Profesa Mohamed Hassan Abdulaziz: Mswahili aliyetambulika kimataifa kuwa gwiji wa isimu

Picha: Shihabuddin Chiraghdin (kushoto) na Mohamed Hassan Abdulaziz (Kulia). Picha kwa Hisani ya Wanafamilia. 

 

Na Ahmed Rajab

 

PROFESA Mohamed Hassan Abdulaziz aliyefariki dunia jijini Nairobi asubuhi ya tarehe 10 Julai akiwa na umri wa miaka 91 alikuwa gwiji wa isimu, Kiswahili na Kiarabu. Zaidi ya hayo alikuwa msomi wa wasomi wenye kuhusika na mambo ya lugha na alikuwa mwalimu wa waalimu wa fani hiyo.

 

Akiheshimika duniani kote katika duru za wanaisimu. Kwa bahati mbaya si wengi waliokuwa wakimjua kwao Kenya au hata Uswahilini kote licha ya kwamba yeye, mzalia wa Mombasa, na Profesa Farouk Topan, mzalia wa Zanzibar, ndio waliokuwa waanzilishi wa usomeshaji wa Lugha na Fasihi ya Kiswahili, na kwa Kiswahili, katika Chuo Kikuu ca Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Nairobi.  Na wala hakutukuzwa na kupewa heshima anayostahiki kwao Kenya na kwengineko Afrika Mashariki.

 

Profesa Abdulaziz alibobea katika taaluma yake ya isimu (Waingereza wanaiita “linguistics”). Hii ni taaluma inayohusika na sayansi ya lugha. Ni bahari kubwa na kuiogolea ni kuogelea katika mawimbi ya maumbo, miundo, matamshi, maana na matumizi.  Kwa ufupi, taaluma  hii inachunguza na kuchambua mfumo na muundo wa lugha.

 

Isimu ina matawi yake. Kamusi Kuu la Kiswahili lililotolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) la Tanzania limeyaainisha matawi hayo ya isimu kama yafuatavyo. Kwa mfano, kuna isimujamii ambayo huchungua uhusiano uliopo baina ya lugha na jamii. Kuna isimunafsia (wengine huiita isimusaikolojia) inayochunguza uwiano uliopo baina ya lugha ya mwanadamu na michakato ya kisaikolojia inayoendana nayo. Kuna isimuamali (wengine huiita isimupragmatiki) inayohusika na uchunguzi na uchanganuzi wa lugha katika mawasiliano ili kubaini namna lugha inavyotumiwa na wasemaji wake katika mazingira halisi.

 

Hali kadhalika, kuna isimufafanuzi ambayo kazi yake ni kutoa maelezo ya ufafanuzi kuhusu vipengele mbalimbali vya lugha.  Na mwisho kuna isimumatumizi. Hii ni taaluma yenye  kujikita katika matumizi ya nadharia na mbinu mbalimbali za kiisimu katika kutatua matatizo yanayojitokeza katika ufafanuzi wa lugha hasa katika usomeshaji wa lugha za kigeni.

 

Kama wasemavyo jamaa mitaani Abdulaziz aliziramba taaluma zote hizo za isimu. Amezisoma, amezisomesha na ameziandikia makala na sura za kwenye vitabu.

 

Mohamed Hassan Abdulaziz alizaliwa Mombasa tarehe 11, Novemba mwaka 1932.  Tangu utotoni hadi ukubwani waliokuwa karibu naye wakimwita Badi Hassani.   Alikulia huko huko Mombasa ambako alisoma chuoni (madrasa) Qur’ani na mafundisho ya dini ya Kiislamu.

 

Baadhi ya wanafunzi wenzake wa chuoni, mtaani kwao Kuze, waliangukia ukubwani mwao kuwa watu mashuhuri katika fani zao. Wote walikuwa wasomi na walihusiana kwa damu.  Nao ni ndugu wawili Abdillahi Nassir Juma Bhalo (aliyepata umaarufu katika siasa akiwa mpigania uhuru wa Kenya, mchapishaji vitabu na mwanachuoni wa Kiislamu) na nduguye mshairi Ahmadi Nassir “Malenga wa Mvita”.  Hawa ni ndugu mama mmoja na mshairi na mwanaharakati Abdilatif Abdalla.

 

Wengine ambao Abdulaziz alisoma nao Qur’ani na dini ya Kiislamu walikuwa Shihabuddin Chiraghdin, aliyekuwa mwanahistoria wa Waswahili na wa lugha ya Kiswahili, na Profesa Mohamed Hyder.  Maalim wao alikuwa babu yao Sheikh Mohamed Ahmed Matano, aliyekuwa maarufu kwa jina la “Mfunzi’ na ambaye pia akiitwa Kibwana wa Bwana.

 

Kuanzia mwaka 1940 hadi 1949 alisoma masomo ya msingi na ya sekondari katika Arab Boys’ School, ambayo haikuwa skuli ya watoto wa Kiarabu peke yao.  Kuanzia 1952 hadi 1954 alisomea ualimu katika Coast Teachers Training College iliyokuwa Shanzu, Mombasa.

 

Mwaka 1958 hadi 1962 Abdulaziz alikuja London kusomea shahada yake ya kwanza katika Chuo cha SOAS, Chuo Kikuu cha London ambako alisomea masomo ya Kiarabu cha jadi na cha kisasa (Classical and Modern Arabic).   Alipomaliza alianza masomo yake ya uzamili katika chuo hicho hicho, Tasnifu yake ilikuwa juu ya ushairi wa Kiswahili wa Muyaka bin Haji Ghassaniy   (1776-18400). Miye nilianza kumjua alipokuwa anaimaliza tasnifu yake mwaka 1965, tasnifu ambayo aliichapisha katika kitabu kiitwacho “Muyaka: 19th Century Popular Swahili Poetry.”

 

Wakati huo nilikuwa mkuukuu katika utangazaji kwani nilijiunga na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London, Novemba 1964 huku nikiwa nasoma masomo ya GCE “A” level.  Nilikuwa nikikaa nyumba moja na mtangazaji maarufu wa BBC, Salim Ibrahim Juma Bhalo (ambaye katika enzi za Rais Daniel arap Moi alikuwa balozi wa Kenya nchini Iran na Saudi Arabia).  Salim, mzalia wa Mombasa, kwa ukarimu wake alimkaribisha Badi Hassani akaye nasi kwa muda katika fleti yetu kwenye mtaa wa Golders Green.

 

Huu ulikuwa wakati ulionipa fursa kubwa ya kupevuka kifikra.  Salim alinichukulia kama mdogo wake na alinijulisha na vijana wengi kutoka Mombasa ambao nao pia walinichukulia kama mdogo wao.  Baadhi yao waliangukia kuwa wasomi wakubwa katika fani mbali mbali.  Kila mwishoni mwa wiki tulikuwa tukikutana kwa mandari au kwa kula na kupiga soga.

 

Katika duru hizo walikuwemo kina Abdalla Bujra aliyekuwa akisomea shahada ya uzamivu (ya udaktri wa falsafa) katika anthropolojia, Ahmed Idha Salim akisomea shahada ya uzamivu katika historia (siku za Moi naye pia aliteuliwa balozi nchini Sweden), na Ali Mazrui, aliyekuwa Chuo Kikuu cha Oxford akisomea shahada ya uzamivu katika siasa na Badi Hassani (Abdulaziz).  Mara kwa mara tukijumuika pia na Mohamed Hyder, aliyekuwa ameshapata shahada yake ya uzamivu wa zuolojia, kila alipokuwa akipita London pamoja na Ahmed Mohiddin (Taji) kutoka Canada ambaye siku hizo alikuwa akisomea shahada ya uzamili katika siasa.  Wote hao baadaye walikuwa maprofesa mashuhuri katika fani zao.

 

Kundi hilo la wanafunzi hao kutoka Mombasa lilikuwa chimbuko la wasomi wa kutoka Pwani ya Kenya waliohitimu katika vyuo vikuu vya nchi za Magharibi.

 

Ilimradi katika miaka hiyo nilikuwa nimezungukwa na jamaa hao wa Mombasa hata wao wenyewe wakisahau na wakinidhania kuwa ni mwenzao wa Mvita.  Jamaa wengine kutoka Mombasa niliokuwa nao BBC ni pamoja na Dalail Mzee, James Kangwana, Sal Davis (Sharif Salim Abdallah), Hassan Mazoa, Mohamed Bakhressa, Abdulaziz Mahmoud Fadhil al Bakry na ‘Dala Mbwana. Utambulisho wangu ulikuwa zaidi utambulisho wa kitamaduni (wa Uswahili) badala ya wa kijiografia na Mohamed Hassan Abdulaziz (Badi Hassani) alinisaidia sana kunifungua macho kuhusu urathi wetu adhimu wa lugha na utamaduni.  Naye alikuwa mtu wa mwanzo aliyenijulisha na ushairi wa Muyaka.

 

Mwaka 1967 aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki tawi la Dar es Salaam kuwa mhadhiri akisomesha Kiswahili na isimu. Baadaye akawa mhadhiri mkuu na kaimu mwenyekiti wa idara hiyo. Baada ya miaka mitatu alihamia Chuo Kikuu cha Nairobi akisomesha katika idara ya fasihi ya Kiingereza.

 

Mwaka 1971 Abdulaziz alianzisha idara ya isimu na lugha za Kiafrika katika Chuo Kikuu hicho hicho. Alikuwa mwenyekiti wa idara hiyo kwa miaka 15. Mwaka 2013 idara ya Kiswahili ilipoasisiwa Abdulaziz alijiunga nayo ingawa aliendelea kusomesha Kiarabu na isimu. Abdulaziz aliwahi kutunga mifumo ya kinadharia katika isimu ambayo hutumiwa ulimwenguni kote.  Mfumo aliouasisi unaotajika zaidi ni ule wa kiisimujamii unaoitwa traiglosia (triglossia) ambao unatumika katika takriban vitabu vyote vya isimujamii.

 

Miaka yote hiyo tangu nianze kumjua alinionesha ukarimu mkubwa wa mtu asiyekuwa na choyo na taaluma yake. Alikuwa pia mtu wafadhila. Nilizidi kumfaidi katika miaka ya mwanzo ya mwongo wa 1980 nilipokuwa nikifanya kazi na shirika la Unesco la Umoja wa Mataifa huko Nairobi.  Nilikuwa nikikaa hoteli na Abdulaziz, siku hizo tayari akiwa profesa wa Chuo Kikuu cha Nairobi, alinishauri nihamie kwake katika mtaa wa Hurlingham wakati akiwa katika likizo ya muda mrefu ya kuongeza taaluma (sabattical) Italia.

 

Aliniachia pia mpishi wake Jimmy aliyechanganya damu ya Kikuyu na Kitaliana.  Ingawa Jimmy alikuwa mpishi na dereva wake, Abdulaziz alimfanya kama mwana wa familia yake.

 

Abdulaziz alikuwa mtu wa haya, asiyependa kujipeleka mbele mbele lakini magwiji wenzake wa isimu walioutambua mchango wake katika fani hiyo hawakukubali.  Walimsukuma, mara nyingi bila ya mwenyewe kutaka, kwenye majopo kadha wa kadha yenye kuhusika na lugha za Kiswahili na Kiarabu pamoja na isimu.  Alisomesha na kuwatahini wanafunzi katika vyuo vikuu vya nchi mbali mbali.

 

Miaka yote hii niliyomjua Abdulaziz sikupata hata siku moja kumuona akiwa na hasira.  Siku zote alikuwa na uchangamfu na mizaha ingawa matani yake aliyawekea mipaka ya heshima na stara.  Masikhara yake hayakuwa yakifurutu ada au ya utovu wa adabu.  Na alipokuwa akifanya masikhara haiba yake ilizidi kupambika kwa kigugumizi chake. Namuona hivi hivi akiniangalia, akifanya mzaha na akisha akitazama chini huku akitabasamu.

 

Profesa Mohamed Hasan Abdulaziz ameacha mke na watoto watano.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com. Twitter: @ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.