Ole wetu Samia akihamia upande wa pili

Picha: Rais Samia Suluhu Hassan

 

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

 

KUJENGA msingi wa hoja yangu kwenye makala haya, ni muhimu kurejea nyuma miaka minane iliyopita.

 

Mwaka 2015, Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu. Katika uchaguzi huo, vyama vya upinzani vilipata takribani asilimia 40 ya kura zote – zikiwa ni kura nyingi kuliko wakati mwingine wowote hapa nchini tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992.

 

Katika uchumi, Tanzania ilikuwa moja ya nchi zilizojulikana kwa uimara wa uchumi wake, ukipanda kwa wastani wa walau asilimia sita karibu kipindi chote cha utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Ni katika wakati huohuo wa Kikwete, mwaka 2005 – hadi 2015, ndipo asilimia kubwa zaidi ya Watanzania iliondoka katika kundi la umasikini wa kutupwa.

 

Katika vigezo vya Demokrasia na Utawala Bora, Uhuru wa Habari na ule wa kujieleza, Tanzania ilikuwa mojawapo ya nchi za Afrika zilizokuwa katika nafasi za juu. Hata Zanzibar, isingekuwa tafrani iliyozushwa na hayati Jecha Salim Jecha, kulikuwa na uwezekano wa chama cha upinzani cha CUF kushinda kwenye uchaguzi ule.

 

Nimejaribu kuweka picha ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Tanzania kwa kuihusisha na utawala unaojali demokrasia. Kwamba enzi za utawala wa Kikwete, uchumi ulipanda, masikini walipungua, uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari uliongezeka na bado amani na utulivu vikatamalaki.

 

Labda nikumbushe kilichotokea mwaka 2020. Wakati huo Tanzania ilikuwa imehama kutoka siasa zinazojali misingi ya kidemokrasia ya Kikwete na kuhamia kwenye utawala wa kiimla wa hayati Rais John Magufuli. Uchaguzi wa mwaka 2020 ulipofanyika, upinzani ulifanya vibaya kuliko wakati mwingine wowote kwenye miaka ya karibuni. Mara nyingi huwa tunatumia neno uchafuzi kuelezea uchaguzi ule lakini ndiyo ulikuwa uchaguzi wa nchi yetu wakati ule.

 

Kufikia wakati huo, 2020, baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vimefungiwa, kuna watu wakawa wametoweka wasijulikane walipo, wanachama mashuhuri wa upinzani wakahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), uchumi wa nchi ukafubaa na vita dhidi ya umasikini vikaingia katika mtihani mzito. Ni kama vile gari ilikuwa imeanza kwenda kinyumenyume kulinganisha na mafanikio yaliyopatikana wakati wa mtangulizi wa Magufuli.

 

Kuingia madarakani kwa Rais Samia

 

Wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani mnamo Machi 2021, alikuwa na machaguo mawili ya kufanya – kurejea zama za Kikwete ambako walau misingi ya demokrasia ilikuwa inafuatwa au kuendelea na namna mambo yalivyokuwa wakati wa utawala wa Rais Magufuli.

 

Siwezi kutumia muda mrefu kueleza Rais Samia aliamua kufuata njia ipi lakini naweza kusema machache aliyoyafanya. Hivi ninavyoandika makala haya, magazeti yaliyokuwa yamefungiwa kama MwanaHALISI sasa yamerejea mitaani, matukio ya watu wasiojulikana kuteka watu yamepungua kwa kiasi kikubwa na vyama vya upinzani vimeruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara.

 

Katika mwaka wake wa kwanza tu wa kutawala, Rais mwenyewe alizungumzia kuhusu R nne ambazo zinaonekana ndiyo msingi wa utawala wake. R hizo zinahusu masuala kama Maridhiano, Mabadiliko, Ustahamivu na Kujenga Taifa lenye Umoja. Kwa vyovyote vile, huyu si aina ya Rais ambaye kichwani kwake ana mpango wa kurejea kule alikokuwa mtangulizi wake.

 

Inawezekana kabisa kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Rais Samia amewakwaza wapinzani au washindani wake kisiasa kwa namna moja au nyingine. Lakini, kama tutaamua kuangalia mambo yote kwa ujumla, utaona Tanzania ya leo ina mabadiliko makubwa katika mahusiano baina ya serikali, wapinzani wake na wananchi wake.

 

Kama CCM ingekuwa imempa Magufuli mgombea mwenza mwenye sifa, haiba na tabia inayofanana naye, sipati picha Tanzania ingekuwa wapi hivi sasa na kuna watu sijui wangekuwa wapi hivi sasa. Ni jambo la bahati kwamba CCM iliweka watu wawili wenye tabia na maono tofauti kwenye tiketi moja na hivyo kifo cha mmoja, kimetupa fursa ya kubadili mambo katika mwelekeo tofauti.

 

Ndiyo maana, kwa maoni yangu, nadhani si jambo la akili kufanya kampeni za kusema Rais Samia na Magufuli wanafanana. Sote tunajua kwamba hilo si kweli. Jambo pekee tunalofanya sasa ni kuanza kumsogeza Rais katika upande ambao unaanza kumwambia taratibu; “Tulikwambia, hao watu hawana shukrani. Dawa wanayoijua ni kutendwa kama alivyofanya mtangulizi wako.”

 

 

Kwa nini ni hatari kumsogeza Rais Samia upande wa pili?

 

Nilianza makala haya kwa kueleza namna Tanzania ilivyokuwa wakati wa utawala uliojali demokrasia kama wa Kikwete. Kwa ujumla, kwa kutazama uchumi, maendeleo ya jamii, uhuru wa kujieleza na vita dhidi ya umasikini, nchi ilipiga hatua katika maeneo yote hayo. Wakati huohuo, nchi ilirudi nyuma wakati wa Magufuli aliyekuwa na mtindo tofauti wa uongozi kulinganisha na Jakaya.

 

Kwa maana hiyo, Tanzania yenye demokrasia na uhuru wa kujieleza, ina uwezo mkubwa zaidi wa kupambana na umasikini, kujenga umoja, kuwa na fursa nyingi za ajira na yenye uwezo mkubwa zaidi wa kupambana na umasikini mkubwa uliotamalaki katika vijiji vyetu. Jumla yake ni kuwa sote tuna maslahi makubwa kwenye Tanzania ya kidemokrasia kuliko ya kidikteta.

 

Hata hivyo, Tanzania yetu ina hatari moja ambayo si wengi wetu wanaifahamu. Katika maandishi ya wasomi wa sayansi ya siasa duniani, nchi yetu huwa inawekwa katika kundi la nchi ambazo zina ushindani usio sawia kidemokrasia. Kwamba Tanzania si nchi ya kidikteta lakini pia huwezi kuiita nchi ya kidemokrasia kama unavyoweza kuita Sweden, Marekani au hata jirani zetu wa Malawi. Sisi tuko kwenye eneo tepetevu  – kwamba tunaweza kuwa taifa la kidikteta kwa hatua moja tu au kuwa kidemokrasia kwa hatua moja pia.

 

Uongozi wa Rais Magufuli ni ushahidi wa wazi kwamba Tanzania inaweza kuwa taifa la kidikteta kama Rais atataka iwe hivyo. Uongozi wa Kikwete ni ushahidi mwingine wa mahali nchi yetu inaweza kwenda endapo tutaamua kufuata mwelekeo anaoufuata Rais.

 

Ndiyo sababu, mara tu baada ya Rais Samia kuingia madarakani, niliandika andishi refu mtandaoni kupitia tovuti ya udadisi nikimsihi Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kufanya jitihada zote kuhakikisha anamsogeza Rais mpya jirani yake ili asiwekwe chini ya mbawa za wale wanaoamini Watanzania ni watu wanaotakiwa kuswagwa kama ng’ombe na si kuongozwa kama wanadamu.

 

Nakumbuka nilishambuliwa sana mitandaoni na wanachama na wafuasi wa Chadema wakisema Mwenyekiti wao hatarudisha mguu chini hadi serikali isalimu amri. Lakini mimi, katika miaka yangu takribani 20 ya uandishi wa habari, nimejifunza mengi sana kuhusu tabia ya Watanzania linapokuja suala la mapambano. Wapo wanaokutanguliza mbele ili uumie wewe ili yeye aendelee kufaidi matunda ya kuumia kwako.

 

Kwa bahati mbaya, Mbowe hakusikia wala kufuata nilichoandika. Nilikuja tu kusikia akiwa yuko mahakamani na baadaye gerezani kutokana na kesi ya madai ya uchochezi iliyofunguliwa dhidi yake. Kwangu, Mbowe alikuwa amepoteza nafasi adhimu ambayo kama angeikumbatia mapema, yeye, chama chake na Watanzania kwa ujumla wangepata manufaa zaidi.

 

Mawazo yangu miaka miwili iliyopita – na ambayo hayajabadilika hadi sasa, ni kwamba Rais Samia ni kiongozi anayetakiwa kuzuiwa kwa gharama yoyote asione kwamba njia inayotakiwa kufuatwa ni ile itakayoturudisha kule tulikokuwa enzi za utawala wa Magufuli. Inawezekana kuna watu walifurahishwa na utawala wa Magufuli lakini takwimu zinaonyesha kwamba watu wengi zaidi walinufaika kwa sababu ya sera za kidemokrasia za Kikwete kuliko zile za Uimla za Magufuli.

 

Labda nitangaze maslahi binafsi kufikia hatua hii. Erick Kabendera, mmoja wa wafungwa mashuhuri wakati wa utawala wa Magufuli, ni rafiki yangu binafsi. Kijana Ben Saanane ambaye ni mmoja wa watu waliotoweka wakati wa utawala wa Magufuli alikuwa mmoja wa wachangiaji wa makala kwenye gazeti nililokuwa nikihariri la Raia Mwema. Zitto Kabwe ambaye ni mmoja wa wananchi waliohangaishwa na kushughulikiwa ipasavyo na utawala wa Magufuli, naye pia ni rafiki yangu binafsi.

 

Ninapoandika makala ya namna hii, siandiki kwa sababu nimesimuliwa matukio yaliyotokea. Nimeishi na kushuhuhudia kwa karibu nini kinaweza kutokea pale ambapo Rais ataamua kuchagua kuhamia kundi la wale ambao hawaamini katika maridhiano, ustahamivu, mabadiliko na ukuaji. Ninachojua hadi sasa ni kwamba kundi hilo lipo na linasubiri kwa hamu siku ambayo Rais ataamua kuhamia upande wao.

 

Umagufuli ni mtaji kwa wengine

 

Ninafahamu pia kwamba kuna watu ambao wanafaidika pale ambapo Tanzania itaonekana kama nchi inayoendeshwa kama ilivyokuwa zama za Magufuli. Kama kuna watu wanatoa fedha kwa ajili ya kusaidia harakati za kupambana na uimla duniani, bila shaka wanaweza kufanya hivyo wakiambiwa na kuaminishwa kuwa Tanzania iko hivyo.

 

Kama maisha yako yanategemea Tanzania ya Magufuli, inayoonea na kutesa watu, inayopoteza watu, inayoumiza washindani na wapinzani, Tanzania yenye R nne ni habari mbaya kwako. Hata ningekuwa mimi, ningezidi kuandika na kuandika kwamba hali ya Tanzania ni mbaya – tena ikiwezekana mbaya kuliko hata enzi za Magufuli, ili niwafanye wanaochangia kutoa fedha zaidi.

 

Hayo pia ni maisha na mindhali Tanzania imepata Uhuru tayari na hakuna wapigania uhuru, njia zozote halali za kutafuta fedha zinaruhusiwa. Tatizo langu moja na kundi hili ni kwamba nchi ikiwa na aina ya Rais ambaye wao hawamtaki, inakuwa na faida kwa watu wengi zaidi kuliko ikiwa na Rais wanayemtaka ambaye uzuri wake kwao ni mateso anayowapa watu wake.

 

Kundi hili lingeweza kabisa kumfufua Magufuli aje kuongoza tena kama ingewezekana. Hilo lingehakikisha kwamba kundi lina ajenda za kudumu ambazo zingekubaliwa na wale walio tayari kufadhili jitihada hizo. Kitu pekee ambacho nina shida nacho na hili ni kwamba wakati wao watakuwa na kazi nyingi za kufanya, wananchi wengi wataumia na nchi kwa ujumla itaumia.

 

Nimetumia muda mrefu wiki hii kumsoma na kumwelewa mwamba wa siasa za China, Chou En Lai. Katika moja ya mafunzo makubwa kuhusu maisha yake ni suala zima la kuvumilia na kuhimili mambo fulani na kusubiri wakati sahihi ufike. Kama lengo letu ni kuishi maisha ambayo uchumi unapanda, watu wanakuwa huru na vita dhidi ya umasikini inapamba moto, kuna gharama ambayo tunatakiwa tulipe.

 

Inaweza kuwa kuonekana tunakubaliana kila kitu na aliye madarakani. Gharama inaweza kuwa kuonekana “chawa” wa Rais. Gharama inaweza kuwa kutoaminika baina na miongoni mwa watu wengine ambao mmeaminiana kwa muda mrefu. Lakini, kama alivyopata kusema Nicolo Machiaveli, matokeo ya mwisho ndiyo kila kitu.

 

Bahati nzuri, tayari tunajua kwamba utawala wa kidemokrasia ni mzuri kwa siasa na uchumi. Angalau kuna ushahidi wa macho na takwimu unaooonyesha kwamba wakati Tanzania inapotawaliwa kidemokrasia, hata uchaguzi huwa hauna umwagaji damu. Uchaguzi wa mwaka 2015 uliweka rekodi ya kukosekana kwa vitendo vyovyote vya matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola – walau kwa Tanzania Bara.

 

Kwa maoni yangu, ni muhimu kuhakikisha kwamba Rais Samia anabaki katika njia hii ya R nne aliyoamua kuifuata. Mabadiliko yoyote kutoka katika njia hii yanaweza kuwa na athari nyingi hasi ambazo zitaathiri watu wengi – ingawa nafahamu kwa wengine huo utakuwa muziki mzuri masikioni mwao.

 

Ninaamini pia kwamba Rais Samia anahitaji uungwaji mkono zaidi kwa sababu mbili zaidi. Sababu ya kwanza ni kwamba amebeba dhamana kubwa ya viongozi wanawake si Tanzania pekee bali Afrika na duniani kwa ujumla. Dunia imetoka mbali kufika hatua hii ambapo wanawake sasa wanaaminika kushika nyadhifa za juu za uongozi. Kufanikiwa kwake, itakuwa ni kufanikiwa zaidi kwa wanawake.

 

Jambo la pili linahusu Muungano wetu. Sina uhakika kama nitamuona Mzanzibari mwingine akiwa Rais wa Tanzania wakati nikiwa hai. Ninatamani kwamba urais wa Samia ndiyo uwe ambao utamaliza kero zilizopo – hasa zile kwa muda mrefu Wazanzibari wamekuwa wakizilalamikia. Kama mimi ningelikuwa Mzanzibari – tena wa umri wangu, ningelitamani kuona anafanikisha ndoto zake kwa Watanzania wote, na Wazanzibari.

 

Nadhani huyu ni Rais tunayetakiwa kwenda naye kwa hadhari kubwa. Hatua moja – moja tu; kushoto au kulia, inaweza kuwa na athari kubwa maisha ya mamilioni ya Watanzania. Nimeandika.

 

Mwandishi ni msomi wa masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kwa email ya; ekamwaga57@gmail.com