa kama Makamu wa Rais kutoka katika maeneo ambayo wana nguvu kubwa ya ushawishi.

 

Hii ilijenga picha ya upinzani ulioungana lakini pia unaoamini kuwa uongozi ni kugawana madaraka badala ya kuwa na mtu mmoja anayeonekana ana madaraka makubwa kuzidi wenzake. Hili lilisaidia kwenye kuongeza wingi wa kura kwani wapiga kura waliwaona watu wao kama sehemu ya uongozi.

 

Pamoja na mambo yote hayo, bado vyama vya upinzani havikupata ushindi kama ilivyotarajiwa. Ukweli unaojulikana ni kuwa si kazi rahisi sana kumwondoa madarakani Rais wa mrengo wa kidikteta kama Erdoğan.

 

Jambo pekee ambalo vyama vya upinzani kutoka kwingineko duniani vinaweza kufanya ni kuchukua baadhi ya mbinu zilizotumiwa na wenzao wa Uturuki. Haikuwezekana Uturuki lakini inaweza kuwezekana kwingine.

 

Murat Sommer ni Profesa wa Sayansi ya Siasa anayesomesha katika Chuo Kikuu cha Koç, IstanbulJennifer McCoy ni Profesa wa Sayansi ya Siasa anayesomesha katika Chuo Kikuu cha Georgia nchini Marekani. Makala haya yalichapwa kwa mara ya kwanza kwenye jarida la Journal of Democracy toleo la Mei mwaka huu. Inaweza kusomwa kupitia. Hii ni tafsiri isiyo rasmi ya lugha ya Kiswahili. Inaweza kusomwa kupitia https://www.journalofdemocracy.org/seven-lessons-from-turkeys-effort-to-beat-a-populist-autocrat/