Watu 13 wamekufa na hakuna kitu?

Picha kwa hisani ya blogu ya Full Shangwe

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

MEI 23 mwaka huu, watu 13 walipoteza maisha baada ya kuungua na mvuke wa moto uliotokea katika kiwanda cha sukari cha Mtibwa kilichopo mkoani Morogoro.

 

Mara baada ya ajali kutokea, tuliambiwa kwamba ripoti ya awali kuhusu nini hasa kilitokea ingetolewa kwa umma wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.

 

Imepita zaidi ya wiki moja sasa na hakuna ripoti ya uchunguzi wa tukio hilo – walau ya awali,  ambayo imetolewa. Na kama hisia zangu za kiuandishi zinanielekeza vizuri, hakuna hamu kwa wahusika kuzungumza chochote kutokana na ajali hiyo.

 

Hii si sawa.  Watu 13 wamepoteza uhai wao katika tukio hilo – wakiwemo raia wa kigeni, na jambo hili haliwezi kuwekwa chini ya kapeti na maisha yakaendelea kama kawaida.

 

Tunasema hivi kwa sababu wapo waandishi wa habari ambao wamejaribu kupata taarifa kuhusu jambo hili kwa vyanzo vyote ambavyo vingeweza kuzungumza na wamekutana na ukuta mzito.

 

Kuna msemo wa Kiswahili kuwa ajali haina kinga lakini kibinadamu na kwa maendeleo ya kisayansi yaliyopo, kuna namna ambayo ajali inaweza kukingwa kwa kiasi kikubwa. Lakini kwa ajali ambayo haikuwa na namna ya kuizuia, ni muhimu watu wakajua kilichotokea ili wajifunze kupitia tukio hilo.

 

Ndiyo sababu inasikitisha kwamba wahusika wa kiwanda cha Mtibwa na mamlaka za serikali zimeamua kukaa kimya bila kutoa taarifa yoyote – walau ya awali, kuhusu nini hasa kilitokea kama walivyoahidi mbele ya kamera.

 

Hakuna kitu kibaya katika jamii yoyote duniani kama tabia ya kuonyesha kutojali uhai wa watu. Katika nchi zinazothamini uhai – zinazoamini kuwa binadamu si kuku, ng’ombe au mbuzi, maisha ya binadamu 13 hayawezi kuchukuliwa kirahisi namna hii.

 

Tunachotaka katika Gazeti la Dunia ni kutolewa kwa taarifa walau ya awali kuhusu suala hilo na kufahamu kama kuna aina yoyote ya uwajibikaji inatakiwa kuchukuliwa. Kama ni jambo la kiufundi na linaloweza kuzuiwa kwenye viwanda vingine lisitokee tena, ni muhimu pia umma ukaelezwa.

 

Lakini hatuwezi kuwa na tukio ambalo watu 13 wamekufa na maisha yakaachwa yaendelee kama kawaida. Waliokufa ni wanadamu. Maisha yao yana thamani kama sisi tulio hai leo. Kama leo hatutawasemea 13 waliokufa, hatutakuwa na haki ya kuwazungumzia 100 au 3,000 watakaopoteza maisha yao kwenye mazingira kama ya Mtibwa.

 

Tunataka majibu ya nini hasa kilitokea kiwandani Mtibwa.