Na Ezekiel Kamwaga
KIFO cha Jecha Salim Jecha kilichotokea jijini Dar es Salaam jana, kimemuondoa duniani mtu ambaye – kwa miaka mingi inayokuja, jina lake litanasabishwa na Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015 ambao – kinyume na matarajio ya wengi na sheria za uchaguzi za visiwa hivyo, matokeo yake yalifutwa.
Jecha ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wakati wa uchaguzi huo na yeye ndiye aliyetangaza kufutwa kwa matokeo hayo akitoa sababu za kuwepo kwa kasoro mbalimbali – hasa kisiwani Pemba, ilikokuwa ngome ya chama kikuu cha upinzani Zanzibar wakati huo; Chama cha Wananchi (CUF).
Kwa tangazo lake hilo, pengine kuliko mtu mwingine yeyote katika historia ya karibuni ya Zanzibar, alilaumiwa kwa kurudisha nyuma jitihada za Wazanzibari kuwa na Rais au Serikali ambayo iliingia madarakani kutokana na kura zao. Hadi sasa, jina la Jecha ni kama lakabu ya uvurugaji wa utaratibu au kukataa jambo lililo dhahiri.
Lakini ilikuwaje Jecha – mtu ambaye aliwahi kuwania nafasi za kisiasa visiwani humo, akaibuka kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi; nafasi ambayo kwa mujibu wa taratibu anatakiwa apewe mtu anayefahamika kwa kutenda haki au ambaye hawezi kuhusishwa moja kwa moja na moja ya washindani wa kisiasa katika nchi husika?
Katiba ya Zanzibar inatoa sifa kuu tatu kwa mtu anayeweza kuwa Mwenyekiti wa ZEC; awe Jaji wa Mahakamu Kuu, mwenye sifa zinazofanana na zile za Majaji au mtu anayeheshimika katika jamii ya Wazanzibari. Kwa sababu Jecha hakuwa Jaji au mwenye sifa zinazofanana na majaji, uteuzi wake ulizingatia sifa hiyo ya tatu.
Miongoni mwa Wazanzibari wote wanaoheshimika, ilikuwaje nafasi hiyo ikaangukia kwa Jecha? Ni vigumu kufahamu. Kwa bahati mbaya, Rais wa Zanzibar amepewa madaraka ya kumteua mtu huyo na hakuna namna ya kumuuliza kwa nini alimchagua mtu X na akaacha wengine. Na wala hatakiwi kutoa maelezo akishafanya uteuzi huo.
Hata hivyo, kuna uzi mmoja unaweza kutoa angalau picha ya sababu za yeye kupata nafasi hiyo. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar mwaka 2015, aliyekuwa mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, alimteua Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, kuwa mwakilishi wake kwenye kuhesabu kura zake. Kwa kawaida, wagombea huwapa nafasi hiyo watu wao wa karibu au wanaowaamini zaidi.
Kwa upande wa aliyekuwa mgombea Urais kupitia CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, yeye alimteua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Mazrui, kuwa wakala wake. Kwa wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar, wanafahamu ukaribu wa uhusiano uliokuwepo baina ya wawili hao.
Kwa sadfa, miongoni mwa wasaidizi wa karibu wa Shein – kuna mmoja aliyekuwa ikijulikana kuwa na uhusiano wa kikazi na Jecha enzi wote wakiwa wanafanya kazi katika Tume ya Haki za Binadamu ya Zanzibar na mtu huyo ni Balozi Ramia. Hakuna mwenye uhakika kama ni Ramia ndiye aliyemshawishi Shein kumpa nafasi hiyo Jecha au kuna sababu nyingine. Mtu pekee ajuaye kwa hakika ni Shein mwenyewe.
Katika mazingira ya SUK na ukweli kwamba Jecha aliwahi kuchukua fomu kutaka kuwania ubunge wa Jimbo la Kwamtipura kupitia CCM kwenye uchaguzi wa mwaka 2010, Shein ana maswali mengi ya kujibu kuhusu ni kwa vipi alimteua mtu wa aina hiyo kuwa Mwenyekiti wa ZEC mnamo Aprili, 2013. Maalim Seif, kwa kuzingatia historia hiyo ya Jecha, alipinga hadharani uteuzi huo akisema hauna nia njema. Nakumbuka vyombo vya habari vilipotaka ufafanuzi kuhusu jambo hilo, majibu ya ZEC yalikuwa “vyombo vinaweza kuandika vinavyotaka”.
Nini hasa kilitokea Oktoba 28 mwaka 2015?
Kwa vigezo vyovyote vile vya kidemokrasia, wanasiasa wa Zanzibar wa CCM na vyama vya upinzani, wanakubaliana kwamba uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa uchaguzi huru na ulioandaliwa na kuendeshwa vizuri zaidi kulinganisha na uchaguzi mwingine wowote uliowahi kufanyika visiwani humo tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992.
Uchaguzi huo ulifuatia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoundwa na vyama vya CCM na CUF kutokana na maridhiano ya kisiasa yaliyotokea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kwa mara ya kwanza, Zanzibar ilishuhudia vyama viwili hasimu vya kisiasa visiwani humo vikifanya kazi kwa pamoja na kuandaa uchaguzi huo.
Hakuna aliyetarajia kuwa Jecha, au mtu mwingine yeyote, angeweza kuvuruga uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, 2015. Kimsingi, yeye na waliokuwa wajumbe wengine wa ZEC walikuwa wakishirikiana kupokea na kutangaza matokeo ya majimbo tofauti hadi yalipofika majimbo 31. Baadhi ya wajumbe wa ZEC walianza kuona Jecha akibadilika kuanzia jioni ya Oktoba 25 wakati matokeo yalipoanza kuwasili kutoka vituoni.
Mmoja wa waliokuwa wajumbe wa ZEC wakati huo, Ayoub Bakari Hamad, ameniambia kwamba Jecha alitoweka kwenye wajibu wa kutangaza matokeo kuanzia siku ya pili, yaani Oktoba 26 na kuacha jukumu hilo kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake, Jaji Abdulhakim Muhsin Ameir. Hata hivyo, kwa mujibu wa Hamad, Jaji huyo naye alichukuliwa na watu wasiojulikana kabla ya Jecha kujitokeza mchana wa Oktoba 28, 2015, kutangaza kufutwa kwa uchaguzi huo.
Siri ambayo Jecha amekwenda nayo kaburini inahusu ni akina nani walimwambia hasa atoke alikokuwa amejificha/kufichwa, na kwenda kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo, akijua kwamba Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984 haimpi mamlaka ya kufuta uchaguzi.
Mara kadhaa nimekuwa nikijiuliza, Jecha alikuwa mtu wa namna gani kufanya alichofanya? Uamuzi aliouchukua ulisukumwa na ukada wake kwa CCM? Chuki yake kwa Maalim Seif na CUF? Au ni matokeo ya vitisho na kubanwa na watu au taasisi ambazo hatutakuja kuzifahamu kwa sababu wa kusema tayari ametangulia mbele ya haki?
Nimemuuliza swali hiyo mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Zanzibar, Juma Duni Haji. Kwa wasiofahamu, Duni na Jecha ni watu waliozaliwa na kukulia katika Kijiji cha Kibeti, Kaskazini A, Unguja. Kwa maneno yake mwenyewe, Duni ameniambia kama isingekuwa baba mzazi wa Jecha, huenda yeye angechelewa sana kwenda shule au asingepata kabisa elimu.
“Mimi baba yangu hakuwa na mpango wa kunipeleka shule. Baba yake Jecha alikuwa mwalimu maarufu wa elimu ya dini pale kijijini kwetu. Yeye alitaka kumpeleka mwanaye shuleni lakini shule ilikuwa mbali. Akaona ni afadhali atafutwe kijana mmoja wa kuwa anaenda naye shule. Kwa bahati nzuri tayari alikuwa ananifahamu na akamwomba baba yangu nianze shule na mwanaye. Hapo ndiyo nikaanza shule. Nimesoma miaka yangu yote ya elimu ya msingi kwa kwenda na kurudi shule na Jecha,” ameniambia Duni.
Ni Babu Duni aliyeniambia kwamba kwa asili, familia ya Jecha haikuwa na uhusiano wa kindakindaki na chama cha Afro Shirazi (ASP) kilichoungana na TANU cha Tanganyika kuunda CCM. Kwa kadri Duni ajuavyo, baba wa Jecha alikuwa mfuasi wa chama cha Hizbu – kilichokuwa hasimu wa ASP kwenye harakati za kudai Uhuru wa Zanzibar. Maelezo haya ya Duni yanaondoa dhana kwamba pengine mahaba ya Jecha kwa CCM ndiyo yalimpofusha.
Lakini yupo rafiki mwingine wa Jecha aliyeniomba nisimtaje jina kwa vile hataki kuonekana anamsimanga marehemu aliyenieleza kuwa kwa hakika rafikiye huyo hakuwa anampenda Maalim Seif. Yeye ndiye aliyenieleza kwamba aliwahi kumsikia Jecha akisema mahali kuwa itakuwa vigumu sana kwake kumtangaza Waziri Kiongozi huyo wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hata kama matokeo yangetaka afanye hivyo.
Nimejaribu kuuliza baadhi ya watu waliokuwa na uhusiano naye wa karibu au waliokuwa makamishina wenzake wa tume baada ya uchaguzi ule wa mwaka 2015 kama aliwahi kuonyesha majuto yoyote kutokana na yaliyotokea baada ya hatua yake ile lakini nimeambiwa hakuwahi kuonyesha hilo hadharani.
Mwisho wa Jecha
Mara baada ya uchaguzi ule wa 2015, maisha ya Jecha hayakuwa tena ya kawaida. Nyumba mbili zilizojulikana kuwa makazi yake ya Unguja zilianza kuwa chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU). Yeye mwenyewe akaanza kutembea kwa kulindwa. Kwa waandishi wa habari, Jecha hakuwa akipatikana kwa ajili ya mahojiano ya aina yoyote. Kwa kifupi, Jecha hakuwahi tena kuzungumza chochote kuhusu uchaguzi ule zaidi ya kuandaa uchaguzi wa marudio wa Machi 2016 ambao ulisusiwa na CUF.
Nilikwenda Unguja mwaka 2016 kwa ajili ya kutazama uchaguzi ule wa marudio. Sitosahau utani mmoja niliousikia wakati nikiwa eneo la Darajani la kijana mmoja aliyesema kuwa amebadili rasmi jina lake kwa vile jina la Jecha alilozaliwa nalo linampa shida kwenye jamii.
Katika tukio lililoonekana kama dhihaka kwa demokrasia na kwa vyama vya upinzani, Jecha alikuwa miongoni mwa wana CCM waliochukua fomu kutaka kupitishwa na chama hicho kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Kilikuwa ni kibao kwa Maridhiano ya kisiasa Zanzibar na hiyo ndiyo ilikuwa taswira ya mwisho ambayo Watanzania walibaki nayo kumhusu.
Ya mtu ambaye alipewa nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa ZEC kupitia dirisha la mtu anayeheshimika kwenye jamii, akavuruga uchaguzi ambao pengine ungesaidia kupunguza makovu mengi kwenye siasa za visiwa hivyo na ambao kama si busara za Maalim Seif, ungeweza kuleta maafa makubwa kwa wananchi wake.
Wakati nikifanya utafiti kuhusu Siasa za Afrika, kama sehemu ya andishi langu la Shahada ya Uzamili, nilijifunza kwamba mara zote katika siasa za bara letu, kuna “mkono wenye nguvu usioonekana” unaoendesha siasa za nchi zetu. Inawezekana Jecha alisukumwa na mkono huo kufanya alichofanya. Lakini hiyo ni siri ambayo amekwenda nayo kaburini maana hakuwahi kuitoa hadharani.
Pamoja na yote waliyopitia baada ya uchaguzi wa mwaka 2015, Duni amenieleza kuwa kama kifo cha Jecha kisingekuwa cha ghafla na mazingira yangeruhusu, yeye angefaa kununua sanda ya kumzikia rafikiye huyo wa zamani. Kama binadamu, amemsamehe kwa yote aliyoyafanya hapa duniani. Hukumu anatoa Mwenyezi Mungu na wanadamu watabaki na kumbukumbu kuhusu namna ulivyoishi na kugusa maisha yao.
Jana Jecha naye ametangulia mbele ya haki. Mtu yule mmoja ambaye uamuzi wake wa kufuta uchaguzi wa mwaka 2015 ulizima ndoto za mamilioni ya Wazanzibari na kwa tafsiri pana zaidi, wapenda demokrasia. Kama alivyopata kusema mshairi mmoja mashuhuri wa Tanzania; “Wote I walaza chali, ina ghururi dunia”.
Tumbo la dunia ni kubwa, na sote siku moja tutalala chali ndani yake.
Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha SOAS nchini Uingereza.